Thursday, 24 March 2016

TAAZIA: SHEIKH TWAHIR HAYDAR MWINYIMVUA

Sheikh Twahir Haidar Mwinyimvua akizungumza na Mwandishi
katika Kipindi Maalum ''Walioacha Alama Katika Historia,'' TV Imaan




Mwaka wa 2012 TV Imaan iliniomba niendeshe kipindi cha historia ya Waislam Tanzania. Hii ilitokama na mahojiano ambayo nilifanya katika kipindi kilichoitwa, ‘’Ulimwengu wa Kiislam,’’ kipindi ambacho kilipendwa na watazamaji wengi sana. 

Tulitengeneza vipindi kadhaa Tanga, Zanzibar na Dar es Salaam kwa kufanya mahojiano na watu maarufu na kipindi changu nilikiita ‘’Walioacha Alama katika Historia ya Tanzania.’’ 

Katika mmoja wa watu niliofanyanao mahojiano alikuwa Sheikh Twahir Haydar Mwinyimvua. Sheikh Haydar huenda si wengi katika watu wa leo walimjua lakini yeye ni mtu maarufu kwa wenyeji wa Dar es Salaam kama alivyokuwa maarufu baba yake Sheikh Haydar Mwinyimvua, mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika TANU na mkono wa kulia wa Nyerere wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika. 


Sheikh Twahir Haydar amefariki tarehe 21 Machi 2016 nyumbani kwake Mwananyamala B. Sheikh Haydar umri wake wote amefanyakazi Kabidhi Wasii hadi alipostaafu kazi miaka michache iliyopita. 

Msaada wake katika ofisi hii ndiyo Waislam watamkumbuka daima. Kusajili taasisi yoyote ya Kiislam nchini petu ni kitu kigumu sana kuanzia mwaka wa 1968 pale BAKWATA ilipoundwa na kufanywa ndiyo kila kitu kwa Waislam. 

Sheikh Twahir juu ya matatizo yote yaliyokuwapo alijitahidi sana kuwaelekeza Waislam nini wafanye ili waweze kusajili taasisi zao. Hii haikuwa kazi nyepesi kwake kwani juu yake walikuwapo wakubwa zake kimadaraka ambao walifanya kila juhudI kuhakikisha kuwa taasisi za Kiislam hazipati tasjila. 

Mfano wa karibu sana ni pale mwaka wa 1992 Waislam walipotaka kusajili Baraza Kuu. Ala kuli hali wakati wa Rais Ali Hassan Mwinyi angalau mambo yalikuwa mepesi kidogo na kipindi hiki Waislam wengi watamkumbuka Sheikh Twahir  alivyowasaidia kusajili taasisi zao. 

Nilipofanya mazungumzonae mwezi Septemba 2012 kwa ajili ya kipindi cha televisheni nilimuomba tutoke katika kazi yake anieleze historia ya East African Muslim Welfare Society (EAMWS) baada ya kupigwa marufuku na serikali ya Nyerere mwaka wa 1968 na Sheikh Hassan bin Amir aliyekuwa Mufti wa Tanganyika kufukuzwa nchini. 

Sheikh Twahir  alinieleza mengi kuanzia maisha yao Kisutu Dar es Salaam yeye akiwa kijana mdogo akisoma Al Jamiatul Islamiyya Muslim School katika miaka ya 1950 na baba yake akiwa mmoja wa wanachama shupavu wa TANU. 

Alinieleza ushuba mkubwa uliokuwapo baina ya baba yake Sheikh Haydar Mwinyimvua, Sheikh Suleiman Takadir na Mwalimu Nyerere. Alinieleza kazi na mafanikio yaliyofikiwa na EAMWS na pigo Uislam uliopata baada ya kupigwa marufuku. 


Picha alonipa Sheikh Twahir Haydar ya viongozi wa EAMWS waliokuwa wakiratibu shule za Kiislam wakiwa na Waziri wa Elimu Nesmo Eliufoo ubavuni kwa Tewa Said Tewa aliyekuwa Mwenyekiti wa EAMWS. Kulia wa pili aliyesimama ni Muft Sheikh Hassan bin Amir


Sheikh Twahir siku ile alinitia chuoni kunisomesha na nilitoka na mengi. Hakika Sheikh Twahir ukimtoa Mzee Waikela hakuna aliyekuwa kamzidi katika kuifahamu historia ya EAMWS na shida zilizokuwakuta Waislam katika miaka ile. 

Bahati mbaya hadi leo vipindi vile vyote nilivyofanya TV Imaan haijavirusha kwa sababu kadhaa kubwa ni kufuatia kufungiwa Radio na TV Imaan kwa kipindi cha miezi sita kwa kile kilichojulikana kama kukiuka taratibu. 

Mpaka pale siku TV Imaan itakaporusha kipindi nilichofanya na marehemu Sheikh Twahir Haydar Mwinyimvua Waislam tutosheke na haya machache  niliyoeleza hapa. 

Tunamuomba Allah amsamehe madhambi yake na amuweke mahali pema peponi. 
Amin

Imaan 
Machi 24 -30, 2016



No comments: