NASAHA ZANGU KWA
WAZANZIBARI WENZANGU
Na Ismail Jussa
Tarehe 5 Novemba,
2009 daima itakumbukwa kuwa ni siku ambayo nchi yetu iliandika historia mpya
pale viongozi wawili wazalendo na mashujaa, Dr. Amani Abeid Karume na Maalim
Seif Sharif Hamad, walipowaongoza Wazanzibari kufikia MARIDHIANO.
Haikuwa kazi rahisi
lakini kwa kuongozwa na hisia za uzalendo na mapenzi kwa nchi yao na wananchi
wenzao, Dr. Karume na Maalim Seif waliamua kujitolea kuongoza enzi mpya za
siasa. Walijua kwamba katika vyama vyao viwili, CUF na CCM, wapo watu ambao
wasingewaunga mkono na pengine wangeyatumia MARIDHIANO yale kutaka kuwahujumu
kisiasa viongozi hao. Na kweli walikuwapo watu wa aina hiyo na wapo hadi leo.
Kwa kutambua kuwa
watu waovu wasiopendelea umoja na masikilizano miongoni mwa Wazanzibari
watakuja kusema kuwa MARIDHIANO hayo yalikuwa ni maamuzi ya watu wawili tu na
hayawakilishi matakwa ya watu, Dr. Karume alipendekeza kwa Maalim Seif kukubali
rai ya kufanya kura ya maoni ili kupata ridhaa ya Wazanzibari kuhusiana na
mwelekeo huo mpya wa siasa na hasa kuhusu haja ya kuanzisha muundo wa Serikali
ya Umoja wa Kitaifa.
Tarehe 31 Julai,
2010 ikafanyika kura ya maoni ya kwanza katika historia ya Zanzibar. Asilimia
66.4 ya Wazanzibari wakapiga kura ya NDIYO kuchagua MARIDHIANO na muundo wa
Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Baada ya maamuzi hayo ya Wazanzibari ndipo Baraza
la Wawakilishi likafanya Marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar na kuingiza
muundo huo ndani ya Katiba.
Maamuzi hayo ya
Wazanzibari yalikuwa na maana kubwa sana kwa nchi yetu na watu wake. Kwa kupiga
kura ya NDIYO, Wazanzibari tulichagua maridhiano na kukataa mfarakano,
tulichagua umoja na kukataa mgawanyiko, tulichagua upendo na kukataa chuki,
tulichagua matumaini na kukataa khofu, tulichagua amani na kukataa fujo.
Inasikitisha kwamba
miaka sita baadaye wale waovu miongoni mwetu ambao hawakutaka MARIDHIANO
(wakiwemo wale ambao kwa dhahiri walijionesha kuyaunga mkono kwa sababu tu
walitaka kulinda ulwa wao kwa kumridhisha Rais aliyekuwa madarakani lakini kwa
siri wakiyapinga) wameturudisha kule kule kwenye mfarakano, mgawanyiko, chuki,
khofu na fujo.
Lakini pamoja na
juhudi hizo ovu za kuturudisha tulikotoka, ukweli mmoja unabaki kwamba
Wazanzibari wengi hawako tayari kurudishwa huko. Wazanzibari wameona faida ya
siasa za MARIDHIANO, UMOJA, UPENDO, MATUMAINI NA AMANI.
Binafsi, bado
naamini kwamba MARIDHIANO, UMOJA, UPENDO, MATUMAINI NA AMANI vitashinda.
Wazanzibari ni watu wema. Kutokana na wema wao, watachagua WEMA dhidi ya UOVU.
Kwa sababu hizo
basi, NATOA NASAHA ZANGU KWA WAZANZIBARI WENZANGU kwamba tukatae njama zote za
kuturudisha tulikotoka. Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na watu WAOVU
ambao wamekuwa wakiandika maneno ya ovyo na matusi katika mitandao ya kijamii.
Wengine ni watu wazima ambao ungetegemea kwa umri wao wangeonesha mfano mwema
kwa kizazi cha leo. Bahati mbaya, baadhi ya vijana wameingia kwenye mtego wa
WAOVU hao na kujibizana nao kwa matusi na lugha zinazoturudisha kwenye
mfarakano, mgawanyiko, chuki na ubaguzi, mambo ambayo tukiyakataa kupitia kura
ya maoni ya tarehe 31 Julai, 2010.
Nawapa NASAHA ndugu
zangu tukatae kuingia katika mtego huo. Tuoneshe kama SISI NI TOFAUTI NA WAO.
Tusijibu lugha zao za matusi, chuki na ubaguzi na sisi tukaandika lugha za
matusi, chuki na ubaguzi. Haitoonekana tofauti kati yetu. Tuithamini na
kuilinda kazi kubwa iliyofanywa na Dr. Amani Karume na Maalim Seif Sharif
Hamad.
TUNAYOPITIA
SASA NI MAJARIBU TU. TUSIKUBALI KUSHINDWA TUKARUDISHWA TULIKOTOKA. TUWAONESHE
WAOVU KWAMBA SISI NI WEMA. NA WEMA SIKU ZOTE HUUSHINDA UOVU.
No comments:
Post a Comment