Monday, 21 March 2016

SHEIKH PONDA ISSA PONDA ALIPOMTEMBELEA MZEE BILAL REHANI WAIKELA


Kushoto Mzee Waikela na Sheikh Ponda

Bilali Rehani Waikela 1963

Ni maneno niliyoandika mimi mwenyewe mwaka wa 1987 kutokana na nyaraka na mahojiano na Mzee Waikela. Lakini kila ninapoisoma historia ya Mzee Waikela nahisi kama ndiyo kwanza leo nakutana na maandishi haya. Wakati mwingine nahisi machozi yananilengalenga. Nakunyambulia kidogo na wewe usome labda utapata hisia kama zangu:

‘’Jaribio la mwanzo la Nyerere kutaka kuivunja EAMWS lilikuwa mwaka 1963. Lakini jaribio hilo halikufanikiwa kwa sababu ya mpango uliopangwa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir na kutekelezwa na Bilali Rehani Waikela, katibu wa EAMWS Tabora. Mwaka huu wa 1963 EAMWS ilifanya mkutano wake katika ukumbi wa Shule ya Wasichana ya Aga Khan. Wajumbe wa mkutano huo walipowasili mjini Dar es Salaam walikuta uvumi kuwa wajumbe wa mkutano wa EAMWS watakamatwa na kuwekwa kizuizini. Chanzo cha uvumi huu hakikufahamika lakini haikuwa vigumu kuhisi. Baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wazee wa TANU mwaka ule ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa amewatupa mkono washirika wake wa zamani na sasa alikuwa akitafuta wapya ili kujenga upya msingi wake wa siasa. Kutokana na mambo yalivyokuwa yakienda ilikuwa ni dhahiri washirika wake wapya hawatakuwa Waislam.

Katibu wa EAMWS Tabora, Waikela alipowasili Dar es Salaam kuhudhuria mkutano aliitwa na Sheikh Hassan bin Amir. Mufti Sheikh Hassan bin Amir mbele ya Mzee Ali Comorian, alimfahamisha Waikela kuwa kulikuwa na njama zilizokuwa zikipikwa na Nyerere kumuungamiza yeye na Tewa Said Tewa ili kuvunja EAMWS ipatikane nafasi ya kuanzishwa jumuiya ya Kiislam ya Watanganyika itakayokuwa chini ya wanafiki. Sheikh Hassan bin Amir alimwambia Waikela kuwa harakati za uhuru zilikuwa zinatekwa nyara na Wakristo kwa manufaa ya makanisa yao. Sheikh Hassan alimfahamisha Waikela kuwa ni lazima yeye afanye kila linalowezekana ili njama za Nyerere zishindwe. Waikela alimuuliza Sheikh Hassan bin Amir kwa nini amechaguliwa yeye kufanya kazi ile. Sheikh Hassan bin Amir alimuambia kuwa yeye ana imani na uwezo wake. Baada ya maneno hayo Sheikh Hassan bin Amir alinyanyua mikono yake juu na kumuombea dua Waikela. Nyerere alikuwa anamfahamu Waikela  kwa kuwa alikuwa muasisi wa TANU na alikuwa ametoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru wa Tanganyika.’’

(Kutoka: Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes 1924-1968 Historia Iliyofichwa Kuhusu Harakati za Waislam Dhidi ya Ukoloni wa Waingereza, Phoenix Publishers, Nairobi, 2002)


Wa mwisho kulia ni Tewa Said Tewa

Sheikh Ponda Issa Ponda Msikiti wa Kichangani 2012


Picha hiyo hapo juu ya Sheikh Ponda inamuonesha yuko mbele ya kibla cha Msikiti wa Kichangani. Ilikuwa mwaka wa 2012 baada ya sala ya Ijumaa Waislam walipopanga kuandamana kuhusu Dr. Joyce Ndalichako aliyekuwa kiongozi mkuu wa NECTA (Baraza la  Mitihani Tanzania). Waislam walikuwa wanamtuhumu kwa kuwahujumu wanafunzi wa Kiislam wasipate elimu ya juu. Maandamano yalikuwa hayana kibali cha Polisi lakini Sheikh Ponda aliwaambia Waislam kuwa wataandamana bila ya kibali kudhihirisha dhulma hii kwa serikali hata kama hakuna kibali. Aliendelea na kuwaambia Waislam kuwa, ''Ikiwa hatutaandamana katika hili tutaandamana kwenye lipi? Sheikh Ponda kujua uzito wa hilo jambo la maandamano bila kibali aliwahakikishia Waislam kuwa yeye atakuwa mbele kuongoza maandano yale. Kabla ya kuanza maandamano Sheikh Ponda alisimama mbele ya msikiti kisha akaelekea kibla na akanyanyua mikono yake juu kumkabili Allah kutaka msaada wake na akaanza kusoma Surat Yasin…moyo wa Qur’an. Alipomaliza aliongoza maandamano kuelekea Kidongo Chekundu huku maandamano yakiwapita askari waliokuwa wametanda Barabara ya Morogoro. Maandamano yalifika salama Kidongo Chekundu. Umma uliofurika Kidongo Chekunde siku ile hausemeki. Ujumbe wa Waislam dhidi ya Dr. Ndalichako ulikuwa umefika.



Mzee wa Waikela na Sheikh Ponda wameishi nyakati tofauti sana lakini kinachowaunganisha ni kitu kimoja – kupigania haki za Waislam wa Tanzania. Mapambano haya sasa ni zaidi ya nusu karne.  Hivi leo yule yule Dr. Joyce Ndalichako ambae Waislam walimlalamikia kuwa anawadhulumu watoto wao na wakafanya maandamano dhidi yake ndiye aliyechaguliwa kuwa Waziri wa Elimu.



No comments: