Nimegundua kitu kimoja
katika tabia za watu wanaoishi kwa hofu ya kusema kweli wakiogopa labda wenye mamlaka wanaweza
wakawadhuru. Wataujua ukweli lakini hawatausema hadi wasikie mtu mwingine kazungumza ukweli ule. Katika hali
kama hiyo na wao watatoka huko walikujificha na kuingiza maneno mawili matatu
ya kusadikisha ukweli ule. Binafsi nina mifano ya watu wakubwa tu katika nchi hii
ambao baada ya kunisikia nikuzungumza au kuandika mambo ambayo kabla ya mimi
kuyasema ilikuwa mwiko kusemwa basi na wao watayazungumza wengine kwa faragha
kwa jamaa zao na wakati mwingine hadharani ingawa hii si mara nyingi
kusadikisha ukweli ule. Sasa watu hawa wanapozungumza ile ithibati ya jambo
lile huwa imekamilika. Ingekuwa si kuhofia kuwaudhi watu hawa ambao waliniunga
mkono kwa yale niliyoandika au kusema ningelitaja majina yao na habari zenyewe
walizothibitisha. Lakini kwa kuwa mazungumzo yetu yalikuwa ya faragha nina
wajibu wa kuheshimu usiri ule.
Siku moja niko msikitini
akanijia mtu mzima mmoja akaniambia kuwa ana sahib wake kanisikia nikifanya
kipindi katika radio kuhusu historia ya Zanzibar na nimemtaja Abdulla Kassim Hanga.
Huyu bwana akanambia kuwa huyo sahib wake alikuwa akijuana na Hanga toka utoto
wao Zanzibar na ana jambo angependa kunieleza kuhusu kifo cha Hanga. Yule bwana
alifika msikitini petu siku ya pili na tukajulishwa. Huyu bwana ni mtu mzima
kiasi cha miaka 80. Nilimkaribisha nyumbani na tukakaa kwa ajili ya mazungumzo
yetu. Rafiki yake yeye alisema atabaki msikitini kumsubiri. Baada ya mazungumzo
mafupi ya hili na lile tulianza mazungumzo yetu. Mimi nilimuomba nifanye, ‘’recording,’’
ya mazungumzo yetu lakini alikataa akasema hapana haja ya kuyanasa mazungumzo
yetu katika chombo. Sikupata tabu nilimwelewa. Nikamuomba nimpige picha
halikadhalika alikataa na nilimwelewa na hata nilipotaka anipe jina la kampuni
aliyokuwa meneja wa shirika la ndege na ndiyo hiyo kuwa sababu ya yeye kuwa
pale Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam siku Hanga aliporudi safari yake ya
mwisho akitokea Cairo pia hakupenda kuniambia. Nami nilimwelewa kwa yote hayo.
Baada ya haya nikawa tayari nishamwelewa mapashaji wangu habari sasa kilichobaki
ilikuwa kwangu mimi kumtoa hofu atulie ili aniahdithie kisa kile vizuri.
Huyu bwana anasema:
‘’Mimi nilikuwa meneja wa
kampuni moja ya ndege hapa Dar es Salaam na kila ndege yetu ikija Dar es Salaam
mimi nilikuwa uwanjani kuipokea. Siku ile wakati niko pale uwanjani majira ya
mchana nikamuona mkewe Hanga, Bi. Mkubwa, pale uwanjani. Nikamfuata kumsalimia
na nikamuuliza mbona yuko pale. Jibu alilonipa Bi. Mkubwa ni kuwa, ‘’Kassim
anakuja na Egypt Air nimekuja kumpokea.’’ Mimi nilishtuka sana kupita kiasi kwa
sababu hapa mjini Dar es Salaam sisi jamaa kutoka siku zile Zanzibar tulikuwa
tunafuatilia kwa karibu na tunapata taarifa ya kila jambo lililokuwa linatokea
Zanzibar khasa katika mambo ya kamatakamata na mauaji. Taarifa ambazo
zilizokuwa zikizunguka katika duru zetu kuhusu Hanga zilikuwa zinatisha kwa
hiyo niliamini Hanga yeye ingawa alikuwa nje ya nchi bila shaka jamaa na
marafiki zake watakuwa wameshamtahadharisha. Ndege ilipotua nilikwenda hadi
chini ya ngazi kumpokea Hanga huku akili yangu ikenda mbio vipi nimpate Hanga
faragha lau kama kwa muda mchache nimfahamishe kuwa maisha yake yapo hatarini.
Wakati tunatembea kutoka nje ya jingo nilikaribisha chakula cha mchana kabla
hajakwenda kwake.
Tulikaa kwenye ‘’restaurant,’’
pale uwanjani tukala na baada ya kula nilipata faragha na Hanga. Sikuuma maneno
yangu nilimweleza Hanga yote yaliyokuwa yakisemwa kuhusu yeye kule Zanzibar
kama nilivyozipokea. Nikamwambia, ‘’Abdulla nakusihi ndugu yangu usiingie hata
mjini rudi na ndege hii hii hali si nzuri kwako.’’ Hanga alinikatalia. Ilikuwa
Qadar ya Allah. Hakika jitihada ya binadamu haiwezi kufuta aliloandika Allah.
Tukaagana lakini aliniacha na moyo mzito sana. Nikamsindikiza Hanga na mkewe
Bi. Mkubwa hadi kwenye gari wakaondoka kuelekea mjini. Hapo hapo nikampigia
simu Ali Nabwa wakati ule yeye akifanya kazi Tanganyika Standard. Nilikutana na Nabwa jioni ile na tulimtafuta
Hanga kote hatukumpata. Nabwa alikuwa anafanyakazi Tanganyika Standard kwa hiyo
alipiga, ‘’stop press,’’ ameagiza gazeti lisichapwe lisubiri habari kubwa ya
Hanga kurejea nchini. Usiku tukampata Hanga Oyster Bay nadhani kwenye nyumba
iliyokuwa ya Kambona. Baada ya mazungumzo tuliamua twende kwa Maalim Muhammad
Matar Magomeni tukafanye dua. Tulifika kwa Maalim Matar na tuliomba dua pale
kuomba salama ya Hanga. Siku ya pili habari kubwa ya Tanganyika Standard ilikuwa
kurejea kwa Hanga nchini. Habari hii ilikuwa katika ukurasa wake wa mbele.
Haukuchukua muda Hanga akatiwa mbaroni na akapelekwa Ukonga Prison na kutoka
hapo akarejeshwa Zanzibar baada ya kufedheheshwa katika ule mkutano mashuhuri
uliohutubiwa na Nyerere pale Mnazi Mmoja. Baada ya mkutano ule Hanga akarejeshwa
Zanzibar na huo ndiyo ukawa mwisho wake.’’
![]() |
Hanga na Nyerere |
![]() |
Ali Nabwa |
Maalim Muhammad Matar |
***
Napenda kuongeza kitu. Ingawa kichwa cha habari kinaeleza kuwa hii ilikuwa safari ya mwisho ya Hanga. Ukweli ni kuwa ilikuwa safari yake ya mwisho akitokea nje ya nchi. Safari yake ya mwisho ilikuwa alipopita tena uwanjani pale wakati akirejeshwa Zanzibar kukabiliana na mauti.
Atakae kusoma habari zaidi za historia ya Zanzibar atapata habari hizo katika kitabu cha Dr. Harith Ghassany, ''Kwaheri Uhuru Kwaheri Ukoloni,'' kitabu kinapatikana:
Ibn Hazm Bookshop Msikiti wa Mtoro na Manyema
Tanzania Publishing House, Samora Avenue
Elite Bookshop Mbezi Samaki
Atakae kusoma habari zaidi za historia ya Zanzibar atapata habari hizo katika kitabu cha Dr. Harith Ghassany, ''Kwaheri Uhuru Kwaheri Ukoloni,'' kitabu kinapatikana:
Ibn Hazm Bookshop Msikiti wa Mtoro na Manyema
Tanzania Publishing House, Samora Avenue
Elite Bookshop Mbezi Samaki
No comments:
Post a Comment