Ahmed Seif |
Naanza kwa kusema kuwa
inawezekana kabisa kuwa Ahmed Seif ndiye muasisi wa TANU mdogo kupita wote
katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika. Yeye alijiunga na harakati
akiwa na umri mdogo wa miaka 18. Nilijuana na Ahmed Seif mwaka wa 1971 kupitia
kwa ndugu yake Iddi Manyanya ambae na yeye sasa ni marehemu. Wakati
nilipomfahamu marehemu Ahmed Seif Tanzania ilikuwa inapitia kipindi kigumu sana
katika uchumi wa nchi na si watu wengi walikuwa na magari yao binafsi.
Brother Ahmed kama sisi wadogo zake tulivyozoea kumwita alikuwa ana gari yake
nzuri ya Kijapani. Wakati ule alikuwa akifanya kazi kampuni kubwa na maarufu ya
wakala wa meli ikiitwa Leslie Anderson ambayo baaadae ikabadilishwa na
kuitwaWafco. Marehemu alikuwa mtu wa fikra pana na ungeweza kuzungumzanae
lolote ulitakalo kuanzia siasa hadi michezo. Mmoja wa wa wadogo zake ambao
ndiyo walikuwa umri sawa na mimi ni Ramadhani maarufu kwa jina la ''Funky.''
Funky kama Iddi Manyanya walikuwa wakifanya kazi East African Airways (EAA).
Funky ndiye aliyenifikishia taarifa ya kifo. Ramadhani ni mtoto wa Bi. Sharifa
Bint Mzee mmoja wa waasisi wa TANU Lindi. Kupitia watu hawa nilikuja kujua
mengi kuhusu mji wa Lindi na neema iliyokuwako kule wakati wa ukoloni. Hakika
nilipofika Lindi niliona ushahidi wa neema ile. Kila nilipokwenda nilipambana
na magofu ya nyuma nzuri na mabaki ya maduka makubwa bado yakiwa na alama za
matangazo ya vitu vilivyokuwa vikiuzwa miaka hiyo ya 1950 na 1960, mfano duka
la Bata Shoes, Hosteli ya Wanafunzi wa Shule ya Aga Khan, vibao vya ofisi
za mawakili wa wakati ule, jumba la fahari la senema na mengi ya kumtia mtu
simanzi kwani nilipofika mimi miaka ya 1990 mji ulikuwa umekufa. Ikutoshe tu
kukupa picha ya hali ya wakati ule, baba yake Ahmed Seif Mzee Seif Khamisi
Manyanya alikuwa amejijengea sifa kubwa na umaarufu wa kupigiwa mfano kama
mshonaji wa suti bingwa mjini Lindi. Wakati ule wavaa suti walikuwa wengi mjini
achilia mbali Wazungu na Magoa bali hata Waafrika nao walikuwapo. Hali ya
maisha ilikuwa nzuri.
Bi, Sharifa bint Mzee na wajukuu zake (Picha kwa hisani ya wanae) |
Katika miaka ile ya 1970
historia ya TANU ilichukuliwa kama kitu nyeti ambacho watu wakiogopa
kukizungumza. Halikadhalika Brother Ahmed kama waasisi wenzake hakuwa anapenda
kuhadithia mchango wake kwani akiwa kijana mdogo wa miaka 18 alikuwa muajiriwa
wa TANU na alishiriki katika kuijenga TANU Jimbo la Kusini. Ukimuuliza kitu
chochote kuhusu TANU alikuwa akiparaza na kukutoa njiani. Sana kabisa
atakuambia, ''Nenda Lindi kawatafute akina Mzee Masudi Mnonji na Yusuf Chembera
hawa watakueleza kila kitu.'' Watu wachache sana siku zile walikuwa tayari
kuizungumza TANU na ikawa kama vile wote wameagana. Hawakupenda mazungumzo ya
TANU na Nyerere. Iwe itakavyokuwa Ahmed Seif Khamisi Manyanya atabaki kuwa
mmoja wa Watanganyika wa mwanzo kujiunga na harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika.
Laiti Brother Ahmed kwa elimu yake aliyokuwanayo angelikuwa tayari kuzungumza
kuhusu historia ya TANU kama mambo yalivyokuwa mwaka wa 1955 chama
kilipoasisiwa Lindi hakika angelituachia urithi mkubwa. Bahati mbaya na kwa
hakika hatuwezi kumlaumu kwa hili Ahmed Seif ameondoka na mengi katika kifua
chake, mengi katika historia ya nchi yetu ambayo hatutaweza kuyapata kokote.
Jambo la kusikitisha ni kuwa
zaidi ya nusu karne sasa historia ya mashujaa hawa haifahamiki vyema na
hazionekani juhudi zozote za kuiadhimisha. Kama alivyokuwa akinieleza Brother
Ahmed kuwa historia ya TANU Jimbo la Kusini wanayo akina Chembera, nilifanikiwa
kufika Lindi mwaka wa 1993 na nilkakutana na Yusuf Chembera na Salum Mpunga
waasisi wa TANU Lindi na watu waliomtia kijana wao Ahmed Seif katika utumishi
wa TANU. Haya yafuatayo hapo chini ni kutoka kitabu ''Maisha na Nyakati za
Abdul Sykes (1924 - 1968)...'' na yanatokana na kumbukumbu za wazee hao wawili
ambao sasa wote ni marehemu. Nilihifadhi yote walionisomesha wazee wale katika
kitabu hicho ambamo msomaji ataona hali ya siasa ilikuwaje wakati ule wa miaka
1950 mwanzoni wakati Watanganyika waliposimama kudai uhuru wa nchi yao kutoka
kwa Waingereza. Katika simulizi hizo ndipo utakutana na marehemu Ahmed Seif:
''Chama cha Waafrika ambacho
kilianzishwa siku nyingi mjini Lindi na kwa hakika ndicho kilikuwa chama cha
pekee kushughulikia maslahi ya Waafrika sehemu za kusini kilikuwa African
Welfrare Association ambacho mlezi wake alikuwa John Nevi, Mjaluo kutoka Kenya
na katibu wake alikuwa Casian Njunde, Mngoni wa Songea. Makopa aliposhindwa
kukishawishi kile kikundi cha wazee wa TAA aliwaendea Yusufu Chembera na Rashid
Salum Mpunga. Chembera alikuwa na umri wa miaka 34 na Mpunga alikuwa kijana wa
miaka 27. Chambera alikuwa amesoma hadi shule ya msingi na Mpunga alikuwa
amemaliza madras. Chembera alikuwa akifanya kazi katika kantini ya Lindi
Welfare Centre, wakati Mpunga alikuwa dereva wa lori aliyeajiriwa na
mfanyabishara wa Kihindi. Makopa aliwashauri Chembera na Mpunga juu ya
uwezekano wa kuwahamasisha wananchi wawaunge mkono ili tawi la TANU lifunguliwe
pale mjini. Aliwaambia alitaka sana kufanya hivyo yeye mwenyewe lakini
asingeweza kwa sababu yeye alikuwa mtumishi wa serikali na hakuwa akifahamika
sana mjini. Uongozi kama wao ndiyo ungeweza kuaminiwa na wananchi na
usingetiliwa mashaka. Makopa, Chembera na Mpunga walikubaliana kuwa kabla ya
kuanza kufanya kampeni waziwazi kwa ajili ya TANU, lazima wawaandikishe
wanachama wachache kama waasisi wa chama. Mpunga na Chembera walimwandikisha
kijana mmoja akiitwa Abdallah Faraj na katika muda mfupi waliweza kuwapata
takriban wanachama kumi na tano walioridhia kujiandikisha kama wanachama
waasisi wa TANU.
Baada ya kuandikisha
wanachama waasisi mkutano wa siri uliitishwa katika Welfare Centre ambako ndiko
alikokuwa akifanya kazi Chembera. Chembera aliwaeleza kwa ufupi wale wanachama
wa mwanzo kuhusu malengo na madhumuni ya chama hicho kipya cha siasa. Mkutano
huo ulichagua kamati ya watu watatu yaani, Makopa, Chembera na Faraj ili
kuwakabili Mnonji na Waziri kuwaleza kuwa TAA haipo tena nchini Tanganyika.
Lengo lilikuwa kuwasadikishia kuwa ilikuwa kazi bure na kupoteza wakati
kujaribu kuihuisha TAA mjini Lindi wakati ambapo Tanganyika nzima ilikuwa
ikisonga mbele na TANU. Baada ya mjadala mrefu sana na mkali wa wale vijana
watatu na ule uongozi wa TAA wa wazee, walikubaliana TANU lazima isajiliwe
mjini Lindi.
Uchaguzi ulifanyika na
Shaaban Msangi, kijana wa Kipare akifanya kazi kwa Smith Mc Kenzie,
alichaguliwa rais na Ahmed Seif, katibu. Mpunga, Chembera, Mnonji na Idd Toto
walichaguliwa wajumbe wa kamati. Ahmed Seif alikuwa kijana
ambaye ndiyo kwanza amemaliza shule, yeye alikabidhiwa kuendesha ofisi kwa niaba
ya uongozi. TANU mjini Lindi ilimwajiri ili kukiandaa chama kiweza
kufanya kazi zake kwa ufanisi. Hassan Mohamed Kinyozi aliajiriwa kama mhudumu
wa ofisi. Hawa wawili walikuwa ndiyo wafanyakazi wa kwanza wa TANU waliokuwa
wakilipwa mshahara katika Jimbo la Kusini na wakawa miongoni mwa wafanyakazi
wachache sana walioajiriwa na TANU kwa wakati ule. Mnonji alitoa nyumba yake
katika mtaa wa Makonde kuwa ofisi ya kwanza ya TANU Jimbo la Kusini. Baada tu
ya kuanzishwa kwa TANU, Athumani Mussa Lukundu, kiongozi wa Lindi Dockworkersí
Union, aliunganisha chama chake na TANU. Jambo hili, kwa TANU lilikuwa la
kuitia moyo sana kwa sababu Dockworkers' Union ilikuwa na wananchama wengi na
hatua ile iliongezea TANU nguvu.
Baada ya muda mfupi tu toka
kufunguliwa kwa TANU Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TANU wa mwaka 1955 ulifuatia.
Tawi la Lindi lilikuwa tayari lina uhusiano na makao makuu ya TANU mjini Dar es
Salaam, na lilikuwa likitarajia kuhudhuria mkutano huo na kukutana na Julius
Nyerere na uongozi mzima wa TANU pale makao makuu Dar es Salaam. Mpunga,
mwanachama muasisi wa TANU, na Ali Ibrahim Mnjawale waliteuliwa kuhudhuria
mkutano huo kama wajumbe kutoka Jimbo la Kusini. Halmashauri ya TANU ya Lindi
iliwaelekeza wajumbe hawa wafikishe ombi rasmi kwa makao makuu ili Julius
Nyerere aje kufanya ziara kusini kwanza, kukutana na wananchi na kufanya
kampeni kwa ajili ya TANU na pili aje kupambana na propaganda dhidi ya TANU
zilizokuwa zikitawanywa na Yustino Mponda. Mponda akitumia uhusiano wake
na serikali ya kikoloni na nafasi yake kama mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria
kutoka Newala; na vilevile akitumia ushirikiano wake wa muda mrefu na kanisa
ambao bila shaka yoyote lilikuwa serikali ndani ya serikali kule kusini,
alikuwa ameanza kampeni yake ya kuipinga TANU. Hili lilikuwa likiathiri msukumo
wa uanachama. Mponda alikuwa mmoja wa wajumbe waliotumwa na Gavana Twining
kwenda Umoja wa Mataifa Februari, 1955 kwa niaba ya serikali ya kikoloni kwenda
kuipinga. Uongozi wa TANU huko Lindi ulitaka Nyerere aende kupambana na Mponda
akiwa katika uwanja wake mwenyewe, ndani kabisa ya ngome ya Ukristo wa
Kikatoliki katika Tanganyika.''
No comments:
Post a Comment