Moja
ya misiba ya historia ya Zanzibar ni kwa watu wengi kutoijua historia ya kweli.
Watafiti wengi walioandika historia ya Zanzibar ni wageni na takriban wote
wamepitwa na mengi ama kwa utashi wao au kwa kukosa kupata taarifa za kweli za
khasa katika kipindi cha kudai uhuru. Mapinduzi ya Zanzibar yamezidi kuvuruga
historia hi kwa kuwa wote waliokuja kuandika baada yake khasa waandishi wa
Tanzania takriban wote wamekwepa kuansika kwa usahihi siasa za kizalendo kama
zilivyokuwa katika ya mwaka 1955 hadi 1964 mapinduzi yalipotokea. Waandishi
wengi wameamua kuipuuza historia hii muhimu ya kudai uhuru na kwa ajili hii
basi ni aghalabu kusikia majina ya viongozi kama Ali Muhsin Barwani wa Zanzibar
Nationalist Party (ZNP) na wengineo. Jina la Abdulrhaman Babu limebaki katika
historia ya uhuru wa Zanzibar kwa sababu alitoka ZNP mwaka wa 1963 katika
kipindi kifupi kabla mapinduzi hayajafanyika na kuanzisha chama kipya Umma Party
ambacho alikivunja na kujiunga na Afro-Shirazi Party (ASP) baada ya mapinduzi,
vingenevyo historia ya Babu kama ilivyokuwa historia ya wazalendo wengine kama
Juma Aley, Maulid Mshangama, Ibun Saleh kuwataja wachache ingepotea.
Ali Muhsin Barwani akitembelea vituo vya kupiga kura uchaguzi wa 1961 |
Aman Thani |
''Tarehe 1 Juni 1957 uchaguzi wa mwanzo wa
Kura Moja kwa Mtu Mmoja ulifanyika Zanzibar na ulikuwa wa salama. Matokeo yalikuwa Afro-Shirazi ilipata ushindi
katika majimbo matatu yote yalikuwa ya Unguja Kasikazini, Kusini na Ngambo.
Jimbo la Mji Mkongwe lilichukuliwa na Muwakilishi wa Indian Muslim Association
na majimbo mawili ya Pemba yalichukuliwa na Wawakilishi binafsi na baadae
waliyaunganisha na Afro-Shirazi.
Hizbu ingawa haikuweza kupata ushindi wa
hata jimbo moja, lakini ndio iliokua imesimama kidete kuitaka serikali ya
Kiingereza ilete mabadiliko zaidi ya katiba.
Serikali ya Kiingereza ilimleta Mchunguzi mwengine Sir Hillary Blood.
Mapendekezo ya Mchunguzi huyu wa pili yalikua ya kuipa Zanzibar uchaguzi wa
majimbo 22.
Kwa sababu walizokua wakizifahamu wenyewe, wananchi wengi khasa wa kutoka Pemba walijimegua kutoka chama cha Afro-Shirazi na walianzisha chama chao kwa jina la Zanzibar and Pemba Peoples Party. Kwa ufupi, ZPPP.
Januari Mosi 1961 wananchi wa Zanzibar wa vyama vitatu Hizbu, Afro-Shirazi na ZPPP waliingia katika midani kuwachagua wawakilishi wao waliokua wakiwataka. Uchaguzi ulikuwa shuwari tokea kuanza mpaka kumalizika. Matokeo yake yalikua, Afro-Shirazi ilipata ushindi katika majimbo 10, Hizbu majimbo 9 na ZPPP majimbo 3 yote yalikua kutoka Pemba.
Kutokana na hali kama hii, yakukosekana kwa chama pekee cha kuweza kuunda serikali bila ya kupata msaada wa kutoka katika chama chengine, Balozi wa serikali ya Kiingereza Sir George Mooring alikipa chama cha Afro-Shirazi muda wa wiki moja kujaribu kuwashawishi wawakilishi wa vyama vya Hizbu na ZPPP ili kipate wingi wa wakilishi wakikiwezesha kuunda serikali. George Mooring alikuwa na uzoefu mkubwa wa siasa za makoloni kwani alikuwa Nigeria Kaskazini kabla hajaja Zanzibar. Kabla ya hapo wakati wa Vita Kuu Vya Dunia alipigana Burma dhidi ya Wajapani. Mooring alikuwa askari shujaa. Chama cha Afro-Shirazi kiliitumia wiki yake kwa kuweza kumpata muakilishi mmoja tu wa ZPPP Bwana Ali Sharif Musa. Wiki ya pili ikawa zamu ya Hizbu. Bila ya kupoteza wakati, Hizbu ilifanikiwa kuwapata wawakilishi wote wawili wa ZPPP waliobakia. Pande zote mbili zikawa na wawakilishi 11:11. Ilivyokuwa haukuweza kupatikana upande uliopata wingi, Hizbu ilitoa pendekezo la kutaka pafanywe serikali ya Umoja wa Taifa.
Afro-Shirazi ilipinga na ilitaka pafanywe uchaguzi mwengine. Mvutano wa maneno ulichukua muda bila ya kupatikana tija ilio njema. Balozi Sir George Mooring kutaka kuunyamazisha mvutano wa maneno, alitoa pendekezo la kufanywa serikali ya mshikizo yaani ‘’Care Taker Government,’’ kwa muda wa miyezi sita baadae pafanywe uchaguzi mwengine. Kwa shingo upande Hizbu ililikubali pendekezo hilo la Balozi Mooring. Tatizo lilio chomoza lilikua la nani ataekuwa Waziri Mkuu wa serikali hii ya mshikizo? Hizbu ilimpendekeza mwananchi Bwana Ahmed Lakha, Afro-Shirazi ilipinga na ilimpendekeza mkoloni Robertson mtumishi mkuu wa serikali ya kikoloni Zanzibar. Palitokea mvutano mkubwa baina ya Hizbu na Afro-Shirazi kwa pendekezo hili la Robertson. Hizbu ilipinga vikali sana. Lakini, damu ni nzito kuliko maji. Robertson alikuwa Muingereza, Balozi Mooring Muingereza pendekezo la Afro-Shirazi la kumukhitari mkoloni badala ya mwananchi lilifanikiwa.
Katika kipindi hichi cha serikali ya mshikizo, Hizbu na ZPPP waliamua kushirikiana na waliamua kuukabili uchaguzi kama ni chama kimoja. Afro-Shirazi walipoona Hizbu na ZPPP wameungana, walihisi kuwa hawatoweza kufanikiwa katika uchaguzi wa Juni. La kulifanya, waliliona halipo isipokuwa kuleta michafuko katika vituo vya kupiga kura ili uchaguzi wote ufisidike. Uchaguzi huu wa tarehe 1 Juni 1961 ulikuwa uchaguzi wa majimbo 23 kwa Unguja na Pemba. Muda mdogo baada ya kufunguliwa kwa vituo vya kupiga kura, wafuasi wa chama cha Afro-Shirazi walianza kufanya fujo la kuwatoa wafuasi wa Hizbu na ZPPP katika mistari ya wapiga kura. Fujo lilianza kwenye vituo vya kupiga kura likaendelea mpaka majiani, majumbani hadi vijijini. Matokeo ya fujo hili la Afro-Shirazi lilimalizika kwa kutolewa roho wafuasi 69 wa Hizbu na ZPPP. Serikali ya kikoloni ambayo ndio iliokuwa na dhamana ya kuweka usalama wa nchi, ilishindwa kuzizidhibiti fujo hizo, wakaviagizia vikosi vya kupambana na fujo kutoka Kenya. Muda mfupi tokea kuwasili kwa vikosi hivyo vya askari wa FFU kutoka Kenya, mji ulirejea katika hali yake ya utulivu. Waswahili wanasema, ‘’Wanja wa manga si dawa.’’ Yote walioyafanya, yalipotangazwa matokeo, waliuona muungano wa Hizbu na ZPPP umetoka na ushindi wa majimbo 13 na Afro-Shirazi kubakia na yao yale yale 10. Muungano wa Hizbu na ZPPP waliunda serikali ya mwanzo ya wananchi na Sheikh Muhammad Shamte Hamad akiwa ndiye Waziri Mkuu.''
Kutoka
katika kalamu hii ya Mzee Aman Thani tuna mengi ya kuijifinza katika historia
ya Zanzibar ndani ya chaguzi za marudio, halikadhalika na jinsi Wazanzibari toka
enzi hizo walivyokuwa wakipiga kura.
Clip hiyo hapo juu inaeleza mengi. Itazame kwa makini yapo mengi ya kujifunza.
Bahati mbaya sana haina sauti.
Clip hiyo hapo juu inaeleza mengi. Itazame kwa makini yapo mengi ya kujifunza.
Bahati mbaya sana haina sauti.
No comments:
Post a Comment