Sunday, 11 October 2015

TAARAB NA LELEMAMA ZILIVYOJENGA HAIBA YA NYERERE NA TANU


TAARAB NA LELEMAMA ZILIVYOJENGA HAIBA YA NYERERE NA TANU KATIKA KUPIGANIA UHURU WA TANGANYIKA

Bi Titi Mohamed na Nyerere

Kuna mambo na watu historia wamesahaulika katika historia ya uhuru wa Tanganyika. Mathalan watoto wa Mzee wa Kizulu kutoka, Afendi Plantan kutoka Imhambane Msumbiji (wakati ule Mozambique) watakumbukwa kwa mchango wao katika kupigania uhuru wa Tanganyika kila mtu kwa lile alilofanya na juhudi aliotia kupeleka mbele mapambano. Mtoto mkubwa wa Afendi Plantan, Mwalimu Thomas Sauti Plantan yeye atakumbukwa kama mmoja wa marais wa TAA na rais pekee aliyetolewa kwa kupinduliwa. Mdogo wake Schneider Abdillah Plantan atakumbukwa kwa mambo mawili. Jambo la kwanza ni ile vurugu alofanya bila woga mbele ya Wazungu katika mkutano wa TAA katika Ukumbi wa Arnatouglo alikolazimisha mkutano wa uchaguzi uitwishe wachaguliwe viongozi wapya na wakoloni waliridhia mkutano kweli uitwishe na viongozi wapya vijana wakapatikana - Dr Vedasto Kyaruzi kama rais na Abdulwahid Sykes katibu. Jambo la pili atakalokumbukwa Schneider ni kule kuwatafuta Tatu bint Mzee na Titi Mohamed kuwaingiza katika TANU ili kuunda kundi la wanawake ndani ya TANU kama alivyoshauriwa na John Hatch wa Labour Party alipotembelea Tanganyika mwaka wa 1955. Ramadhani Mashado Plantan yeye atakumbukwa kwa kuipa TANU sauti kupitia gazeti lake Zuhra. Nyerere amesomeka kwa mara ya kwanza katika gazeti la Zuhra mwaka wa 1954 na hii iliendelea hadi TANU walipoanzisha gazeti lao Sauti ya TANU mwaka wa 1956.

Schneider aliwatia hima akina  Bi. Titi, Tatu bint Mzee na wanawake wengine kuingia katika TANU. Katika mji wa Dar es Salaam kulikuwa na vikundi vya akina mama na hivi vikundi hasa vilikuwa vya kusaidiana katika harusi, misiba nk.  Lakini ilikuwa katika sherehe za harusi ndipo hasa vikundi hivi vilionyesha nguvo zao. Wanawake wake watafunga sare. Kwa kawaida sare zilikuwa ni khanga na endapo magauni yatakuwepo basi hiyo ni ziada lakini juu ya hilo gauni utatupwa upande wa sare ya khanga. Khanga hizo zilikuwa zikichaguliwa kwa maneno yaliyoandikwa ambayo yalikuwa na ujumbe maalum. Kwa mfano utakuta khanga imeandikwa, “Mvua ya Nyeminyemi Haimzuii Mgeni Kwenda Kwake Wala Mwenyeji Kula Chake,” au “Kelele za Mlango Hazimzuii Mwenye Nyumba Kulala.” Mwaka 1949 zilitoka khanga na jina, “Ahsante William Nason.” William Nasson alikuwa kapteni wa timu ya Tanganyika iliyochukua kikombe cha Gossage kilichokuwa kikishindaniwa kati ya Tanganyika, Kenya na Uganda. 


Timu iliyoshida kombe la Gossage 1949

Vikundi maarufu vya lelemama vilikuwa “Saniyyat Hubbi,” (Ndugu Wapendanao), “Goodluck,” “Coronation,” na “Bomba Kusema.”  Vikundi hivi vilikuwa na usushuba na vikundi vya taarab maarufu Dar es Salaam ilikuwa “Al-Watan” na “Egyptian.” Ilikuwa si tabu kuvitia vikundi hivi kwenye TANU kwa kuwa kwanza tayari akina mama wenyewe walikuwa weshajikusanya. Schneider kazi yake ilikuwa nyepesi ilikuwa ni kuwaongozea jukumu jipya nalo ni kuwa sasa pamoja na sherehe za harusi, misiba, mikole, kucheza wali na mengineyo sasa akina mama watie juhudi kuunga mkono harakati za kudai uhuru. Kwa bahati nzuri sasa ikawa hao viongozi wa lelemama akina Hawa bint Maftah, Tatu bint Mzee, Bi Titi Mohamed. Kidawa bint Abdallah na wengine haukupita muda wakawa wanachama wa mbele katika TANU na Titi na Tatu bint Mzee wakaja kuwa wajumbe katika Halmashauri Kuu ya TANU pale Makao Makuu, New Street.

Bi. Titi Mohamed
Hawa binti Maftah alikuwa mwanamke wa Kimanyema akikaa Mtaa wa Mkunguni na New Street na kama kiongozi wa lelemama, alijulikana kwa jina la “Queen.” Hakuna hata mtu mmoja Tanganyika nzima, mbali na Nyerere mwenyewe, aliyeweza kuifanya TANU kuwa maarufu kama Bibi Titi Mohamed. Bibi Hawa Maftah ndiye aliyeiingiza kwa mara ya kwanza nyimbo za lelemama ziimbwe katika mikutano ya TANU kama mbinu ya kuhamasisha wananchi kukipenda chama. Huko Tabora kulikuwa na vyama vingine vya wanawake “Nujum ul Azhar,” “Waridatil Hubb” na “Egyptian Club.” Hapo Tabora ilikuwa Bi Nyange binti Chande na Dharura binti Abdulrahman ndiyo waliovitia vyama hivi katika TANU. Vyama hivi vya akina mama vilisaidia sana kuipa TANU nguvu katika Jimbo la Magharibi. Akina  mama hawa walitunga nyimbo zenye na ujumbe wa kuhamasisha wananchi na nyimbo hizi zilikuwa na athari kubwa katika harakati.


Kushoto wa kwanza ni Tatu Biti Mzee, wa tatu ni Julius Nyerere na wa tano ni Titi Mohamed picha ilipigwa Uwanja wa Ndege Dar es Salaam safari ya Nyerere UNO 1955

Inasemekana miongoni mwa matawi yote ya TANU nchini Tanganyika, tawi pekee lililoungwa mkono na wanawake na wao kuwa ndiyo nguvu kuu ya chama, lilikuwa tawi la TANU  Moshi mjini. Hapa Moshi nguvu kuu ya TANU ilikuwa wanawake waliokuwa wakiuza mbege, pombe maarufu ya kienyeji huko Kilimanjaro. Uuzaji wa pombe huko Kilimanjaro ilikuwa ni kazi ya wanawake tu, kuuza mbege haijapata kuwa kazi ya wanaume. Moshi mjini mkuu wa kilabu cha pombe alikuwa bibi mmoja wa Kimasai akijulikana kwa jina la Mama Binti Maalim. Ingawa mume wa Binti Maalim, Jumbe Mohamed, alikuwa mtumishi wa serikali, na kwa hiyo alijitenga na siasa, hili halikumzuia mke wake, Binti Maalim kuwa mwanachama na mwanaharakati wa TANU. Binti Maalim alihakikisha kwamba kila mwanamke aliyekuwa akifanya biashara mahali pale alikuwa mwanachama wa TANU na alikuwa akitoa sehemu katika kipato chake kusaidia harakati za kudai uhuru. Wanachama wa mwanzo kujiunga na TANU walikuwa wale akina mama wauza pombe waliohamasishwa kujiunga na chama na Mama Binti Maalim. Nafasi ya wanawake katika harakati mjini Moshi inaweza kuonekana katika katika safari yake ya pili ya Nyerere Kilimanjaro. Katika safari hiyo Nyerere alifikia nyumbani kwa Bibi Halima Selengia aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya tawi la TANU Moshi. Safari yake ya kwanza Nyerere alifkia KNCU Hotel (Kilimanjaro Native Cooperative Union). Wakati huo TANU ilikuwa haijaota mizizi. Lakini katika safari yake ya pili wanachama walidai kwamba lazima Nyerere atayarishiwe malazi yake na TANU.

Kuna wakati serikali ya kikoloni ilimpiga marufuku Nyerere kufanya mikutano ya hadhara. Ili kuepuka kadhia hiyo TANU ilikuwa ikiandaa taarab na Nyere alikuwa akikaribishwa kama mgeni wa heshima. Nyerere alikuwa akisimama kufungua hafla na katika kufanya hivyo alisema maneno machache. Kwa namna hii ule moto wa kudai uhuru ulibaki ukiwaka. Kwa njia hii Nyerere aliweza kuwasiliana na wananchi. Halikadhalika kupitia taarab TANU ilikusanya fedha kwa ajili ya harakati. Kulikuwa na wimbo mmoja wa lelemama ambao uligeuzwa kuwa kama ndiyo mwimbo wa Nyerere, mwimbo huu  na ulikuwa akiimbiwa yeye tu. Mwimbo huo ulikuja kuwa maarufu sana kiasi kwamba ulipoimbwa katika mikutano ya TANU watu wote waliimba kwa pamoja. 

Mashairi yake yalikuwa kama hivi:

“Muheshimiwa nakupenda sana, wallahi sina mwinginewe Insha Allah Mungu yupo, Tanganyika tutajitawala.”

Huu mwimbo si kama ulikuwa maarufu kwa mama zetu bali hata watoto katika michezo yetu ya kuwamba kopo na plastiki kutengeneza ngoma mwimbo huu ulikuwa maarufu.

Ilikuwa katika taarab iliyoandaliwa kusheherekea  kufunguliwa kwa tawi la TANU Dar es Salaam ya Kaskazini katika mtaa wa Mvita, nyumba namba 10, tarehe 10 Agosti, 1957, ulimi wa Sheikh Takadir ukateleza, akamuita Nyerere “Mtume.” Tawi la TANU Dar es Salaam ya Kaskazini lilikuja kuwa lenye nguvu sana kuliko yote na tawi likawa na mafanikio labda kupita matawi yote katika Tanganyika. Mwenyekiti wake alikuwa Mtoro Kibwana na mweka hazina Haidar Mwinyimvua, ambae baadae aliingia kamati kuu ya TANU ya taifa. Kwenye hafla ile, katika kumtambulisha Nyerere na kummiminia sifa, Sheikh Takadir bila kufikiri aliwaambia wasikilizaji wake kuwa Nyerere ni “Mtume wa Afrika.” Kama kauli ile ingetolewa siku nyingine yoyote ile, huenda tamko hilo lisingezua kishindo, na huenda lingepita bila kuwa na taathira yeyote mbaya. Lakini ufunguzi wa tawi la TANU la Mvita katika siku hiyo tarehe 10 Agosti, 1957 ilikuwa siku maalum kwa wakazi wa Dar es Salaam.

Kwanza, Dar es Salaam ilijitokeza kushuhudia kutoka kwa mwimbaji stadi, Nuru binti Sudi, kutoka Al-Watan na kujiunga na wapinzani wao Egyptian. Hivi vilikuwa vikundi viwili vya taarab vilivyokuwa na ushindani mkubwa mjini Dar es Salaam. Siku hiyo Nuru alikuwa anaimba pamoja na kikundi chake kipya kwa mara ya kwanza na mashabiki wake walikuwa wamekuja kumwona bingwa wao akiimba katika hafla ya TANU. Halikadhalika mashabiki wa Egyptian walikuwa wamekuja vile vile kushangilia na kuwazomea washindani wao kwa kumchukua bingwa wao. Kulikuwa na sababu nyingine kwa watu kushangilia. Katika kuhama huko kutoka Al-Watan na kuingia Egyptian, Nuru alikuwa ameweka msimamo wa kisiasa. Nuru alikuwa na damu mchanganyiko. Baba yake alikuwa Mwarabu na mama yake alikuwa Mwafrika.  Kabla ya kutoka Al-Watan na kuingia Egyptian alikuwa mwanachama wa Coronation ambacho kilikuwa chama cha akina-mama wenye asili ya Kiarabu. Kwa hiyo ilichukuliwa kwamba, maadam Egyptian ilihusiana na Waafrika, kwa kitendo kile cha kuhama Al-Watan, Nuru alikuwa ameasi na kurudi kwa ndugu zake, yaani Waafrika.  Wapenzi wake  wakipita mitaani wakisema Nuru amerudi kwenye asili yake, kwenye tumbo la mama yake aliyemzaa. Hivi ndivyo mambo yalivyokuwa siku zile, kila jambo lilipewa tafsiri ya kisiasa. Wakati huo United Tanganyika Party (UTP) ilikuwa tayari imeshanzishwa na Egyptian ilikuwa imetunga nyimbo maalum kwa ajili ya hafla hiyo ambayo Nuru aliimba kuidhihaki UTP. Sehemu ya mashairi yake yalikuwa yanasema hivi, “UTP wana majambo, TANU wanaichukia.” Makamu wa Rais wa UTP alikuwa Sheikh Hussen Juma, muungwana wa Kimanyema.

Pili, ili kuadhimisha kufunguliwa kwa tawi la TANU Mvita, TANU iliwaalika wajumbe wa Baraza la Kutunga Sheria, wengi wao machifu, ili kushuhudia sherehe hiyo. Miongoni mwao walikuwa Chifu Kidaha Makwaia, Humbi Ziota, Msabila Lugusha, Mwami Theresa Ntare na wengine wengi. Vilevile walikuwepo watu wengine mashuhuri kama Hamis Mfaranyaki ambae ndiye alikuwa kiongozi wa Wangoni mjini Dares Salaam, Paul Bomani, Said Chaurembo, kaka yake Sheikh Abdallah Chaurembo na wengine wengi. Kwa hakika shughuli ile ya TANU ilikuwa kubwa. Pamoja na watu wote hawa mashuhuri kuhudhuria, huu ulikuwa usiku adhimu kwa TANU. Hapakuwa na shaka yoyote kuwa chochote kitakachosemwa katika hafla kama hiyo kitakuwa na athari kwa watu. Ilikuwa katika hafla hii ndipo siku ulimi wa Sheikh Takadir ukateleza.

Katika hotuba zake Sheikh Takadir alikuwa akiitaja TANU kama “tano” na alipotamka neno “tano” alikuwa akionyesha vidole vyake vitano vya mkono wa kulia, bila shaka yoyote akifananisha na  sala tano za fardh katika Uislam. Sheikh Takadir alikuwa akipandisha hisia kali za Kiislamu kwa wasikilizaji wake kwa kutoa mifano mingi katika Qur'an Tukufu, akihadthia mifano ya mathalan, kisa cha Daudi na Jalut, kisa cha Firauni na waziri mkuu wake, Haman na jinsi walivyowakandamiza Bani-Israil. Sheikh Takadir alikuwa akimaliza hotuba zake kwa kuonyesha kuwa mwishowe haki hushinda batil akimaananisha kuwa uovu wa Waingereza utashindwa. Ilikuwa katika hotuba zake nyingi kama hizi za kumsifu Nyerere, Sheikh Takadir aliteleza na kumwita Nyerere “mtume.”

Katika hafla hiyo waheshimiwa, wageni waalikwa walipewa vitafunio, vinywaji baridi na chai. Nyerere katika kutoa shukrani kwa wanachama wa TANU alikamata kikombe cha chai na kukionyesha juu kwa wasikilizaji wake. Aliwaambia watu kwamba wasidhani kitendo cha kumpa mtu kikombe cha chai ni kitu kidogo. Nyerere aliendelea kusema kuwa watu wameiuza nchi hii kwa kupewa kikombe cha chai na wakoloni. Nyerere alikuwa akitoa maneno hayo akiwa anawapigia vijembe watu maalum. Nyerere kwa maneno yake  alikuwa akiwakusudia machifu. Baadhi yao walikuwa pale pale katika meza kuu wakinywa chai na yeye. Wakati huo baadhi ya machifu walikuwa wakishirikiana na Gavana Twining na UTP katika hila za kuipiga vita TANU ishindwe kuikomboa Tanganyika kutoka makucha ya ukoloni. Ilikuwa dhahiri kuwa makombo waliyokuwa wakipata machifu kutoka kwa Mwingereza hayakuwa hata na thamani ya kikombe cha chai. Maneno ya Nyerere hayakuwa fumbo kwa wale machifu. Yalikuwa maneno ya wazi ambayo waliyaelewa. Machifu walitambua kuwa wao ndiyo walikuwa wakisemwa katika hotuba ile ya shukurani. Lakini kijembe kile kwa hakika yake kilikuwa kimeelekezwa kwa Chifu Kidaha. Chifu Kidaha alikuwa na bahati mbaya sana. Abdulwahid Sykes miaka michache nyuma alimbembeleza sana ajiunge na TAA wamfanye rais kisha waje kuunda TANU na yeye wamchague kuwa rais lakini alikataa.  Ilikuwa katika usiku huu Sheikh Takadir katika hotuba yake alimweleza rais wa TANU, Nyerere, kama ''mtume'' aliyeletwa na Allah kuja kuikomboa Afrika.

Chief Makongoro
Maneno haya yalimuudhi sana Sheikh Hassan Bin Amir na Waislam wengine. Siku chache baada ya maneno yale ya Sheikh Takadir, Mufti Sheikh Hassan Bin Amir akiwa amefuatana na Chifu Makongoro alikutana na Sheikh Suleiman Takadir njiani, katika makutano ya Mtaa wa Swahili na Mkunguni, Sheikh Hassan Bin Amir alimkabili Sheikh Takadir na kumwambia asirudie tena maneno hayo kwa kuwa yalikuwa kufr. Kwa Sheikh Takadir kumtaja Nyerere kama “Mtume,” alikuwa anampandisha Nyerere kwenye daraja isiyoweza kufikiwa na kiumbe chochote.



Kushoto: Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Said Omar bin Sumeit, Ally Mwinyi Tambwe, Abbas Sykes
na chini yao katika ni Sheikh Kassim bin Juma
Waislam wengine waliopinga kauli hiyo walichukuliwa kama si wazalendo, watu wenye kuipinga TANU na Nyerere, kwa hiyo wao ni sawasawa na vibaraka wa mkoloni. Maneno ya Sheikh Takadir bila chembe yoyote ya shaka yalitamkwa kwa nia nzuri katika kilele cha hamasa. Maneno yale hata hivyo yalikuja, si muda mrefu, kumsuta na kutibua akili yake hata mwaka haujapita, Sheikh Takadir alipomshutumu Nyerere kuwa ni adui wa Uislam na Waislam. Insha Allah nitasimulia ugomvi huo baina ya Sheikh Takadir na Nyerere hapo baadae. Sheikh Suleiman Takadir alimtabiri Nyerere kuwa atakuja kuwa adui wa Waislam. Kisa hiki ni katika visa vyenye msisimko wa pekee katika historia ya TANU kiasi kwamba juu ya mchango wake mkubwa katika TANU, hivi leo Sheikh Takadir amefutwa katika historia ya Tanzania na hajapatkana yeyote kueleza habari zake lau kama kwa uchache.

Juu ya yote haya nyota ya Nyerere ilizidi kung'ara siku baada ya siku kwani akina mama kila kuchao walikuwa wakija na nyimbo na mashairi mapya ya kumsifia.

No comments: