Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!
(Mlango wa Kwanza:
Siri Nzito)
Written by mas-albimany //
26/11/2015 // Makala/Tahariri // Hakuna maoni
Mwandishi
(Makala kwa Hisani ya Mzalendo.Net)
(Makala kwa Hisani ya Mzalendo.Net)
Kushoto: Dr. Harith Ghassany akiwa Tanga na Mzee Mohamed Omari Mkwawa wakati wa utafiti wa kuandika kitabu ''Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru'' |
Harith Ghassany ni Muafrabia kindakindaki
aliyezaliwa na wazazi wa Kiarabu na mabibi wa Kiafrika kuumeni kwake kutoka
kabila la Kimanyema na la Kimwera. Amekhitimu kutoka chuo cha Msikiti Baraza na
Skuli ya Tumekuja (Mtakatifu Yusuf) Zanzibar, na Shule ya Popatlal, Tanga.
Alitunukiwa shahada yake ya kwanza kwa daraja ya “heshima” katika masomo ya
Mashariki ya Kati kutoka Chuo Kikuu cha Kimarekani, jijini Cairo – Misri. Pia
alitunukiwa shahada ya Masters mwaka 1988 kutoka Chuo Kikuu cha Kimarekani cha
Michigan katika masomo ya Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Karibu, na
shahada ya Masters ya pili kutoka Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani, na
kumaliziya na shahada ya Udaktari wa Falsafa pia kutoka Chuo Kikuu cha Harvard
katika masomo ya Ilimu ya Binaadamu (Anthropology) na ya Mashariki ya Kati.
Harith Ghassany ni msomi/mtafiti huru na anaishi Marekani, Washington D.
Mlango wa Kwanza: Siri Nzito
Mtawaliwa siku zote anataka kumuigiza
mtawala katika maumbile yake, mavazi yake, kazi zake na yote yanayokhusiana na
hali yake na dasturi zake. —Ibn Khaldun
Mapinduzi Tanganyika na Kenya
Picha kubwa ya Mapinduzi ya Zanzibar ya
1964 haiwezi kufahamika bila ya kuyafahamu ijapokuwa kwa mukhtasari mfupi
mapinduzi ya kabla yake yaliofanyika Tanganyika, na baadaye Kenya. Mapinduzi ya
Tanganyika, ya Zanzibar, na ya Mwambao wa Kenya ni mifano ya mapinduzi ya
kalamu na ya umwagaji damu.
Tanganyika iliupata uhuru wake tarehe 9
Disemba 1961 na Waislam wa Tanganyika walikuwa na mchango mkubwa sana katika
kuupiganiya uhuru huo. Hayati Julius Kambarage Nyerere alitowa mchango mkubwa
na yeye mwenyewe alikiri hivyo kwenye hotuba yake ya kuwaaga wazee aliyoitowa
Dar es Salaam katika mwezi wa Novemba mwaka 1985. Kwa mara ya kwanza Mwalimu
alielezeya namna alivyopokelewa, kujuulishwa na kusaidiwa sana na wazee wa
Kiislamu wa Dar es Salaam. Kwenye shughuli za TANU yeye alikuwa ni Mkristo peke
yake na mara nyingine alikuwepo John Rupia.
Muhimu pia na kwa mara ya kwanza Mwalimu
alisikika akisema kwenye hotuba hiyo kuwa hata jina la Tanganyika African
National Union (TANU) lilifikiriwa na kuundwa na akina marehemu Abdulwahid
Sykes walipokuwa askari Burma katika vita vya pili vya dunia.1
Historia iliyofichwa ya mchango wa Waislam
katika kuupiganiya uhuru wa Tanganyika imeandikwa na kuelezwa kwa ufasaha
mkubwa na mwandishi maarufu wa Tanzania Bwana Mohamed Said kwenye kitabu chake
kwa lugha ya Kiingereza, The Life and Times of Abdulwahid Sykes (1924–1968), na
kwa Kiswahili Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924–1968) Historia
Iliyofichwa Kuhusu Harakati za Waislam Dhidi ya Ukoloni wa Waingereza katika
Tanganyika. Kitabu hicho ni muhimu sana kwa wanaotaka kufahamu vipi Waislam
waliupiganiya uhuru wa Tanganyika na namna walivyopinduliwa kwa mapinduzi
baridi kwanza kabla ya kupinduliwa kwa Dola ya Zanzibar tarehe 12 Januari 1964.
