Hemed Seif |
Timu ya Taifa 1960s Kushoto Kwenda Kulia: Hemed Seif, Mbwana Abushiri, Awadh Matesa, (sina jina lake), John Limo, Mathias Kissa, Abdallah Aziz, (sina jina), Miraji, (sina jina) Chaki |
Waliosimama wa Kwanza Kutoka Kulia Hemed Seif |
Hemed Akida Seif |
Kushoto Kwenda Kulia: John Limo, Mbwana Abushiri, Hemed Seif na Salehe Zimbwe |
Kushoto ni Marehemu Salim Kajembe na Kulia ni Hemed Seif |
Zimenifikia taarifa hivi punde kutoka Tanga za kifo cha Hemed Akida Seif. Hemed Seif amefariki jana baada ya kuugua kipindi kifupi akalazwa hospitali kasha akatoka. Hemed Seif amezikwa leo asubuhi, Jumapili tarehe 13 Aprili 2014 sawasawa na tarehe 12 Mfungo Tisa 1435 na kazikwa kwenye makaburi ya familia yao Magaoni Tanga ambako ndiko alikozaliwa na kuishi maisha yake yote. Huenda leo pakawepo wengi ambao hawamjui Hemed Seif ni nani.
Hemed Seif alikuwa mchezaji mpira maarufu katika miaka ya 1960 na siku zote akivaa jezi na. 10. Hapakuwahi kutokea mchezaji akamnyang'anya jezi hiyo wakati yeye alipokuwa bado anacheza. Jezi namba 10 ilikuwa imegongewa misumari mgongoni kwake. Hemed Seif alikuwamo katika ile timu ya taifa iliyochukua Kikombe cha Gossage mara mbili mfululizo mwaka 1964 na 1965 chini ya kocha Myugloslavia, Celebic.
Sifa kubwa ya Hemed Seif ilikuwa ni kufunga magoli kutoka mbali, yaani nje ya kumi na nane au nje ya ''box,'' kwa mashuti mazito na hapa ndipo palipokuwa na ''uchawi'' wake. Hemed Seif alikuwa mwembamba mrefu na anapokuwa uwanjani ikiwa humjui, picha itakayokujia ni kuwa ni mchezaji ambae mabeki watamzoa kwa vibuyu kirahisi na kumwangusha chini kwa wembamba wake. Lakini haikuwa hivyo kwani ingawa alikuwa mwembamba Hemed Seif alikuwa na kasi na ujanja wa kuwatoka mabeki kirahisi. Zaidi ya hayo miguu ya Hemed Seif ilikuwa ikibeba mabomu na mizinga mizito.
Free-kick'' zote pamoja na ''penalty'' iwe katika timu yake ya Tanganyika Planting Company (TPC) kutoka Moshi au Timu ya Taifa alikuwa anaachiwa Hemed Seif kupiga na kwa hakika mara nyingi sana nyavu ilikuwa lazima zitikisike. Hemed Seif alikuwa mtaalam wa magoli. Mikwaju yake ilikuwa gumzo kwa timu pinzani na magolikipa wote wa Afrika ya Mashariki wakati akicheza katika mashindano makubwa ya wakati huo ya Taifa Cup na Kombe la Gossage. Kombe ambalo likishindaniwa na nchi zote za Afrika ya Mashariki, Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar. Hemed Seif katika timu ya taifa alikuwa akicheza na ‘’Director’’ Mbwana Abushiri kuliani kwake na John Limo akiwa mbele katikati ‘’centre forward,’’ au ‘’half back’’ wa kulia. Wingi wa kulia akiwa Sembwana na kushoto Abdallah Juma Aziz.
Nakumbuaka kama jana vile jinsi tulivyokuwa tukilisubiri basi la TPC liingie uwanjani na sisi watoto tukimbilie kuwaangalie wachezaji nyota wa zama zile kama Hemed Seif mwenyewe na kaka yake Marshed Seif, Mbwana ''Director'' Abushiri, Sembwana, John Limo, Awadh Maseta, Ishaka Mzee, Dracula, Emil Benadicto Kondo, Shariff Salim, Hospitali, Okoth ambae alikuwa golikipa wa timu ya taifa Kenya kasha akaja kucheza TPC. Enzi zile takriban timu nzima ya TPC ilikuwa ikichaguliwa katika timu ya taifa. Wachezaji hawa mimi nimewafaidi sana katikia utoto wangu wakija kucheza Ilala Stadium katika miaka ya 1960 katikati.
Lakini kabla ya hapo niliwaona akina Hemed Seif wakati nikiishi na wazee wangu Moshi. Niliwaona wachezaji hawa wakicheza timu ya TPC ikija Moshi, King George Memorial Stadium, Lukaranga kuja kupambana na timu kama Kahe au Tanganyika Coffee Curing Company (TCCC) timu ambazo ndizo zilizokuwa zikishiriki katika ligi Moshi mjini. Kahe ndiyo timu angalau ikijitahidi kutoa upinzani mkali kwa TPC lakini bila mafanikio. Kahe ilikuwa timu ya wafanyakazi katika shamba la mkonge la Kahe na walikuwa na wachezaji vijana wa Kijaluo kutoka Kenya.
Wachezaji hawa wa Kahe walikuwa wakitegemea nguvu zao zaidi ya ujuzi wa mpira. Hapo ndipo palipokuwa na raha kuangalia mpira wa TPC na Kahe wakati nguvu zilipogeuzwa zikawa kichekesho wakati wachezaji wa TPC wakigonga pasi kuanzia nyuma hadi mbele kisha ikapigwa ''back pass na Mbwana wakati mwingine kwa kisigino na Hemed Seif kama vile simba aliyekuwa akisubiri mawindo akapokea pasi bila kutuliza na ghafla nyavu zinacheza.
Mwaka 2000 nilikwenda kufanya kozi Nairobi na mmoja wa walimu wangu alikuwa mchezaji wa timu wa zamani wa timu ya taifa Kenya Mohamed Abdilkadir. Alipojua natokea Tanga akaniuliza kama namjua Hemed Seif. Nilipomweleza kuwa Hemed Sief nikonae barazani kila siku na tunafanya kazi pamoja bandarini alifurahi sana ndipo akanipa kisa chake kuhusu Hemed Seif. Alinambia kuwa yeye katika miaka ya 1960 alikuwa mwanafunzi Chuo Kikuu cha Nairobi na alikuwa akicheza timu ya taifa ya Kenya akiwa katika safu ya ulinzi kama ''half back.'' Anasema siku ilipojuliikana kuwa Kenya watakutana na Tanzania, kocha na wachezaji wenzake walimuonya kuwa awe makini sana na Hemed Seif, amwangalie sana asimuachie hata kidogo kwani ni mfungaji mabao hatari mno.
Mohamed Abdilkadir anasema ikawa sasa kwake ni vitisho wenzake wakimtisha kwa kumpigia makelele, ''Mohamed, Hemed Seif huyo nyuma yako...'' Basi katika mazoezi ikawa ni vicheko na vitisho kwake kuhusu Hemed Seif na mashuti yake. Maelezo haya yakanitia hamu nikamuuliza nini kilitokea Nairobi City Stadium siku ya mechi ya Kenya na Tanzania. Mohamed Abdilkadir alitingisha kichwa akasema,''Bwana ilikuwa kazi. Mimi nilimpania Hemed Seif. Sikuwa nabanduka nyuma yake. Nilikuwa kama kivuli chake, kila anapokwenda niko mgongoni kwake...wapi bwana. Kama walivyonitahadharisha wenzangu kitambo...Hemed Seif alifunga bao kama kawaida yake. Nikakumbuka maneno ya wachezaji wenzangu kuwa Hemed Seif hatoki uwanjani bila ya kutingisha nyavu.'' Hemed Seif alikuwamo katika timu ya Tanzania ilipocheza na timu kali ya daraja la kwanza kutoka Uingereza, West Bromwhich Albion ilipokuja nchini na kucheza na timu ya Tanzania Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru). Kama kawaida Hemed Seif aliwatoka mabeki wa West Bromwhich na kufunga goli. Picha yake ilitoka kwenye ''Tanganyika Standard'' ikimuonyesha Hemed Seif akifunga bao hilo. Huyu ndiye Hemed Seif aliyekuwa msakata kabumbu maarufu.
Hemed Seif alistaafu kazi Tanzania Ports Authority (TPA) Tanga kiasi cha kama miaka kumi iliyopita na tofauti na wenzake wengi aliochezanae mpira wakati mmoja, Hemed alikuwa na maisha mepesi ya kupendeza na alikuwa akicheza mpira na utu uzima wake kila alipopata nafasi. Mmoja wa marafiki zake na mwanabaraza nilipompigia simu kumpa mkono wa pole akanambia kuwa,’’Hemed Seif siku zote alikuwa mwanamichezo hadi umauti ulipomfika.’’ Nilikuwa nikimtania Hemed Seif kuhusu gari zake nzuri za kupendeza alizokuwa akiendesha pale mjini. Yeye alikuwa siku zote akinipa jibu kuwa, ''Ah! Sheikh Mohamed watoto hao wananiletea.''
Nyakati za jioni Hemed Seif alikuwa anapenda kukaa kwenye baraza yao ya ''watoto wa mji,'' akina Said Bembea, Saleh Makubeli na nduguye Athmani Makubeli, Salim Mohamed Kajembe, Mzee Ali ''Ma-White,'' ambao wote ukimtoa Said Bembea wameshatangulia mbele ya haki. Baraza hii ilikuwa kwenye kituo cha kuuza mafuta cha Agip karibu sana na Mkwakwani Stadium ambapo hadi leo napakumbuka maana palikuwa na chai nzuri sana jioni ambayo nikisimama kusalimia wanabaraza watanilazimisha kunywa angalau kikombe kimoja kabla sijashika hamsini zangu. Kituo hiki cha mafuta kilikuwa kikimilikiwa na marehemu Saleh Makubeli. Baraza hii ya Hemed Seif na wenzake ilikuwa baraza ya manufaa ikipigwa adhana wote wananyanyuka kwenda msikiti wa jirani maarufu Msikiti wa Maalim Jumbe kwenda kusali. Hemed Seif alikuwa mtu wa ibada na ukiangalia picha yake na Salim Kajembe utaiona sijda yake jinsi ilivyomuenea usoni.
Allah amsamehe sahib yangu na kaka yangu dhambi zake na amweke mahali pema peponi.
Amin.
Kushoto Kewnda Kulia: Kitwana Manara, Rashid Seif Hemed Seif, Abdallah Luo |
Waliosimama wa Kwanza Kushoto: Hemed Seif |
No comments:
Post a Comment