Dondoo Fupi Kuhusu Mali za Waislamu Zilizodhulumiwa mwaka 1968 Ilipoundwa
Bakwata
1.
Kulikuwa na jumuiya ya Waislamu
wakati wa ukoloni wa Muingereza ikiitwa East African Muslim Welfare Society (EAMWS).
Jumuiya hii ilifanya kazi za kuwaletea maendeleo Waislamu wa Tanganyika
na kusimamia mali zao zilizokuwa ndani ya jumuiya hiyo.
2. Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa
1961wakajitokeza Waislamu wachache katika jumuiya hiyo ya EAMWS kwa kurubuniwa
na Wakaanza kuleta chokochoko dhidi ya katiba na mfumo wake. Hata hivyo,
Waislamu wengi wanachama wa jumuiya hiyo walikataa madai yale ya
wachache.
3.
Hatimae mwaka 1968 wale wachache
wakaamua kuunda jumuiya yao iitwayo Bakwata kwa msaada wa kuungwa mkono na
serikali. Lakini Waislamu walio wengi nchini hawakuitaka Bakwata. Waliipenda
EAMWS.
4. Mwaka huohuo katika kipindi cha
kuundwa Bakwata, serikali ikaivunja jumuiya ya EAMWS, Waislamu wanachama
wa EAMWS waliipinga hatua hiyo ya serikali wakiungwa mkono na Waislamu walio
wengi nchini.
5.
Serikali haikuishia hapo. Ikachukua
mali za Waislamu zilizokuwa zikimilikiwa na zikisimamiwa na EAMWS na
kuzikabidhi Bakwata. Waislamu wanachama wa EAMWS wakiungwa mkono na Waislamu
wengi nchini walikipinga kitendo hicho cha serikali na kuendelea kuikataa na
kuitenga Bakwata. Pamoja na mali za EAMWS, mali za jumuiya nyinginezo nazo
zikachukuliwa na serikali na kukabidhiwa Bakwata. Jumuiya hizo ni pamoja na Al Jamiiyyatul
Islamia fii Tanganyika, ambapo Bakwata hadi waliweka makao yao makuu katika
majengo ya jumuiya hiyo huru iliyoanzishwa kabla ya EAMWS.
6. Sasa tunatangaziwa kuwa kumeundwa Tume
ya Mufti wa Bakwata kurudisha mali za Waislamu zilizopewa Bakwata na serikali
mwaka wa 1968. Swali kubwa ni kuwa Je, Tume ya Mufti wa Bakwata hii
itazirudisha mali za Waislamu wa EAMWS na za Aljamiiyyatul Islamia fii
Tanganyika pamoja na zile za jumuiya nyinginezo kadhaa ikiwemo Arusha Muslim
Union?
7. Imetangazwa kuwa Tume hii ni ya Mufti
na si Tume ya Bakwata. Lakini hapohapo tunaambiwa kuwa Mufti kaunda Tume
hii kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo chini ya katiba ya Bakwata.
8. Hebu na tujaalie kuwa mtangazaji
amejichanganya katika kutangaza hayo ya kumtofautisha Mufti na Bakwata.
Ni vema basi tukaambiwa, Mufti huyu asiye Bakwata alichaguliwa na jumuiya au taasisi
ipi, katiba ya jumuiya au taasisi hiyo ni ipi, huyu Mufti hivi sasa anatumikia
nafasi yake kwa kulipwa ujira wake na jumuiya au taasisi gani?
9.
Kwa kuwa tangazo limeonesha kuwa mali
hizi chini ya Bakwata zimekumbwa na matatizo kadhaa yakiwemo ya kutojulikana
zilipo, kufujwa, kukabidhiwa au kutumika chini ya mikataba isiyoeleweka, je,
uchunguzi unaweza kuwa huru endapo itaonekana kuwa Mufti na hata baadhi ya
wajumbe ni Bakwata? Je, mali hizi endapo zitapatikana zinaweza kuwa
salama endapo zitaendelea kuwa mikononi mwa Bakwata au kitengo chake?
10.
Mwisho, kwa kuzingatia haki na
uadilifu chini ya misingi ya sharia za Uislamu zitokanazo na Allah, kama baada
ya Tume kumaliza kazi au hata pasipokuwepo kwa Tume, je, ni halali kwa Mufti au
Bakwata kushiriki katika kuhodhi na kuzitumia mali zisizo zao, mali ambazo
zilizoporwa kwa uonevu? Mali za dhulma zilizoporwa kwa kutumia mabavu,
toka jumuiya zilizokuwa na wanachama wake na malengo waliojiwekea wenyewe,
ambayo si ya Kibakwata na Mufti wake?
Al Jamiatul Islamiyya Muslim School |
Chuo cha Maalim Mzinga kilichoanzishwa mwaka wa 1935 |
Moja ya shule walizojenga Waislam baada ya nakama ya mwaka wa 1968 |
No comments:
Post a Comment