Saturday, 19 March 2016

MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE ALIPOZUNGUMZA TATIZO LA UDINI TANGANYIKA 1962


Haiwezekani kuielewa ahadi ya Nyerere katika haki na usawa kwa raia wote kama alivyoahidi wakati wa kudai uhuru, hadi usome hotuba yake aliyoitoa tarehe 10 Desemba, 1962 katika Bunge wakati Tanganyika inakua jamuhuri. Hotuba ya Nyerere ilijikita kwenye matatizo ya upogo kati ya Waislam na Wakristo. Nyerere alifanya hivi labda akijua kuwa ingawa yeye alikuwa Rais Mkatoliki lakini waliomuweka madarakani kuitawala Tanganyika walikuwa Waislam. Nyerere alikuwa na haya ya kusema:

Hakuna njia nyepesi ya kuondoa tafauti baina ya raia wetu Waafrika na wasio Waafrika; hakuna njia nyepesi ya kuondoa tofauti za elimu kati ya Wakristo na Waislam, au baina ya wachache wenye elimu na wengi wa watu wetu wasio kuwa na elimu; hakuna njia nyepesi ambayo Wamasai na Wagogo wanaweza wakalingana na Wahaya na Wachagga na Wanyakyusa.

Hii ilikuwa kauli ya serikali ya kudhihirisha nia yake njema. Kauli hii ilikuwa ya kuwapa matumaini na kuwahakikishia Waislam na wale wote walioathirika na dhulma ya wakoloni, kuwa serikali ilikuwa inatambua shida zao na itachukua hatua zifaazo kurekebisha hali hiyo. Wakati Nyerere anatoa kauli hii ya kutia moyo, serikali iliyokuwa imejaa viongozi wa Kikristo na taasisi za Kikristo zilikuwa imejaa hofu wakiogopa harakati za Waislam za kujiletea maendeleo zilizokuwa zinatapakaa nchi nzima kwa kasi. Walifahamu fika nguvu na umoja wa Waislam ukitumiwa vyema hapana shaka Waislam watakuja juu. Kwa viongozi wa Kikristo waliokuwa wameshika madaraka ya serikali hii ilimaananisha kugawana madaraka sawa na Waislam, kwao wao harakati hizi mpya ziliashiria kuanguka kwa himaya yao katika madaraka kama viongozi.

(Kutoka: Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 – 1968)…)

No comments: