Kwanza umenifurahisha kwa utulivu wako wa fikra na kuleta hoja kiungwana.
Kusema kuwa naandika udini labda mimi niwe sijui maana ya udini.
Kitabu cha Abdulwahid Sykes kimefanyiwa ''review,'' na wasomi maarufu duniani
katika historia ya Africa kama John Iliffe, Jonathon Glassman na James Brenan.
James Brenan na mimi Dar es Salaam
Hakuna hata mahali pamoja wamesema kuwa kuna udini ndani ya kitabu hicho.
Wote kwa umoja wao wamekubaliana kuwa ni kitabu kilichosahihisha historia ya
Tanganyika.
Hawa hawakuishia hapo.
Baadhi yao wamenialika kwenye vyuo vyao nikatoe muhadhara na nimekwenda na
kufanya hivyo.
Prof. James Giblin kanialika University of Iowa na niliitika mwaliko na nimezungumza
chuoni kwake.
Prof. James Gibblin na mimi Chuo Kikuu Cha Iowa
Prof. Jonathon Glassman amenialika Northwestern University Evanston, Chicago na
nimetoa muhadhara hapo chuoni kwake.
Dr. Kai Kresse wa Zentrum Moderner Orient (ZMO) aliniaika kwenye taasisi yake ya
utafiti katika historia Berlin, Ujerumani nimeitika mwito na nimezungumza hapo.
Kai Kresse na mimi Berlin
Hata katika maswali na majibu katika mihadhara hii yote hakuna hata mtu mmoja
aliyezungumza kuhusu udini katika maandishi yangu.
Ikiwa wewe kwa ujuzi wako unaona kuwa mimi naandika udini hii itakuwa bahati mbaya
kwako.
Hii mosi.
Pili kuzungumza msikitini ndiko ninakoalikwa na Waislam na hata ikiwa nitaalikwa kanisani
In Shaallah nitakuja.
Labda nikukumbushe kuwa William Lukuvi alizungumza kanisani na aksema Zanzibar
lazima iwe chini ya uangalizi wa Bara ili Uislam usipate nguvu.
Unazungumza kuwa mimi, ''nataka muamini hii historia ndiyo ya kweli.''
Hapana kuamini au kutoamini kunategemea akili ya mtu anavyoliona jambo na kutafakari.
Mimi silazimishi mtu kuniamini ingawa napenda mtu asome historia hii kisha mwenyewe
ataamua nani anasema kweli.
Ni hii historia rasmi iliyodumu kwa miaka na miaka iliyowafuta wazee wangu au hii yangu
iliyochapwa London mwaka wa 1998.
Nyerere hakuombwa na wazee wowote kuja TAA.
Inaonyesha huijui historia ya Nyerere ambae unataka kumtetea katika maandishi yangu.
Nyerere alikuja na barua kutoka kwa Hamza Mwapachu aliyekuwa masomoni Chuo
Kikuu cha Wales, Cardiff kwenda kwa Abdul Sykes na aliyempeleka Nyerere kwa Abdul
nyumbani kwake alikuwa Joseph Kasella Bantu.
Hii ilikuwa mwaka wa 1952 na ni mwaka huo baba yangu alipomjua Nyerere hapo kwa
Abdul Sykes kwani kila mwisho wa juma Nyerere aifika kwa Abdul kumtembelea na
kuzungumza mustakbali wa nchi yao.
Hakika hakuna mtu anaeweza kufuta mchango mkubwa wa Nyerere katika TANU hili
haliwezekani hata kidogo.
Na hakuna mtu anaeweza kufuta mchango wa Mzee Klesit Sykes (1894 - 1949) katika
kuwaandaa Waafrika wa Tanganyika kuelekea kuwa na chama cha siasa.
Kwa msisitizo huu huu hakuna anaeweza kufuta mchango wa Abdul Sykes na mdogo
wake Ally katika kuiunda TANU na kupigani uhuru wa Tanganyika na haya ni majina
machache tu.
Labda hapa ndipo ilipo tofauti yetu kati mimi na wewe.
Wewe ungependa Nyerere aenziwe pweke.
Mimi nakueleza kuwa hakuwa peke yake.
Alikuwapo Hamza Mwapachu, Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Suleiman Takadir,
John Rupia, Stephen Mhando, Zuberi Mtemvu, Ali Mwinyi Tambwe, Bi. Tatu biti
Mzee, Bi. Sharifa biti Mzee, Bi. Halima Selengia, Bi. Titi Mohamed, Mshume Kiyate,
Jumbe Tambaza, Idd Tulio, Idd Faiz Mafongo, Dr. Vedasto Kyaruzi, Kasella Bantu,
Said Chamwenyewe, Yusuf Chembera, Salum Mpunga, Saadan Abdu Kandoro na
wengi wengi wengi sana ambao wote mimi najua michango yao na nimeiandika hapa siku
zilizopita na wengine nimekuwekeeni hadi picha zao wakiwa na Nyerere.
![Click this image to show the full-size version. [IMG]](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEht_CctWLtRRs37VF3KxUGxTRDXXo3FkVNDXjDqacxFFCa4ixJSxSAkpA8YobqPZJmahmJqJFxFRoeIuMugqn5hndMsMa8vMGOisHEPL50e-oMkOzK4l0_nZcj4bMgyo3LVwrF20qAwksk/s480/facebook_1425848560953+%25281%2529.jpg)
Kushoto aliyesimama ni Ally Kleist Sykes, na kulia kwake ni
Abdulwahid Kleist Sykes, mbele kushoto ni Kleist Sykes
Mbuwane na Abbas Kleist Sykes. Katika hawa aliye hai ni Abbas.
Ukoo huu umeacha kumbukumbu nyingi kwa maandishi katika harakati za
kuunda African Association 1929 na kuunda TANU 1954. Picha hii imepigwa
mwaka wa 1942 Abdul aliporudi Dar es Salaam kutoka Lower Kabete Kenya
alipokuwa akipata mafunzo ya kijeshi katika King's African Rifles kabla
hajakwenda Burma kujiunga na Burma Infantry. Angalia utaona Abdul amevaa
sare ya Jeshi la Mfalme wa Uingereza. Ilikuwa akiwa Burma Vita Vya Pili Vya Dunia
(1938 - 1945) ndipo alipoamua kuwa 6th Battalion iliyokuwa na askari kutoka
Tanganyika waunde TANU wakirudi Tanganyika kudai uhuru.
No comments:
Post a Comment