Kilele cha mapinduzi ya Tanganyika ni kudhoofishwa nguvu za umma wa Kiislamu
pale ilipovunjwa East African Welfare Muslim Society (EAMWS) na zilipozimwa
juhudi za kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiislam mwaka 1964.2
Bwana Mohamed Said pia amefafanuwa katika
kitabu chake Uamuzi wa Busara wa Tabora namna gani uongozi wa Waislam kutokeya
African Association mpaka kuundwa kwa TANU walivyopinduliwa kwa mapinduzi ya
kalamu. Baraza la Wazee la TANU ambalo Mwenyekiti wake alikuwa marehemu Mzee
Suleiman Takadiri lilipinduliwa chali kwa kazi iliofanywa na kiongozi na
viongozi wa Kiislam waliouweka mbele uzalendo wa Kiafrika kuliko mafundisho ya
dini yao.
Kushoto: Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, Clement Mtamila na Bi. Titi Mohamed |
Chanzo cha mapinduzi hayo yalikuwa masharti matatu yalioikabili TANU
katika kushiriki uchaguzi wa kwanza wa Tanganyika wa kulichaguwa Baraza la
Kutunga Sheria. Mkutano wa TANU wa Tabora wa tarehe 21–26 Januari 1958 uliamua
kuingiya uchaguzi wa kibaguzi wa kura tatu ambao ulikuwa na masharti matatu
magumu:
1) Ili Mwafrika aweze kupiga kura alitakiwa
awe na kipato cha pauni mia nne za Kiingereza kwa mwaka.
2) Awe na kiwango cha elimu ya darasa la
kumi na mbili.
3) Na awe ameajiriwa katika kazi maalumu.3
Uamuzi wa busara wa Tabora haukuwanasa
Waingereza kama ulivyowanasa Waislam wa Tanganyika ambao wengi wao hawakuweza
kuwachaguwa viongozi wao kwa sababu uchaguzi wa kura tatu “ulikuwa ukizuia
uongozi wa kuchaguliwa kuingia kwenye madaraka.”4
Kwa upande mwengine, Kenya kabla ya kupata
uhuru wake tarehe 12 Disemba 1963, siku mbili baada ya uhuru wa Zanzibar,
ilikuwa imegawanyika sehemu mbili: Koloni la Kenya, au bara, na Himaya ya
Kenya, au Mwambao. Sheikh Abdillahi Nassir ni mmoja kati ya viongozi wa Mwambao
ambaye alihudhuriya mkutano wa Mwambao uliofanyika Lancaster House, London,
baina ya tarehe 8–12 Machi mwaka 1962.
Sheikh Abdillah Nassir akiwa nyumbani kwake Mombasa na Mohamed Said |
Anaelezeya Sheikh Abdillahi kwenye kanda
iitwayo “Mwambao: Historia ya Pwani ya Afrika Mashariki,” kuwa Himaya ya Kenya
ilikuwa ni nchi kabla ya Koloni la Kenya kuwa ni nchi kwa miaka isiyopunguwa
1,300, na namna chuki za uzalendo wa Kiafrika zilivyowaathiri Waislam na khasa
chuki za kikabila na propaganda ya utumwa na Uarabu.5
Sehemu hizo mbili za Kenya, Koloni la
Kenya na Himaya ya Kenya au Mwambao, zikawa ni nchi moja ya Kenya kwa
makubaliyano ya mabadilishano ya barua baina ya Waziri Mkuu wa Kenya, Mzee Jomo
Kenyata na Waziri Mkuu wa Zanzibar Bwana Mohammed Shamte walizoandikiyana
London tarehe 5 Oktoba 1963. Barua zote mbili zilikubaliyana juu ya mambo
matano yafuatayo:
1) Uhuru wa kuabudu wa watu wa dini zote
katika sehemu hiyo utalindwa kwa mujibu wa dini zao; na khasa wale raia wa
Sultani na vizazi vyao, ambao ni wa dini ya Kiislamu, watahakikishiwa uhuru wao
wa kuabudu katika nyakati zote na hifadhi za nyumba na sehemu zote za dini yao.
2) Uwezo wa Kadhi Mkuu na Makadhi wengine
wote kuhukumu kwa sharia ya Kiislamu utahifadhiwa kufuatana na sharia ya
Kiislamu katika kesi zote za ndoa, talaka na mirathi.
3) Katika zile sehemu ambazo wakaazi wake
wengi ni Waislamu, watawekwa, kila inapowezekana, Maafisa Utawala (Mabwana
Shauri) Waislamu.
4) Watoto wa Kiislamu, kwa kadri
inavyowezekana watasomeshwa lugha ya Kiarabu katika kudumisha dini yao ya
Kiislamu kwa vile lugha hii ndiyo lugha ya dini yao. Ule msaada wa fedha
unaotolewa kuzisaidia skuli za msingi za Kiislamu katika hilo jimbo la Mkoa wa
Pwani utaendelea. Hautakatwa.
5) Umilikaji wa ardhi kutokana na mikataba
iliyokwisha kusajiliwa utatambulikana na kukubalika wakati wote. Mwenendo
huohuo utaendelea na kuhifadhiwa katika kusajili mikataba mipya ya kumiliki
ardhi isipokuwa tu pale itakapokuwa ni lazima kuchukua ardhi kwa masilahi na
faida ya umma; lakini papo hapo wale wenye ardhi zao watabidi kulipwa fedha.6
Kwa mujibu wa Sheikh Abdillahi,
makubaliano hayo baina ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Kenya
hayakutimizwa na amethibitisha namna nguvu za umma zilivyoporwa na umuhimu wa
kujenga muamko wa kuelewa badala ya muamko wa hamasa. Mfano mkubwa ambao
ameutowa Sheikh Abdillahi am-bao ni kinyume na makubaliano waliyotiya sahihi
Mawaziri Wakuu wa Zanzibar na wa Kenya, ni kunyanganywa Waislam, wa makabila
yote, Taasisi muhimu sana ambayo ikijulikana kwa jina maarufu la Mombasa
Insititute of Muslim Education (MIOME) ambayo ilikuwa ni:
baraka kubwa kwa Waislam wa Afrika
Mashariki. Hapa ndipo mustakbal wa vizazi vya Waislam vinapewa mafundisho
katika masomo ya ufundi chini ya Maprofesa mabingwa ambao wameajiriwa na
Serikali kutoka Ulaya. Sir Phillip Mitchell ambaye alikuwa ni Gavana na sasa ni
Mwenyekiti wa Baraza la Waendeshaji wa Taasisi alikuwa ndiyo nguvu ya usukumaji
wa Taasisi [MIOME]. Mtukufu Sultan wa Zanzibar alitowa mchango wa Shs.
2,000,000/-kutoka mfuko wa Colonial Welfare Fund, Mtukufu Aga Khan alichangiya
Shs. 2,000,000/-: Mtukufu Sheikh Mkuu wa jamii ya Kibohora amechangiya Shs.
1,000,000/-; na Sheikh Khamis Mohammed bin Juma [El Mutwaji] amekodisha ekari
34 na nusu za ardhi nzuri na kwa muda mrefu kwa matumizi ya Taasisi, na kwa bei
khafifu kwa kila mwaka.7
Mbali ya Muslim Teachers’ Training College
iliyokuwepo Kibuli, Kampala, Uganda, Khamisi Sekondari ya Mombasa, Muslim
School ya Soroti, ya Jinja, na kadhalika.
Iliyovunja rekodi zote na ambayo marehemu
Sheikh Ali Muhsin akiamini kuwa ndiyo moja kati ya sababu za kupinduliwa
Zanzibar, ilikuwa ni fikra na mipango ya kuanzisha Chuo Kikuu Cha Kiislam cha
Afrika Mashariki na Kati. Kwa mujibu wa Sheikh Ali Muhsin, Chuo hicho kilikuwa
na lengo la kuwafundisha Waislam kutoka sehemu zote za Afrika Mashariki na
Kati. Mwandishi wa ramani wa Chuo hicho alikuwepo Zanzibar mapinduzi
yalipotokeya na alisaidiwa kuondoka na Bwana Ahmed Omar Jahadhmy. Wamasri
waliishauri serikali ya Zanzibar wasubiri mpaka watakapokuwa na wanafunzi wa
kutosha ambao wataweza kufundishwa kwenye Chuo hicho. Fikra iliyoona mbali kwa
wakati huo ni hii ambayo leo inaitwa Open University. Redio na televisheni
vilikuwa viwe ndiyo vyombo viwiili vikubwa vya kufundishiya kote Afrika
Mashariki na Kati. Majaribio ya kwanza yalifanywa kabla ya mapinduzi lakini
yalifeli.8 Baada ya kuvunjwa kwa East African Muslim Welfare Society ambazo
khabari zake zinapatikana kwa urefu kwenye kitabu cha Kiswahili cha Bwana
Mohamed Said cha Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes, taasisi na mali zake
zote zikataifishwa na badala yake pakaundwa BAKWATA Tanzania, SUPKEM Kenya na
UMSC Uganda. Hali ya Waislam chini ya utawala wa Kiingereza ilikuwa ni ya
kuridhisha zaidi kuliko hali waliyokuwa nayo baada ya kupatikana uhuru
Tanganyika, Kenya na hata Uganda.
Waingereza Walijuwa Nini Kuhusu Mapinduzi?
Ukiangaliya kwa makini utakuja kuona kuwa
walikuwepo Waingereza na mamishionari ambao walikuwa hawana chuki dhidi ya
Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu lakini kwa bahati mbaya sauti zao sio
zilizokuwa zikisikilizwa na kupewa nafasi. Kwa mfano alikuwepo Dk. Gerald
Broomfield ambaye alikuwa ni mmishionari wa Kianglikani aliyekuwa na uzowefu
mkubwa Zanzibar. Dk. Broomfield alinukuliwa na Arab Association ya Zanzibar
kutoka kitabu chake Colour Conflict in Africa kwa maneno yake yafuatayo:
Afrika iliyobakiya ina jambo la kujifunza
kutoka Zanzibar…Zanzibar inaonyesha uwezekano wa kuwepo amani na kuhishimiana
baina ya makabila. Huenda likawa ni jambo zuri kwa roho zetu kukumbuka
[Zanzibar] inafanya hivyo kwa sababu Sultan wa Kiarabu ndiye mkubwa wa Dola.9
Hilo halistaajabishi kwa sababu Ukristo
uliingiya Zanzibar na bara kwa kupewa hishma na Masultani waliokuwa ni Waarabu
na Waislamu. Lakini Muingereza mtawala alipoona kuwa Ufalme umegeuka na kuiunga
mkono siasa ya kizalendo ya chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) ambayo
ilikuwa karibu sana na siasa ya uzalendo wa Kiarabu (Pan-Arabism au Arab
Nationalism) wa Gamal Abdel Nasser wa Misri, akaamua kuwatupa mkono ZNP-ZPPP na
kuubwaga uhuru wa Zanzibar ambao ulikuwa hauna salama kwa Waingereza au kwa
Mwalimu Nyerere kwa sababu, na kama alivyoelezeya Sheikh Abdillahi:
Zanzibar ilikuwa ni nchi pekee katika
Afrika nzima ambayo isingelihitajiya Mzungu hata mmoja. Zanzibar ilikuwa ina
watu wa kuendesha nchi na kuwaazima majirani kuendesha nchi zao.10
Sababu kubwa ya Wazanzibari wenye asili ya
Kiarabu kuwageuka watawala wa Kiingereza na watawala hao kupanga kuwakomowa
Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu, kulianza kwa kupigwa mabomu Misri na
Muingereza mwaka 1956.11 Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu walihisi kuwa
Uingereza haiaminiki na kuwa ilikuwa dhidi ya Waarabu. Hisia hii ilisababisha
kudai uhuru kamili bila ya kungojea maendeleo zaidi ya baadae.
Mwisho wa mivutano Muingereza alikataa
kuisaidiya serikali ya Zanzibar ilipopinduliwa tarehe 12 Januari 1964 na sababu
kubwa iliyowafanya kukataa ni imani yao kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yalikuwa ni
suala la ndani ya Zanzibar na kuwa hakukuwa na mkono au uvamizi kutoka nje ya
Zanzibar. Kwa upande wa Tanganyika Muingereza aliamuwa kuzuwiya fujo na
kumrejesha kitini Mwalimu Nyerere pale jeshi la Tanganyika lilipoasi tarehe 20
Januari 1964 na Nyerere akakimbilia mafichoni siku tisa tu baada ya mapinduzi
ya Zanzibar.12 Viongozi wa Serikali ya Tanganyika haraka walikwenda kuomba
msaada kutoka kwa wakubwa wa Kiingereza. Anaelezeya Brigadier Douglas:
Kambona, akifuatana na [Paul] Bomani,
Waziri wa Fedha, akionekana ana jambo ameficha, na ana khofu zaidi kuliko
kabla, walikuja nyumbani kwangu na barua kutoka kwa Naibu Raisi Kawawa ilosema:
Nimeelekezwa na Raisi wa Jamhuri ya Tanganyika kuiletea ombi la msaada wa
kijeshi serikali ya Kiingereza ili utuwezeshe kuweka sheria na amani ndani ya
nchi.13
Mara nyingi uasi wa jeshi la Tanganyika
umekuwa ukihusishwa na mapinduzi ya Zanzibar kwa kuwa wanajeshi wa Tanganyika,
Kenya na Uganda waliingiwa moyo wa kuasi kutokana na kufaulu kwa Mapinduzi ya
Zanzibar ingawa hakukuwa na uhusiano wowote baina ya matukio hayo mawili.
Uamuzi huu unatokana na kukosekana kuyafahamu Mapinduzi ya Zanzibar kwanza, na
pili, kukosekana huko kufahamika kwa mapinduzi ya Zanzibar kumeondowa hoja ya
kufanywa utafiti wa mahusiano baina ya mapinduzi na uasi wa kijeshi wa
Tanganyika.
Suala moja muhimu ambalo linavutiya hoja
ya uhusiano baina ya mapinduzi ya Zanzibar na uasi wa kijeshi wa Afrika
Mashariki ni suala la kukamatwa kwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi baada ya
kutokeya uasi huo Tanganyika. Tarehe 29 Januari 1964 Balozi wa Kiingereza kwa
niaba, alipeleka ujumbe wa telegram kwa Commonwealth Relations Office, London,
uliopitiya Ubalozi wa Kiingereza Kampala, Nairobi, Aden na Washington:
Matokeo ya kuasi kwa jeshi la Tanganyika
ni kundi kubwa la viongozi wa vyama vya wafanyakazi kukamatwa Jumapili usiku
Tanganyika nzima pamoja na takriban viongozi wote wa chama cha Shirikisho la
Wafanyakazi wa Tanganyika (Tanganyika Federation of Labour). Wote walipelekwa
kwenye vituo vya polisi kwa kuhojiwa na baadhi yao baadaye waliwachiwa huru.
Rais [Nyerere] kwenye hotuba yake ya redio ya jana usiku aliligusiya suala hili
na aliongeza kwa kusema kuwa Mkuu wa Wilaya mmoja pia amekamatwa.
Nyerere alitamka kwenye hotuba hiyo ya
redio kuwa watu hawa, wa vyama vya wafanyakazi, walikuwa wamekula njama na
viongozi wa uasi wa kijeshi “kusababisha mtafuruku zaidi.” Kulikuwa na uvumi
mwingi wiki iliyopita kuwa vyama vya wafanyakazi vilikuwa vinapanga mgomo wa
jumla au angalau mgomo wa wafanyakazi wa gatini na wa reli. Pia inaaminiwa kuwa
viongozi kadhaa wa vyama vya wafanyakazi walikuwa wakipitisha wakati wao mwingi
kwenye kambi ya kijeshi ya Colito.14
Msomaji anaombwa baadaye aunganishe
mchango wa vyama vya wafanyakazi katika mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12
Januari 1964 na uasi wa jeshi la Tanganyika wa tarehe 20 Januari 1964.
Waingereza hawakuwacha kuuhusisha uasi wa
jeshi la Tanganyika na mchango wa Oscar Kambona ambaye wakati huo alikuwa ni Waziri
wa Mambo ya Nje na Ulinzi. Walimuandikiya makala kwenye ukurasa wa nyuma wa
gazeti la Daily Telegraph la tarehe 22 Januari 1964 ambayo ilimuudhi sana
Kambona. Balozi wa Kiiengereza aliyekuwepo Dar es Salaam alielezeya kwenye
barua yake aliyompelekea Bwana W.G. Lamarque wa Commonwealth Relations Office,
Downing Street, London, kuwa “Stephen Miles alipokutana na Rais [Nyerere] wiki
iliyopita waligusiya kuwa Kambona alikuwa kiongozi wa uasi wa kijeshi, na Rais,
kama unavyojuwa, alimwambiya Oscar kuwa ‘Masikini Oscar, maisha yeye ndiye
mwenye kulaumiwa.’ Kwa kusema kweli, Oscar alikasirishwa sana alipozisikiya
habari hizo na akaanguwa kilio na ikabidi apewe siku moja nzima ya
mapumziko.”15
Waingereza walimtiliya shaka sana Kambona
kuwa alikuwa amehusika na uasi wa jeshi la Tanganyika kwa kuzingatiya kuwa
katika siku mbili za kwanza za uasi, Kambona alikuwa akitangaza kwenye redio
kila baada ya nusu saa na kuwa alikuwa tayari achukuwe khatamu za serikali na
ajitangaze kuwa ni Rais lakini aliogopa dakika za mwisho. Pia walilalama kwa
kusema “Lazima iulizwe kwanini ulinzi wa ndani wa Tanganyika dhidi ya tukio
kama la uasi wa jeshi ukawa dhaifu namna hii. Hapana shaka kukosekana kwa
taarifa kutoka vyombo vya usalama kuipa serikali kumetokana na Kambona na [Job]
Lusinde kulibomowa Tawi la Usalama na badala yake kuwaweka watu wa T.A.N.U.
aliowachaguwa Kambona.”16 Licha ya kuwa hawakuwa na taarifa za kiusalama
watawala wa Kiingereza waliamuwa kupeleka jeshi la Makamandoo kurudisha amani
na utulivu Tanganyika na kumrudisha kitini Mwalimu Nyerere.
Na Zanzibar ikapinduliwa, mauwaji ya
halaiki yakafanywa, na Bwana Adrian Forsyth-Thompson aliyekuwa Permanent
Secretary katika ofisi ya Waziri Mkuu Bwana Mohammed Shamte akaondoka Zanzibar
tarehe 8 Februari 1964, na alitarajiwa kuondoka Nairobi kuelekeya Cape Town,
Afrika Kusini, tarehe 11 Februari 1964. Baba yake Adrian alikuwa ni ofisa
katika serikali ya kikoloni ya Kiingereza na alistaafu Cape Town. Adrian
aliondoka Cape Town tarehe 18 Machi kwenda kwenye kazi yake mpya katika visiwa
vya Seychelles.
Chini ya ngazi kwenda juu: Ali Muhsin Barwani, Mohamed Shamte, Hasnu Makame na Abeid Amani Karume |
Forsyth-Thompson alikuwa ni ofisa wa
usalama kwenye ofisi ya Balozi wa Kiingereza Zanzibar na punde tu kabla ya
mapinduzi alikabidhiwa kazi na Katibu Mkuu wa Kiingereza, Bwana Mervyn Vice
Smithyman, katika ofisi ya Waziri Mkuu Bwana Mohammed Shamte kuleta mabadiliko
katika vyombo vya usalama vya Zanzibar. Alipokuwapo Nairobi na tayari kuondoka
kwenda Cape Town, Forsyth-Thompson alitowa ripoti muhimu ambayo ilipelekwa
Commonwealth Relations Office, London kwa njia ya telegram na kopi zikapelekwa
ubalozi wa Kiingereza Dar es Salaam, Aden, Kampala, Washington na Cape Town.
Ujumbe huo ulikuwa ni mfupi ukiufananisha na ripoti yake yenye kurasa nane
aliyoiandika alipokuwa Nairobi tarehe 10 Februari 1964.
Kwenye ripoti fupi aliyoitowa Nairobi na
iliyopelekwa London na Washington, Forsyth-Thompson aliziwasilisha nukta tano
lakini hapa tutainukuu nukta ya kwanza na nukta ya nne:
1) Hakuna (rudia hakuna) ushahidi wa mkono
kutoka nje katika mapinduzi ambayo yalikuwa ni mapinduzi ya Afro-Shirazi Youth
League dhidi ya siasa ya Kiarabu ya Serikali iliyokuwepo, na mapinduzi
yalifanywa katika kipindi ambacho viongozi wa ASYL na washabiki wao wakiamini
patatokeya ukamataji wa viongozi wakati wowote. Babu alichupiya, na Karume (?
Alichaguliwa) na wanamapinduzi kuwa ndiye kiongozi anayejulikana na Okello
alichomoza tu.
4) Kwa mtizamo wa mbali mustakbal wa
Zanzibar umo katika uhusiano wa karibu na maeneo ya bara ikiwa ndani ya
Shirikisho au kuunganishwa na Tanganyika. Hili litafanyika kwa urahisi ikiwa Tanganyika
au Kenya watakuwa tayari kupeleka vikosi vya polisi (kwa mfano kikosi cha
huduma) kutokana na ombi la Karume ambaye atakubali kutokana na hali ya mambo
ilivyo ikiwa Watanganyika na Wakenya watampa ishara kuwa wako tayari.17
Kwenye ripoti yake ya kurasa nane,
Forsyth-Thompson anaelezeya kuwa:
Umma Party na viongozi wa ASP wenye
mitizamo isiyo mikali hawakujuwa chochote [kuhusu mapinduzi]. Saleh Saadalla
labda akijuwa…Alkhamisi tarehe 9 [ASYL] walisikiya kuwa mzigo wa meli wa silaha
kutoka Algeria ulikuwa utaletwa na Serikali…Hadithi za silaha kutoka Algeria
zilikuwa zimezagaa kwenye wiki baada ya mapinduzi: na kwa hakika ulikuwa ni
upuuzi mtupu.18
Kuhusu mapinduzi yenyewe, anaelezeya
Forsyth-Thompson, “yalipangwa na kutekelezwa ndani ya muda mfupi na hii ni
dalili ya kukosekana kabisa taarifa zozote kutoka kitengo cha usalama (Special
Branch) kuwa kulikuwa na mpango. Kwa muda mrefu kulikuwa na mazungumzo ya
kufanya fujo, lakini hakukuwa na pendekezo la mpango wa kuipinduwa Serikali kwa
kutumiya nguvu.”19
Kamati ya Ukombozi wa Afrika
Mkutano wa nchi huru za Kiafrika
uliofanyika Addis Ababa mwezi wa Mei 1963 uliunda Kamati ya Ukombozi wa nchi
tisa yenye makao makuu Dar es Salaam. Nchi zilizounda kamati hiyo zilikuwa
Tanganyika, Nigeria, Uganda, Algeria, Umoja wa Jamhuri ya Kiarabu (U.A.R.),
Guinea, Senegal, Ethiopia na Kongo. Ghana haikuwemo.
Nyerere hakupendeleya makao makuu ya
Kamati ya Ukombozi ichukuliwe na Ghana, U.A.R. au Algeria. “Alikhofiya kuwa
kati ya nchi hizo Kamati ingelitumiliwa na Rais wa Dola kujijengeya sifa, na
mtizamo wa kamati ungelikuwa juu ya utumiaji nguvu badala ya shinikizo la
amani.”20
Baada ya uchaguzi wa mwisho wa Zanzibar wa
kabla ya mapinduzi wa tarehe 8 Julai 1963, Mwalimu Nyerere alifanya ziara ya
Marekani na alionana na Rais John F. Kennedy, na Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa U Thant. Pia aliitembeleya nchi ya Canada kwa muda mfupi na alikuwa na
mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Bwana Lester Pearson. Tarehe 21–25
Julai alikuwa mgeni wa Serikali ya Uingereza. Mwalimu na ujumbe wake uliondoka
London siku ya Alkhamisi tarehe 25 Julai kuelekeya Algiers, mji mkuu wa
Algeria.
Katika msafara wa Rais Nyerere walikuwemo:
Rais Nyerere
Bwana Oscar Kambona, Waziri wa Mambo ya
Nchi za Nje na Ulinzi
Bwana I. M. Bhoke Munanka (Waziri Mdogo,
Ofisi ya Makamo wa Rais)
Bwana A. B. C. Danieli (Katibu Msaidizi,
Mambo ya Nje)
Bwana G. Rockey (Katibu wa Habari)
Bwana F. Sangu (A.D.C.)
Bwana P. Mwimbo (Mkuu wa Maofisa
Wafanyakazi)
Bwana J. M. Simba (Katibu Khasa wa Rais)
Bwana U. Nyondo (Ofisa Mfanyakazi wa Rais)
Bwana K. Kondo (Ofisa Mfanyakazi wa Bwana
Kambona)
Ziara rasmi ya Rais Nyerere na msafara
wake nchini Algeria ilikuwa kuanziya tarehe 25 mpaka tarehe 28 Julai.
Inavyoonesha Ubalozi wa Kiingereza mjini Algiers hakuambuliya kitu chochote cha
maana kati ya mazungumzo ya Rais Nyerere na Ahmed Ben Bella, Waziri Mkuu wa
Algeria na baadaye Rais wa nchi hiyo.
Katika mwezi huohuo wa Julai 1963
Waingereza walikuwa wameshazipata habari kutoka jeshi la Tanganyika kuwa
kulikuwa na silaha zikitarajiwa kutoka Algeria. Baina ya mwezi wa Agosti na
Septemba 1963 listi ya silaha ilionekana Wizara ya Ulinzi. Halafu kimya mpaka
wiki ya kwanza ya Januari 1964.21
Tarehe 2 Januari 1964, meli iliyopewa jina
la mwanafalsa maarufu duniani wa historia, MV Ibn Khaldun kutoka nchi ya
Kiarabu ya Afrika ya Kaskazini ya Algeria, ilitia nanga Dar es Salaam huku
ikibeba shehena ya silaha zilokusudiwa kupelekwa Msumbiji na kwa ajili ya
mapinduzi ya Zanzibar. MV Ibn Khaldun haikuwa Sultana iliotiya nanga New York
Alkhamisi, tarehe 30 Aprili mwaka 1840 na iliyobeba ujumbe wa amani na biashara
kutoka Zanzibar kwa Sultan Sayyid Said bin Sultan.
Meli ya MV Ibn Khaldun ilikuwepo Dar es
Salaam kwa siku nane, kuanziya tarehe 2 Januari 1964 na iliondoka tarehe 9
Januari 1964. Ilipowasili mara ya kwanza meli hiyo “ilikaa nje ya bandari ya
Dar es Salaam kwa muda wa masaa arubaini na nane. Kutokana na kuhojiwa kwa
maofisa wa Kiafrika waliohusika na upakuwaji wa mizigo ya meli ilikuwa dhahiri
baadhi ya mizigo iliondolewa na inawezekana sana kuwa baadhi yake iliondolewa
kabla ya meli kufunga gati.”22 Rais Nyerere aliongozana na Bwana Djoudi
aliyekuwa Charge d’Affaires katika Ubalozi wa Algeria Tanganyika katika
kuikaguwa meli hiyo. Djoudi pia alikuwa mhusika wa mafunzo ya kijeshi wa Kamati
ya Ukombozi wa nchi tisa za Kiafrika. Kijana mdogo mwenye umri wa miaka 24
aitwaye Racchid Ben-Yelles alikuwa Kepteni wa meli hiyo ya MV Ibn Khaldun.
Kepteni Ben-Yelles alitowa maelezo kuwa
meli hiyo ambayo alichukuwa dhamana ya kuiyendesha miezi mitatu nyuma ilikuwa
kwa kawaida yake ikifanya kazi kwenye Bahari ya Mediterranean. Mzigo wa kawaida
wa meli hiyo ulikuwa ni ulevi wa zabibu na meli hiyo ambayo ikimilikiwa na
Serikali ilikuwa na matenki yenye uwezo wa kubeba tani 2,000. Meli ilipoondoka,
Rais Nyerere aliwapungiya mkono kepteni na wafanyakazi wake na kuwaombeya
safari njema. Wakati inaondoka meli hiyo ilikuwa imebeba shehena ya tani 80 za
kahawa na tani 100 za mbao kutoka Tanganyika na ilielekeya Tanga kuongeza
mizigo zaidi.23
Kwa mujibu wa ripoti ambayo haiyoneshi
imetoka kwa nani na inakwenda kwa nani, Serikali ya Tanganyika iliwalipa Waalgeria
“thamani ya pauni za Kiingereza 260,000 za kahawa na bidhaa nyengine.”24 Wapi
pesa hizo zilitoka bado ni suala la michirizi yake kufuatiliwa. La muhimu ni
kahawa na mbao yalikuwa ni malipo kwa ajili ya silaha zilizoletwa kutoka
Algeria na meli ya Ibn Khaldun. Kwa amri ya Oscar Kambona, kazi ya upakuwaji wa
mizigo ya silaha hizo alipewa Kepteni Nyerenda na aliamrishwa mzigo wote wa
silaha auweke kunako ghala za P.W.D. (Public Works Department).25
Huo ulikuwa ni wakati wa uanzishaji wa
harakati za ukombozi wa Msumbiji na baadaye kuanzishwa kambi za kuwapa mafunzo
wapiganiya uhuru wa Msumbiji Tanganyika. Oscar Kambona aliwababaisha waandishi
wa habari kwa kuwaambiya kuwa silaha kutoka Algeria zilikuwa kwa ajili ya
Tanganyika Rifles lakini Waingereza walipotaka taarifa zaidi kutoka kwake
aliwajibu kuwa “…ni za Tanganyika Rifles isipokuwa maboxi yaliopigwa krosi
nyeusi. Maboxi haya yanatakiwa yawekwe karibu na mlango wa ghala ili yaweze
kuondolewa kwa haraka. Pia alisema kuwa maboxi hayo yasifunguliwe. Tuliyafunguwa
baadhi yake…Zanzibar ilitokeya Jumapili iliyofuatiliya, tarehe 12 Januari na
maboxi yale bado yalikuwepo kunako ghala. Baada ya hapo yakawa hayana umuhimu
wowote.”26
Usikose kufuatilia Sehemu ya Pili In shaa
ALLAH.Ingia hapa chini kwa maelezo kuhusu Dr. Harith Ghassany na kitabu chake:
No comments:
Post a Comment