Thursday, 21 January 2016

KUTOKA JAMIIFORUMS: HISTORIA YA TANU SIKUANDIKA UONGO




Kituko,
Unaandika huku umeghadhibika.
Ghadhabu inaondoa fikra njema na inakaribisha shari.

Historia niliyoandika si kuwa haina upungufu kwa kutokuandika habari za Ali Msham tu
ina upungufu kwa kuwa ni kazi ya mikono ya binadamu.

Kazi yoyote ya binadamu ina upungufu.

Hili la kasoro katika kitabu changu si jambo la ajabu katika kazi yoyote ya kitafiti.
Ikiwa wewe unajua zaidi yangu kuhusu historia ya TANU ahlan wa saalan andika tukusome.

Kuhusu ubaguzi.

Si kweli kuwa kuna ubaguzi katika historia niliyoandika na hili nina ushahidi wenye yakini
kabisa.

Kitabu hiki kimepitiwa na wasomi mashuhuri katika historia ya Afrika kama John Iliffe wa
Cambridge, Jonathon Glassman wa Northwestern University wa Chicago, Jim Brenan 
wakati ule akiwa London School of Oriental and African Studies (SOAS) na wasomi wengi
wengine.

Hakuna hata mmoja katika hao aliepata kuandika na kusema kitabu changu kina ubaguzi.

Mimi sijapata kulalamika wala sijui unakusudia nini kwa kauli hiyo.

Mimi nimeona historia ya kweli ya uhuru wa Tanganyika imekosewa nimeshika kalamu na
kusahihisha kwa kuandika kitabu.

Huku si kulalamika.

Hakika wako akina Ali Msham wengi hawajaandikwa na ni wajibu wetu sasa tukaandika habari
zao.

Baada ya kutoka kitabu nililetewa habari za Rashid Ali Meli mmoja wa wanachama wa TANU
waliosaidia fedha katika safari ya Mwalimu Nyerere UNO mwaka wa 1955.

Hizo fedha zilikuwa na mkasa mkubwa sana.
Rashid Ali Meli alihudhuria kikao cha kwanza cha TANU Arnautoglo Hall, Dar es Salaam.

Baada ya kitabu kuchapwa nikapokea pia habari za Biti Kitete mama mpika uji wa Kariakoo
aliyotoa fedha si haba katika safari ya Nyerere UNO.

Michango ya wazalendo hawa wote inatakiwa kuandikwa.

Mwisho mimi sina haja ya kujibizana kuhusu duka la mafuta ya taa kwani hilo ni katika vitu
vidogo sana vilivyofanyika katika historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika.

Hatuwezi tukapoteza muda kwa kuvutana kwa vitu vidogo vidogo kama duka la mafuta ya taa
jirani ya kwa Mwalimu Fatina.

Mwalimu Fatina ni shangazi yetu.

Basi ikiwa mimi ni muongo na yeye ni muongo lakini napenda nikufahamishe kuwa alikuwa
mmoja wa wanawake wa Dar es Salaam walioona yote katika historia niliyoandika.

Haishangazi ikiwa duka la mafuta ya taa ni historia iliyosahaulika.

Historia nzima ya TANU iliandikwa mwaka wa 1981 na Kivukoni College na jina la Abdul Sykes
halikutajwa.

Hii ndiyo balaa kwa kuwa kadi yake ni namba 3 na mikutano ya siri yote ya kuasisi TANU ikifanywa
nyumbani kwake Mtaa wa Sikukuu na Aggrey na ndiye alikuwa mfadhili wa harakati zile.

Hakuna cha kustaajabisha sisi kukisahau kiduka kidogo cha mafuta ya taa kilichokuwa nyumbani kwa
Ali Msham fundi serremala wa Kariakoo.

No comments: