Tuesday, 5 April 2016

HISTORIA YA JOMO KENYATTA NA ABDULWAHID SYKES 1950


Utangulizi

Leo nilipokuwa nikipitia gazeti la Mwananchi (Jumanne Aprili 5, 2016) nilikuta kipande hicho hapo chini kuhusu Jomo Kenyatta:

Si wengi wenye kuijua vyema historia ya harakati za uhuru wa Tanganyika. Hii imesababisha kwa historia hii kubaki kizani takriban sasa inakaribia miaka 70. Mpenzi msomaji nimeona baada ya kusoma na kuona kuwa leo ndiyo siku Jomo Kenyatta alihukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani ni aula nikaiadhimisha siku hii kwa kukunyambulia habari za Jomo Kenyatta kutoka vyanzo vya Tanganyika ya wakati ule.

Hapo chini nakunyambulia historia ya Jomo Kenyatta na Abdulwahid Sykes kama nilivyoandika katika kitabu changu, ''Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 - 1950)...''


''Mwaka 1950, Abdulwahid alisafiri kwenda Nairobi kukutana na Jomo Kenyatta ili kuanzisha uhusiano na Kenya African Union (KAU).Abdulwahid alifunga safari hii wakati wa mashindano ya kandanda ya Kombe la Gossage. Haya yalikuwa mashindano ya kila mwaka ambayo nchi tatu za Afrika ya Mashariki pamoja na Zanzibar zilikuwa zikishiriki. Huenda Abdulwahid alichagua wakati huu mahsusi ili kuficha dhamiri ya safari yake. Kama mtu labda angetaka kujua sababu ya safari yake ingewezekana kwa urahisi kabisa kuelezwa kuwa alisafiri kwenda Nairobi kutazama mashindano ya Gossage. Abdulwahid alifikia Railway Hotel na alikwenda kuonana na Kenyatta usiku akifuatana na rafiki yake mpenzi kutoka Zanzibar, mmoja wa wacheza mpira katika timu ya Zanzibar. Abdulwahid na rafiki yake walikwenda nje kidogo ya Nairobi kwenye nyumba moja iliyokuwa imegubikwa na giza na kuzungukwa na walinzi wa Mau Mau. Abdulwahid alikuwa anatarajiwa. Kenyatta alipofahamishwa kuwa Abdulwahid amefika na yupo nje, alitoka kumlaki. Kenyatta alikuwa akimfahamu Ally Sykes tangu mwaka 1946. Inawezekana kuwa kazi ya Abdulwahid ilirahisishwa na uhusiano huu wa Kenyatta na mdogo wake. Mzanzibari huyu aliyemsindikiza Abdulwahid alikutana na Kenyatta na wakapeana mikono. Baada ya kutambulishwa Kenyatta, Abdulwahid, Fred Kubai, Bildad Kaggia na Kungu Karumba waliingia kwenye chumba kingine ambako mkutano ulifanyika. Mzanzibari, rafiki yake Abdulwahid alibakia nje na mlinzi.


Timu ya Tanganyika iliyochukua kikombe cha Gossage mwaka wa 1949
Miaka mingi baadaye Mzanzibar yule, rafiki yake Abdulwahid na sasa akiwa ofisa mwandamizi serikalini alikutana na Rais Kenyatta Ikulu ya Nairobi wakati wa sherehe za uhuru wa Kenya mwaka wa 1963. Jambo la kustaajabisha ni kuwa Kenyatta alimkumbuka kuwa alifuatana na Abdulwahid kwenye ule mkutano pale Nairobi mwaka wa 1950.  Kenyatta aliyekuwa akizungumza Kiswahili kibovu chenye lafidhi nzito ya Kikikuyu alimkubusha juu ya ule mkutano. Alimwita mpiga picha wake na wakapiga ya pamoja. Picha hii inapamba sebule ya huyu mcheza mpira wa zamani hadi leo. Vilevile Kenyatta alimtunukia tai yenye rangi za taifa la Kenya.

Ajenda kuu ya mkutano huu ilikuwa namna ya kuunganisha harakati za wananchi wa Kenya na Tanganyika dhidi ya Waingereza. Wakati huo Wakikuyu walikuwa tayari wamekwishaanza mapambano ya silaha na majeshi ya Waingereza na hali ya siasa nchini Kenya ilikuwa ya wasiwasi sana. Inawezekana mkutano huu ulifanyika katika mtaa wa Eastleigh, sehemu ambayo mikutano mingi ya Mau Mau katika miaka ya 1950 kabla ya kutangzwa hali ya hatari ilikuwa ikifanyika.

Mwaka wa 1951 Kenyatta kwa mara nyingine aliitisha mkutano mwingine baina ya KAU na TAA mjini Arusha.  Katika ujumbe alioutuma kwa TAAw, Kenyatta alisisitiza kuwa uongozi wa chama cha TAA uende mkutanoni na silaha.  TAA iliwateua Abdulwahid, Dossa Aziz na Stephen Mhando kuhudhuria mkutano huo. Abdulwahid alikuwa na bastola aliyopewa wakati wa vita na ofisa mmoja mzungu kama zawadi. Ilitokea kuwa siku ya kuzaliwa ya Mzungu yule ilikuwa sawa na yake na kwa sababu yule mzungu akampa bastola yake kwa ukumbusho. Dossa Aziz alikuwa na bunduki iliyokuwa ikipiga risasi tano kwa mfululizo. Hajuijulikani kama Mhando alikuwa na silaha.

Wajumbe wa TAA walisafiri kila mtu peke yake kupoteza lengo. Dossa Aziz alikuwa wa kwanza kuondoka kuelekea Arusha kupitia Dodoma. Siku zile kulikuwa hakuna barabara ya moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha. Wasafiri waliotaka kwenda Arusha ilibidi wasafiri wapitie Dodoma. Dossa Aziz alifungasha ile bunduki yake ya risasi tano. Mjini Dodoma, Dossa Aziz alipokelewa na Mwalimu Ali Juma Ponda, katibu wa TAA Central Province. Baada ya kuelezwa na Dossa kuhusu ule mkutano wa TAA na KAU uliopangwa kufanyika Arusha, Ponda aliwaarifu Dossa Aziz  kuwa kulikuwa na mapigano makali kati ya Mau Mau na vikosi vya Waingereza yaliyosababisha  viongozi wa KAU kusakwa na kukamatwa. Ponda alimfahamisha Dossa kuwa ingelikuwa vigumu katika hali kama hiyo kwa Kenyatta na ujumbe wake kuja Arusha. Dossa Aziz aliamua kuvunja safari ya Arusha na kuelekea Mwanza kwa gari la moshi kukagua matawi ya TAA. Mjini Mwanza, Dossa Aziz alipokewa na Dr Joseph Mutahangarwa, makamu wa rais wa TAA katika kanda ya ziwa. 


Kushoto ni Ali Juma Ponda

Dr Mutahangarwa alikuwa Mwafrika wa kwanza kufuzu udaktari.  Baada ya kuelezwa kuhusu ule mkutano wa Arusha, Dr Mutahangarwa alimwonya Dossa kuhusu hatari ya mwenendo aliokuwa akichukua Abdulwahid kama katibu na kaimu rais wa TAA. Dr Mutahangarwa alimweleza Dossa hatari ambazo TAA na uongozi wake ungezikabili pindi serikali ikigundua kwamba TAA ilikuwa ikijaribu kuunganisha mapambano ya TAA na yale ya KAU. Hofu hii aliyoonyesha Dr Mutahangarwa ilikuwa bila wasiwasi wowote hofu ya kweli kabisa kwa sababu KAU ilikuwa inaunga mkono harakati za Mau Mau na Waingereza waliamini kuwa uongozi wa mapambano yale ulikuwa ukitoka KAU na Kenyatta wakiwa na Kaggia walishukiwa kuwa kati ya viongozi hao. Kutoka Mwanza Dossa alipanda meli hadi Bukoba ambako alipokewa na Chifu Rutinwa pamoja na mwanasiasa mkongwe, Ally Migeyo na Suedi Kagasheki  na wanachama wengine wa TAA katika tawi la Bukoba.


Ali Migeyo
Aliporudi Dar es Salaam, Dossa alikamatwa katika stesheni ya gari moshi na kupelekwa Central Police. Kituo hiki kilikuwa mkabala la lango kuu la steshini ya treni. Dossa alipelekwa pale na kuhojiwa. Ofisa wa polisi Mzungu alitaka kujua kwa nini Dossa alikuwa akisafiri na bunduki. Baba yake Dossa Aziz Ally aliingilia kati na Dossa akaachiliwa huru bila ya kufunguliwa shtaka lolote.''


Kushoto: Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdulwahid Sykes na Lawi Sijaona 1957
NB: Kuna mtu anatajwa kama rafiki ya Abdul Sykes nikimjulisha kama Mzanzibari. Wakati ule nilipokuwa naandika kitabu hiki hakutaka jina lake lijulikane. Hivi sasa yeye ni marehemu. Mtu huyu ni Ahmed Rashad Ali.


No comments: