Utangulizi
Nimepokea makala hii kutoka kwa Prof. Ibrahim Noor na kwa ajili ya umuhimu wake nimeona niiweke hapa kwa faida ya wote wenye kutaka kujua historia ya kweli ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964.
Katika msiba mkubwa wa historia ya Zanzibar ni kule kufutwa katika historia ya Mapinduzi ya Zanzibar majina ya watu muhimu sana katika kuielewa historia ya mapinduzi. Marehemu Badawy Qulatein ni mmoja wa watu hao na umuhimu wake unaweza ukauhisi kwa kuwa yeye alikuwa mshtakiwa no. 1 katika kesi ya mauaji ya Abeid Amani Karume.
Katika msiba mkubwa wa historia ya Zanzibar ni kule kufutwa katika historia ya Mapinduzi ya Zanzibar majina ya watu muhimu sana katika kuielewa historia ya mapinduzi. Marehemu Badawy Qulatein ni mmoja wa watu hao na umuhimu wake unaweza ukauhisi kwa kuwa yeye alikuwa mshtakiwa no. 1 katika kesi ya mauaji ya Abeid Amani Karume.
Sayyid Ahmad-Badawy bin Shibly bin Omar bin Mudh-hir bin Abubakar Al-Nadhiry |
Assalamu Alaykum,
Sayyid Ahmad-Badawy bin Shibly bin Omar Qulatayn bin Mudh-hir bin Abubakar Al-Nadhiry ni mtu aliyetokana na ukoo wa masharifu, kutoka Tarim, Yemen, wengi wao wakiwa wasomi wa dini ya Kiislamu na wacha-Mngu. Hadithi yao ni ndefu na inahitajia kikao mbali kukizungumzia. Ukoo wake wa karibu ulitokea Tarim na kuishi Barawa, ambako kulikuwa na vyuo vikubwa vya dini na kutoa mashkhe wengi, na kwa ilimu yao wengi walipewa uqadhi kuanzia wakati wa Sayyid Majid mpaka kunofolewa Banadir (Mwambao wa Somalia) kutokana na mamlaka ya Zanzibar na kutiwa katika ukoloni wa Kitaliana. Kutokea Banadir walipitia mwambao na baadaye kuja kuishi Zanzibar. Babake Syd Shibly alikuwa ni mwanachuoni na mcha Mngu wa kupigiwa mfano na kadhalika alikuwa ni mwalimu aliyesomesha shule za serekali mjini Zanzibar na Garisa, Kenya kwa mika mingi. Ami yake Syd Ali Kulatyn na mababu zake walikuwa ni wana vyuoni wajulikaniwao mwambao mzima. Jina lake tunayemzungumza alipewa kwa kutabaruku na jina la mwanachuoni, Sharifu na Mcha Mngu kutoka mji wa Lamu, Sayyid Ahmad Badawy bin Habib Saleh Jamalilyl.
Almarhum na tumbo lake lote lajulikana kwa laqb “Qulatyn” kuanziya Mogadisho, Barawa na mwambao mzima kutokana babu yao Sayyid Omar Qulatyn ambaye alikuwa karimu, aliyekuwa akiwasaidia watu kwa hali na mali, msafi wa umbo na tabiya, Mwanachuoni na mcha Mngu wa kusifiwa kwa kila sifa njema kama “maji yalofika kiwango cha ‘Qulatayni.’
Cha muhimu hapa ni kuwa Sayyid Ahmad-Badawy tunayemzungumza alipata masomo ya msingi au tuseme makapi ya msimamo wa Kiislamu katika kutetea haqi za wanyonge na ndio imani na mtizamo huo ambao uliompelekea kupigania haqi za wanyonge na walalahoi. Haya yameshaelezwa kwa kiasi na Salim Msoma na pia Ahmed Rajab. Kuna na wengine pia walioangalia maisha ya Sayyid Ahmad-Badawy kidoto kukhusiana na yale yaliyokuwa ni muhimu kwao. Ni ya kama hadithi ya vipofu na wasifa wa tembo. Kila mmoja akatoa swifa za tembo kwa kile alichoweza kukikamata kwa mikono yake. Aliyeushika mkia akasema tembo ni kama ufagio. Aliyeshika mkonga akaelezea kuwa tembo ni kama chatu; aliyeupapasa mguu wa ndovu akasema tembo ni kama nguzo; mradi kila mmoja na mtizamo wake. Na mimi pia ninao mtizamo wangu pengine ni wa kidoto zaidi kuliko wa hao niliowazungumzia.
Walilokuwa hawakulielezea waandishi hao wawili niliowataja kwa majina ni ule msingi wake Sayyid Ahmad-Badawy uliompelekea kurudi kulekule alikoanzia, nako ni katika dini ya Kiislamu na maagizo ya Mwenye-enzi Mngu Subhanah waTaala na ya Mtume wake Muhammad Swala ‘lLahu alayhi waSalam. Kwa mtizamo wangu naamini kuwa kuna jambo moja ambalo Makomred wetu wa Zanzibar limewapita, nalo ni kuwa kwa upungufu wao mkubwa wa wengi wao, kama si wote, kuyaelewa ya dini yao, basi pia wamepitwa na kufahamu kuwa hakuna nidhamu (system) iliokuwa ya kijamaa (hata kisosialisti) kuliko Uislamu, na tafauti na huo ujamaa wa akina Marx na Nyerere na wengineo, Uislamu si ujamaa wa kutoana roho kwa dhulma wala kuwanyang’anya watu mali zao kwa dhulma. Inaonesha kuwa awali Sayyid Ahmad-Badawy pia hakulielewa hili na akaona kuwa nidhamu ya ujamaa wa kisosialisti ndiyo iliyo bora. Jambo lililokuja kumgutua ni kule kuja kuwaona wengi wa wanyonge walewale waliokuwa watetewe, waliuliwa bure, wengi walikuja kuadhibiwa bure na kufungwa bila ya sababu na kushuhudia mengi ya dhulma na ya uchafu. Ahmed Rajab anatuelezea haya yafuatayo:
“Kama wengi waliokuwa wakiyaunga mkono Mapinduzi, baadaye Badawi akisikitika kuwa mapinduzi yaliendeshwa sivyo. Nakumbuka siku moja katika miaka ya 1990 nikitembea Dar es Salaam pamoja na mwandishi Mohamed Said wa Tanga na tukasadif kukutana na Badawi njiani. Nilipokuwa ninawajulisha watu wawili hao nilimwambia Mohamed kwamba akitaka kuyaandika ya Mapinduzi ya Zanzibar basi amwendee Badawi.”
“Papohapo Badawi akasema kwa masikitiko: ‘Mapinduzi gani, ilikuwa ni wanawake tu.’ Nilishangaa na kumuuliza alikusudia nini. Alijibu kwamba Mapinduzi yalifisidika na akanitajia visa vya watu waliofungwa gerezani na waliouliwa kwa sababu baadhi ya viongozi wa Mapinduzi wakiwataka ama wake zao ama hawara zao.”
Lakini si mapinduzi ya Zanzibar (ambayo kwa hakika hayakuwa mapinduzi) pekee ndiyo yaliyokuwa na matatizo. Bali ni ule mfumo mzima wa kutaka kuleta mabadiko kwa kutumia njia zilizokatazwa na Uislamu zenye kumpeleka muubwa motoni milele, kwa mujibu wa qauli yake Subhana waTaala katika Qur’ani Tukufu. Baada ya kuyashuhudia maovu na maonevu hayo Sayyid Ahmad-Badawy alijijutia na alikwenda kumwangukia baba yake na baba yake akamwambie arejee kwa Mwenye-enzi Mungu upesi sana na kwanza ende Umra na akirudi aanze kusoma upya juu ya Uislamu na sharia zake. Akampeleka kwa Sheikh Suleiman Al-Alawy na akakaa upya na kusomea Uislamu kwa kituo. Alipofariki Sheikh Suleiman akaenda kwa Sayyid Abdulqadir Juneidy na kuendelea kujiilimisha. Kila alipozidi kuuelewa zaidi Uislamu ndipo alipozidi kutubia kwa aliyoyaamini ujanani.
Imani yake na Maisha yake ya ukubwani yalikuwa tafauti kabisa na alivyokuwa kabla ila katika hamu yake ya kuwasaidia wanyonge. Na ndipo Bwana Mtume ( S.A.W.) aliposema “Amali za mtu ni za mwisho wake.” Sayyid Ahmad Badawy, alikuja kuelewa vizuri sana kabla ya mwisho wa maisha yake, kuwa usoshalisti ulioanzia Ulaya ni wa dhulma tupu na hauna mlingano wowote wa maana na ujamaa wa haqi uliomo katika Uislamu.
Ni mazishi na masikitiko mapevu sana ukiwaangalia masoshalisti kutoka makwetu. Huku hawako wala kule hawako, wameula huu. Sayyid Ahmad-Badawy alijiilimisha upya na akafanikiwa katika kuona ukweli wa mambo yalivyo na hikma za Mwenye-enzi Mungu aliyotuteremshia katika Dini yake. Sayyid Ahmad-Badawy alitubia tawban nasuha na naamini Mola Karimu Rahimu alimkubalia. Kwanza, hakushiriki katika mauwaji wala kumfunga mtu bure ingawa alikuwa na uwezo wa kuyatenda hayo. Pili, alikuja kulaani yaliyotokea Zanzibar kwa moyo wake na kwa maneno na vitendo vyake. Tatu, alipata radhi ya baba yake mzazi. Nne, watu walikuja kumpenda na kumwombea dua njemanjema wakati yu hai na baada ya kufariki. Huu ni mfano wa tafauti baina ya wale walioongoka na wale ambao bado wamo kutafakhari na dhulma na uchafu walioufanya.
Lakusikitisha katika maandishi ya baadhi ya waandishi ni juu ya kuwa Sayyid Ahmad-Badawy amebadilika na kubadilisha itiqadi na msimamo wake na kuendelea mbele na kumwelekea Mwenye-enzi Mungu na kutubia, lakini katika maandishi yao hao waandishi sehemu hii wameiacha na kug’ang’ania palepale kuwa Sayyid Ahmad-Badawy ni Komredi ilihali alitokana nao zamani sana na kuwa mtu mwingine kabisa. Ndipo jana nipotoa mfano wa Sayyidna Omar. Niliandika kwa mukhtasari, haya:
“Kuna Sayyidna Omar ibn Khatab wawili. Yule aliyeyezaliwa katika ujahiliya akamzika mwanawe akiwa yu hai na yule Sayyidna Omar aliyesilimu na akabashiriwa pepo.”
“Wengine tunamzungumzia Sayyid Ahmad-Badawy aliyetubia na wengine wanamzungumza yule aliyefuata siasa za Kikomunisti katika ujana wake. Wewe fuata akili yako inavyokuelekeza!”
Nakutakia kila la kheri,
Ibrahim
Prof. Ibrahim Noor |
No comments:
Post a Comment