Azam TV |
Abdul Sykes na Dr. Kleruu walianza kuandika historia ya TANU 1962/63
baada ya mazungumzo kati ya Abdul Sykes, Mwalimu Kihere na Dossa
Aziz.
Aliyekuja na fikra hii alikuwa Mwalimu Kihere na Nyerere akaunga mkono
na yeye ndiye aliyesema Abdul aandike kwa kuwa yeye anajuwa mengi
kutokana na historia ya baba yake Kleist Sykes, kuwa muasisi wa African
Association.
Abdul Sykes akajitoa baada ya kumdhihirikia kuwa kilichokuwa kinatafutwa si
historia ya kweli ya TANU na uhuru wa Tanganyika.
Dr. Klerruu alikamilisha ule mswada lakini kitabu hakikuchapwa hadi hii leo.
Inasemekana huu mswada na baadhi ya yale ambayo Abdul aliyoandika upo
katika maktaba ya CCM mahali fulani hakuna ajuaye wapi.
Hata hivyo kuna mwana TANU mmoja katika vijana wa Youth League aliuiba
huu mswada akabadilisha hapa na pale na kuchapa kitabu kwa jina lake alichokiita
historia ya TANU.
TANU walimuonya asichape tena kitabu kile.
Kitabu hiki mimi alinipa baba yangu na naamini kilimvunja moyo sana kwa yale
aliyokuta mle kwani yeye aliiona TANU ilivyoanza toka ile siku ya kwanza kwani
Abdul Sykes alikuwa rafiki yake wa karibu sana toka utoto wao.
Kitabu hiki hakina tofauti kubwa sana na kile kitabu cha Kivukoni College, ''Historia
ya TANU.''
Ikawa sasa kama imewekwa sheria fulani kuwa ni marufuku mtu kuja na historia
ambayo haitaanza na Mwalimu Nyerere.
Ikawa hata inaposemwa kuwa Nyerere alichukua uongozi wa TAA mwaka wa 1953
haielezwi kachukua vipi na kachukua kutoka kwa nani.
Ikawa kwa njia hii jina la Abdul Sykes halitajwi.
Ikawa vilevile ni mwiko mkubwa kueleza historia ya Waislam katika kuunda TANU na
kupigania uhuru wa Tanganyika kiasi mwaka wa 1988 gazeti la Africa Events (London)
toleo zima lilikusanywa kwa mimi kule kumtaja Abdul na Ally Sykes, Saadan Abdul
Kandoro, John Rupia na mchango wa Waislam katika kuasisi TANU.
Lakini jambo la kustaajabisha sana ni mfano wa Earle Seaton na Japhet Kirilo.
Hawa waliandika kitabu maarufu, ''The Meru Land Case,'' kuhusu mgogoro wa ardhi
iliyoporwa na Wazungu kule Meru.
Hii ilikuwa mwaka wa 1952 na wakati ule Abdul alikuwa Kaimu rais wa TAA na secretary.
Abdul alishughulika sana na kesi hii na yeye ndiye aliyemtaka Seaton aichukue kesi ile
na kuandika ''petition,'' kwenda UNO.
Ilipofika wakati wa Kirilo kwenda New York UNO Waingereza wakakataa kumpa pasi ya
kusafiria.
Abdul akahangaika kama rais wa TAA kusimama kidete hadi Waingereza wakasalimu amri
wakampa Kirilo pasi.
Kirilo na Seaton walipokuja kuandika kitabu chao, hakuna popote Abdul ametajwa.
Hili mimi linanistaajabisha hadi leo.
Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa kila mwandishi aliyekuja kuandika historia ya uhuru wa Tanganyika ukimtoa Judith Listowel, ''The Making of Tanganyika.''
Lakini kubwa kabisa ambalo mimi linanishangaza ni kuwa katika ''review'' ya John Iliffe na ya Jonathon Glassman kuhusu kitabu cha Abdul wote hawakubali kuwa Abdul ndiye muasisi wa TANU.
''Review'' zote hizi mbili ziko katika Cambridge Journal of African History.
Glassman yeye alinialika kuzungumza chuoni kwake Northwestern University, Evanston Chicago na nilizungumza katika ukumbi wa Eduardo Mondlane.
Mjadala ulikuwa mkali.
Lakini aliniambia kitu kimoja kuwa wao kabla yangu hawakujua kuwa katika kupigania uhuru wa Tanganyika kulikuwa, na kwa kutumia maneno yake, ''strong Muslim movement.''
No comments:
Post a Comment