Sunday, 6 December 2015

SHEIKH KHALFANI KIUMBE: MAKALA YA SHEIKH HASSAN KABEKE

Wa kwanza kushoto ni Sheikh Khalfani Kiumbe, Sheikh Omar Himidi Mkunda, Sheikh Abdul Muhsin Kitumba
Nyuma kushoto Sheikh Taufiq Ibrahim Malilo, Sheikh Hammad Ibrahim Kabeke

Asalaam Alaikum kwa taarifa nilizo nazo siku ya Jumapili tarehe sita 6/12//2015 ndiyo siku ya hauli ya mwanazuoni mkubwa alie acha athari kubwa duniani. Mwanazuoni ambae maisha yake yoote aliyatoa kwa ajili ya dini nae si mungine ni Mufti Sheikh Khalfani Kiumbe. Sheikh Khalfani Kiumbe alizaliwa miaka ya 1925 kwa kumbukumbu zangu na katika maisha yake yoote ameitumikia dini bila kuchoka. Nawapongeza familia na wana Ujiji Kigoma kwa ujumla kwa kutenga siku ya kumkumbuka mwanazuoni huyu. Sheikh Khalfani Kiumbe atabakia Kwa muda mrefu katika nyoyo za Waislam wa Ujiji Kigoma Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Sheikh Khalfani Kiumbe ni mzaliwa wa mji mkongwe wa Ujiji.

Sheikh Khafani amezaliwa na mwanazuoni mkubwa wa zama hizo Sheikh Muhamed Maqsudi Kiumbe. Na mara tu baada ya kuzaliwa Sheikh Kiumbe alimpeleka Kwa Sheikh wake akiitwa Sheikh Khalfani bin Muhammed Zindijali. Akamwambia, Sheikh nimepata mtoto wa kiume basi palepale Sheikh Khalfani akamwambia, ‘’Huyu ni mimi atakua kama mimi na zaidi ya mimi.’’ Hapo Sheikh Khafani akabeba jina la sheikh wa baba yake.  Sheikh Khalfani Kiumbe alikuwa ana elim kubwa na hasa kwa zama zake upande wa ilmu ya aala hakua na wa mfano wake. Sheikh Khalfani yeye na mwenzie Maalim Bakari Suleimani Urembo (Bwera) waliasisi kituo cha Ghazali. Kituo ambacho kilipata barka kubwa kwa kutoa wanazuoni wakubwa walio bobea na wakawa msaada mkubwa katika dini nchini Tanzania.  

Sheikh Khalfani Kiumbe alishirikiana na Sheikh Omari Himidi Mkunda wa Ghazali. Kwa kweli wazee hawa ni mfano wa kuigwa na sisi sote. Sheikh Khalfani Kiumbe amesoma kwa masheikh mbali mbali kwanza ilim yake ilikua ya nyumbani.  Masheikh wakubwa wakubwa wa zama hizo waliotembelea Kigoma kama kina Sheikh Hasani bin Amiri (Abalmubarak) na wengine wengi pia aliifata elim Unguja ya zama hizo. Hakuna Sheikh wa Unguja katika miaka hiyo ya 1950 kwenda 1960 ila alitabarku nae. Sheikh Khalfani ni katika masheikh wachache ktk miaka 80 alibakhtika kuwemo katika msafara wa masheikh waliopata mualiko wa kutembelea Hijaz (Saudia Arabia). Na huko aliwashangaza wengi. Sheikh Khalfani kimaumbile alikua ana umbile dogo mpaka watu walikua wakimtembelea hawakuamini sifa zake elmu yake na umbile lake.

Sheikh Khalfani Kiumbe ni mwanazuoni wa aina yake katika maisha yake halijulikani genge lake muda wote anafundisha ama anajisomea ama anajibu maswali. Sheikh Khalfani darsa yake ya Ramadhani sijapata kuona ilikua inafunga mtaa mpaka mtaa mahudhuria hayo ni mwezi mzima. Sheikh Khalfani huwezi kumueleza kwa saa wala kwa siku ni bwana wa msimamo na mpenzi wa Mtume (SAW) kisawasawa. Wanafunzi wake wame enea karibu maeneo mengi ya dunia. Katika wanafunzi wake wako mpaka waliopata daraja ya umufti katika baadhi ya nchi Watanzania tu hawana idadi. Wapo kina Sheikh Taufiiq Ibrahim Malilo,  Sheikh Muhamed Ibrahim Kabeke, Sheikh Amrani aliwahi kua mufti wa Rwanda, Sheikh Ali Kahenga, Sheikh Swaleh Ramadhani Ndauga, SheikhThabiti Sibumwe, Sheikh Raajabu Kiingiza. Katika amia nimetaja wachache mnoo wapo wengi. Wajukuu zake katika elmu hawana idadi. Kwa haya aliyo yafanya nina hakika Allah  atamuingiza katika pepo yake  nimeona na mimi nikiwa katika vitukuu vyake nitabaruku nae katika masiku haya anapokumbukwa. Kwani pamesemwa wanapo tajwa waja wema baraka huteremka.

Ewe mola tushushie baraka kwa kazi ya mja wako ambae tunaitaqidi alikua mwema akafanya mema katuachia mema Mola tusamehe madhambi yetu na uwaraham walio maqaburini akiwemo Sheikh wetu na nuru yetu Sheikh Khalfani Kiumbe. 

Sheikh Hassan Kabeke
Mwenyekiti Juqusuta Taifa

No comments: