ZANZIBAR KONGWE MAHUTUTI KUPONA YATAKA DOZI KUBWA NA JOSEPH MIHANGWA
Raia Mwema
Z’bar
kongwe mahututi, kupona yataka dozi kubwa
Joseph
Mihangwa
ZANZIBAR
inaumwa; tena inaumwa ugonjwa unaoua hima (terminal disease) isipopata tiba
makini, tiba yenye nguvu na kwa dozi kubwa.
Vipimo
vya kitaaluma vinaonesha inasumbuliwa na mashetani, mizuka yenye kukalia kigoda
cha mzimu wa watu wa kale. Mzimu huu unayumbisha Muungano wa Tanzania pia.
Juhudi
za Serikali ya Muungano kutibu ugonjwa huu zimepwaya, kwamba badala ya kutibu
ugonjwa wenyewe, mara nyingi zimeelekezwa kutibu dalili za ugonjwa pekee.Mzimu
wa ubaguzi kwa misingi ya rangi na uchama wa vyama mfu vya kale unaitafuna
Zanzibar kwa kificho cha vyama vya siasa vya sasa – Chama cha Mapinduzi (CCM)
na Chama cha Wananchi (CUF) kwa staili ya mababu. Kwa vipi?.
Harakati
za kisiasa za uhuru (modern independence struggles) Visiwani, ziliongozwa na
vyama vikuu viwili: Zanzibar Nationalist Party (ZNP), kilichoundwa mwaka 1955;
na Afro-Shirazi Party (ASP) kilichoanzishwa mwaka 1957.
Kipindi
cha uchaguzi Mkuu wa mwisho, Julai 1963 kuelekea uhuru, kulijitokeza vyama
viwili vibanzi (splinter parties) – Zanzibar and Pemba Peoples’ Party (ZPPP)
cha waliojiengua kutoka ASP, na Chama cha Umma Party (UP) cha Abdulrahman
Mohamed Babu na wenzake waliojiengua kutoka ZNP. UP hakikushiriki Uchaguzi Mkuu
wa mwisho wa 1963, lakini kilishiriki kupanga na kuratibu kwa mafanikio,
Mapinduzi ya Januari 12, 1964.
ZPPP
na ZNP viliunda umoja (Ukawa) dhidi ya ASP na kushinda uchaguzi na hivyo
kukabidhiwa serikali chini ya Waziri Mkuu Mohamed Shamte wa ZPPP. Siku 33
baadaye, serikali hiyo ilipinduliwa.
ASP
ni muungano wa vyama viwili vya kijamii, “African Association” (AA) na “Shirazi
Association” (SA), kufanya “Afro-Shirazi Party” (ASP). Chama hiki
kilijipambanua kuwa cha Waafrika zaidi, kama ambavyo tu Chama cha “Tanganyika
African National Union” – TANU cha Tanzania Bara kilicholeta uhuru wa nchi hiyo
mwaka 1961, kilivyojipambanua mwanzoni, lakini kikajisahihisha haraka kuachana
na ubaguzi na kuwa cha watu wa rangi zote. Mapinduzi ya 1964 yalikiweka ASP
madarakani, chini ya Serikali ya Mapinduzi iliyoongozwa na Abeid Amani Karume
wa ASP. Hapo ndipo ugonjwa unaoitesa Zanzibar hadi sasa ulipoanzia.
Kwa
kuanzia, Wazanzibari wote waliokuwa wanachama wa ZNP/ZPPP na ndugu zao
walihesabiwa kama maadui wa Mapinduzi na kuvurumishwa nje ya Zanzibar, na
waliobakia waliteswa kwa kutwezwa kwa ubaguzi mkubwa. Mohamed Babu wa UP,
aliyekuwa na asili ya Visiwa vya Ngazija, alitakiwa kuvunja Chama chake, naye
akakubali ambapo yeye na baadhi ya vijana wake, kwa kutambuliwa mchango wao
katika Mapinduzi ya 1964, walipewa Uwaziri katika Serikali ya Mapinduzi na
baadaye katika Serikali ya Muungano.
Kufuatia
kifo cha Karume Aprili 7, 1972, mzimu wa ubaguzi ukakita kwa kishindo kikubwa
zaidi. Kwanza, Wazanzibari wote waliokuwa wanachana wa ZNP, ZPPP na Umma Party
na koo zao, walitiwa ndani ya kapu moja la mauaji ya Karume bila udadisi na
hivyo kuitwa maadui wa Mapinduzi. Kisha ikapitishwa amri kwamba, Wazanzibari wa
kundi hilo wasipewe nafasi za uongozi Visiwani, wala kuruhusiwa kujiunga na
Jeshi la Ulinzi na Polisi.
Pili,
Zanzibar ilifanywa kuwa ya Wazanzibari weusi; suriama (chotara) na wahamiaji
wengine wa rangi tofauti, bila kujali walifika lini Zanzibar, hawakustahili
kuitwa Wazanzibari. Ubaguzi huu na manyanyaso yalikuwa yalisimamiwa na Serikali
ya Mapinduzi chini ya Usimamizi wa kundi katili, maarufu kama “Genge la watu
14” – (the Gang of fourteen), likiongozwa na Kanali Seif Bakari wa idara ya
Usalama Zanzibar.
Hata
pale Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964, ubaguzi huu uliendelea kwa
chukizo kubwa kwa Mwalimu Nyerere, ukifanywa kwa jina la Serikali ya Mapinduzi
chini ya ASP kilichokuwa juu ya Serikali ya Muungano; Karume akageuka kuwa
mwiba kwa Mwalimu.
Ili
kukomesha ukatili na ubaguzi huu, mwaka 1976, Mwalimu Nyerere (TANU) alibuni
Muungano wa Vyama vya TANU na ASP (kama alivyobuni mapema Muungano wa nchi hizo
mbili) kwa madhumuni ya kudhibiti maovu ya Zanzibar ndani ya Jamhuri ya
Muungano, ili chaka la hayo yote (ASP) liweze kudhibitiwa na chama kipya chenye
kushika hatamu za uongozi wa Jamhuri ya Muungano, Zanzibar ikiwa ndani.
Wazo
hili lilipingwa vikali na Wahafidhina wa siasa za ubaguzi visiwani kiasi cha
Rais wa Zanzibar wa wakati huo, Aboud Jumbe, kulazimishwa aachane na “mbinu za
Nyerere” za kutaka “kuimeza” Zanzibar; akatoa sababu za kutaka muda zaidi
kufikiria. Lakini baada ya vuta nikuvute, na kwa tishio la kuvunja Muungano, wahafidhina
hao, waliojiita “Wakombozi” (Liberators), walikubali ASP na TANUviungane,
lakini kwa masharti.
Sharti
la kwanzalilikuwa kwamba, jina la Chama kipya lisiwe kwa lugha ya Kiingereza
ili kutowakumbusha Wazanzibari enzi za ukoloni wa Mwingereza Visiwani; la pili,
kwamba neno “Mapinduzi” lionekane na kusomeka bayana ndani ya jina la Chama
kipya ili kutopoteza historia ya Mapinduzi ya 1964. Tatu, tarehe ya kuzaliwa
kwa Chama kipya ioane na tarehe ya kuasisiwa kwa ASP, na kwamba angalau
tarakimu moja ya mwaka 1957ionekane pia.
Potelea
mbali, TANU ya Nyerere haikupoteza muda kwa hayo; ikakubali jina la Chama liwe
“Chama cha Mapinduzi” (CCM) bila tafsiri ya Kizungu ambapo kingeitwa
“Revolutionary Party of Tanzania” – RPT; na ikakubalika kianzishwe Februari 5,
1977, tarehe ya kuasisiwa ASP, 5 Februari 1957.
Kisha,
CCM kikatangaza kushika hatamu za uongozi hivi kwamba kiongozi yeyote
aliyekwenda kinyume na maagizo ya Chama, alikwenda kinyume na Muungano na hivyo
mhaini, Mzanzibari kwa Mtanzania Bara.
Kwa
hatua hiyo, wahafidhina wa siasa za ubaguzi na ukatili Visiwani walivurumishwa;
Baraza la Mapinduzi na “the Gang of 14” likamalizwa nguvu kwa nafasi yake
kuchukuliwa na Baraza la Wawakilishi; demokrasia ikamea Zanzibar. Ukuu wa Chama
(Party Supremacy), ndio uliomng’oa madarakani Rais wa awamu ya pili Visiwani,
Aboud Jumbe, alipojaribu kuungana na Wahafidhina wa siasa za chuki, kuhoji
uhalali wa Muungano, mwaka 1984.
Baadhi
ya waliojaribu kufanya hivyo mwaka 1986, akiwamo Kada wa CCM wa zamani na
kipenzi cha Mwalimu Nyerere, aliyesaidia kung’olewa madarakani kwa Jumbe, Maalim
Seif Sharrif Hamad; walifukuzwa uanachama wa CCM kwa kusaliti Mapinduzi.Wengine
waliofukuzwa pamoja na Hamad ni Shaaban Mloo, Ali Haji Pandu, Khatib Hassan,
Soud Yusuf Mgeni, Hamad Rashid (sasa yupo ADC) na mwingine mmoja.
Kufukuzwa
kwa kundi hili, maarufu kama “The Magnificent Seven” (Waadhimu Saba), kulifanya
waungane na kuanzisha upinzani kwa mwavuli wa “Kamati ya Mwelekeo wa Vyama
Huru” – “KAMAHURU”, iliyozaa Chama cha “Zanzibar United Front” [ZUF] mwaka
1992. BaadayeZUF kiliungana na “Chama cha Wananchi” (CCW) cha Bara, kuunda
Chama cha kitaifa cha sasa – “Civil United Front” (Chama cha Wananchi) – CUF.
Vyama
hivi viwili, CCM na CUF vina nguvu sawa Visiwani kiasi kwamba hakuna aliye na
uhakika wa ushindi kwa chaguzi zote. Kwa wahafidhina wa siasa za kale Visiwani,
ASP hakijafa, kinaishi ndani ya kivuli cha CCM; na vivyo hivyo Baraza la
Mapinduzi na nadharia zake.
Kwa
wahafidhina hao, Chama chochote cha upinzani kwa CCM ni cha upinzani kwa ASP
mfu na Baraza la Mapinduzi, “upinzani” wenye kuibua hisia za mzuka wa ZNP na
ZPPP za kujitakia.
Wakati
CCM Zanzibar kinaishi kwa hofu ya mzimu wa watu wa kale, CCM Bara kinasumbuliwa
na hofu itokanayo na Katiba shaghalabagala ya Muungano, inayozua maswali mengi
kuliko majibu kama vile: Je, iwapo, kwa mfano, CUF kitashinda uchaguzi Zanzibar
na Seif Sharrif Hamad kuwa Rais wa Zanzibar, na Magufuli wa CCM kama Rais wa
Tanzania; hali ya kisiasa itakuwaje kwa vyama viwili tofauti kutawala sehemu
mbili tofauti za Tanzania?
Kwa
kuwa Rais wa Zanzibar ni Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Serikali ya Muungano
(Angalia Katiba, - ibara 54 (1) ambalo wajumbe wake ni pamoja na Rais wa
Muungano, hali itakuwaje kama Seif Sharrif Hamad wa CUF atakuwa mjumbe wa
Baraza hilo? Je, litaweza kufanya kazi ipasavyo?, wakahoji.
Kwa
kuwa Baraza la Mawaziri linawajibika kwa Bunge la Muungano na kwa Rais katika
ujumla wake, Je, Hamad naye atawajibika kwa Bunge hilo na kwa Rais wa Chama
tawala Tanzania? Je, atawajibika pia kutekeleza uamuzi wa Baraza hilo la
Mawaziri nchini Zanzibar? Kama nani?
Rais
wa Zanzibar kuwa Mjumbe wa Baraza la Mawaziri la Muungano kulitokana na hofu
nyingine kubwa zaidi, juu ya uwezekano wa Hamad kuwa Rais wa Zanzibar na hivyo
kuwa Makamu wa Rais wa Muungano, jambo ambalo halikuingia kichwani mwa CCM.
Hivyo, haraka haraka ikateuliwa Tume ya Jaji Mark Bomani mwaka 1994,
kupendekeza marekebisho ya Katiba kama ilivyo sasa kwa kukiuka mmoja wa misingi
ya Muungano, kama inavyofafanuliwa kwenye Mkataba wa Muungano [Articles of
Union] wa mwaka 1964.
Tatizo
ni upungufu katika Katiba ambao umeandikwa kana kwamba hapana uwezekano wa
sehemu mbili za Tanzania kutawaliwa na vyama viwili tofauti, licha ya kufungua
milango kwa mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Inapofikia hapo, hofu ya
wahafidhina wa siasa za ubaguzi Visiwani na hofu ya wenye uchu wa madaraka
Bara, zinaungana kwa kivuli cha CCM kubaka demokrasia na umoja wa kitaifa kwa
kusigina Katiba na Sheria tulizozitunga wenyewe. Sheria zinazotakiwa
kuzingatiwa na kuheshimiwa ni Katiba ya Zanzibar, Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania na Sheria ya Uchaguzi Zanzibar, na kwa Wasimamizi wake kujiepusha
na ushabiki wa vyama vya siasa.
Historia
ya Zanzibar inaonesha kwamba, umwagaji damu wote uliowahi kutokea Visiwani
ulitokana na machafuko yaliyosababishwa na chaguzi kuu zisizokuwa huru na za
haki. Kwa mfano, uchaguzi wa kwanza, uliofanyika Januari 1961 haukutoa mshindi
kati ya ASP na ZNP; ghasia zikazuka na watu kadhaa kuuawa na wengine
kujeruhiwa.
Hata
hivyo, chuki na uhasama wa kisiasa enzi hizo haukuwa mkubwa kama ilivyo sasa;
wanasiasa waliongozwa na azma moja ya kuipatia nchi uhuru kutoka kwa Waingereza
bila kuingiza ubaguzi wa aina yoyote miongoni mwa Wazanzibari. Ndiyo maana,
baada ya Vyama vyote kukosa ushindi katika uchaguzi wa Januari 1961, iliundwa
serikali ya mseto ya mpito ya vyama vya ASP, na ZNP/ZPPP kuelekea uchaguzi
mwingine uliopangwa kufanyika Juni 1961.
Kabla
ya uchaguzi huo, Karume alimwomba Kiongozi wa Chama cha ZPPP, Mohamed Shamte
waunganishe vyama vyao (ASP na ZPPP) ili kukipiku, lakini Shamte alikataa.
Juni
1961 ilipowadia, ZNP na ZPPP viliunda mseto dhidi ya ASP; ghasia kubwa
zikazuka, huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kupinda kanuni za uchaguzi.
Katika ghasia hizo, watu 70 waliuawa, 400 walijeruhiwa na wengine 1,002 kutiwa
mahabusu na Serikali ya Uingereza. Hapo ndipo uhasama mkali wa kisiasa ambao
umedumu hadi leo uliposhika kasi.
Uchaguzi
wa tatu na wa mwisho kabla ya uhuru uliofanyika Julai 1963 ulilalamikiwa na
Chama cha ASP kwamba haukuwa huru na wa haki. Hata hivyo, Karume aliamua kutupa
karata yake ya mwisho kwa kutaka kuundwe Serikali ya Umoja wa Kitaifa kati ya
ZNP/ZPPP na ASP ili kumaliza manung’uniko na uhasama wa kivyama.
Aliwatuma
Viongozi wawili waandamizi wa ASP – Othman Sharrif na Hasnu Makame, kumwomba
Shamte akubali kuundwa kwa serikali hiyo, ambapo Shamte angeongoza serikali
akiwa na uhuru kamili wa kuteua mawaziri kutoka ZNP, ZPPP na ASP. Kwa mara ya
pili, Shamte alikataa katakata na badala yake akashauri ASP kivunjwe na
wanachama wake wajiunge na ZNP/ZPPP.
Sote
tunafahamu kilichotokea; Serikali ya Shamte ilipinduliwa katika Mapinduzi ya
umwagaji damu, yaliyopangwa na kuongozwa na vijana wenye itikadi za
Kisoshalisti wa vyama vya ASP na UMMA, Januari 12, 1964. Siku 100 baadaye tangu
Mapinduzi hayo kufanyika, Zanzibar na Tanganyika ziliungana kuunda Tanzania.
Wazanzibari
bado wanabaguana kwa misingi ya vyama vya siasa hai na mfu, rangi na kwa nasaba
za koo zao; ubaguzi ambao haupo Tanzania Bara. Haya yote ni ishara ya kuzorota
kwa umoja wa kitaifa na chanzo cha ghasia. CUF Zanzibar kinahesabiwa kuchukua
nafasi ya ZNP/ZPPP, na CCM Zanzibar nafasi ya ASP.
Tunayoshuhudia
sasa ni vituko vya uhuru vinavyofanywa na Wazanzibari waliochoka na hali ya
amani. Kwa nini hatujifunzi kutoka Darfur, Sudani, Rwanda na Burundi na
kwingineko kwa yanayotokea Visiwani. Mzee Karume hakukosea alipowataka
wapinzani wake kuunda serikali ya mseto mwaka 1961 na 1963 kama njia ya
kumaliza mgogoro; na pale waliposhindwa kumsikiliza, ghasia ziliendelea
kuitafuna nchi hadi Mapinduzi.
Kwa
hali ilivyo Visiwani Zanzibar, kuna kila dalili kuonesha kwamba historia
inaweza kujirudia kama nguvu za CCM na CUF hazitaweza kushabihishwa (harmonize)
ziweze kutumika kwa maendeleo ya Wazanzibari. Ushabiki na unafiki wa kisiasa
unaochochewa na maswali magumu tuliyoyataja mwanzo hautalifikisha mbali taifa
hili, badala yake utaliangamiza. Ilivyo, sasa Zanzibar inaumwa; tena ni
mahututi kitandani.
Kauli
tata na hasi za baadhi ya viongozi kwamba “Uhuru wa Zanzibar hauwezi
kukabidhiwa kwa yeyote kwa njia ya sanduku la kura”; au kwamba, “kama
lolotelisilotarajiwa (kushindwa uchaguzi) litatokea, tuko tayari kutumia silaha
za Mapinduzi ya 1964 kwani CCM Zanzibar wanazo funguo za sanduku la silaha
hizo”, zinachochea chuki na kuvuruga umoja wa kitaifa Zanzibar na kuzua tufani
kwa Muungano pia.
Kiongozi
bora ni yule anayeweza kuchukua hatua, hata kama hatua hizo hazitakuwa za
manufaa kwa Chama chake cha siasa, mradi tu ni za manufaa kwa nchi nzima; au
kuchukua hatua zinazogongana na matakwa ya wengi kwenye Chama chake, lakini ni
hatua sahihi kwa nchi. Hapa iwe ni nchi kwanza, siasa baadaye.
Kurudia
Uchaguzi Mkuu wote kama ZEC ilivyoamua, kwa sababu tu CUF kimeonekana kushinda
baada ya baadhi ya matokeo kutangazwa, hakutaifanyia mazuri Zanzibar, badala
yake kutakaribisha mtafaruku, chuki, hasira na pengine kuvunjika kwa amani. Kwa
utamaduni wa Kizanzibari ulivyo, haya si mambo magumu kuweza kuyang’amua.
Kwa
mantiki hii, tunapenda kuamini kwamba viongozi wa CCM na CUF Zanzibar pamoja na
ZEC ni watu wazima, wenye akili timamu kuweza kuiweka Zanzibar ya kwanza rohoni
mwao badala ya matakwa yao binafsi au yale ya vyama vyao na marafiki zao.
Hatutaki
umwagaji damu wa mwaka 1961 na 2001 ujirudie kwa kuziba masikio kukidhi
matakwa, uchu na uroho wa madaraka wa “wateule” wachache Visiwani. Mungu
ibariki Zanzibar na Wazanzibari wote.
Tufuatilie
mtandaoni:
Wasiliana
na mwandishi
Joseph
Mihangwa
jmihangwa@yahoo.com
+255-713526972
MAONI YA PROF. IBRAHIM NOOR
MAONI YA PROF. IBRAHIM NOOR
Ndugu Mihangwa,
Nakupa kongole kubwa sana kwa mengi ya ukweli uliyoyaelezea katika makala yako hii. Pahala pamoja hujafanya hivyo -- pale ulipoandika kuwa ni Karume aliyetaka washirikiane baina ya ZNP na ZPPP pamoja na ASP -- Si kweli. Ukweli ni kuwa, walipokuwa London pamoja, Karume ndiye aliyeombwa na ZNP na ZPPP akubali waunde Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuwa ASP watapewa nyadhifa za uwaziri na "Veto Power" alisema ni fikra nzuri na atajibu siku ya pili, lakini, inasemekana, baada ya kushauriana na Julius Kambarage Nyerere, akakataa. Kumbe Kambarage alikuwa ameshapanga mikakati yake ya kuivamia Zanzibar (Kitendo ambacho kiliwaulisha Wazanzibari wengi sana) na kumuahidi Karume kuwa atampa khatamu zote za serikali.
Sheikh Thabit Kombo, ambaye alikuwa katibu Mkuu wa Chama cha Afro-Shirazi anatutuelezea yafuatayo katika ukurasa wa 124 wa kitabu kiitwacho Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha:
Baada ya majadiliano marefu serikali ya Uingereza ilitaka vyama vyote vitatu, ASP, ZNP, na ZPPP viungane kuunda serikali. Wenzetu Hizbu wakalikubali haraka haraka pendekezo hilo, na kupendekeza kutoa nafasi 3 kati ya 9 za Uwaziri. Lakini Afro-Shrazi wakayakataa kabisa mapendekezo hayo; wakasisitiza uchaguzi tu. Hivyo Mkutano wa Katiba ukamalizika huko Uingereza bila ya mafanikio yoyote ya kupata Serikali ya Ndani wala Uhuru za Zanzibar.Na katika sehemu yenye anuani ya “Mkutano wa katiba, 1963”, kurasa 128 na 129, Katibu Mkuu wa ASP anazidi kufafanua ni nani walioikataa serikali ya umoja wa kitaifa na kwa maneno yake mwenyewe anamaliza sehemu hiyo kwa kusema: “Lakini wazo la serikali ya mseto wa Afro-Shirazi kushiriki tulilikataa tena kata kata.”
Sheikh Aman Thani, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa ZNP naye pia anaelezea katika ukurasa wa 45 wa kitabu chake kiitwacho Ukweli ni HUU haya yanayofuata:
[…] Waongozi wa upande wa Serikali, walipoona waongozi wa upande wa Upinzani hawataki kubadili msimamo wao, walijaribu kuzungumza nao nje ya mkutano. Katika mazungumzo hayo, upande wa Serikali waliutaka upande wa Upinzani wakubali kufanyika serikali ya pamoja, yaani "Government of National Unity" (hii ni mara ya pili ASP kupewa shauri na wenzao ZNP/ZPPP kufanya serikali ya pamoja.) Katika serikali hiyo ya pamoja, upande wa Serikali watawapa ASP wizara tatu kati ya wizara nane na pia watawapa uwezo wa kutumia "veto" kwa jambo lolote litalotokea nao wakaliona si maslahi kwa upande wao. Yaani ASP watakuwa na madaraka sawa sawa na ZNP/ZPPP katika uendeshaji wa hiyo serikali ya pamoja. Waongozi wa AfroShirazi baada ya kuyasikia hayo, walitaka muda wa kuyazungumza na kuyazingatiya wakiwa peke yao, na waliahidi kutoa uamuzi wao siku ya pili kabla ya kuhudhuria kwenye kikao cha mkutano wa Katiba. Kwa dalili zote, walionesha kuwa wamevutika na mashauri hayo, na ilikuwa kuna tamaa kuwa watawafik. Upande wa Serikali walingojea kwa hamu na matumainio (pia na wasi wasi) kuwa shauri waliyoitoa itakubaliwa au sana watataka wazidishiwe wizara moja badala ya tatu ziwe nne, yaani wawe wao ASP na wizara nne na ZNP/ZPPP wizara nne. Wakati ulipofika siku ya pili, waongozi wa ASP wakiongozwa na Sheikh Karume walifika kwa Mawaziri. Walikataa hata kukaa kitako, Karume alisema, “Tumeyazingatia mashauri yenu. Mazuri! Lakini sisi hatutaki kushirikiana na nyinyi!” Wakazunguka wakatoka.
Na Sheikh Ali Muhsin Al Barwani, ambaye alikuwa Waziri na kiongozi wa ZNP, naye pia anazungumzia hayohayo katika ukurasa wa 43 wa kitabu chake kiitwacho Conflicts and Harmony in Zanzibar.
Ndugu yetu Mihagwa, "Msema kweli ni kipenzi cha Mungu" nawe inaonesha unaelekea huko.
Kila la kheri
Ibrahim Noor
No comments:
Post a Comment