Saturday, 19 March 2016

ABOUD JUMBE ALIPOZUNGUMZA TATIZO LA UDINI TANZANIA 1992


Uonevu na Udini Upo Tanzania
Na Alhaj Aboud Jumbe

Maandamano Maalim Aboud Jumbe, Maalim Aboud Maalim na Abdulrahman Babu

HOJA zimekuwa zikijengwa kuwa nchi yetu imefanikiwa kujenga utaifa ambapo hakuna ubaguzi wa kidini au kikabila. Aidha, Mtanzania yeyote ukimuuliza atakuambia kuwa serikali yetu haina dini. Kwa mtazamo huo viongozi hawaongozi kwa utashi wa dini zao kuwahujumu wananchi wasio katika dini moja.

Wanasiasa wanapotoa shutuma dhidi ya watu, wanaodai wana udini, taswira inayojengwa ni k uwa Muislamu ndiye mdini, bali Mkristo hawezi kuwa mdini. Ndio maana japo serikali yaweza kuwa imejaa Wakristo ikilinganishwa na Waislamu, haionekani kuwa ni tatizo.

Aidha, ndio maana uongozi wa juu wa CCM una Wakristo wengi, lakini hausikii CCM ikiambiwa ni chama cha Wakristo au kina udini. Lakini inapotokea chama kingine, kuwa na viongozi Waislamu basi hubatizwa kuwa chama cha kidini.

Si wananchi wote wanayoyatazama mambo kwa mtizamo huu. Wako wanaotoa hoja kuwa ubaguzi wa kidini umekuwa ukifanyika, lakini kwa ustadi mkubwa.

Alhaj Aboud Jumbe, Rais mstaafu wa Zanzibar, ametoa hoja kuonyesha kuwa Waislamu hawatendewi haki na kwamba Kanisa Katoliki limepewa fursa ya pekee nchini.

Sehemu katika kitabu chake inasema:

MTIRIRIKO wa matukio ya kisiasa unaashiria agenda ya siri ambayo inaelekezwa kutumikia Kanisa Katoliki ambalo siku zote linakuwa na uhusiano wa karibu na serikali (hii) yenye kujenga mtizamo wa Kikristo ya Jamhuri ya Muungano na huku Waislamu wakihasirika.

USHAHIDI uliopo unaonesha kuwa Waislamu wa Tanzania Bara wamekuwa na uonevu ulioendelea na kukoseshwa haki zao za msingi pamoja na kuwa katiba ya mwaka 1977 ilikuwa na vipengele vya kuhakikisha haki za binadamu na usawa kwa raia wote.

Ushahidi wa ziada unaonesha Kanisa nchini Tanzania ndilo linatowa maelekezo ya kisiasa na mfumo wa kisiasa umekuwa ukitumiwa kutoa upendeleo kwa Wakristo ambao tayari wamo katika kudhibiti nafasi mbalimbali katika asasi za umma.

Kama tukichukulia maendeleo ya hali ya kisiasa nchini hivi sasa kuhusiana na Muungano nina hakika ya kuwa na shaka kuwa utaratibu mzima wa kuwabana Waislamu wa Tanzania Bara unaendeshwa kwa mbinu za mchwa sambamba na ule wa kuikaba Zanzibar ili kuilazimisha kuingia katika mpango wa muda mrefu wa kuiingiza katika serikali moja ili kuhakikisha Waislamu kutoka pande zote mbili za Bahari ya Hindi hapa Tanzania wanasujudu kwa Bwana mmoja.

Sura hii inataftishi suala la dini na siasa katika Jamhuri ya Muungano. Mada hii huenda ikawaudhi baadhi ya watu. Lakini siku zote ukweli hauwafurahishi wale ambao hawapendi ujulikane kwa sababu zinazoeleweka ambazo ni za kuchukiza za kibinafsi na zenye makusudio maovu.

Tangu nusu ya pili ya mwaka 1993 mashambulizi mbalimbali yasiyo na msingi yamekuwa yakielekezwa na kuongezewa nguvu dhidi ya Waislamu maalum, lakini pia kwa Uislamu kwa jumla.

Mashambulizi ya awali yaliyofanywa na mtu binafsi, vikundi vya watu, vyombo vya dola na mwisho vyombo vya habari yalielekezwa kwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kujiunga na Jumuiya ya Mkutano wa Kiislamu (OIC).

Hii ilikuwa ni rasharasha tu ya mabomu kabla ya matusi hasa hayajafuatia baadae. Katika muda huo huo lilipitikana jaribio lililoshindwa ambapo uvumi usio na msingi ulienezwa kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano ilitaka kujiunga na Jumuiya nyingine ya Kiislamu inayoitwa Islam in Africa Organization (IAO), hili likitowa mwanga, mashambulizi haya yalipangwa kulenga shabaha gani. Na ilikuwa wazi kuwa waliojikita katika majadiliano hayo hawakuelekeza mabishano yao nje ya Uislamu na Waislamu.

Kwa mfano, kuwepo kwa ubalozi wa Vatican nchini Tanzania hakukupata kuhojiwa pamoja na kuwa serikali hii inadai kuwa si ya kidini. Kanisa, CCM na serikali vyote vimekaa kimya huku vikijua kutendeka kwa hilo lakini vikizibwa mdomo.
Kana kwamba hiyo haikutosha kuonesha kuwa kuna mlalio dhidi ya upande mmoja, kulifuatia jaribio la kumng'oa Rais Mwinyi kupitia taratibu za Bunge, kudai kufukuzwa Rais wa Zanzibar Dk. Salmin Amour na baadhi ya Mawaziri wake na kelele za kuwataka mawaziri Waislamu katika Jamhuri ya Muugano wajiuzulu kwa kutaka kusilimisha Tanzania, inaonesha malengo ya mashambulizi hayo.

Mkakati ukaandaliwa ambao ulitakiwa kuonesha kuwepo "kwa hila za Kiislamu" ili kujenga hoja ya kuwasaka Waislamu ambao walionekana kuwa kero isiyostahimilika. Fursa ilipopatikana basi ikatumiwa haraka. Uchokozi mbalimbali dhidi ya Waislamu ambao mwengine haukuripotiwa ukaanza kuzua hisia tofauti za wakandamizaji na wakandamizwaji kufuatia na ukamataji mkubwa na kesi katika mahakama ambazo baadhi yake zimekuwa zikiendelea kwa muda mrefu.

Matukio haya yamedhihirika kwa Waislamu wengi kuwa kumekuwa na hatua za makusudi kuchanganya siasa na dini katika mambo ya serikali.

Kinyume na kampeni inayosambazwa, Waislamu sio chanzo ila wao ni waathiriwa wa mbinu za makusudi za kujenga mfumo wa uhasama ambao unazinyonya dini zote mbili na siasa ili kuwabana Waislamu na pia kupata uwezo wa kuwakandamiza.

Dhana ya kutenganisha dini na siasa katika wakati huu ilianzishwa na baadhi ya nchi za Magharibi ili kuanzisha taifa lisilo na dini ili kuepuka uingiliaji wa Kanisa ambao wakati huo ulikuwa ni mkubwa.

Awali kitendo kama hicho kilionekana kama ni cha upinzani juu ya mamlaka ya Papa ambae alikuwa ameigawa dunia, upande wa magharibi ukiwa kwa Uhispania iliyokuwa na nguvu na upande wa mashariki kwa Ureno ambayo pia ilikuwa na nguvu na kuyaacha mataifa makubwa ya Ulaya yakiwa yanakosa pahala pa kushika katika zama hizo.

Utaifa mpya katika bara la Ulaya ulipingana na Papa na kundi lake kwa kuanza kuvamia maeneo yaliyokuwa chini ya Uhispania na Ureno. Sio tu walianza kujitangazia mamlaka zao huru, lakini pia walianza kujikatia maeneo mapya nje na ndani ya Ulaya.

Baada ya kufanikiwa kuunda mataifa yao walianzisha pia Makanisa yao ambayo yalikuwa na lengo moja la kukuza dini. Kidogo kidogo mataifa haya "yasiyokuwa na dini" yalianza kupeleka baadhi ya madaraka kwa wafalme, malkia na wabunge.

Wakati ambapo kuna mgawanyo unaoeleweka na ulio wazi baina ya mamlaka ya kiroho na kiserikali kwa upande wa dola na Kanisa, taasisi mbili hizo hazijaweza kusita kuingilia mambo ya kidini, kiuchumi na kisiasa katika nchi zinazoendelea na kusababisha hali ya kutoelewana, kutoaminiana, kukosekana kwa utulivu na pia kusababisha fujo wakati wa utekelezaji wa mipango yao ya kihaini.

Hili hutokea zaidi pale kunapokuwa na idadi kubwa ya Waislamu na Wakristo wanapoishi pamoja. Tunaushahidi wa kutosha na usiopingika juu ya jambo hili kwa Tanzania.

Upitizi wa makini wa kitabu "Kanisa Katoliki na siasa Tanzania Bara 1953-1985" unatoa habari za ndani zisizo za kawaida juu ya kampeni dhidi ya Uislamu.

Kwa maneno mengine kitabu hicho kwa kiasi fulani ni kukiri kwa yeye mwenyewe mwandishi juu ya shughuli za Kanisa la Katoliki za kisiasa Tanzania, Kanisa ambalo haliwezi kutenganishwa na Vatican na ambalo ubalozi wake ni mmoja katika balozi kongwe nchini Tanzania.

Kwa sababu zisizoeleweka kitabu hiki kimeandikwa na kuchapishwa na waumini wa Kanisa hilo. Yaliyomo ndani ya kitabu hicho hayajakanushwa wala kubishiwa na serikali ya Muungano ya Tanganyika au CCM, huu ukiwa ni ushahidi kamili juu ya ukweli wa kukiri juu ya neno hilo.

Kwa sababu na malengo yoyote ya kutolewa kitabu hicho , na lazima ziwepo sababu za msingi za kufanya hivyo, kitabu hiki ni ufunuo mzuri juu ya mbinu za chini kwa chini za Kanisa katika medani ya kisiasa Tanzania.

Kitabu kinaeleza ni Kanisa Katoliki lililojenga njia ambazo ziliwawezesha kuwa na mahusiano ambayo kitabu hicho inaeleza yalikuwa ya karibu kabisa na TANU wakati wa miaka ya kupigania uhuru. Kinaonesha ni vipi Kanisa lilitayarisha waumini wake shupavu ambao walikuwa wameshika karibu nafasi zote muhimu katika serikali mpya ya Kiafrika ya Tanganyika.

Kinaeleza ni vipi serikali ya Jamhuri ya Muungano ilirithi mfumo huo, na kuupanua kuingia katika mamlaka ya Muungano na pia katika mambo yahusuyo Tanganyika. Na hapa tunaweza kupata mwanga juu ya maana na ulazimishaji wa kuwepo serikali mbili badala ya tatu kwa njia zilizogubikwa kama ilivyobainishwa na mkataba wa Muungano (mapatano ya Muungano) na katiba zote zilizopitishwa Tanzania.

Hapa ndipo unapoona kuna neno katika kudai kusimamishwa mfumo wa serikali moja. Nguvu hizo zikapenya zaidi kupelekea Muungano wa ASP na TANU ambapo CCM iliendeleza kazi za TANU kuhusiana na ushirikiano wa karibu na Kanisa Katoliki.

Kwa wale viongozi, wawe wa Kanisa, CCM au serikali ya Muungano ambao walikuwa wakijipigia kelele kutenganisha kwa siasa na dini, lakini wao wenyewe wakiwa ndio waendelezaji wakubwa wa hilo, wana kazi ngumu ya kuelezea kwa umma kwa ujumla lakini zaidi kwa Waislamu. Sivalon anaelezea juu ya mpango na njama zinazoendelea zikishirikisha Kanisa Katoliki, Chama (TANU-CCM) na serikali ya Muungano.

Tangu njama hizo ziwekwe wazi 1992 hapakuwa na kauli moja ya kupinga au kutolea maelezo juu ya hilo. Huku ni kukiri kwa dhahiri juu ya mipango na njama za Kanisa zinazofanywa hali zikiwa zinaeleweka na mkono wa chama na serikali yake.

Yafuatayo ni baadhi ya madondoo kutoka kitabu hicho:

"Mwishowe tutakuja kuonesha jinsi Rais mstaafu Nyerere alivyokuja kuwa kiungo cha pekee kati ya chama/kanisa na Kanisa Katoliki. Uhusiano huo unaelezwa kwanza kama msingi wa kuelewa jinsi gani na kwa kiasi gani viongozi wa Kanisa walivyoingilia kati maendeleo ya siasa hapa Tanzania (uk. 5).

Huo uhusiano ukawaweka viongozi wa Kanisa katika nafasi nzuri ya kuelekeza maelekezo ya siasa Tanzania. (uk. 9).

Aboud Jumbe na Mwandishi 2000

No comments: