Ukipunguza hamaki na ghadhabu utaweza kufikiri vizuri sana na kuja
na hoja nzuri.
Mimi nakushinda kwa kitu kimoja.
Nimesomeshwa na Maalim wangu Sheikh Haruna adab za majadiliano.
Ndiyo maana ninapoandika hutoona tusi katika maandishi yangu wala
hamaki.
Ungeweza kusema yote uyapendayo bila ya kutumia maneneno, ''ushenzi,''
''ujinga,'' ''upuuzi,'' nk.
Naingia katika mnakasha.
Ningeweza kukuomba uonyeshe mahali nilipoandika kuwa ''mapinduzi hayana
maana,'' lakini nitakutaabisha bure na mimi sipendi mjadala wa nipe nikupe.
Hapa tupo barzani na barza ni moja ya mila zetu Waislam.
Mko barzani mnabishana lakini hambughudhiani na ukipiga duru ya kahawa na
kashata na anaekupinga na yeye pia anakunywa kwa starehe hakuna kinyongo.
Huu ndiyo utamaduni wa barza.
Kustahiana na kuheshimiana.
Nilichosema katika mapinduzi ni mauaji sikusema hayana maana.
Ikiwa kulisema hilo naweza labda kwenye muktadha mwingine si huu ulio jamvini.
Jibu na mbili ulivyosema ndiyo hivyo hivyo ila kwa hilo la ''dharau,'' na ''kejeli.''
Hilo hapana.
Hakuna mtu yoyote duniani awezae kumkejeli au kumdharau Mwalimu Nyerere.
Heshima yake inatambulikana dunia nzima.
Kuwa Abdul Sykes hakuwahi kutawala nchi hii hilo wala halihitaji kusemwa kila
mtu analijua ila umelileta kwa kuwa kifua chako kina joto chembelecho Maalim
Faiza na ndiyo maana ukasema ''umuhimu wake uliishia Kariakoo.''
Hilo si kweli.
Umuhimu wa Abdul ulianza Burma akiwa katika 6th Battalion ya KAR wakati wa
Vita Kuu ya Pili.
Hapo ndipo alipowaeleza askari wenzake umuhimu wa kuunda chama cha siasa
kuwaondoa Waingereza Tanganyika.
Wakati huo Abdul alikuwa na umri wa kiasi cha miaka 23 hivi.
Angalia hiyo picha yake hapo chini akiwa Burma:
Ukipitia Tanganyika Intelligence Gazette kuanzia 1950 hizi ni taarifa
za kikachero za Waingereza zikiandikwa na Special Branch utaona
habari za Abdul akiwa Dar es Salaam na mikoani alikokuwa akipita
kuongea na viongozi wa TAA kuhusu hali ya baadae ya Tanganyika.
Moja ya taarifa hizi ambazo mimi ninayo ni ni safari ya Abdul Sykes
ya Kanda ya Ziwa aliyofanya mwaka wa 1952 akiwa Katibu na Kaimu
Rais wa TAA kukutana na Paul Bomani na kisha kuelekea Uganda.
Lakini kabla ya hapa mwaka wa 1950 Abdul Sykes alifanya mkutano
na Jomo Kenyatta na kundi lake la kina Paul Ngei, Kungu Karumba,
Bildad Kaggia na wengine Nairobi agenda kuu ikiwa kuunganisha nguvu
za Waafrika wa Tanganyika na Kenya kupambana na Waingereza.
Huu ulikuwa wakati wa Mau Mau.
Nimeeleza habari hizi kwa kirefu kwenye kitabu chake.
Mimi sikulaumu kuwa wewe hujui historia hii.
Utaijuaje ikiwa haikupatapo kuandikwa hadi nilipoiandika na kitabu kuchapwa
Uingereza mwaka wa 1998?
Tatizo lako ndugu yangu Nguruvi3 ni kuwa unataka kuleta ubishi katika jambo
ambalo wewe huna ujuzi nalo.
Katiba iliyoandikwa na wazee wangu mwaka wa 1950 ipo.
Abdul Sykes kaieleza katika taarifa yake kwa wanachama wa TAA (Angalia:
Annual Report of the Secretary of Tanganyika African Association, 7 January,
1951 Sykes' Papers).
Cranford Pratt katika kitabu chake ''Critical Phase in Tanzania,'' kaieleza na
kaisifia (Angalia: Cranford Pratt, The Critical Phase in Tanzania 1945-1968,
Cambridge University Press, London, 1976, uk. 29-31.)
''Document'' hii hutoweza kuiona popote pale kwa sababu hata Tanzania National
Archives (TNA) imenyofolewa jalada liko tupu.
Hata kwenye maktaba yake ya ''microfilm,'' pia imeondoshwa.
Halikadhalika katika Maktaba ya CCM Dodoma jalada pia liko tupu.
Nimepata kuandika kuhusu, ''Lost Documents,'' naitafuta hii paper nikiipata nitaileta
barzani In Shaallah.
Leo sishangai kwako wewe kunitaka mimi nikupe ushahidi wa katiba iliyoandikwa
na wazee wangu mwaka wa 1950.
Wakati tunahariri mswada wa kitabu kulikuwa na ubishani mkubwa kati yangu na
wachapaji kwa kuwa neno nililoandika ni kuwa nyaraka hii ya katiba ''imeibiwa.''
Mhariri hakupenda neno hili na akasema niseme, ''imepotea,'' au ''haionekani.''
Isiwe ''imeibiwa.''
Nguruvi3,
Nimekupa ushahidi wa katiba iliyoandikwa na wazee wangu waliokuwa katika
TAA Political Subcommittee.
Document hii ilijadiliwa katika mkutano mkuu wa TAA 1954 mkutano uliounda
TANU na mwaka wa 1955 Nyerere alisoma yaliyokuwa katika ''document,'' hii
UNO mbele ya Kamati ya Udhamini.
Ikiwa hujaridhika na haya niliyokueleza mimi nipo hapa In Shaallah nasubiri.
Bahati mbaya unachoshwa na kusoma vitabu.
Mimi vitabu ndiyo maisha yangu toka nina umri wa miaka 6.
No comments:
Post a Comment