Monday, 8 August 2016

KUTOKA JF: HISTORIA YA TANZANIA ITAKAVYO WAHUKUMU AHMED RASHAD ALI, ALI MUHSIN BARWANI, ABDUL SYKES NA JULIUS NYERERE




Dangaguri,
Prof. Haroub Othman 
alikuwa Marxists na mimi alinisomesha Chuo Kikuu
Cha Dar es Salaam.

Kwa ajili hii nilijua vyema msimamo wake katika Uislam na imani ya dini.

Prof. Haroub alikuwa akimuusudu sana Nyerere na akiamini yote yale
yaliyoandikwa kuhusu Mwalimu hadi imani hii yake ilipokuja kutiwa doa na
Ali Muhsin Barwani katika kitabu chake ''Conflict and Harmony in Zanzibar.''

Bahati mbaya sana kitabu hiki hakikuweza kuingizwa nchini kwa hiyo ni watu
wachache sana walikuwa nacho na zilikuwa ni ''photocopy.''

Nakala niliyokuwanayo mimi ilikuwa ni photocopy niliyotolesha kutoka kwa
kitabu alichokuwanacho Ahmed Rashad Ali.

[​IMG]
Ahmed Rashad Ali

Ahmed Rashad Ali ana historia ya pekee katika uhuru wa Zanzibar na
Afrika kwa ujumla.

Ahmed Rashad Ali wakati wa harakati za uhuru wa Zanzibar alikuwa Cairo
kama mtangazaji wa Radio Free Africa kituo alichoanzisha Nasser kwa ajili
ya propaganda kusaidia uhuru wa Afrika.

Ali Muhsin 
alipokwenda Cairo kwa nia ya kukutana na Gamal Abdul Nasser 
alifikia nyumbani kwa Ahmed Rashad. 

Halikadhalika Abdul Sykes alipokwenda Cairo baada ya uhuru wa Tanganyika
na yeye pia alifikia nyumbani kwa Ahmed Rashad Ali.

Ahmed Rashad kwa hiyo akiwajua wazalendo hawa wawili ndani nje, nje
ndani.

Ahmed Rashad
 ameniambia kuwa alisoma na kukua Zanzibar na Ali Muhsin 
na alimjua Abdul Sykes mwaka wa 1939 wakiwa watoto wadogo na walibaki
marafiki hadi Abdul alipofariki mwaka wa 1968.

Ahmed Rashad mimi alikuwa baba yangu.

Nilikuwa mtoto wa nyumbani nikiingia kwake saa yoyote bila taarifa na kweli
Mzee Rashad alinipenda na alinifungulia mengi kutoka kwenye moyo wake
kuhusu siasa za Zanzibar na katika uongozi wa Abdul katika siasa za Dar es
Salaam ya 1950.

Mengine akiniambia,''Mohamed haya utayaandika mie nitakapokuwa nimekufa.''

Kitabu cha Abdul Sykes kilipotoka Mzee Rashad alikuwa mmoja wa watu
niliowapa nakala za bure nilizopewa na ''publisher.''

Siwezi kukueleza furaha yake.

Mzee Rashad alikuwa heshi kila tunapomzungumza Abdul Sykes kumwombea
dua na kunieleza, ''brilliance,'' yake na roho yake ya ukarimu.

Kisha atageuka kuwalaani wale waliomsaliti.
Sasa hebu tugeuke kwa Ali Muhsin Barwani.

Allah ana maajabu.

Kitabu cha Abdul Sykes kilipotoka 1998 na Ali Muhsin kukisoma kilimuathir
sana moyo wake.

Ali Muhsin akawaagiza wanae wanialike Dubai na Muscat ili niifahamu pia na
historia ya Zanzibar.

[​IMG]
Kushoto: Farouk Abdulla, Mohamed Said, Sheikh Ali Muhsin Barwani na Abdallah Muhsin Barwani, Muscat 1999

Alinipongeza sana na yeye kama alivyokuwa Mzee Rashad akanifanya mimi
mwanae.

Nimeuleta huu mkadama mrefu ili msomaji ajue kuwa mimi naandika habari za
watu ambao niliingiliana nao vizuri licha ya elimu zao kubwa, makamu yao
yaliyopea na ukubwa wao na ujuzi wao katika historia ya Tanzania.

Hawa ndiyo waalimu wangu niliopiga goti kwao na wao wakanisomesha na
kuniombea dua.

Naamini Prof. Haroub alishangazwa sana na kile nilichokuwa nakijua na
nikimweleza kuhusu historia ya TANU na historia ya Waislam na Nyerere.

Kwa ajili hii basi alizungumza na Nyerere akiwa na taarifa kamili na uoni wa
mbele nini itakuwa matokeo yake ikiwa Nyerere na yeye hataandika kitabu
kutujibu mimi na Ali Muhsin kuhusu yeye.

Nyerere alikubali kuandika historia ya maisha yake ili katika kitabu chake hicho
ajibu kila shutuma tulizomshutumu kwayo.

Lakini akamuambia Prof. Haroub kuwa yeye hawezi kuandika hivyo Prof.
Haroub 
ateue kamati ya wasomi na yeye atakuja kuzungumzanao na wao
wataandika hicho kitabu.

Nyerere wakati ule kumbe alikuwa ndiyo maradhi yanamuanza.
Kamati iliundwa lakini Nyerere alitopewa na maradhi na kitabu hakikuandikwa.

Habari zaidi za Ahmed Rashad Ali na Ali Muhsin Barwani ingia:


Mohamed Said: MAISHA YA SIASA YA SHEIKH ALI MUHSIN BARWANI (1919 - 2006) - KUMBUKUMBU YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR

No comments: