Utangulizi
Katika moja ya misiba mikubwa ya
Tanzania ni kukosekana kuwapo kwa historia ya kweli ya kupigania uhuru na kwa
ajili hiyo kusababisha kutokuwapo kwa mashujaa wa taifa. Mzee Omar Suleiman ni
mmoja wa waasisi wa TANU Dodoma na kwa ajili hii ni kati ya mashujaa
waliopigania uhuru wa Tanganyika ambao si wengi wanamfahamu na kujua khasa nini
ulikuwa mchango wake. Mara kwa mara hasa kwa siku hisi za mwisho wa maisha yake
kila ilipotokea nafasi ya kutaja Mzee Omar Suleiman kilichokuwa kikielezwa ni
uhusiano wake na Julius Nyerere na kusema kuwa Nyerere alikuwa akifikia
nyumbani kwake basi. Nini ulikuwa mchango wake haukuwa unaelezwa na sababu
khasa ni kuwa hakuna aliyekuwa anaujua. Hata alipokufa hakuna taazia yoyote
iliyoandikwa kumweleza Omar Suleiman alikuwa nani. Ili kumjua Omar Suleiman ni
lazima mtu arudi nyuma sana na kumtafuta Omar Suleiman katika kundi la wazalendo
wenzake aliokuwanao katika siasa wakati wa kuiunda TANU Jimbo la Kati mwaka wa
1955.
Kuipata picha ya siasa katika Tanganyika
ya 1950 hatuna budi uitazama African Association mtangulizi wa TANU. African
Association mjini Dodoma ilikuwa ikiongoza katika harakati baada ya Vita Kuu ya
Pili. Ilikuwa na wanasiasa wenye juhudi sana na wabunifu kuliko wanasiasa
wengine wote waliopata kutokea katika historia ya Tanganyika. Wanasiasa hawa
walikuwa Ali Ponda, Mmanyema na Hassan Suleiman, Myao, rais na katibu wake.
Mwaka 1945 Ali Ponda alitoa wito kwa Waafrika wote kuungana kama umma mmoja.
Lakini kuanzia mwaka 1948 harakati za siasa mjini Dodoma zilififia, na TANU
ilipoanzishwa mnamo Julai, 1954, tawi la TAA Dodoma lilikuwa limedorora kiasi
kwamba kilishindwa hata kupeleka mjumbe kwenye mkutano ule wa TAA wa kuundwa
kwa TANU. Pamoja na ukweli kuwa mji wa Dodoma kulikuwa na Kikuyu Secondary
School (sasa Alliance Secondary School) ambako kulikuwa na walimu wa Kiafrika,
wengi wao kutoka Makerere, ambao kama wasomi, wangechukua juhudi kuihuisha
African Association. Labda kwa kuhisi kuwa hapakuwapo na ukinzani unaokwenda
kinyume na maslahi yao katika mfumo wa kikoloni, walimu wale waliamua
kujitenga na siasa. Kwa hiyo basi, harakati dhidi ya serikali ya kikoloni
ziliachwa kuwa mikononi mwa wa Waislam wa mjini Dodoma, wengi wao wakiwa
hawakujaliwa kupata elimu ka ajili ya siasa za Waingereza walioacha elimu iwe
mikononi mwa Wamishionari.
Gazeti la Mwananchi Jumanne 20 Septemba 2016 |
Mji wa Dodoma unatarajia
kuipa mitaa na barabara majina ya viongozi. Majina yaliyoanza kutajwa kwa
heshima hiyo ni Job Lusinde, Rashid Kawawa, Pius Msekwa na Anna Abdallah. Hakika hawa walikuwa viongozi katika Tanzania lakini tusisahau kuwa wakati wa
kudai uhuru wa Tanganyika walikuwapo wazalando waliojitolea kwa hali na mali
kusimama bega kwa bega na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kupigania uhuru. Hawa pia wanastahili kufikiriwa majina yao kupewa mitaa na barabara. Hebu
tusome historia ya wazalendo hawa hapo chini:
Kulia: Haruna Taratibu, Saadan Abdu Kandoro, Julius Nyerere, Sheikh Mohamed Ramia na Idd Faiz Mafungo Dodoma 1955 |
''Mwaka
1953, Haruna Taratibu, alikuwa na umri
wa miaka 23. Wakati akifanya kazi Public Works Department (PWD) kama mwashi,
alijaribu kuunda chama cha wafanyakazi kwa kuwahamasisha na kuwakusanya vibarua
walioajiriwa katika kazi za ujenzi. Kwa sababu ya harakati hizo za kutaka
kuanzisha chama cha wafanyakazi, Taratibu alionekana na wakoloni kama mtu mkorofi
na mzusha vurugu. Hata hivyo Taratibu hakufanikiwa kuanzisha chama hicho na
matokeo yake akapewa uhamisho kwenda Singida kama adhabu. Taratibu alivutiwa
sana na harakati za Mau Mau nchini Kenya na alizoea kufuatilia matukio yake
katika gazeti lake alilokuwa akilipenda sana, Baraza, gazeti la Kiswahili la
kila wiki kutoka Kenya.
Ilikuwa
katika Novemba 1954 wakati Taratibu alipokuwa akipekuapekua gazeti hilo ndipo
alioposoma habari kuhusu TANU. Taratibu aliuliza pale Singida mjini kama kuna
tawi la TANU. Taratibu alifahamishwa kuwepo kwa tawi la TANU pale mjini na katibu wake alikuwa mzee mmoja
kwa jina la Mzee Kinyozi. Taratibu alikata kadi yake toka kwa huyo mzee na
akawa mwanachama wa chama cha siasa. Asubuhi iliyofuata Taratibu aliingia
ofisini kwake na akaiweka kadi yake
ya uanachama wa TANU yenye rangi nyeusi na kijani juu ya meza yake, kila
mtu aione. Ofisa Mzungu wa PWD Singida hakuweza kuvumila ufedhuli kama ule,
alishauri Taratibu apewe uhamisho kurudi Dodoma alikotoka, kabla hajaeneza sumu yake kwa Waafrika wengine.
Seif Khatib na Mzee Omar Suleiman |
Mwaka
1955 wakati wimbi la utaifa wa Tanganyika lilipokuwa limepanda sana nchini
Tanganyika Omari Suleiman alikuwa na umri wa miaka 43. Suleiman alikuwa fundi
cherahani akifanya shughuli zake katika nyumba moja katikati ya mji wa Dodoma.
Mkabala na nyumba ambamo Suleiman alikuwa amepanga chumba kimoja ilikuwa nyumba
aliyopanga Taratibu. Mara baada ya kupewa uhamisho kutoka Singida, Taratibu
alimuuliza jirani yake, Suleiman, kama kuliwepo na tawi la TANU pale mjini.
Suleiman alimwambia Taratibu kuwa hapakuwepo na tawi la TANU mjini Dodoma na
alimjulisha habari kuwa kulikuwa na tetesi mjini kuwa Hassan Suleiman
amemuahidi na kumhakikishia DC kuwa yeye, akiwa katibu wa Jimbo wa TAA,
hatairuhusu TANU kusajiliwa katika Jimbo la Kati bila ya idhini yake.
Lakini
ukweli ulikuwa Hassan Suleiman alikuwa tayari ameisajili TANU lakini
hakumfahamisha mtu yoyote wala kufanya juhudi yoyote kuitisha uchaguzi au
kufanya mkutano. Hassan Suleiman kama, Omar Suleiman alikuwa na umri wa miaka
arobaini na tatu mwaka 1955. Tofauti na Omari Suleiman, Hassan Suleimani
alikuwa ameelimika na alikuwa mwanasiasa mwenye uzoefu akiwa amekiongoza chama
cha African Association. Halikadhalika alikuwa amehudhuria mikutano ya African
Association Tanganyika na Zanzibar. Baba yake Hassan Suleimani, Taufik bin
Suleiman alikutana na Burton, mvumbuzi mashuhuri, kisiwani Zanzibar; na
aliajiriwa kama mmoja wa wapagazi katika safari yake ya kutafuta chanzo cha mto
Nile. Alisafiri na Burton hadi Bagamoyo ambako kuanzia hapo ndipo walipofunga
safari ya bara. Taufik alifariki mwaka 1920 Hassan Suleiman akalelewa na
shangazi yake, Binti Taufik. Kisa cha kusoma kwa Hassan Suleiman ni mfano mmoja
muhimu sana unaoonyesha jinsi wazazi wa Kiislam walivyokuwa waiuthamini Uislam.
Hassan Suleiman alichaguliwa kuingia daraza la sita St. Andrewís College
Minaki, mwaka 1925. Shangazi yake alipopata taarifa kuwa mtoto wa ndugu yake
alikuwa anasoma shule ya wamishionari alipata hofu ya kile ambacho huenda
kitamtokea mwanae, yaani kubatizwa. Alitembea kwa miguu kutoka Dar es Salaam
hadi Minaki kumchukua mtoto wake. Siku hizo njia iliyokuwapo kwenda Minaki
kutoka Dar es Salaam ilikuwa njia ya miguu kupitia vichakani. Hassan Suleiman
alikuwa hajasoma hata majuma mawili mara akamuona shangazi yake anaingia
darasani kumtoa shule na akarudinae nyumbani. Sababu aliyoitoa bibi mkubwa yule
kwa mwalimu mkuu mmshionari ilikuwa, anahofu mwanae atakuwa murtadi. Safari ya
miguu ya kurudi Dar es Salaam iliwachukua siku mbili.
Mwaka
1953 Nyerere alipokwenda Dodoma kuhudhuia mkutano wa Kamati ya Elimu ya
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Nyerere alifikia kwa Hassan Suleiman na
Nyerere akatambulishwa kwa wazalendo wengine waliokuwa wakiondokea katika siasa
kama Oscar Kambona, wakati huo akifundisha katika Kikuyu Secondary School,
Nsilo Swai na Kanyama Chiume ambao wote hapo baadae walikuja kuwa mawaziri
katika Tanganyika huru. Kanyama Chiume naye vilevile alikuja kuwa waziri
Nyasaland (Malawi) ilipopata uhuru.
Haruna
Taratibu, Omari Suleimani na marafiki zake wachache waliunda kamati ndogo kisha
wakaandika barua kwenda makao makuu ya TANU Dar es Salaam kuomba ruhusa ya
kufungua tawi la chama. Katibu mwenezi wa TANU, wakati ule Oscar Kambona,
aliwaandikia kuwaeleza kuwa Hassan Suleiman tayari alikuwa ameshaisajili TANU
na ikiwa uchaguzi wa viongozi haujafanyika basi waonanena na yeye pamoja na Ali
Ponda. Omari Suleiman na Haruna Taratibu hawakuridhika na majibu kutoka makao
makuu ya TANU kwa hiyo walikwenda kutafuta ushauri kwa Edward Mwangosi,
aliyekuwa mwanachama mkongwe wa African Association. Mwangosi aliishauri kamati
ile iitishe mkutano Community Centre ili kujadili kufungua tawi la TANU, na
Hassan Suleiman na Ali Ponda waalikwe kuhudhuria. Kadhalika Mwangosi aliishauri
kamati ile kuwaalika walimu waliokuwa wakifundisha Kikuyu Secondary School,
wengi wao wasomi kutoka Makerere kuhudhuria mkutano huo. Mwangosi aliwaambia wajumbe wa kamati ile
ndogo kuwa wasomi wa Makerere walikuwa ni muhimu sana kwenye chama kwa kuwa
wangetoa uongozi uliokuwa unatakiwa.
Karibu
ya watu arobaini pamoja na wale wasomi wa Makerere, miongoni mwao Job Lusinde
walihudhuria mkutano ule. Lusinde alikuja kuwa waziri, na Amon Nsekela, alikuja
kushika nyadhifa muhimu katika serikali na vilevile kuwa balozi wa Tanzania
nchini Uingereza. Hassan Suleiman na Ali Ponda hawakutokea mkutanoni. Wakati
wanakusanyika kwa ajili ya mkutano, afisa wa Community Centre aliwaambia kuwa
alikuwa amepokea amri kutoka kwa DC kuwa mkutano huo usifanyike. Kufuatia amri
ile watu walitawanyika mara moja. Alexander
Kanyamara aliyekuwa Mwafrika tajiri mjini Dodoma na rafiki wa John
Rupia, wakati ule makamu wa rais wa TANU, aliwataka kuahirisha mkutano huo kwa
sababu ya kutokuwepo kwa viongozi wa juu wa TAA, Hassan Suleiman na Ali Ponda. Kutokana na sababu hii na vile vitisho vya
DC, mkutano uliahirishwa bila kupanga tarehe ya mkutano mwingine.
Asubuhi
iliyofuata Taratibu alikamatwa na polisi na kupelekwa kwenye ofisi ya DC, (hivi
sasa ofisi hiyo ni ofisi ya Waziri Mkuu). Taratibu alimkuta Hassan Suleiman
pale ofisini akizungumza na DC, Bwana Smith. DC alianza kumsaili Taratibu kwa
kumuuliza kama alikuwa akijua kuzungumza Kiingereza. Taratibu alijibu kuwa yeye
hakusoma. Akizungumza Kiingereza Hassan Suleiman alimwambia DC kuwa yeye ndiye
katibu wa TANU mjini Dodoma. DC, Bwana Smith, alimshutumu Taratibu kwa kuunda
chama haramu na kwa kuitisha mkutano usio na idhini ya serikali katika
Community Centre jana yake ambao ulielekea kuvuruga amani. Bila woga Taratibu
alijibu kwamba yeye alikuwa na mamlaka ya kuitisha mkutano kwa sababu alikuwa
mwanachama wa chama cha siasa kilichosajiliwa kihalali. Taratibu aliichomoa
kadi yake ya TANU kutoka mfukoni kwake yenye rangi nyeusi na kijani na
kumwonyesha DC. Bwana Smith alimuuliza Hassan Suleiman kama ikiwa na yeye pia
alikuwa na kadi ya TANU. Hassan Suleiman hakuwa nayo. Hassan Suleiman na DC
walizungumza Kiingereza kwa muda baada ya hapo aliwataka wote wawili kuandika
maelezo yao. Baada ya kuandika maelezo yake Taratibu aliruhusiwa kurudi
nyumbani. Inasadikiwa kuwa wakati ule mwanachama pekee wa TANU mjini Dodoma
walikuwa Haruna Taratibu na Alexander Kanyamara ambae yeye alikata kadi yake Dar es Salaam.
Wasomi
wa Makerere, ambao Mwangosi aliwaamini sana katika kuunda TANU, walipopata
habari kuhusu mkasa wa Taratibu na DC, Bwana Smith, waliogopa. Waliamua
kujiweka mbali kabisa na mambo ya siasa
na kuendelea na kazi yao ya kufundisha. Haruna Taratibu na Omari Suleiman sasa
waliamua kugeuza mbinu, waliitisha mkutano wa siri usiku nyumbani kwa Swedi bin
Athumani. Mkutano huu uliamua kuwa Taratibu lazima aende makao makuu ya TANU
Dar es Salaam akazungumze na Nyerere ana kwa ana kuhusu matatizo yaliyokuwa
yakiikabili TANU Dodoma. Mahdi Mwinchumu aliyekuwa mwanachama wa TANU
Dar es Salaam alijitolea kufuatana na Taratibu hadi makao makuu ya chama Dar es
Salaam kwa kuwa alikuwa akijuana na viongozi wa TANU. Said Mussa mjumbe
mwingine wa ile kamati ya siri alijitolea vilevile kufuatana na Taratibu na
Mwinchumu hadi Dar es Salaam. Siku ya kuondoka Job Lusinde alikwenda stesheni
ya gari moshi kuagana na ule ujumbe uliokuwa ukielekea Dar es Salaam, makao
makuu ya TANU. Lusinde aliuambia ule ujumbe kuwa jamaa wa Makerere wanaunga
mkono maamuzi yote yatakayoamuliwa na ile kamati ya siri.
Job Lusinde |
Kwa
bahati nzuri katika gari moshi lile lile ambamo Taratibu na wenzake walikuwa
wakisafiri kulikuwa na wajumbe wa TANU kutoka Kigoma, Bukoba na Mwanza
wakisafiri kwenda Dar es Salaam kuhudhuria mkutano mkuu wa kwanza wa mwaka wa
TANU. Wahudumu ndani ya gari moshi walipofahamu kuwa walikuwa na wajumbe wa
TANU kwenye gari moshi lile, waliwafanyia heshima kubwa. Mmoja wa wahudumu
wale alijitolea kumpa malazi Salum Mussa
nyumbani kwake Dar es Salaam. Mahdi Mwinchumu aliwapeleka Haruna Taratibu na
Said Mussa makao makuu ya TANU New Street ambako walifanya mazungumzo na
Nyerere pamoja na Rupia. Uongozi wa makao makuu ulielezwa kwa ufupi matatizo
yaliyokuwa yakikabili Dodoma katika kufungua tawi la TANU. Papo hapo Nyerere
alimwalika Taratibu kuhudhuria mkutano mkuu Hindu Mandal Hall kama mjumbe wa
Jimbo la Kati. Mkutano ule ulimchagua
Taratibu kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya TANU. Taratibu na ujumbe wake walirudi Dodoma
washindi, walikwenda Dar es Salaam watu wasiojulikana na walirudi nyumbani
wakifuatana na mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa wa TANU, chombo cha juu kabisa
katika chama. Nyerere alimpa Taratibu dafari ya tasjili ya wanachama, kadi mia
moja hamsini za uanachama wa TANU na nakala hamsini za
Bill of Rights. Kazi ya kuwahamasisha na kuwaingiza watu TANU alipewa Omari
Suleiman, na fundi cherahani mwingine aliyejulikana kwa jina la Abdu Mohamed
Mkamba. Mara tu baba mwenye nyumba wake alipopata habari za kuwa mpangaji wake,
Haruna Taratibu alikuwa mwanachama wa TANU, alimfukuza kutoka kwenye nyumba
yake.
Baada
ya kupata kikundi kidogo cha wanachama, Taratibu alipiga simu makao makuu ya
TANU na kuzungumza na kaimu katibu, Elias Kissenge akaomba ruhusa ya kufanya
uchaguzi. Kissenge hakuweza kutoa uamuzi wowote wa maana kuhusu tatizo la
uongozi wa TANU Dodoma. Taratibu alifanikiwa kumpata Kambona ambae aliidhinisha
uchaguzi ufanyike kwa shuruti moja la kuwa Hassan Suleiman na Ali Ponda
waruhusiwe kushiriki na kugombea uongozi wa chama. Kusisitiza kwa Kambona juu
ya uongozi wa zamani wa TAA kuongoza chama kipya huenda kulishawishiwa na
mafanikio ya zamani ya uongozi wa Hassan Suleiman mbae alimfahamu huko Dodoma
wakati Kambona alipokuwa mwalimu akifundisha
Kikuyu Secondary School. Kwa bahati mbaya, wanachama wa TANU waliokuwa
wanainukia na chama pale mjini Dodoma waliwaona Hassan Suleiman na Ali Ponda
kama wasaliti kutokana na kutokushirikiana na wenzao katika kuanzisha TANU.
Wakati
ametatizwa na tatizo la uchaguzi wa TANU, Taratibu alijulishwa na makao makuu
kuwa makamo wa rais, John Rupia, atapita Dodoma kwa gari moshi akiwa njiani
kwenda Tabora kushughulikia mambo ya chama. Gari moshi liliposimama Dodoma
Rupia alishangazwa kuona kundi la wananchama wa TANU wakimsubiri katika kituo
cha gari moshi wakimtaka avunje safari waende mjini kujadili na kutatua tatizo
la uchaguzi. Rupia aliwaeleza wanachama wa TANU wa Dodoma kuwa yeye hakuwa na idhini kutoka makao makuu
kufanya shughuli yoyote ya chama mjini Dodoma. Wanachama wa TANU hawakutaka
kusikia lolote na walimwambia Rupia kuwa wamechoshwa na makao makuu kwa
kushindwa kwake kutoa uamuzi wa tatizo la uchaguzi. Mizigo ya Rupia ilishushwa
chini kutoka kwenye gari moshi na Rupia akawa hana khiyari isipokuwa kuwafuata
wale wanachama wa TANU hadi mjini.
Ghafla
mji mzima ukavuma tetesi kuwa makamu wa rais wa TANU, John Rupia, yupo mjini
kufungua tawi la TANU. Rupia alimwita Hassan Suleiman na akamtaka alete hati ya
tasjili ya TANU Hindu Mandal siku inayofuata, mahali ambako mkutano utafanyika.
Hassan Suleiman hakutokea mkutanoni lakini alimtuma mtu apeleke ile hati. Ali
Ponda alihudhuria mkutano ule. Rupia alikuwa mwenyekiti wa mkutano na TANU
ikafanya uchaguzi wake wa kwanza.
Alexander Kanyamara alichaguliwa Rais; Haruna Taratibu Makamu wa Rais,
Abdu Mohamed Mwamba, Katibu na Omari Suleiman Mweka Hazina. Miongoni mwa
wanachama waasisi alikuwa mwanamke mmoja wa Kimanyema, Binti Maftah Karenga;
wengine walikuwa Bakari Yenga, Maalim Khalfan, mwanachuoni wa Kiislamu
aliyekuwa akiheshimawa sana, Idd Waziri na Said Suleiman. Wale wasomi wa Makerere
hata mmoja hakujitokeza kwenye mkutano huu wa kuasisi TANU. Ali Ponda,
mwanasiasa mkongwe alipuuzwa na hakuchaguliwa kushika wadhifa wowote. Walipoona
hawakupewa wadhifa wowote katika TANU, Ali Ponda na Hassan Suleiman walijiunga
na UTP kuipinga TANU.
Baada ya uchaguzi
huo, wale mafundi cherahani wawili, Abdu Mohamed Mkamba na Omari Suleiman,
walianza kuhamasisha wananchi wazi wazi kujiunga na TANU ili wapiganie uhuru wa
Tanganyika. Tawi la TANU la Dodoma baada ya kujizatiti pale mjini, lilituma
wanaharakati kuwahamasisha watu wa Kondoa ili wafungue tawi la TANU katika
wilaya hiyo. Abdallah Jumbe alizipenyeza kadi za TANU na kuzipeleka kwenye
wilaya hiyo kwa siri akaanza kuandikisha watu. D.C. wa Singida alikuwa jeuri
sana kiasi kwamba ni baada ya Mkutano Mkuu wa Tabora wa mwaka 1958 ndipo
Abdallah Jumbe aliweza kufanikiwa kufungua tawi mjini Singida. Wakati huo TANU
ilikuwa na nguvu sana ikiwa na wajumbe wake katka Baraza la Kutunga Sheria. Kwa
ajili hii hakuna Mzungu aliyethubutu kuwa fedhuli kwa TANU na kuwabughudhi
wanachama wake.''
No comments:
Post a Comment