Monday, 1 February 2016

KICHEKESHO CHA SIASA ZA UGOZI


Mabango ya kampeni Uchaguzi Mkuu Mji Mkongwe Zanzibar 2015

Nimekuta katika "archives" zangu picha hizi za kampeni ya uchaguzi wa mwaka 2010 kutoka Mji Mkongwe. Mabango mawili ya juu kushoto linamuonyesha mgombea wa CUF Ismail Jussa na pembeni kuna bango la marehemu Nassor Mughery na chini Simai Mohammed Said. Mbele ya mabango hayo amesimama mwandishi. Sote tuliokuwa katika picha hiyo hapo juu ni Watanzania lakini...

Nimeileta "lakini," kwa sababu moja tu nayo ni kuwa ikiwa fikra zako zimeathirika na siasa za ubaguzi wa rangi utamwaona mwandishi ni "Mwafrika," na hao waliokuwa nyuma yake ni ''Machotara.''

Bango la ''Machotara''

Bango la CUF

Mwandishi muonekano wa rangi yake kwa hakika ni "nyeusi," na hao nduguze nyuma yake kwa muonekano wao ni "weupe."

Tunakabiliwa na siasa za kibaguzi.

Kuna swali litafuatilia hapa kwa upande wa CCM. 

Ikiwa chama hicho hakitaki "Machotara," imekuwaje akina Mughery wakafikia hadi ngazi ya kuaminiwa kuwa wagombea wa uongozi katika Zanzibar ilhali hawa si katika ''wao?''

Lakini ni kweli kuwa hawa  akina Mughery na Said si Waafrika? 

Jibu linalokuja kwa haraka ni kuwa hapana.

Bango la Dr. Shein na Maalim Seif 

Hawa ni Waafrika kwa kuwa wana damu za Waafrika kutoka upande wa bibi zao nenda nyuma vizazi na vizazi kutoka makabila tofauti yaliyokuwa Zanzibar karne kwa karne kuanzia Wamanyema hadi Wanyamwezi.

Swali lingine litakuja.
Sasa imekuwaje haya yakaingizwa katika siasa za Tanzania?

Wazanzibari

Mtu aliyekuwa katika taharuki hurukwa na akili na akafanya maamuzi mabaya. 

Inawezekana taharuki ya kushindwa uchaguzi Zanzibar umeifanya CCM Zanzibar ipoteze kwa muda uwezo wa kutafakari na hii ndiyo ikawa sababu ya wao kutoa kauli ambazo kwa hakika zimefedhehesha Tanzania kama nchi.

No comments: