Tuesday, 29 March 2016

ZITTO ZUBERI KABWE AZUNGUMZA : ''KILA MCHUMA JANGA HULA NA WAKWAO''


Mbunge wa
      Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

Wakati Serikali ya Tanzania ikiwa bado imepigwa bumbuwazi baada ya Bodi ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) kuzuia msaada wa awamu ya pili wa jumla ya shilingi trilioni 1 sawa na Dola za Marekani milioni 472.8, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe ameibuka na kudai kuwa hatua hii ni matokeo ya ubabe wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mheshimiwa Zitto ametumia ukurasa wake wa Facebook kuelezea hisia zake huku akielekeza lawama zote kwa CCM na kuwasihi watu wa Zanzibar kuendelea kuwa na subira kwani kamwe Mola hatawatupa.

Zitto ameandika kama ifuatavyo, “Uzalendo ni kutaka haki ya kidemokrasia Zanzibar. Haki ya Wananchi waliochagua viongozi wao Oktoba 25, 2015. Sitakubali kuvishwa koti la uzalendo kwenye suala la MCC. Hilo ni suala la CCM, kukosa misaada ya Marekani ni matokeo ya ubabe wa CCM kuhusu Zanzibar. Haina mahusiano yeyote na Uhuru wa Nchi yangu. Nawasihi Wazanzibari wawe na subra Mola kamwe hatawatupa. Haki itapatikana tu. #DemokrasiaTu. Nawasihi Watanzania kuelewa kwamba CCM ndio imetufikisha hapa na iubebe mzigo huu bila kuufanya ni mzigo wa Nchi.”

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Bodi ya MCC, hatua hii imekuja kufuatia uchaguzi wa marudio uliofanyika visiwani Zanzibar Machi 20, huku ikidaiwa kuwa uchaguzi huo haukushirikisha watu wote na pia haukuakisi maoni ya walio wengi licha ya malalamiko kutoka Serikali ya Marekani na Jumuia ya Kimataifa.

Vilevile bodi hiyo imesema sababu nyingine ya kusitisha msaada huo ni baada ya serikali ya Tanzania kushindwa kuchukua hatua za kuhakikisha kuheshimiwa kwa uhuru wa kujieleza na uhuru wa kujumuika katika utekelezwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao.

Zitto Zuberi Kabwe na Mwandishi

No comments: