Sunday, 3 July 2016

BETI ZA MOHAMMED GHASSANI: RUNGU NA PINGU


Mimi na Wewe
Mimi sina marungu, wewe unipigayo
Wala similiki pingu, wewe unifungayo
Jela ni yako si yangu, wewe unitiayo
Sina bunduki wala risasi, wewe unifyatuliayo
Lakini nina nafusi, ambayo wewe hunayo
Isiyo kisisi, kwa yote unitendayo
Sina wasiwasi, ambao wewe unao
Ndipo pale
Uinuwapo rungu, kichwani ukanishushiya
Na mikono yangu, pingu ukaizungushiya
Jela ufunguapo, ndani ukanisukumiziya
Mtutu unielekezeapo, risasi ukanimwagiya
Huwa nafsini mwako, woga wakutembeya
Machoni mwako, miale ya hofu yakuwakiya
Waogopa siku yako, ya mimi kukugeukiya
Basi hapo…
Giza litapoondoka, kwa asubuhi kungiya
Jogoo atapowika, watu wakamsikiya
Mnadi ‘tapoinuka, kwa nguvu akanadiya
Umma utapoamka, ni muda wa kuamua
Utaona...
Ilo rungu, siku litapokwanguka
Hiyo pingu, siku itapokatika
Bundukiyo, siku itapovunjika
Hizo risasi, zitashindwa kufyatuka
Lango la jela, mbeleyo litafunguka
Humo utupwe, kisha utasahaulika
Thamma utasahaulika
Kama vile hukuwapo!
© Mohammed K. Ghassani
3 Julai 2016

No comments: