Ukristo
ni dini mpya Tanzania kwa kuwa uliingizwa katika karne ya kumi na nane na
wamisionari. Kanisa na Mwafrika Mkristo ni matokeo ya ukoloni. Kwa ajili hii basi historia ya Kanisa katika
Afrika ni ile ya kuhirikiana na kuwa tiifu kwa serikali ya kikoloni. Chini ya
ukoloni, taratibu Kanisa likaweza kujenga uhusiano maalum kati yake na serikali
pamoja na Mkristo Mwafrika ambae imemuelimisha katika shule zake. Mwafrika
Mkristo akawa ananufaika na mfumo wa kikoloni. Waislam wakawa wanataabika kwa
kuwa dini yao ilikuwa inapingana na dini ya mtawala. Mwafrika Mkristo akawa
mnyeyekevu kwa serikali wakati wa ukoloni na baada ya kupatikana kwa uhuru
akaja kushika madaraka ya serikali. Waislam wakatengwa na kuteswa katika ukoloni
kwa kubaguliwa na kunyimwa elimu hivyo kuwaondolea fursa ya maendeleo. Kuwepo
kwa Waislam kama raia na ili kuinusuru dini yao ilibidi Waislam wasimame
kuutokomeza ukoloni. Baada ya uhuru Kanisa likabaki na msimamo wake wa enzi ya
ukoloni wa kutii na kujipendekeza kwa serikali mpya iliyokuwa madarakani.
Ushirika huu kati ya Kanisa na serikali, uliojengwa na tabia ya Kanisa ya
kukubaliana na mfumo wowote wa serikali ulililelewa vyema na umeisaidia sana
Kanisa. Kanisa likaweza kujijengea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zake
bila ya kipingamizi wala wasiwasi. Kutokana na uhusiano huu maalum Kanisa
likajifanyia msingi imara wenye nguvu
kutokana wa Wakristo waliowasomesha katika shule zao. Kanisa likatumia
nafasi na uhusiano huu kwanza na serikali ya kikoloni kisha na serikali ya
wananchi kujijengea himaya ambayo wafuasi wake wakaja kushika nafasi zote
muhimu katika uongozi wa juu wa serikali, bunge na mahakama katika Tanzania.
Katika miaka yake mia moja tu Kanisa likaweza kupata safu yake ya viongozi
ambao wanadhibiti kila sekta katika jamii ya Watanzania.
Waingereza
walipoja kuitawala Tanganyika (kama Tanzania inavyojulikana) baada ya
kuondoka Wajerumni baada ya Vita Kuu ya
Kwanza, Wajeruamani walikuwa wameshafanya kazi ya kutosha ya kuiweka Tanganyika
ndani ya mamlaka mbalimbali za Kikristo. Tanganyika ilikuwa imegawanywa katika
mamlaka mbalimbali za Kikristo kutoka nchi tofauti za Ulaya. Kanisa Katoliki
ambalo ndilo lenye nguvu zaidi, lilikuwa tayari limeshajikita Tanganyika. White
Fathers walikuwa wapo Tabora, Karema, Kigoma, Mbeya, Mwanza na Bukoba; Holy
Ghost Fathers walikuwa Morogoro na Kilimanjaro; Benedictine Fathers walikwepo
Peramiho na Ndanda; Capuchin Fathers walikuwepo Dar es Salaam; Consolata Fathers
walikuwepo Iringa na Meru; Passionist Fathers walikuwa Dodoma; Pallotine
Fathers walikuwa Mbulu; Maryknoll Fathers walikuwapo Musoma; na Rosmillian
Fathers walikuwa Iringa.
Wamisionari
hawa walipotia mguu pwani ya Afrika ya Mashariki, nia yao hasa ilikuwa kuufuta
Uislam. Wakazi wa pwani hii iliyokuwa ikijulikana kama Zanj waliuona Ukrsto kwa
mara ya kwanza kabisa mwaka 1498 Wareno walipofika sehemu hizo. Mwaka 1567
wamishionari wa Augustinian waliingia Afrika ya Mashariki ili kupambana na
Uislam ili Ukristo uwe dini ya dunia nzima. Kadinali Lavigirie alianzisha The
White Fathers, taasisi ya Kanisa Katoliki kwa kusudi maalum la kuupiga vita
Uislam Wakati huo huo Church Missionary Society (CMS) ilikuwa imjitwisha kazi
ya kuondoa ulimwengu kutokana na Uislam, ujinga na giza. Hadi hii leo White
Fathers wapo Tanzania wapo Tanzania wakiendelea kufanya kazi iliyowaleta
Tanganyika zaidi ya miaka mia iliyopita.
Wajerumani
walipofika Tanganyika waliwakuta Waislam wanafahamu kuandika, kusoma na
walikuwa wameelimika katika hesabu. Mmishionari Ludwig Krapf alipofika kwa
Chifu Kimweri wa Usambaa mwaka 1848 alimkuta yeye na wanae wote wanajua kusoma.
Herufi walizokuwa wakitumia zilikuwa za Kiarabu. Wajerumani kwa ajili hii basi
waliwaajiri Waislam kama walimu, wakalimani na makarani serikalini. Wamisionari
na wakoloni waliona wivu kwa maendeleo haya waliyoyakuta kwa Waislam. Kubwa
zaidi ni kuwa walikuwa wamekuja kustaarabisha watu ëwashenzi' badala yake
wamewakuta watu walistaaarabika na wanye utamaduni wa kupendeza. Elimu hii yote
na utamaduni huu wa hali ya juu ulikuwa unatokana na Uislam na shule zake na
madras. Hapo ndipo zilipoaanza mbinu ya kuvunja maendeleo haya yote.
Herufi
za Kiarabu zikapigwa marufuku kutumika na badala yake watu wakalazimishwa
kujifunza herufi za Kirumi. Muislam ambae jana alipoingia kulala alikuwa
anaitwa ameelimika akaamka asubuhi yake mjinga, hana elimu, hajui kusoma wala
kuandika. Njama hizi zote dhidi ya Uislam ilikuwa sehemu ya makubaliano kama
ilivyoandikwa katika kifungu IV cha
Mkutano wa Berlin wa mwaka 1884. Kifungu hicho kilikuwa kinasema kuwa Ukristo
ni lazima ulindwe dhidi ya Uislam. Kati
ya mwaka 1888-1892 katika kutekeleza kifungu hicho kama ilivyokubalika katika
Mkutano wa Berlin, Imperial British East Africa Company ilitumia nguvu za
kisiasa na kijeshi kuulinda Ukristo katika Afrika ya Mashariki. Ombwe lililoachwa na elimu ya Kiislam
ikajazwa na elimu ya Kanisa chini ya usimamizi wa Waingereza. Kanisa hivi sasa
linaeneza uongo na propaganda kuwa lenyewe ndilo lililoweka msingi wa kwanza wa
elimu Tanganyika. Ukweli ni kuwa Wamisionari walifuata nyayo za madras na
walimu wa kwanza katika shule za misheni walikuwa Waislam ambao hawakusoma
katika shule za kanisa bali katika madras. Kwa kipindi cha zaidi ya miaka mia
moja Kanisa likaelekeza nguvu zake katika katika kuwatayarisha raia ambao wengi
wao walikuwa Wakristo, watakaokuwa watiifu kwa Kanisa na serikali. Ni katika
mtandao huu ndiyo Wakristo wanaimiliki serikali na Chama Cha Mapinduzi na
kuiamrisha ifanye linavyopenda Kanisa, wakati Waislam na Uislam ukifanywa kama
vitu visivyokuwa na maana yoyote.
Hadi
kufikia mwaka wa 1960 Kanisa likawa taasisi kubwa inayomiliki mamilioni ya dola
ya misaada inayopokelewa kutoka wahisani na wafadhili walioko katika ulimwengu
wa Kikristo. Kanisa sasa hivi linahodhi mahospitali, misururu ya ndege binafsi,
viwanja vya ndege, makampuni ya uchapaji na mitambo ya kupiga chapa, stesheni
za radio na magazeti. Kanisa limekuwa na nguvu na udhibiti wa mambo kiasi
kwamba wakati mwingine watendaji, hasa Wakristo katika serikali na ndani ya
chama tawala CCM hawajui utii wao upo kwa nani, serikalini au katika
Kanisa? Ni katika kuchanganyikiwa huku
kwa watendaji wa serikali kuhusu uhusiano wao na Kanisa na serikali ndiko kulikoamsha
kutoaminiana kati ya Waislam na serikali mara tu baada ya uhuru kupatikana.
Serikali ikaonekana kama moja ya taasisi za Kanisa na Waislam wakiwa ni
watazamaji tu. Mara baada ya uhuru Kanisa likaangalia nafasi yake na serikali
mpya iliyokuwa madarakani. Wakati wa kudai uhuru Kanisa lilijiweka mbali na
siasa na ikaonekana kuwa Kanisa lilikuwa likiheshima ule mpaka kati ya dini na
siasa. Wakati ule mgongano kati ya
Kanisa na serikali haukupata kusikika hata kidogo. Baada ya uhuru
kupatikana tu na serikali ikawa mikononi mwa wananchi, Kanisa likaanza kusikika
likisema kuwa lina haki na wajibu kuwa na ushawishi ndani ya serikali, kuikosoa
serikali na kuingooza pale inapoona serikali haifanyi mambo sawa kwa matarajio
yake. Katika msimamo huu mpya, Kanisa likajipa fursa ya kuwa msemaji wa watu.
Huu ulikuwa ni mwelekeo mpya katika mambo ya siasa na utawala.
Katika
Uislam siasa na dini ni kitu kimoja. Vitu hivi viwili havitenganishwi. Lakini
mwaka wa 1955 wakati wa siku za mwanzo kabisa za TANU, tuliona jinsi Waislam
katika TANU walivyoweza kukiogoza chama katika misingi ya kisekula na utaifa
ili kulinda umoja wa wananchi.. Kutochanganya dini na siasa ikawa moja ya
maadili makuu ya TANU. Kuanzia hapa ndipo sasa tunaweza kuelewa mapambano kati
ya Waislam kwa upande mmoja na serikali na Wakristo kwa upande wa pili
yalivyokuja kigubika Tanganyika mara baada ya uhuru.
No comments:
Post a Comment