Utangulizi
Kwa kawaida na
kwa miaka mingi huwa siipiti makala yoyote ya Jabir Idrissa ila nitaisoma. Napenda
kusoma makala za Jabir Idrissa kutokana na staili yake ya uandishi. Jabir
anaandika kwa upole sana kiasi cha makala nzima kuwa baridi kwa kipimo cha joto
lakini ndani yake kila neno kila sentensi, kila mstari na kila paragrafu
imesheheni miba na misumari inayochoma na kutoboa kwa ncha kali sana. Lakini juu
ya haya yote makala kila ukiirudia ubaridi wake katika hoja, lugha na mantiki
inabakia na ubaridi wa kuzizima. Hii ndiyo kalamu ya Jabir Idrissa. Msome Jabir
Idrissa anavyoeleza jinsi CCM Zanzibar walivyoshindwa uchaguzi wa kwanza wa
vyama vingi mwaka 1995 na nini CCM ilifanya kujipa ‘’ushindi.’’
Jabir Idrissa |
Namdurusu Ali
Ameir Uchaguzi wa Zanzibar 1995
Na Jabir Idrissa
(Makala kwa hisani ya Mwandishi na Gazeti la ''Mawio'')
(Makala kwa hisani ya Mwandishi na Gazeti la ''Mawio'')
NIMEIKUMBUKA sinema ya matokeo ya
uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka 1995, wa kwanza tangu mfumo wa vyama vingi
urudishwe kwa Sheria Na. 5 ya Mwaka 1992, iliyopitishwa na Bunge. Nipo na
waandishi wenzangu nje ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) mkabala na
sekondari ya Benbella (iliitwa kuheshimu jina la Ahmed Ben Bella, aliyekuwa
Rais wa Algeria). Ilikuwa siku ya pili baada ya uchaguzi mkuu 1995, tunasubiri
Tume itangaze matokeo ya kura zilizozidi kidogo 300,000. Siku nne
haijakamilisha. Sasa wakati tunapiga soga, akatokea Ali Ameir Mohamed,
aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar. Hakuwa tu
mtendaji mkuu kwa Zanzibar, ukweli alikuwa bosi wangu kwani mwajiri wangu
wakati ule alikuwa Shirika la Magazeti ya Chama (SMC), moja ya asasi zilizokuwa
milki ya CCM.
Ali Ameir, nimuite kwa utambuzi rahisi,
ni bwana wa Donge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambako alipata kuwa Mbunge wa
kuchaguliwa. Kiongozi makini katika viongozi wa kisiasa nchini zama zile. Mwerevu
na mjuzi, tofauti na wengine. Lakini kama kawaida ya wanasiasa wa nchi zetu za
Afrika, alikuwa mjanja wa mambo, mpanga mikakati na msimamizi wa utekelezaji
katika kukiimarisha chama chao. Ali Ameir ambaye sasa yu mtu mzima
aliyedhoofika afya kutokana na kupatwa na ugonjwa wa kiharusi, alipofika mbele
yetu, na kusalimia, alitoa malalamiko CCM imehujumiwa katika uchaguzi. Akasema,
“Hatukubali matokeo kwa sababu Tume imekula njama na CUF kutuhujumu.” Kila muandishi
alishtuka kumsikia.
Ali Ameir Mohamed |
Hakuna aliyepata uhakika kama ni kweli
CCM ililalamika rasmi kwa hayo aliyotuambia Ali Ameir siku ile. Hatukuona barua
hiyo wala majibu kama yalikuwepo. Hatukuona. Nilimwambia muandishi rafiki yangu
aliyekuwa karibu yangu, “ukiona hivi, ujue CCM inahangaika kutafuta ushindi wa
kulazimisha; ishashindwa uchaguzi vituoni.” Hakuamini. Ikaichukua Tume siku
mbili zaidi ya pale ndipo ikatangaza matokeo ya urais. Ilikuwa siku ya sita
tangu Wazanzibari walipopiga kura kuchagua Rais wa Zanzibar, wajumbe wa Baraza
la Wawakilishi na Madiwani. Nasema tena kura zilizopigwa hazikufika 350,000.
Siku sita? Twende tutaona mbele.
Siku ilipofika, tukaona ofisi zimejaa
mapolisi kwa idadi iliyozidi kwa sana waandishi tuliokuwepo – kwa kweli
tulishachoka – tukisubiri matokeo. (Siku ya nyuma yake, katika njia ya
‘kijasusi’ tulipata karatasi ya matokeo ya majimbo yote iliyokuwa ikionesha
kuwa CUF na mgombea wake wa urais, huyuhuyu Maalim Seif Shariff Hamad,
ameshinda uchaguzi). Televisheni ya DTV ikayatangaza usiku ule na asubuhi yake.
Sisi gazeti la Uhuru hatukutangaza. Sababu ni dhahiri,
“tungechinjwa.” Mwalimu wangu Mwadini Hassan nilimuuliza tufanyeje, akaashiria
kusema, “Tuachane nayo haitatoka.” Kweli isingetoka.
Tukaona maandalizi ya kutangaza matokeo.
Ghafla kundi la polisi limemuweka kati Mwenyekiti Zuberi kuelekea ukumbini. Du
askari wengi wale, tena wenye bunduki. Tukafukuzia ukumbini. Nafasi finyu,
mwenyekiti kabanwa kila upande. Sasa anasoma kijikaratasi kwa shida, labda
alijua amelazimishwa. Kijasho tele. Akasoma na mwisho akamtamka mshindi ni
mgombea wa CCM, Dk. Salmin Amour Juma, wakati huu akiitwa Komandoo Dk. Salmin.
Matokeo yalimpa ushindi mwembamba – asilimia 50.8 dhidi ya 49.2 wa Maalim Seif
– ambao mwenyewe Komandoo Dk. Salmin tulipokutana naye nyumba ya Bosnia,
Maisara, aliuita “wa goli moja... lakini ni ushindi.”
Salmin Amour |
Si uongo ningekuwa pia ningeanza
kusherehekea ushindi, japo najua ulitengenezwa mezani kama ilivyokuja
kudhihirika. Pata picha ile ya uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi
ambao ulikwenda kwa amani kubwa, lakini ukaja kuharibiwa na matokeo ya mwisho
yaliyoonesha kupangwa mezani. Unapovuta picha hiyo ya miaka 20 iliyopita, hebu
tafakari na kile kilichotokea safari hii katika uchaguzi ambao ulikwenda vizuri
kabisa na kusifiwa na asasi za uangalizi zilizoshuhudia kinagaubaga vituoni na
tangu wakati wa kampeni. Maalim Seif hakulalamika Oktoba 26 alipokutana na
waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya CUF Mtendeni mjini Zanzibar.
Hakulalamika. Alitaja takwimu za kura kama alivyokabidhiwa na wasaidizi wake
katika chama, zikionesha alikuwa ana asilimia 52.87 (kura 200,077) dhidi ya
47.13 (kura 178,368) za Dk. Ali Mohamed Shein. Tofauti ya kura ni 21,714.
Mpaka hapo, Tume ilikuwa imehakiki kura za
majimbo 40, ikiwa na maana majimbo 14 tu yalibakia kuhakikiwa. Lakini mpaka
asubuhi ile ya Press Conferece ya Maalim Seif, Tume ilikuwa
imetangaza matokeo ya majimbo manne tu. Ni Kiembesamaki (CCM 4,413 v CUF
2,989); Fuoni (CCM 889 v CUF 429); Malindi (CCM 2,334 v CUF 5,697) na Kwahani
(CCM 5,960 v CUF 2,879). Mpaka Jecha Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume, anatoa
tangazo la kufuta uchaguzi mchana wa Oktoba 28, alikuwa ameshatangaza matokeo
ya majimbo 31, akibakisha 21 kukamilisha.
Mpaka hapo hakukuwa na malalamiko yoyote
rasmi ya chochote kilichotokea si vituoni wakati wa kupigakura wala kuhesabu
kura. Tukiwa ukumbi wa Hoteli ya Bwawani, kituo cha kutangazia matokeo,
tulisikia CCM walipeleka barua Oktoba 27 kulalamika. Tafadhalini, asasi za
waangalizi zilishatoa ripoti za awali za kusifia uchaguzi, zikisema ulisimamiwa
vizuri zaidi ya ilivyokuwa 2010. Kisheria, malalamiko ya vituoni huwasilishwa
kupitia fomu maalum kwa wasimamizi. Haikuwepo hata moja. Kwa hivyo basi, fikiria unapoambiwa uchaguzi
umefutwa wote, wakati mwenyekiti mwenyewe alishatangaza asilimia 70 hivi ya
majimbo, unaendelea kuuliza kulitokea nini? Usijisumbue akili, njama za CCM
kulazimisha watakavyo si kwa vile walivyoamua wapigakura. Tena isitoshe,
unaposikia wasomi na makada wanavimbisha mishipa ya shingo na kutetea uamuzi wa
Jecha, na huku wakivizonga vifungu vya sheria kuhalalisha walichotumwa kufanya,
ujue tatizo ni moja tu – demokrasia ya kweli haijapewa nafasi na hawa CCM.
No comments:
Post a Comment