Sunday, 7 August 2016

BADAWI QULATEIN ALIANZA KAMA ''COMRADE'' AKAMALIZA KAMA SUFI

  Utangulizi
Hapo chini ni aliyoandikia Salim Msoma kwa kichwa, ''Al Marhum Comrade Badawi Qulatein,'' na kuniletea kuhusu Badawi Qulatein. Nami nimeona niweke hapa ili jamii inufaike na historia hii ya Badawi Qulatein na mchango wake katika historia nzima ya mapinduzi ya Zanzibar. Kichwa cha habari nilichotumia ni changu na nimekiandika hivyo kwa makusudi. Naomba radhi kwa kaka yangu Salim Msoma. 

Mimi sikupatapo kumjua Badawi Qulatein wakati akiwa comrade. Nilikuja kumjua wakati akiwa mmoja wa wanafunzi wa Sharif  Abdulkadir Juneid msikiti wa Kitumbini Dar es Salaam. Kaipa mgongo siasa na kamuelekea Allah. Hatukujuana kwa karibu, kujuana kwetu ilikuwa kukutana hapo msikitini katika sala za jamaa tukapeana salaam na huo ndiyo ulikuwa mwisho wetu. Lakini ikatokea siku moja Ahmed Rajab alikuja kutoka London na akataka mimi na Dr. Dau tumsindikize nyumbani kwa Ahmed Diria Upanga. 

Ilikuwa katika pilkapilka hizi za kumpeleka Ahmed Rajab huku na kule ndipo tukakutana na Badawi Qulatein Mtaa wa Mkunguni na Ahmed Rajab akatutambulisha mimi na Dr, Dau kwake kama ndugu zake. Kuanzia siku ile Badawi Qulatein akawa rafiki yangu na  mzungumzaji wangu mkubwa. Nilikuja kugundua kuwa tulikuwa tumeshahabiana kwa mengi sana. Hata siku alipofariki Makka katika hija wakati ule ule hata saa moja haijamalizika Ahmed Rajab akaniletea taarifa za kifo chake. Kwangu nilikuwa nimepoteza rafiki na ndugu. 

Hayo hapo chini ya kuchoma moto mji aliyoandika Salim Msoma, Badawi Qulatein alinieleza hivyohivyo. 

Nina mengi niliyopokea kutoka kwa Badawi Qulatein In Shaallah fursa ikijitokeza nitayaeleza.
Mohamed Said

Hayati Comrade Badawi ndie aliemshindikiza Babu wakati akitoroka kukimbilia Daresalaam kwenye pwani ya Chukwani akiambatana na Ali Mahfoudh mapema wiki ya mwanzo ya Januari 1964.Ngarawa ya kumvusha Babu ilipatikana kwa msaada wa makada wa ASP hayati Saleh Sadalla na mzee Aboud Masai.Siku hiyo Comrade Badawi alimkabidhi Ali Mahfoudh bastola ya aina ya Browning ili amlinde Babu wakati wa safari ya kuvuka bahari hadi mrima kuelekea Dar. Yeye Badawi pia alikua kiungo(link-man) kati ya Babu(Umma Party) na Kamati ya Watu 14 iliyohusika na Mapinduzi ya Jan 1964.Hakika ndie mtu wa mwanzo kwa upande wa Umma Party kujulishwa na mjumbe mmoja wapo wa Kamati 14 kwa jina la Pili Khamis kuhusu kuwepo azma na mpango wa kuteketeza kwa moto mji wa Zbar pamoja na kuanzisha vurugu nyengine ambazo zingesababisha Serikali ya ZNP/ZPPP kushindwa kutawala.

Habari hizo nyeti aliziwasilisha kwa viongozi wengine wa Umma P na kuagizwa azungumze na awanasihi Kamati 14 kuachana kabisa na maandalizi ya kuchoma mji na badala yake wa-focus kwenye kuteka kambi za polisi za Zawani na Mtoni  ambazo zilikuwa na bohari za bunduki na kisha kupindua utawala.(Azma na nia ya kuwasha moto ilithibitishwa hapo awali kwa Badawi na Yusuf Himid na hivi karibuni ilielezwa na Mhe Ibrahim Amani wakati wa sherehe za kumbukumbu ya Mapinduzi).


No comments: