SERIKALI ya Umoja wa Kitaifa (SUK) katika Visiwa vya Zanzibar imefikia tamati, anaandika Yusuph Katimba.
Uchambuzi wa kisheria
unaonesha kuwa utawala wa sasa wa Zanzibar haufuati katiba, na kwamba hata kama
ingefuatwa, haiwezekani tena kuwa na SUK, kutokana na mazingira ya kisiasa
yaliyojengwa kati ya tarehe 25 Oktoba 2015 na 20 Machi 2016.
Tundu
Lissu, wakili wa mahakama kuu, anaamini kwamba Zanzibar sasa hivi inatawaliwa
kwa mtutu badala ya katiba; akiungwa mkono na Awadhi Ali Said, Wakili wa
Mahakama Kuuu Zanzibar.
Lissu
anasema: “Hakuna hoja ya kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar kwa
kuwa serikali haifuati katiba. Hakuna jambo lolote Zanzibar linalofanywa kwa
kufuata Katiba, Zanzibar inaendeshwa kwa mtutu wa bunduki.
“Serikali
ya Umoja wa Kitaifa ni ya Chama Cha Mapinduzi na Chama cha Wananchi – CUF, na
wala si ya ADC na vyama vingine vinavyosindikiza.
“CCM
na haiwezi kufuata lolote kuhusu Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Inafanya namna
inavyoweza. Kama serikali ingekuwa inafuata katiba basi Maalim Seif (Maalim
Seif Sharif Hamad) angekuwa Rais wa Zanzibar.
“Haiwezekani
kuwepo kwa serikali hiyo kwa kuwa uchaguzi huo (wa 20 Machi 2016) ulikuwa
haramu, uliitishwa na tume haramu, chini ya serikali haramu.
“Hakuna
kitu kinachoitwa Serikali ya Umoja. Tume haramu, uchaguzi haramu, na
ulisimamiwa na serikali haramu. Chochote kinachofanywa kwa sasa ni haramu.”
Naye
Said anasema katiba inaelekeza kuwa lazima chama kitakachoingia kwenye serikali
kiwe na asilimia kuanzia 10 na kuendelea.
“Kama
hakuna chama kilichofikisha asilimia hizo, basi chama cha pili chenye
wawakilishi wengi wa majimbo ndio kitakachotoa makamu wa kwanza wa rais.
“Sasa
hapa utawezaje kuunda serikali ya umoja wa kitaifa? Kama serikali inayoundwa
itaachana na vyama vingine hakutakuwa na serikali ya namna hiyo,” amesema.
Kuhusu
hoja kama itabidi serikali ya sasa ibadili katiba ili kufuta rasmi SUK,
anasema: “kubadilisha katiba nako hakuwezi kufanikiwa kwa kuwa serikali
haijakamilika. Hakuna Makamu wa Kwanza wa Rais anayekubalika kwa Katiba ya
Zanzibar. Maana yake ni kwamba huwezi kupeleka muswada katika Baraza la
Wawakilishi ili baadaye iitishwe kura ya maoni.”
Anasema
uchaguzi wa marudio Zanzibar haukukidhi matakwa ya katiba ya Zanzibar, kwa hiyo
kila kinachofanywa na serikali ya sasa ni batili.
Zanzibar
imeingia katika mgogoro mpya wa kisiasa tangu 28 Oktoba 2015, baada ya Jecha
Salim Jecha, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kufuta matokeo ya
uchaguzi ambayo yalikuwa yanaelekea kumpa ushindi Maalim Seif Sharrif Hamad wa
Chama cha Wananchi (CUF).
Jecha
hakuwa na mamlaka ya kikatiba kufuta uchaguzi huo, na taarifa zinasema
alishurutishwa na vyombo vya dola vilivyoamriwa na Dk. Ali Mohamed Shein,
aliyekuwa anagombea tena kiti hicho akiwa rais.
Hatimaye,
Jecha alitangaza kuwa uchaguzi huo ungefanyika tarehe 20 Machi 2016. CUF
kilisusia uchaguzi huo, kukafanyika uchaguzi wa upande mmoja ulioshirikisha CCM
na vyama vidogo vilivyo upande wa CCM na visivyo na wafuasi Zanzibar, chini ya
ulinzi mkali wa majeshi.
Katika
matokeo ya uchaguzi huo wenye utata, Dk. Ali Mohamed Shein wa CCM alitangazwa
mshindi kwa kupata kura 299,982 (91.4%) akifuatiwa na Hamad Rashid Mohamed wa
ADC kwa kura 9,734 (3.0%).
Katiba
ya Zanzibar inasema akishapatikana rais, anayemfuata kwa kura, iwapo atakuwa
amefikisha walau asilimia 10 ya kura, ndiye atakuwa makamu wa kwanza wa rais,
akitoka chama cha upinzani.
Katika
uchaguzi wa Machi 20 hakuna mgombea aliyefikisha asilimia 10. Hivyo, kikatiba,
haitawezekana kumpata makamu wa kwanza wa rais kutoka upinzani; na hivyo SUK
itakuwa imefikia tamati.
Chanzo: MwanaHalisi
Online, 29 Machi 2016
No comments:
Post a Comment