"MIMI Aboud Jumbe Mwinyi, namshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kunibariki kuzaliwa ndani ya Uislamu na namuomba aniruzuku kufa na
kufufuliwa ndani ya Uislamu".
Hayo ni sehemu ya yaliyomo katika Wasia wa Rais
Mstaafu wa wa Zanzibar Alhaj Aboud Jumbe ambaye hivi sasa ametimiza umri wa
miaka 80.
Akiwa na akili timamu kabisa Mzee Jumbe ameandika
wasia huo wiki hii ambao nakala zake zimesambazwa kwa watu mbalimbali likiwemo
gazeti hili.
Wasia huo wenye kuashiria kutahadharisha juu ya yale
yanayoweza kuja kufanywa kinyume na ridhaa yake, umekuja siku chache baada ya
kifo cha Rais mwingine Mstaafu wa Zanzibar Sheikh Idris Abdul Wakil.
"Ni matumaini yangu kwamba kama Mwenye Enzi Mungu
alivyonirehemu kuwa Muislamu, atanijaalia nikifa kukoshwa, kuvishwa sanda,
kutiwa katika jeneza, kusaliwa na kuzikwa kwa mujibu wa sunna ya Mtume Muhammad
(sa.w.)", umeagiza wasia huo uliosainiwa kwa niaba yake na Msaidizi wake Bwana Abubakar.
Agizo hilo linahusisha pia jeneza lake kutofunikwa
bendera ya Taifa au ya CCM, kuwepo na utabaka katika kubeba jeneza na ufukiaji
wa kaburi.
Akiwashuhudisha Mufti wa Zanzibar, Kadhi Mkuu wa
Zanzibar, Naibu Kadhi Mkuu, Mwanasheria Mkuu, Sharrif Juneid, Masheikh wengine
na wanawe, Alhaj Jumbe amesisitiza kuwa kufanyiwa si ombi bali ni haki yake
kama binadamu, kama Muislamu na kama Mtanzania.
Amesema haki ya uhuru wa kuabudu imeelezwa katika
katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 19 (1) na (2).
Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu mtu anapokufa ni
haramu kwa ndugu au jamaa zake kuomboleza kwa nyimbo, kunyoa vipara, kuvaa
vitambaa au nguo nyeusi wala kulia kupita kiasi.
Aidha, imesuniwa kuwafariji (taa'zia) wafiwa kwa muda
wa siku mbili tu.
"Atta'azia marrataan" ameagiza Mtume (s.a.w)
akiwa maana ya kuwafariji wafiwa ni mara (siku) mbili.
Katika wasia wake Alhaj Jumbe amesema maana ya kuumbwa
mauti na uhai sababu na lengo lake ni kuwafanyia wanaadamu mtihani kupimwa
miongoni mwao mwenye vitendo vizuri.
"Nikiwa hai, dhamana ya vitendo vyangu
inaniangukia mimi mwenyewe, nikifa dhamana ikiwa vitendo vyema au vibaya
nitakavyofanyiwa itawaangukia waandalizi, watendaji na wenye kushiriki katika
vitendo hivyo", amesisitiza mzee huyo aliyekuwa pia Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akimshudisha Mwenyezi Mungu katika wasia huo amekataa
maziko yake kufanywa kinyume na taratibu za Kiislamu.
"Sitaki bendi, sitaki mizinga, sitaki maombolezo
wala lolote lingine lenye hata chembe ya kufuru", ameandika kwa mkazo mzee
huyo.
Aidha, amewaapiza kwa kumshuhudia Mwenyezi Mungu wale
watakaojaribu kufanya kinyume na anavyoagiza.
"Sitaki hivyo nikiwa hai, nitakapoondoka katika
dunia Mwenye Enzi Mungu anatosheka kuwa shahidi wangu, duniani na akhera",
Mzee Jumbe amemaliza wasia wake alioutanguliza aya ya Qur'an isemayo "Enyi
wenye kuamini, mcheni Mwenyezi Mungu vile ipasavyo waja kumcha, wala msife ila
Ilhali ni miongoni mwa Waislamu. (3:101)
No comments:
Post a Comment