Thursday 8 September 2016

TAAZIA: HAMZA RIJAL MCHEZAJI WA ZAMANI WA MALINDI ANAMKUMBUKA MOHAMED MSOMALI


Photo
Mohamed Msomali
(Picha kwa hisani ya Vijana Wapenda Soka wa Kariakoo)
ASALAAM ALAYKUM!
In Lilahi wa Ina Ilahi Rajiuna.

Mohamed Msomali Katutoka
na Hamzah Rijal

Mohamed Msomali katutoka.Katika mchezaji ambaye namkumbuka kwetu huku Afrika Mashariki mwenye ‘’quality,’’ ya Boby Moore wa England na Frantz Backenbeur sio mwengine ila ni Mohammed Msomali na Kadir Farah. 

Tanzania Bara na Tanzania Visiwani ni sehemu mbili katika nyakati tafauti zilizopata bahati huko nyuma kuwa na wachezaji mahiri na wenye sifa, Zanzibar imekwenda mbele zaidi kwa kuwa ilikuwa na wachezaji ambao wakicheza zaidi ya futuboli na hiyo michezo mengine wakiwakilisha taifa kati ya hao ni Machaprala akicheza Futboli na Hockey, Mzee Ahmed Islam akiitwa mchawi akicheza futboli, cricket, hockey na zote akichaguliwa taifa, mtu kama Zaghaluli Ajmy huyu ajabu yake aliwahi kuiwakilisha timu ya kabumbu ya Zanzibar akiwa mlinda mlango kisha akacheza mkoba.


Zaghaluli akawa anacheza Hockey na ndio muasisi wa watu weusi kucheza hockey Daresalamaa, akiwa na akina Oliver Maruma, Kombe na wengineo. Zaghaluli alikuwaw Pener katika Cricket, uchezaji wake kwa leo unaweza kumfananisha na Chris Gayle kwa kila sifa, mmoja ‘’height,’’ yao pili namna alivyokuwa akipiga ‘’boundries,’’  kuna mwenginenaye akicheza mpaka golf na tenis mbali ya football na hockey. Huko nyuma walikuwepo mzee Kidevu, Chepe, Mzee Sadati hawa wote wakicheza Futboli na Cricket. 

Zanzibar ikitoa wachezaji wa kupigiwa mfano kutoka kina Chepe, mpaka Shagoo, Nylon, Mohammed Kassim, Hijja Saleh na wengi wengineo. 

Bara kwa upande wake ilikuwa ni soka tu, utapotaja ‘’list,’’ kama ya Lukongo, Moyo, Mbwana Abushiri, Sharif, Azizi, Emanuel, Abdalla Luo, Omar Zimbwe, Saleh Zimbwe, Mweri Simba, Mwabuda, Haidar Abeid, Chuma wa Mtwara, Emanuel, Jella Mtagwa, Gilbert Mahinya na wengi wengineo hao wote kila mmoja ukimchukua unaweza kumfananisha na mchezaji yoyote yule wa Uingereza, Abdalla Luo hakuwa ana tafauti na Peter Crouch, Msoamali na Boby Moore, Zimbwe na Brian Lebone, Azizi na Lee Sharp, Haidar Abeid na Owen Hargrevas, Chuma na Teryy Cooper, Gilbert Mahinya na Billy Bremner, Mwabuda na Matta, kila mmoja utamlinganisha na mchezaji wa sasa au wa zamani na hana tafauti.

Tumzungumze Mohammed Msomali  ambaye leo nimeona maziko yake kupitia Star TV Alhamdulillahi watu wameitika. 

Msomali akiweza kuzuwia mpira kwenye box akaanza safari taratibu, mwili wake ulikuwa mwembamba lakini akiweza kucheza rafu usiweze kuamini na katika maziko yake leo amezungumzwa hata ufundishaji wake alikuwa akitaka wachezaji wamiliki zaidi mpira kuanzia nyuma, ikiwa ni Philosophy ya Gadiola hio, Msomali bahati mbaya kazaliwa Afrika na amefariki akiwa Afrika, lau angezaliwa Ulaya angekuwa anazungumzwa vyengine. 

Marehemu Kilambo alikuwa ni beki anayotumia nguvu zaidi na akitisha yeye na Kapera pale Yanga washambuliaji wakitafakari mara mbili kabla hawakuwa tayari kukabiliana nao, mara mmoja Yanga na Cosmopolitan, Kilambo kishachafua sawasawa kina Jamil, Aden, Marando, Iddi Balozi, ikawa wapo taabani, Msomali akampa fundisho Marehemu Kilambo alichukua mpira kisha akafanya umemponyoka, Kilambo hakujuwa kama ametegewa kwenda kupaua aliekewa kile tukikita kisiki, Kilambo alianguka akagarara akajua amepambana na kisiki lakini alikuwa mzima akarudi kiwanjani kwa kujua kakutana na mwamba mwenzake. 

Bahati mbaya sana Tanzania kuwa na watu kama Msomali, Emil Kondo, Sharif, Hemed Seif, Khalid Abeid wa nyakati zile ambao kwa leo wangesaidia sana pale ‘’midfield ,’’ ambayo haina ubunifu. 

Msomali akiweza kucheza namba 4 au 6 na mara nyengine akicheza 5. Kwenye Taifa kabla ya ‘’pair’’ ya Omar Zimbwe na Goboss ilikuwa unastaladha.  

Mwaka wa 1999 nilikutana na Marehemu Msomali pale Morogoro nikiwa kwenye mkahawa karibu na stand ya mabasi nikikaa lodge ikiitwa ''Maraha,'' hapo ndipo nikila chakula, Msomali alikuwepo hapo kenda kula hali yake wakati huo aliokuwa nayo sikuamini nilipomuona ''star,'' ambaye kama nilivyokwisha kutaja alikuwa anaitumikia taifa Yanga na Cosmopolitan akiwa amechoka. Sipendi kusema haya niyasemayo lakini nilikwenda kuzingumzanae  na nikamwambia mie ni mdogo wa kipa wao wa Cosmopolitan, Abdimout alifurahi sana. 


Msomali kwa umbo ni kama Allan Ball ambaye alikuwa katika timu ya Uingereza iliobeba World Cup mwaka wa 1966 kwani uchezaji wa Msomali nikutumia akili saa zote, mara nyengine unaweza ukamzungumza Msomali kama Johan Cruyff pale anapozuia mpira kisha akatoa pasi akakuambia umrejeshee palepale ambao kazongwa na wapinzani, wakati wake Afrika Mashariki alikuwa ni yeye na Kadir Farah wa Kenya ndio peke yao wakifanya hivyo, ila Kadir Farah alikuwa na kasi, Msomali hakuwa na hiyo kasi. 

Cosmopolitan imeondokewa na Taifa Star nayo imeondokewa, Tunamlilia Msomali, kaondoka kama walivyoondoka kina Kilambo, Lukongo, Hemed Seif na wengineo, baada ya kuzikwa taifa litamsahau kama walivyosahuliwa wengine,


Allah amjaalie Janahnatul Firdaws, Ameen.

Kushoto wa kwanza ni Mohamed Msomali akicheza timu ya Kombaini ya East African
Cargo Handling Services katika miaka ya1960/70

Rafiki na ndugu yangu Hamza Rijal ni mchezaji wa zamani wa Malindi Sports Club Zanzibar. 

Kaniandikia binafsi mistari michache kunieleza habari za Mohamed Msomali lakini nimeona niweke hapa kwa faida ya wasomaji na wapenda soka kwa ujumla. 

Kwanza nimecheka nilipokuwa namsoma Hamzah khasa pale alipoeleza staili ya uchezaji wa Msomali katika kupunguza nguvu za wapinzani wake. 

Nimecheka kwa saabu yeye Hamza akicheza nyuma na alikuwa ‘’no nonsense defender.’’ 

Alikuwa kama Msomali bingwa wa kuwaadhibu, ‘’strikers.’’ 


Photo
Kushoto watatu waliochuchumaa ni Hamzah Rijal Malindi Sports Club 1973
Sasa ungekuwa unamjua Hamza nje ya uwanja kwa ule upole na ustaarabu wake kisha ukamuona uwanjani anavyowaparamia, ‘’strikers,’’ ungejiuliza inakuwaje huyu mtu akawa hivi? 

Njiwa nje ya uwanja na tai ndani ya uwanja? Sijashangaa hata kidogo kwa ''tasnifu,'' hii yake ya Mohamed Msomali kwani Waingereza wana msemo wao, ‘’Birds of a feather fly together.’’

Hamzah Rijal amepata elimu yake ya juu Libya na Scotland. Baba yake marehemu Zubeir Rijal alisoma Chuo Kikuu Cha Oxford katika miaka ya 1940. 


Hamzah Rijal


No comments: