Umenipeleka mbali sana kaka.
Ngoja nami nikupeleke Scotland Milimani kuna sehemu nadhani
wanaita Castle huko ni Edinburgh.
Hii ni sehemu maarufu kwa watalii.
Basi siku moja nimetoka Glasgow nimekuja Edinburgh kisha nikapandisha
mlimani kwenye ''castles,'' nanyoosha miguu.
Edinburgh, 1992 |
Nje kuna kibao kuwa Rider Haggard alikuwa akikaa hapa na kuandika vitabu
vyake.
Roho ikanindunda.
Huyu Rider Haggard ndiye mwandishi wa ''Allan Quatermain,'' ambamo ndani
ya kitabu hiki utamkuta huyo Umslopogaas.
Ninazo picha nikizipata nitazileta jamvini tustaladhi sote.
Kitabu hiki kilikuwa maarufu sana kwa sisi tuliokuwa shule katika miaka ya 1960.
Pamoja na kitabu hiki kulikuwa na kingine, ''Machimbo ya Mfalme Suleiman.''
Ukikishika hukiweki chini.
Siku hizo serikali ikitoa vitabu vya kusoma bure kwa shule.
Siku nyingine niko Paris nanyoosha miguu.
Nikakuta mtaa unaitwa, ''Alexandre Dumas,'' au ''Victor Hugo.''
Hawa pia walikuwa waandishi maarufu sana katika wakati wao.
Victor Hugo ndiye mwandishi wa ''The Hunchback of Notre Dame'' na Alexandre
Dumas aliandika, ''The Count of Monte Cristo.''
Nikasimama kuzubaa na kibao kile kwa muda.
Mwili unanisisimka kwani najua raha niliyokuwa nikipata utotoni katika vitabu hivi.
Mwandishi na James Brennan nyumbani kwake Magomeni Mapipa, Dar es Salaam 2010
Siku nyingine niko kwenye gari ya rafiki yangu James Brennan tunatoka Iowa ananileta
Chicago nipande ndege kwenda New York.
Tukafika Mississippi River.
Akawa ananieleza kuwa huu mto unaitwa Mississippi.
Nikamwambia, ''Jim hebu pumzisha pumzi zako mimi mto huu nyumbani kwangu.''
Mmarekani kashtuka hajanifahamu vyema.
Nikamwambia, ''Jim, mimi nilikuwa na rafiki zangu hapa - Tom Sawyer na Huckleberry
Finn.''
Jim akacheka sana huku anatingishwa kichwa.
''Mohamed you never cease to amaze me!''
Hawa Tom Sawyer na Huckleberry Finn ni ''characters'' katika kitabu cha Mark Twain.
Mmarekani kashangaa kuwa huyu Mswahili kawajuaje hawa watu?
Mshana Jr,
Ahsante sana kwa kunitia katika ''Time Machine,'' na kunirudisha nyuma nikawa mtoto tena
wa miaka 12.
No comments:
Post a Comment