Thursday, 21 January 2016

IKIADHIMISHA KUASISIWA JE CCM INA KUMBUKUMBU ZA MZEE KINYOZI MUASISI WA TANU SINGIDA 1954?

Utangulizi

Kushoto: Idd Faiz Mafongo, Sheikh Mohamed Ramiya, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Saadan Abdu Kandoro na Haruna Taratibu wakiwa Dodoma Railway Station 1955/56

Mwaka 1988, katika sherehe ya kuadhimisha miaka thelathini ya Azimio la Tabora, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwasifu wanachama wa mwanzo wa TANU ambao walijiunga na chama kati ya mwaka 1954 na mwaka 1958. Nyerere alisema: 

''Hicho kilikuwa kipindi kigumu sana katika historia ya Chama chetu na ni watu wachache sana walikuwa na ujasiri wa kujiunga na chama na kukifanyia kazi.''

(Daily News, 6 October, 1988)

Hayo hapo juu ni maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akiwaadhimisha wazalendo wa mwanzo katika TANU waliopigania uhuru wa Tanganyika.

Mwalimu Nyerere aliyasema maneno haya akiwa Tabora katika sherehe ya kuadhimisha miaka 30 ya Azimio la Busara la Tabora lililoamua TANU kuingia katika Uchaguzi wa Kura Tatu mwaka wa 1958.

Waasisi wa TANU Central Province

Mwaka huu sherehe za kuasisiwa kwa CCM zitafanyika kitaifa Singida. Itapendeza sana ikiwa CCM itawaadhimisha waassisi wa TANU Singida kama Mzee Kinyozi. Soma hapo chini umsikie Mzee Kinyozi akitajwa pamoja na Haruna Taratibu mmoja wa waasisi wa TANU Dodoma mwaka wa 1954:

''Mwaka 1953, Haruna Taratibu, alikuwa  na umri wa miaka 23. Wakati akifanya kazi Public Works Department (PWD) Dodoma kama mwashi, alijaribu kuunda chama cha wafanyakazi kwa kuwahamasisha na kuwakusanya vibarua walioajiriwa katika kazi za ujenzi. 

Kwa sababu ya harakati hizo za kutaka kuanzisha chama cha wafanyakazi, Taratibu alionekana na wakoloni kama mtu mkorofi na mzusha vurugu. Hata hivyo Taratibu hakufanikiwa kuanzisha chama hicho na matokeo yake akapewa uhamisho kwenda Singida kama adhabu. 

Taratibu alivutiwa sana na harakati za Mau Mau nchini Kenya na alizoea kufuatilia matukio yake katika gazeti lake alilokuwa akilipenda sana, ''Baraza,'' gazeti la Kiswahili la kila wiki kutoka Kenya. 

Ilikuwa katika Novemba 1954 wakati Taratibu alipokuwa akipekuapekua gazeti hilo ndipo alioposoma habari kuhusu TANU. Taratibu aliuliza pale Singida mjini kama kuna tawi la TANU. 

Taratibu alifahamishwa kuwepo kwa tawi la TANU  pale mjini na katibu wake alikuwa mzee mmoja kwa jina la Mzee Kinyozi

Taratibu alikata kadi yake toka kwa huyo mzee na akawa mwanachama wa chama cha siasa. Asubuhi iliyofuata Taratibu aliingia ofisini kwake na akaiweka  kadi yake ya  uanachama wa TANU yenye  rangi nyeusi na kijani juu ya meza yake, kila mtu aione. 

Ofisa Mzungu wa PWD Singida hakuweza kuvumila ufedhuli kama ule, alishauri Taratibu apewe uhamisho kurudi Dodoma alikotoka, kabla hajaeneza  sumu yake kwa Waafrika wengine.''

Kutoka kitabu ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 - 1968)...'' (Phoenix Publishers, Nairobi, 2002) uk. 216.

No comments: