MAISHA
NA NYAKATI ZA ABDULLA KASSIM HANGA
Ahmed Rajab
ASALAAM alaykum wa RahmatuLlah wa
Barakatuhu. Nina mawili matatu ninayotaka kusema kabla ya kuiingilia mada
yetu.
Kwanza, nawashukuruni kujumuika nasi
kumkumbuka mwana wa Zanzibar, ambaye licha ya udhaifu wake na pengine makosa ya
hapa na pale, ni mmoja wa vigogo wa siasa za Zanzibar. Na ninamshukuru
zaidi ndugu yetu Sheikh Muhammad Yusuf na taasisi yake kwa kutupatia nafasi hii
ya “kumfufua” Hanga.
Pili, nawaomba radhi kwamba siko nanyi
tukaweza kumzungumza pamoja Al Marhum Sheikh Abdulla Kassim Hanga.
Madhumuni ya mhadhara kama huu yawe si kusikiliza tu mtu kama Hanga amesoma
wapi, amefanya nini au amekula mandazi kwa mbazi au kunde, lakini yaweze pia
kutupa fursa ya kujifunza mawili matatu kutokana na maisha yake.
Yupo wa kumlaumu kwanini sipo hapa
nanyi. Na si mwengine ila Muhammad Yusuf kwa ubakhili wake wa
kutoniwezesha kufika.
Mwisho nataka kuwajulisha kwamba mengi
nitayoyasema leo nimeyadokoa kutoka kwenye muswada wangu wa maneno
yanayokaribia 20,000 (elfu ishirini), muswada ambao bado haujakamilika
kuchapishwa na uitwao “The Killing of Hanga” (Mauaji ya Hanga).
Bado muswada huu ungali “work in progress”
na kwa hivyo, kutadhihirika mapengo ya hapa na pale katika nitayoyasema
leo. Ni matumaini yangu kwamba kutatokea hapa wataoweza kuyajaza mapengo
hayo.
Ama baad,
Wiki iliyopita nilihudhuria hafla moja
jijini London ambapo mshairi mmoja binti wa Kipalestina, Jehan Bseiso, akisoma
baadhi ya mashairi yake.
Kuna kipande cha mshororo wa shairi lake
moja kilichonikaa moyoni tangu nikisikie. Chasema: “Hata waliokufa nao
huzeeka…”
Lau angelikuwa hai, Abdulla Kassim Hanga
leo angelikuwa “Mzee” wa miaka 84. Alipouliwa 1969 alikuwa kijana wa
miaka 37 tu.
Sijui kuna siri gani lakini wanaharakati
wengi walio vipenzi vya umma huiaga dunia wakiwa katika rika hilo. Frantz
Fanon, aliyezaliwa kisiwani Martinique na aliyeyakumbatia Mapinduzi ya Algeria
na akawa Mualgeria, alifariki akiwa na miaka 36; kadhalika, Patrice Lumumba wa
Congo, naye alikuwa na umri huohuo wa miaka 36; Walter Rodney, mwanahistoria
kutoka Guyana aliyewahi kusomesha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliuliwa akiwa
na umri wa miaka 38. Malcolm X naye aliuliwa miezi mitatu kabla hajatimia miaka
40.
Hanga wa kihistoria hakuwa na
bahati. Alionewa kwanza na wenzake alioshirikiana nao kuyaandaa na
kuyaongoza mapinduzi ya Zanzibar ya 1964. Wao ndio waliomdhulumu
roho yake. Akaonewa tena na historia iliyomnyanyua halafu ikamtupilia
mbali, asisikike tena.
Hii leo Hanga, aliyekuwa akivuma zama za
kupigania uhuru wa Zanzibar, amesahaulika.
Nimesema “amesahaulika” ingawa sidhani
kama “amesahaulika” ni tamko sawa. Hanga hakusahaulika. Amesahauliwa
kwa kusudi. Watawala hawataki akumbukwe. Nasema hivi kwa
sababu kumkumbuka Hanga ni kuufichua uhaini aliofanyiwa na wapinduzi wenzake
pamoja na Mwalimu Julius Nyerere, aliyemleta machinjoni Zanzibar ya siku zile.
Kwa kadhia hiyo tu Nyerere hawezi
kusafishika. Na nathubtu kusema kwamba itamyima “utakatifu” (sainthood) ambao
wapambe wake wanampigania apewe huko Vatikani, kwenye Makao ya Papa.
Angelikuwa Hanga ameishi nchi nyingine,
hii leo tungeshuhudia mengi yakiitwa kwa jina lake: majengo, skuli,
viwanja vya mpira, barabara au taasisi mbalimbali. Lakini bahati yake
ilikuwa kuzaliwa nchi isiyowathamini watoto wake.
NIMKUMBUKAVYO HANGA UTOTONI MWANGU
Ingawa siasa zikimwenda katika damu yake
tangu alipokuwa mwanafunzi Hanga aliangukia kwanza kuwa mwalimu kabla hajawa
rasmi mwanasiasa. Alikuwa mwalimu aliyekuwa akipendwa na wanafunzi wake
wa kila kabila lakini umaarufu wake aliupata katika medani ya kisiasa,
hasa katika siasa za usoshalisti wa kimataifa na katika mapinduzi ya Zanzibar.
Mimi binafsi nilianza kumjua alipokuwa
mwalimu na nilipokuwa nasoma skuli ya “primary” ya Darajani katika miaka
ya kati ya 1950. Wakati huo Hanga alikuwa anamaliza masomo yake ya ualimu
katika Seyyid Khalifa Teachers’ Training College, Beit-el-Ras.
Aliletwa Darajani kufanya mazoezi ya
kusomesha (teaching practice). Kwa muda mfupi alinisomesha somo la
Kiingereza. Alipohitimu masomo yake ya ualimu, akarudishwa skuli ya
Darajani ambako pamoja na kusomesha alikuwa pia akisimamia mambo ya riyadha na
kuogolea. Alikuwa “sports Master”.
Miaka hiyo ya 1950 mara kwa mara
nikikumbana naye jioni nilipokuwa nikitoka kwetu Vuga kwenda Baraste Kipande
kumzuru bibi yangu. Nyumba ya bibi yangu ilikuwa karibu sana na nyumba ya
dada yake Hanga. Saa hizo za jioni Hanga akipendelea kwenda Jogoo Club
kucheza bao au dhumna.
Jogoo Club ilikuwa kama barza ya
Mahizbu, wafuasi wa chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP). Hanga
alikuwa Afro, mfuasi wa Afro-Shirazi Party (ASP), chama kilichokuwa kikipingana
vikali na kile cha Hizbu. Jogoo ndiyo iliyokuwa nembo ya chama cha
Hizbu. Juu ya yote hayo, Hanga hakuona taabu yoyote kwenda kupiga soga
Jogoo Club.
Hanga wa siku hizo alikuwa mtu wa
mbwembwe na mikogo. Alikuwa na mwendo wa kuyumbayumba, akipiga hatua huku akitikisa
mabega yake. Mtu mwengine angelikuwa anakwenda kama yeye angeonekana kinyago
cha kuchekwa. Lakini huo mwendo wa mbwembwe ulimsibu Hanga kwa urefu wake na
umbo lake. Ilikuwa kama mwendo huo aliumbiwa nao.
Hanga alifanikiwa kuitia mikogo yake
bila ya kuonesha kama akijidai. Na hakuwa mtu wa kujidai wala mwenye majivuno.
Wala Hanga hakuwa na watu waliokuwa
wakimfuata na kumuigia lakini walikuwepo watu waliokuwa wakimhusudu kwa namna
alivyokuwa akiipenda lugha ya Kiingereza. Walikuwepo wengine waliokuwa
wakimdhihaki kwa alivyokuwa akiupenda uzungu; si bure kwamba kuna baadhi ya
watu waliokuwa wakimwita “Ba Zungu”.
Alikumbwa na ule ugonjwa aliouelezea
Frantz Fanon kwenye kitabu chake Black Skin, White Mask, ugonjwa
uliokuwa ukiwafanya Waafrika wadanganyike kimawazo kwamba wakifikia kiwango
fulani cha elimu watakubalika kwa watawala na watapewa dhamana katika dola.
Viongozi wengi wa Kiafrika waliokuwa na
hamu ya kuwaiga wakoloni Wakizungu waliambukizwa ugonjwa huo, hata kiongozi
mfano wa Kwame Nkrumah katika ujana wake. Na walikuwa nao ugonjwa huo
mpaka walipotanabahi kwamba nawasome vipi lakini wakoloni Wakizungu
hawatowakubali kuwa ni sawa nao. Daima wataendelea kuwa chini yao.
Hanga aliishi na ugonjwa huo mpaka
alipoanza kuamka kisiasa. Mwamko wake, hata hivyo, haukuwa wa mara moja.
Aliamka pole pole. Akaanza kufuata itikadi nyingine.
Alipoiangalia jamii ya Zanzibar aliiona
jamii iliyogawanyika. Licha ya kuwa na dini moja na utamaduni unaoweza
kusema kuwa ulikuwa mmoja kwa kiwango kikubwa, hata hivyo kila jamii (kabila)
ilikuwa na ya kivyake. Nadhani hichi ndicho alichokiona mwandishi wetu
adhimu wa riwaya, Abdulrazak Gurnah.
Katika riwaya yake inayosifika sana na
iitwayo Admiring Silence, Gurnah ameandika kwamba miaka hiyo kila
kabila la Zanzibar lilikuwa likiishi katika “historical ghettoes” zake.
Kila kabila lilikuwa limefungika na ya kwake. Ndiyo tulikuwa na utamaduni
mmoja lakini kila kabila lilikuwa na mkondo wake wa kitamaduni uliokuwa
umefungika ndani ya kabila hilo.
Lililozidi kumshughulisha Hanga,
aliyekua anaanza kuamka kisiasa, ni imani yake kwamba mfumo wa kikabila
uliokuwepo ulilinufaisha tabaka fulani la wakaazi wa Zanzibar na kwamba mtu
kama yeye, aliyejiona kuwa ni “Mwafrika halisi”, akiangaliwa vingine.
Hanga wa ujanani na aliyeanza kuamka kisiasa hakuamini kwamba Wazanzibari
walikuwa wakiishi katika jamii moja iliyojaa furaha tupu.
Wacha nisimumunye maneno, Hanga akiamini
kwa dhati kwamba wale waitwao “Waarabu” hapa Zanzibar au wale wanaojinasibisha
na “Uarabu" ndio waliokua na ulwa, ndio waliokuwa juu katika jamii na
Waafrika ndio waliokuwa chini.
Najua kuna wengi wanaoipinga dhana hii
na kuna hoja nyingi ambazo mtu anaweza kuzitoa kuonesha kwamba dhana hiyo ni
potovu. Juu ya hayo, hatuwezi kuipuuza kwasababu hisia za waliokuwa
wakiiamini dhana hiyo ndizo zilizochangia pakazuka mapinduzi na chuki
zinazoenezwa na watawala ingawa si na wananchi.
Isitoshe, kwa sababu ya kuwepo kwa hisia
hizo Sheikh Abeid Karume, kiongozi wa ASP, aliweza kuwashawishi zaidi ya nusu
ya wakaazi wa Zanzibar kwamba “ukabila” na “upendeleo wa kikabila” yalikuwa
mambo ya hakika. Walimuunga mkono kwa sababu walimuona kuwa yeye ndiye
sura ya uananchi wa Kiafrika. Wapinzani wake, kwa upande mwingine, walikuwa na
hakika kwamba alikuwa sura ya uovu.
Hivyo ndivyo jamii ya Zanzibar
ilivyokuwa imegawika siku hizo. Kuiangalia Zanzibar hivyo ni kuitathmini
kijuujuu kwa sababu si Waarabu wote waliokuwa katika tabaka la mabwanyenye
(bourgeois class), wengi wakiishi maisha ya chini sawa na hao waliokuwa
wakiitwa “Waafrika”. Lakini tusiyaingilie hayo kwa sasa asije Hanga
akatupotea.
HANGA NA SIASA ZA KIKABILA
Hanga wa ujanani mwake alikuwa
akizifuata siasa za kikabila zilizokuwa zikihubiriwa na chama chake cha ASP,
kilichokuwa kikiupinga, kile chama hicho ilichokiita “ubwana wa Waarabu”.
Hanga akavuka mpaka. Akaanza kuupinga na ufalme, usultani. Kulikuwa
gazeti lililokuwa likiitwa MWIBA, ufupisho wa “More Work Illustrate Better Africa”,
lililokuwa likimilikiwa na kuhaririwa na Marehemu Jamal Ramadhan Nasib.
Gazeti hilo liliporipoti matamshi ya
Hanga ya kuupinga usultani, Jamal Nasib alilazimishwa kumuomba radhi sultani
kupitia redio ya Sauti ya Unguja na pia kwenye gazeti la serikali lililokuwa
likiitwa Maarifa.
Hanga aliupinga usultani licha ya kwamba
dadake, yule aliyekuwa akiishi Baraste Kipande alikuwa mke wa pili wa jamaa wa
aila ya Kifalme, Seyyid Farid. Huyu alikuwa mwana wa Sultan Seyyid Ali
bin Hamoud, ambaye 1911 baada ya kwenda London kuhudhuria sherehe ya kutawazwa
Mfalme George V (wa tano) alilazimishwa na Waingereza ajiuzulu. Ufalme
akapewa shemeji yake Seyyid Khalifa bin Haroub, babu yake Sayyid Jamshid bin
Abdulla, mfalme wa mwisho wa Zanzibar.
Mama yake Seyyid Ali alikuwa
Mnyasa. Alipokuwa mdogo alipelekwa Uingereza kusoma katika skuli ya
Harrow na alikuwa mfalme pekee wa Zanzibar ambaye baadhi ya nyakati akiacha
kuvaa majokho na akipiga suti na tai. Baada ya kupokonywa ufalme aliishi Paris,
Ufaransa, ambako alifariki Desemba 20, 1918.
Kama nilivyokwishasema mwanawe, Seyyid
Farid, alikuwa shemeji yake Hanga. Alizaa watoto kadhaa na dadake Hanga.
Kwa vile akiupenda usomi na akizipenda
siasa Hanga aliwavutia viongozi wa jumuiya ya African Association ambayo
ilikuwa dhaifu. Jumuiya hiyo iliasisiwa 1934 na wafanyakazi Wakiafrika,
wengi wao wakiwa wahamiaji Wakikristo kutoka Tanganyika na hadi Malawi.
Haikuchukua muda Hanga akawa kipenzi cha
jumuiya hiyo kabla haijaungana na jumuiya ya Washirazi, Shirazi Association,
kuunda chama cha siasa cha Afro-Shirazi Party (ASP). Jumuiya hiyo
ilimpenda Hanga kwa sababu alikuwa na ujasiri wa kuyatamka yale ambayo yakiogopwa
kutamkwa na viongozi wa Jumuiya hiyo waliokuwa wamesoma na waliokuwa wakiogopa
wasivitie vitumbua vyao mchanga kwa vile walikuwa watumishi wa serikali ya
kikoloni.
Miongoni mwa viongozi hao walikuwa
Maalim Aboud Jumbe, aliyekuwa mwalimu wa skuli ya serikali ya sekondari ,
na Sheikh Ali Khamis, mtumishi wa serikali aliyesomea Uingereza.
Watu kama hao waliliacha jukumu lao la kihistoria la kuwatetea Waafrika wenzao.
HANGA AELEKEA ULAYA
Nadhani ilikuwa 1957 baada ya kuasisiwa
ASP Hanga alipoondoka Zanzibar kwenda London akifadhiliwa na chama hicho.
Marafiki zake wanakumbuka kwamba alikodi chumba katika nyumba ya bibi mmoja wa
Kizungu katika mtaa wa Clapham Common, kusini mwa London. Wanakumbuka pia
kwamba chumba chake kilikuwa nadhifu sana.
Alipofika alikuwa akisomea masomo ya GCE
“A” levels katika skuli ya Westminster College ili aweze kuingia chuo kikuu.
Ilisadifu kwamba mwishoni mwishoni mwa 1964 nami nilijiunga na skuli hiyohiyo,
iliyokuwa eneo la Westminster karibu na Victoria, kwa madhumuni hayo hayo.
Hanga alikuwa na hamu akimaliza ajiunge
na London School of Economics And Political Science (LSE), ambayo ni sehemu ya
Chuo Kikuu cha London. Huko ndiko alikosoma Jomo Kenyatta, Rais wa mwanzo
wa Kenya, na ndipo aliposoma Salim Rashid, katibu wa kwanza wa Baraza la
Mapinduzi la Zanzibar.
Bado sikujua kwa nini lakini mambo
yalimwendea vingine Hanga. Alipewa msaada wa masomo (scholarship), na
akaukubali, wa kwenda Moscow kusomea mambo ya uchumi katika Chuo Kikuu cha
Lumumba.
Kuna jambo jengine lililomtokea London
na bado sikuupata undani wake wa namna lililovyoanza. Na jambo lenyewe ni
usuhuba mkubwa aliokuwa nao na Oscar Kambona, mwanafunzi wa sheria aliyetokea
Tanganyika. Kambona hakumaliza masomo yake kwa sababu Nyerere alimwita arudi
Tanganyika kwenda kusaidia harakati za kupigania uhuru.
Hadithi ya Kambona ni ndefu na hapa sipo
mahala pake. Naitoshe tu tukikumbusha kwamba Hanga alikuwa na usuhuba naye na
kwamba usuhuba huo ulichangia baadaye kuyaponza maisha yake.
HANGA AKIWA MOSCOW
Huko Moscow, Hanga alimuona, akampenda
na hatimaye akamuoa mwanamke wa Kirussi, Lily Golden. Lily alikuwa Mrussi
mweusi. Babake alikuwa Mmarekani mweusi, John Oliver Golden na mamake,
Bertha Bialek, alikuwa Yahudi aliyezaliwa Poland.
Baba mkwe wa Hanga alikuwa mtaalamu wa
kilimo na Mkomunisti maarufu kutoka Mississippi. Alikuwa rafiki wa
wanaharakati wengine Wamarekani weusi waliokuwa pia maarufu. Miongoni mwao
walikuwa mwimbaji Paul Robeson, mshairi wa Harlem na mwandishi Langston Hughes,
mshairi mwengine na mwandishi wa riwaya Claude McKay na kiongozi wa wafanyakazi
George Padmore.
Nina mengi kuhusu wakwe zake Hanga ambao
wote wawili walikuwa Wakomunisti. Hapa nitayafupisha maelezo yao. Kwa ufupi,
walihamia Urussi katika miaka ya 1930 ambako binti yao Lily alizaliwa.
Hanga hakumuona babamkwe wake kwa sababu
alifariki 1940. Lakini alimuona mama mkwe wake aliyefariki 1985. Binti
yao Lily alisomea historia katika Chuo Kikuu cha Moscow State University na
baadaye akawa profesa katika Taasisi ya Mitaala ya Kiafrika, Moscow. Aliwahi
pia kuuwakilisha Muungano wa Sovieti katika mashindano ya mchezo wa
tenis. Alifariki Desemba 2010 akiwa na miaka 76.
Mara ya mwanzo Hanga kumuona Lily
ilikuwa 1957 alipohudhuria Tamasha la Kimataifa la Vijana, jijini Moscow.
Kuna Wazanzibari wenzake waliomuona mwanzo na wakamhadithia Hanga.
Sikuwajua walikuwa akina nani ingawa nadhani Ali Sultan Issa alihudhuria
tamasha hilo.
Siku moja saa za usiku 1958 Hanga
alipiga hodi kwa Lily, akamlilia hali akitaka kumuoa. Alikuwa ameolewa
kwa muda wa miezi michache tu na mpiga piano na mumewe akafa katika ajali ya
gari. Huyo mumewe alikua mtoto wa watu, wa familia ya wasomi Wakirussi waliokuwa
wakiheshimika.
Lily mwanzo akisitasita kumkubali Hanga
lakini mamake akimshikilia amkubali. Ilipita miaka miwili kabla ya Lily
kukubali kuolewa na Hanga na ndoa yao ilifungwa 1960. Walijaaliwa binti mmoja,
Yelena Khanga.
Nilikutana na Yelena alipopita London
akiwa njiani kuja Zanzibar kuwatafuta jamaa zake. Nililetewa na mjombake
Hanga, Marehemu Mohamed Ibrahim aliyekuwa baharia aliyeishi London kwa maka
mingi. Sadfa nyingine ni kwamba huyu bwana ndiye aliyenipokea London 1964
na akanikaribisha kukaa kwake. Alipomleta Yelena ofisini kwangu akitaka
nikamjulishe na Abdulrahman Babu, ambaye siku hizo akiishi London. Ukimuangalia
Yelena ni kama Hanga aliyejizaa, sema yeye ni mwanamke.
Yelena anatafahari kuwa yeye ni Mrusi
mweusi na Mmarekani. Ni maarufu Urussi kwa vile alikuwa akiendesha vipindi vya
televisheni vyenye kuvutia. Yeye na mama yake wote wameandika
vitabu. Chake kinaitwa Soul to Soul na cha mama yake
kinaitwa My Long Journey Home. Alikiandika baada ya kuhamia
Marekani 1988. Mwaka 1993 akisomesha Chuo Kikuu cha Chicago State
University.
Masomo ya Hanga Moscow yalikuwa ya muda
wa miaka mitano lakini Lily ameandika kwamba alimaliza masomo hayo kwa muda wa
mwaka tu. Vipi Hanga aliweza kufanya hivyo sijui.
Hata hivyo, baada ya kumaliza masomo
alibaki kwa muda Moscow na akisafirisafiri kwenda Zanzibar na London ambako
akishiriki katika mazungumzo kuhusu katiba mpya ya kuipatia uhuru Zanzibar.
Alipokuwa Moscow, Hanga alikuwa
akidekezwa na kuengwaengwa na Warussi. Maisha yake na mkewe yalikuwa ya raha.
Walipewa fleti nzuri iliyokuwa na vitu vya anasa. Ilikuwa fleti waliyowekewa
waheshimiwa kutoka nchi za nje. Lily amesema kwamba alikuwa akipata mambo
asiyowahi kuyapata kabla. Walikuwa na watumishi waliokuwa wakiwahudumia.
Wakiletewa matunda na nyama. Na waliekewa sinema yao ya kuangalia michezo
kwenye chumba chao cha kulala.
Kuna mambo aliyoyasema Lily ambayo
yamenivunja moyo. Kwa mfano, ameeleza kuwa japokuwa Hanga alikuwa mfuasi wa
Marx na hivyo mtu wa kimaendeleo, moyoni mwake khasa alikuwa mtu wa ujinsia,
yaani akipendelea mfumodume. Akaongeza kuwa Hanga alikuwa kama mchukia
wanawake (misogynist) kwa sababu alipozaliwa Yelena, alivunjika moyo kwamba
hakujaaliwa mtoto wa kiume.
Si hayo tu lakini Lily pia alieleza
kwamba Hanga alikuwa na wivu kupita kiasi. Alikuwa hamruhusu mkewe achanganyike
na wanaume, hata wenzake kazini au marafiki zake yeye Hanga. Kila Lily
alipotaka kutoka ilimbidi kwanza amuombe ruhusa Hanga. Wakiwakaribisha wageni
wa kiume nyumbani, Hanga alimlazimisha mkewe akae kimya, asifungue mdomo. Pia
alimzuia asende kazini alipokuwa Hanga yuko mjini Moscow.
Hanga alikuwa na wake wengine wawili:
mmoja Mguinea na mwengine Mzanzibari, Marehemu Bimkubwa Said “Maghee” aliyekuwa
mwalimu wa skuli na aliyefariki dunia Dar es Salaam miaka michache iliyopita.
HANGA NA BABU
Hatuwezi kumzungumza Hanga bila ya
kumgusa Abdulrahman Mohamed Babu kwa sababu baada ya Mapinduzi ya 1964, nchi za
Magharibi zikiwaona kuwa ndio wakorofi wa Zanzibar waliokuwa na nia ya kuueneza
ukomunisti Afrika ya Mashariki nzima.
Babu na Hanga walikuwa waumini wa
itikadi ya Kimarx. Lakini Zanzibar walikuwa wafuasi wa vyama tofauti. Babu
alikuwa katibu mkuu wa zamani wa ZNP (Hizbu) na baadaye Mwenyekiti wa Umma
Party. Hanga alikuwa mmoja wa vigogo vya ASP na aliporudi Zanzibar baada
ya kumaliza masomo Moscow aliteuliwa msaidizi wa katibu mkuu.
Hata Ukomunisti wa kimataifa ulipogawika
na kuwa na mapande mawili la Sovieti na la China, Babu na Hanga nao pia
waligawika. Babu akiwaunga mkono Machina na Hanga Wasovieti. Mapambano ya pande
hizo mbili yalikuwa makali.
Hanga na Babu wakitafautiana kwa mengine
pia. Kwanza walipita njia tafauti kuufikia Umarx. Hanga aliufikia kwa
kupitia tarika ya uananchi wa Kiafrika. Babu, ingawa alikuwa muumini wa
umajumui Wakiafrika (pan-Africanism) aliufikia Umarx kwa mtazamo wa kimataifa
(cosmopolitan outlook) ingawa siasa zake za awali zilikua zikielemea falsafa ya
“anarchism”, ya mfumo wa utawala huria usio na serikali.
Ingawa wote walikuwa na haiba lakini
khulka zao zikitafautiana. Hanga akionekana kama saa zote akisononeka, akiwa
katika mafikra. Babu lilikuwa jitu la raha, akipenda kustarehe na alikuwa
mcheshi na mtu wa mizaha.
Ntatoa mfano wa nämna walivyokua
wakiangalia sinema. Wakati Babu akionekana kama mgaagaa na njia
(Bohemian) akenda sinema ili kujifurahisha, Hanga, kwa mujibu wa mkewe Lily,
alikuwa hendi sinema kwa kujipumbaza tu. Alikuwa akenda sinema alipokuwa
akijua tu kwamba atajifunza kitu cha kisiasa, kitachoitanua elimu yake ya
kisiasa.
Lily amesema kwamba baada ya kufunga
ndoa, Hanga alimwambia amuandikie orodha ya filamu za Kisovieti zitazoweza
kumuendeleza kisiasa. Akampa mifano ya filamu bubu Battleship Potemkin na October (maarufu
kwa jina la Siku Kumi Zilizoutikisa Ulimwengu). Filamu zote mbili
zilifanywa na mwananadharia wa filamu za kimapinduzi Sergei Eisenstein.
Hanga alikuwa kama mtu aliyepandwa na
pepo wa kisiasa, aliyehitaji kupungwa. Alikua kama akichukua hatua zake zote
kwa sababu za kisiasa, tena siasa kali.
HANGA NA MAPINDUZI
Sitozungumzia jinsi Hanga alivyoshiriki
katika Mapinduzi. Dk. Harith Ghassany ameyaeleza mengi kwenye kitabu
chake Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru.
Labda niseme tu kwamba juu ya tafauti
zao zote, Babu na Hanga walikuwa na lengo moja wakati wa mapinduzi ya Zanzibar.
Hata kabla ya mapinduzi, Babu na wafuasi wake wa Umma Party
wakishirikiana na viongozi wa mrengo wa kushoto wa ASP, wakiwemo Hanga, Hassan
Nassor Moyo, Abdul Aziz Ali Twala na Saleh Saadalla.
Umma Party haikuyapanga mapinduzi ya
Zanzibar ya 1964 ingawa makada wake walishiriki baada ya serikali ya Shamte
ilipokuwa imekwishaangushwa.
Mpangilio wa Serikali ya kwanza ya
Mapinduzi ulimuorodhesha Sheikh Karume awe Rais, Hanga waziri mkuu na Babu,
waziri wa mambo ya nje.
Mkutano wa kwanza wa Baraza la Mapinduzi
ulikuwa na vituko vyake. Karume aliwashangaza wote waliohudhuria kwa namna
alivyonuna na alivyoukataa urais. Hakutafuna maneno.
“Sitaki kuvishwa kilemba cha ukoka,”
aliwafokea wajumbe wa Baraza la Mapinduzi.
Hanga alishtuka. Akaanza kubabaika.
Karume alisema aliyoyasema kwa sababu akijua kwamba madaraka halisi alikuwa
nayo Hanga aliyekuwa waziri mkuu mwenye nguvu za utendaji (executive
powers). Cheo cha urais alichopewa Karume kilikuwa kama cha kumfutia
machozi.
Hanga alikuwa dhaifu mbele ya Karume na
akasema hakuwa akiyataka madaraka aliyopewa. Babu alinieleza mara kadhaa
kuhusu kisa hicho na kila mara akinambia kwamba akimvuta suruali yake Hanga
chini ya meza ili asiyaachie madaraka lakini Hanga alikuwa amekwishamridhia
Karume.
Kisa hiki niliwahi kuhadithiwa pia na
Salim Rashid, aliyekuwa katibu wa Baraza hilo, pamoja na nikikumbuka na Khamis
Abdalla Ameir, aliyekuwa mjumbe wa Baraza. Khamis Abdalla Ameir alikuwa mmoja wa viongozi wa Umma Party
na wengi tukimuona kuwa ndiye aliyekuwa
theoretician wetu.
Kama Sheikh Khamis yupo hapa leo labda atatueleza zaidi. Sisemi kama Hanga alikuwa hajui kuzicheza siasa sawasawa lakini labda ilikuwa moyo wake safi na utiifu wake kwa Karume uliomponza.
Kama Sheikh Khamis yupo hapa leo labda atatueleza zaidi. Sisemi kama Hanga alikuwa hajui kuzicheza siasa sawasawa lakini labda ilikuwa moyo wake safi na utiifu wake kwa Karume uliomponza.
Hamna shaka yoyote kwamba lau Hanga
asingetetereka basi Zanzibar ingeufuata mkondo mwingine. Kwa hivyo, kuanguka
kisiasa kwa Hanga na hata kuuliwa kwake ni mambo aliyojichongea mwenyewe kwa
kuridhia kuuacha uwaziri mkuu.
Wadhifa wa uwaziri mkuu ukafutwa na
Hanga akateuliwa Makamu wa Rais.
Muungano ulipoundwa miezi mine baadaye
Karume akaongezewa cheo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania. Hanga
pamoja na Babu wakahamishiwa Dar es Salaam na wakateuliwa mawaziri.
Hanga alijichongea pia kwa kumshikilia
Karume aukubali Muungano. Kwa mujibu wa Sheikh Aboud Jumbe katika kitabu
chake The Partner-ship Nyerere alimpelekea Karume
wajumbe wawili, Oscar Kambona na Bi Titi Mohamed, kumshawishi akubali
kuiunganisha Zanzibar na Tanganyika. Hakufanikiwa.
Nyerere alifanikiwa pale tu alipomtumia
Hanga na Saleh Saadalla wamshawishi Karume. Ilikuwa kama Hanga alijichimbia
kaburi mwenyewe, kwani usuhuba wake na Kambona baadaye ulimghadhibisha Nyerere
na lazima ulichangia katika uamuzi wake wa kumpeleka Hanga Zanzibar alikotakiwa
na Karume na alikouliwa.
Tangu mapinduzi nchi za Magharibi
zilitishika na Zanzibar. Na zilizidi kutishika mwezi mmoja kabla ya
Muungano kuundwa pale Salim Rashid, mmoja wa viongozi wa Umma Party,
alipolisoma uwanja wa Mnazi Mmoja lile liitwalo “Tangazo la Machi 8”. Tangazo
hilo liliainisha sera za Serikali ya Mapinduzi. Kwa hakika, tangazo zima
lilikuwa ilani ya Umma Party. Ndipo nchi za Magharibi zilipoanza kuiita
Zanzibar kuwa ni “Cuba ya Afrika”, hasa baada ya kuimarisha mahusiano
yake na nchi za Ulaya ya Mashariki, zikiwa pamoja na Ujerumani ya
Mashariki ya wakati huo.
Mwezi uliofuatia Julius Nyerere
alimshawishi Sheikh Karume, kwa msaada wa Hanga, kwamba Tanganyika na Zanzibar
ziungane. Nyaraka za siri za Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA)
zinaonyesha kwamba Nyerere alichukua hatua hiyo kwa kuhimizwa na Marekani
pamoja na Uingereza.
WASIA ALIONIPA HANGA
Mara yangu ya mwisho kukutana na Hanga
ilikuwa London. Siku moja mtangazaji mwenzangu wa BBC, Emmanuel Vivian
Kassembe, alininong’oneza kwamba Hanga akitaka kuniona pamoja na Wazanzibari
wengine wawili: Salim Hamdan, ambaye siku hizi anaishi Maskati, Oman, na Khamis
Nura, ambaye sasa ni marehemu.
Salim aliwahi kuwa mhandisi wa Sauti ya
Unguja na alikuwa Uingereza akisomea teknolojia ya elektroni. Nura alikuwa
mwanasheria wa kimataifa aliyesomea Moscow. Siku hizo akiogopa kurudi
nyumbani na akifanya kazi ya ukarani serikalini London. Mimi nilikuwa kijana wa
miaka 23 niliyekwishafanya kazi miaka mine BBC na nilikuwa karibu namaliza
masomo yangu ya shahada ya falsafa katika Chuo Kikuu cha London.
Kati ya sisi watatu, Nura ndiye
aliyekuwa karibu sana kisiasa na Hanga. Na ni Hanga aliyemkuta London
akampatia msaada wa kwenda kusoma Moscow.
Lakini siku ya miadi yetu na Hanga
ilipowadia, Nura hatukumuona. Kassembe akatuchukua miye na Salim
kutupeleka alikokuwako Hanga. Ilikuwa nyumbani kwa Oscar Kambona karibu
na stesheni ya treni ya Belsize Park, kaskazini mwa London.
Kambona alitufungulia mlango na
kutukaribisha. Kulikuwa vyumba viwili chini ndani ya nyumba hiyo. Kambona
alikuwa katika chumba cha mwanzo na mtu mwengine na baadaye Kassembe.
Kambona akatuonyesha mimi na Salim
chumba cha pili akisema: “Maalim yuko humo”.
Mara tukamuona Hanga ametoka chumbani
akitabasamu na akatukaribisha ndani.
Yeye na Salim wakikaa vitini na mimi
nikajipachika kitandani.
“Nimekwiteni kukuhakikishieni kwamba mimi sina matatizo yoyote na Mzee (akiwa
na maana ya Karume). Sina matatizo naye lakini anahisi mimi ni kitisho kwake,
kwa jinsi ninavyopendwa na watu,” alisema.
Halafu Hanga akatueleza maisha yake
alipokuwa waziri Zanzibar na Dar es Salaam. Alitueleza jinsi alivyokuwa
akipenda kwenda kwa miguu badala ya kuendeshwa katika gari la waziri na pia
kwamba alikuwa akimsikiliza kila mtu aliyetaka msaada wake.
Baada ya hapo akawa kama akitoa mawaidha
marefu kupinga ukabila. Alianza kwa kutwambia kwamba alifanya makosa alipokuwa
na siasa za kikabila na akatuasa “kama viongozi wa siku za mbele” tuepukane na
siasa kama hizo.
Alisema aliwakasirisha baadhi ya
viongozi wa ASP alipowasaidia waalimu Wakizanzibari wenye asili ya Kiarabu
wapatiwe kazi Bara. Aliwataja baadhi ya waalimu aliosema aliwasaidia wakiwa
pamoja na Maalim Salim Sanura na Maalim Shaaban Saleh Farsy. Waalimu wote hao
wazuri waliokuwa na ujuzi walifukuzwa kazi na serikali ya Mapinduzi bila ya
sababu yoyote ya maana na walikuwa wakizurura tu mjini Zanzibar.
“Nilipowasaidia waje kufanya kazi Bara
sikuwaona kuwa wao ni Waarabu. Niliwaona kuwa ni Wazanzibari tu,” alisema
Hanga.
Akaanza kunukuu aya za Qur’ani khasa
mkasa wa Nabii Musa na Bahari ya Shamu kama ulivyoelezwa humo.
Nikimsikiliza lakini nilikuwa na hamu ya kujua fikra zake juu ya Babu na Karume
akimuonaje Babu.
“Akiwa Marxist mwenzangu namtakia
kheri,” alisema na halafu akaongeza: “Yuko salama kwa sababu si kitisho kwa
Karume kama nilivyo mimi.”
Alitwambia kwamba Karume akimuogopa yeye
lakini khofu hiyo haikuwa na msingi kwa sababu hakuwa na nia mbaya dhidi ya
Karume.
Nilipomuuliza kuhusu mipango yake na
atafanya nini, alinijibu hivi:
“Kama ujuavyo nina mke Guinea na
amejifungua mtoto wa kiume. Kwa hivyo ntakwenda huo nimpe jina mwanangu kabla
sikurudi Zanzibar.”
Alipotutajia kwamba atarudi nyumbani,
mimi niliruka nikionyesha wasiwasi wangu na nikamuuliza haogopi?
Hanga alikuwa mtulivu, alimgeukia Salim
na akamwambia: “Mtizame kijana huyu. Kwa nini niogope? Sikufanya makosa yoyote.
Sikuua wala sikuiba kitu.”
Alitushangaza alipotupa jicho na
kukonyeza upande wa ukuta wa chumba alichokuwa Kambona akisema: “Angalau huyo
[Kambona] ameiba pesa za TANU.”
Tulimuombea kheri tukaagana naye.
Miaka kadhaa baadaye Kambona alinambia kwamba hata yeye alimsihi asirudi
Tanzania lakini Hanga hakumsikiliza. Pia alinieleza kwamba Hanga alipofika
Conakry alikuwa na mazungumzo ya muda mrefu na Kwame Nkrumah, aliyekuwa akiishi
huko uhamishoni. Nkrumah naye alimbembeleza asirudi, akimwambia kwamba
hamuamini Nyerere.
Kambona pia alinambia kwamba hata kabla
ya Hanga kwenda Conakry, Nkrumah alimwandikia barua alipokuwa London akimtaka
asirudi Tanzania. Lakini Hanga alishikilia lazima arudi. Aliiamini ahadi
aliyopewa Rais Ahmed Sekou Toure wa Guinea na Nyerere kwamba Hanga akirudi
hatodhuriwa.
Baada ya kuwa na familia yake ya Guinea
kwa muda Hanga akafunga safari ya kurudi Tanzania kwa kupitia Cairo. Huko
alikaa kwa mwenziwe Ahmed Diria Hassan aliyekuwa balozi wa Tanzania. Sijui
walizungumza nini Hanga alipokuwa kwa Diria. Lakini katika miaka ya 1980,
balozi mmoja mstaafu wa Tanzania alinieleza kwamba aliambiwa na rafiki yake ya
kuwa aliiona barua ambayo Diria alimwandikia Karume akimuelezea kuhusu kukaa
kwake Hanga jijini Cairo.
Inasemekana kwamba barua hiyo ilieleza
kwamba pale Diria alipomsindikiza Hanga uwanja wa ndege wa Cairo, alimuona
Hanga akikumbana na Mohamed Fayek, ambaye wakati wa Rais Gamal Abdel Nasser alikuwa
waziri wake wa mambo ya Afrika.
Kwa mujibu wa barua aliyopelekewa
Karume, Hanga alikumbatiana na Fayek na halafu wakasimama wakizungumza kwa
muda. Pakazuka dhana kwamba Hanga akitaka msaada wa Misri kumpindua Karume.
Nakumbuka 1984, Diria alipokuwa balozi
Bonn, Ujerumani, alinialika kwake kwa chakula cha usiku. Nilimuuliza
kuhusu hiyo barua anayosemekana kumuandikia Karume. Alikanusha.
Hanga alirudi Dar es Salaam na baadaye
alikamatwa kwa amri ya Nyerere na kupelekwa Zanzibar alikotakiwa na Karume.
Kabla ya hapo, Nyerere alimuadhir Hanga hadharani katika uwanja wa Mnazi Mmoja,
Dar es Salaam. Mkutano ulifanywa karibu na Arnaoutoglou Hall. Nyerere
alimwita Hanga “baradhuli”.
“Huyu ni baradhuli,” alisema Nyerere.
“Mnajua maana ya baradhuli nyinyi? Haijambo liji-Babu [yaani Abdulrahman Babu]
linachapa kazi. Lakini huyu baradhuli.”
Babu alikuwa hayuko mjini alikuwa
mikoani na baadhi yetu tukifikiri akirudi atajiuzulu, lakini hajajiuzulu.
Alipofika Unguja, Hanga aliuliwa kwa
kupigwa risasi. Inasemekana maiti yake ilifunganishwa na mawe mazito halafu
ikazamishwa baharini. Mkewe wa Kirussi, Lily, alijaribu kuulizia
yaliyomfika mumewe. Alijaribu hata kumuomba Svetlana Yosefna, binti wa dikteta
Josef Stalin, amsaidie.
Hakufanikiwa hadi ulipoporomoka Muungano
wa Sovieti. Nyaraka za siri za Shirika la Ujasusi la Kisovieti (KGB)
zimeeleza vingine kidogo. Nyaraka hizo zinasema kwamba baada ya Hanga kupigwa
risasi maiti yake ilikatwa vipande vipande, ikatiwa kwenye gunia lililozamishwa
baharini. Hakuna mwanadamu anayestahili kifo kama hicho.
Nina na “version” nyingine, maelezo
mbadala, ya jinsi alivyouawa lakini bado ningali nikiyafanyia utafiti.
Hanga, aliyekuwa mtiifu kwa Karume, hakustahiki kuuliwa. Si yeye, si
Othman Sharif, si Saleh Saadalla, wala si Abdulaziz Ali Twala. Wote
walionewa. Waliliwa na mapinduzi.
Hakuna serikalini aliyetwambia walikuwa
na hatia gani au kulikuwa na ushahidi gani wa kuwaingiza hatiani au
walihukumiwa na nani. Na huyo aliyewahukumu, au hao waliowahukumu,
walikuwa na haki gani ya kuwahukumu? Ni sheria gani iliyowapa madaraka ya kuwa
majaji?
Serikali ina dhima si kwa familia zao tu
lakini kwa jamii nzima ya Wazanzibari itwambie kwanini viongozi hao waliuliwa
na maiti zao ziko wapi.
Tumkumbuke Hanga kama mzalendo
Wakizanzibari aliyekuwa mfano wa mwanasiasa aliyeteleza kwa kufuata siasa za
kikabila lakini ambaye baadaye alitanabahi kuwa alikosea na akiwataka
Wazanzibari waungane, wawe kitu kimoja.
Magharibi ya Aprili 7, 1972 ilipothibitika
kwamba Sheikh Karume aliuawa, kuna bibi mmoja kizee aliyetoka nje ya nyumba
bila ya kujistiri sawasawa. Alikuwa akirukaruka nje akishangilia mauaji
ya Karume. Bibi huyo akiitwa Mashavu binti Hassan. Alikuwa mamake Hanga.
Oscar Kambona kama alivyokuwa katika miaka ya 1960 katikati alipokuwa suhuba wa Abdulla Kassim Hanga |
Muhammad Yusuf Mwenyekiti |
Salma Maulid aliyewasilisha mada kwa niaba ya Ahmed Rajab
Kulia Prof. Ahmed Gurnah akijibu swali akiangaliwa na Prof. Sharif kushoto na kulia kwa Dr. Gurnah na Mohammed Yusuf |
Kushoto Othaman Miraj Mtangazaji Maarufu Mstaafu DW akichangia mada pembeni ni Prof. Abdul Shariff |
Kushoto Ali Said Mtaalamu Mstaafu wa IT mbele mwenye miwani ni Prof. Mohamed Lodhi |
Khamis Abdalah Ameir mwanachama wa iliyokuwa Umma Party na aliyekuwa na Hanga Uingereza wakati Hanga alipokwenda kusoma akichangia |
Kushoto Msomi Maarufu wa fani nyingi na mwandishi Hamzah Rijal |
Ahmed Hanga mtoto wa Hanga aliyezaliwa Guinea 1967 akieleza kuhusu baba yake |
Ahmed Hanga akifuatilia mhadhara wa baba yake |
No comments:
Post a Comment