Tuesday, 20 September 2016

KISA CHA SHARIFF ABDALLAH ATTAS NA MWALIMU JULIUS NYERERE OFISI YA TANU BAADA YA UHURU




Shariff Abdalla Attas
(Picha kwa hisani ya Bwana Shomari)

Sie wengine tumekuja kumjua Shariff Abdallah Attas katika utu uzima wake akikaa Mtaa wa Twiga na Sikukuu nyumba yake mkabala na Msikiti wa Shadhili Dar es Salaam.Katika miaka ya 1950 Shariff Attas alikuwa akifanyakazi Soko la Karikaoo Market Collector wa ushuru wa mnada wa nafaka. Market Master akiwa Abdulwahid Sykes. Sifa kubwa ya Shariff Attas ni ubingwa wake katika hesabu. Yeye alikuwa na uwezo wa kukokotoa hesabu ndefu kichwani bila ya kutumia ‘’calculator.’’ 

Kisa chake hiki ninachokieleza nimekisikia kwa masikio yangu mwenyewe miaka kadhaa nyuma takriban zaidi ya 25 hivi sasa..

Ilikuwa siku ya Eid El Fitr mimi na Kleist, mtoto wa Abdul Sykes tumekwenda kusali Eid Msikiti wa Kitumbini. Kleist ana uhusiano mkubwa sana na msikiti huu kwani hapo katika miaka ya 1930 babu yake alikuwa akienda kuswali hapo huku kafatana wa wanae Abdul, Ali na Abbas. 

Habari hii kanihadithia Ali Mwinyi Tambwe. Mzee Ali Mwinyi alikuwa kaniita nyumbani kwake Kinondoni Block 41 ili asahihishe baadhi ya mambo ambayo alikuwa kasoma katika mswada wa kitabu cha Abdul Sykes, mswada ambao mwane mmoja Abdulrahman Mbamba alikuwa kamwonyesha. Kabla ya kuanza mazungumzo yetu akanambia, ‘’Mimi Abdul hanipati kabisa mimi nikimuona akija kuswali na baba yake pale Kitumbini mtoto mdogo kashikwa mkono. Si huu msikiti unaouna hii leo, msikiti ule wa zamani.’’ 

Msikiti huu ndipo baba yake Kleist, Abdulwahid Sykes alipofanyiwa sala ya jeneza kabla hajakwenda kuzikwa Makaburi ya Kisutu. Kwa hiyo sikushangaa Kleist aliponiambia tukasali Eid Kitumbini. Nakumbuka wakati ule Kleist alikuwa na Mercedes Benz nyekundu, gari ya kupendeza sana. Nami nikawa sishi kumtia tashtiti kuwa kafuata nyayo za baba yake kwa kuwa baba yake amekufa gari yake ikiwa Mercedes Benz. Nikimpiga vijembe hivi yeye kazi ilikuwa kucheka tu.

Baada ya kumaliza kuswali na kupena mikono na wazee wetu…Kleist hapo yeye ndipo alikuwa anakutana na rafiki wa maehemu baba yake na sasa ni watu wazima sana yeye akawa kila akitoa mkono anaufumba anamwachia kitu mzee wake. Tulipomaliza akanambia, ‘’Mohamed sasa twende kwa Shariff Attas.’’ Tulipofika kwa Shariff Attas tukakuta veranda yake imejaa ‘’who’s who’’ katika wazee maarufu wa Dar es Salaam, mmoja wapo marehemu Bwana Hamida Tuli, muungwana wa Kizaramo kutoka Masaki. Bwana Tuli akiishi Mtaa wa Matumbi hapo jirani. Mikeka ya rangi nzuri nzuri imetandikwa na udi unatoa riha nzuri, Sinia zimejaa maakuli - kaimati, maandazi, visheti, vitumbua, tambi, katlesi, kababu, sambusa nk. Tumewakuta wazee wetu wanafuturu. Shariff kumuona Kleist kafurahi sana kupita kiasi anamwashiria aje akae ubavuni kwake. Mara tumeletewa sahani na vikombe tunakaribishwa chai.

Mara Bwana Hamida Tuli kasimama anaomba ruksa kwa niaba ya wenzake anasema, ‘’Shariff tunaomba ruksa tuondoke kwa kuwa tumelaikwa chai Ikulu kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.’’ 

Basi ikapigwa fatha ikaombwa dua wazee wakapeana mikono na Shariff Attas hao wakatimka kwenda Ikulu kunywa chai na rais. Ukumbi ukabaki mtupu tuko sie watatu tu - Shariff Attas, Klesit na mimi. Kleist akaangua kicheko kile cha kejeli. Shariff Attas yeye ni babu yake anamtania na kumuogelea atakavyo. Hizi ndizo mila zetu watu wa pwani.

‘’Duu, Shariff wenzako wote wanaalikwa Ikulu kwa rais, wewe uko hapa huna akujuaye!’’ Kleist anaangua kicheko. Shariff Attas hakuwa mdogo hivyo ni mtu maarufu kwa watu maarufu wa mjini na wenye  majina ya kutajika.

Shariff Attas yuko kimya kaagemea ukuta anamtazama kwa jicho la deko hasemi kitu. Kleist kamaliza kumcheka Shariff. Mkono unakwenda kwenye sambusa, kababu, kaimati.

‘’Kleist sikiza bwana. Mimi kama kuingia Ikulu ningeliingia enzi za Nyerere yeye ndiye alikuwa mwenzangu. Mimi Mwinyi atanijulia wapi?’’ Shariff Attas akaanza.

Mimi masikio yangu yashakuwa walu namtazama Shariff usoni. Picha naniyoiona siyo ile ya dakika mbili zilizopita. Namuona Shariff ghafla amebadilika anaacha maskhara anataka kusema jambo.

‘’Sikiza Kleist, hiyo ni 1954 Nyerere anakaa kwa baba yako pale Stanley ndiyo TANU inakuja juu. Nyerere kesha acha ualimu. Anakuja ofisini kwa baba yako pale Kariakoo Market. Ikifika mchana Abdul ananiita ananiambia nifatane  na Nyerere nyumbani kwa ajili ya chakula cha mchana. Mimi na Nyerere mguu kwa mguu, tunaingia Swahili, Narung’ombe, Gogo, Mchikichi, Sikukuu hadi Stanley kwa mama yako Mama Daisy. Njia nzima mimi na Nyerere tunazungunza. Wakati ule hakuna anaemjua. Tunafika nyumbani kwa baba yako chakula kipo mezani tunakula tukimaliza tunarudi ofisini pale kwa baba yako pale sokoni. Yeye alikuwa hatoki anaendelea na kazi. Nyerere alikuwa mwenzangu na mzungumzaji wangu sana wakati ule. 

Basi miaka ikenda hadi tukapata uhuru na Nyerere akawa Waziri Mkuu.

Siku hiyo mimi niko ofisi ya TANU ghafla Nyerere anaingia watu hamkani wamesimama na Nyerere anaanza kupeana mikono na watu walioko pale hadi akafika kwangu nami nikampa mkono. Nyerere akanitazama nami nikamtazama tukawa sote tunatazamana usoni. Nyerere akasema,‘’Mzee tumepata kukutana?’’ Mimi nikamjibu, ‘’Hapana hatufahamiani.’’ 

Basi akapita kusalimiana na watu wengine. Sasa Kleist mimi ilikuwa niingie Ikulu enzi za Nyerere rafiki yangu lakini bahati mbaya kanisahau.’’ 

Shariff Attas alikuwa mtu wa tasnifa sana. 

Akajinyoosha kaegemea ukuta anamtazama Kleist kwa mtazamo wa jicho la pemebeni huku uso umejaa tabasamu kama vile anamwambia mjukuu wake Kleist, ‘’Nimekukomesha kwa kutaka kwako kunicheka ati sijaalikwa Ikulu.''

Mimi nilishusha pumzi kwani nilikuwa nimechoka kwa kisa kile kilichokuwa kimetokea kwa wakati ule zaidi ya miaka arobaini nyuma. 

Kleist akaomba ruksa na Shariff akaturuhusu baada ya kupiga fatha. Kleist wakati tunatoka akaingia jikoni kwa mke wa Shariff Attas kwenda kuaga. 

Tulipokuwa sasa tunatoka nje Shariff Attas akampigia kelele Kleist, ‘’Kleist bibi yako umempa shilingi ngapi?’’ 

Kleist akacheka akamjibu Shairff, ‘’Nenda kamuulize mwenyewe.’’ 

Shariff akawa anacheka kwa ndani ya nyumba na sisi tunacheka hapo nje.



Kulia: Mwandishi, Yusuf Zialor, Kleist Sykes, Bubby, Abdallah Tambaza,
Waliochutama kulia: Abdul Mtemvu, Wendo Mwapachu na Kessy
Picha ilipigwa 1968

Mwandishi na Kleist Sykes kama walivyo hivi sasa
Picha imepigwa Msikiti wa Kipata 2014
Kulia: Dossa Aziz, Julius Nyerere, Abdul Sykes na Lawi Sijaona
Picha ilipigwa Arnautoglo Hall 1957 katika kunuaga Nyerere safari ya pili UNO
Photo
Hiyo hapo juu kulia katika gazeti ndiyo ilikuwa nyumba ya Abdul Sykes aliyoishi na Nyerere 1954
Nyumba hii ilikuwa Mtaa wa Stanley na Sikukuu

No comments: