Aziz Ali
Kleist Sykes alikuwa na duka la vyakula Kipata Street
sasa mtaa huo umepewa jina lake unaitwa Mtaa wa Kleist. Hizi zilikuwa juhudi za
Kitwana Selemani Kondo alipokuwa Meya wa
Dar es Salaam kuwaadhimisha watu maarufu wa waliopata kuishi Dar es
Salaam na wakaitumikia jamii. Nilipata kumsikia Mzee Kondo akisema, ‘’Hivi vipi
litawekwa jina la mtu ambae hana nasaba yoyote na mji wa Dar es Salaam katika
mji huu na kuwaacha wenye mji wao?’’ Hakika jambo hilo halikughalis. Mzee Kondo
aliendelea na kusema, ‘’Hivi jina la Matola kwa nini lisiwekwe Dodoma lije
liwekwe Dar es Salaam na wakati huo huo wakawasahau wazee wetu wa Dar es
Salaam?
Turejee kwa Kleist Sykes. Hili duka lilikuwa nyumbani
kwake na hapo ndipo ilipokuwa barza ya
wazee maarufu wa mjini kukutana jioni inapoingia alasiri kuzungumza. Miaka ile
Dar es Salaam kulikuwa na wauza kahawa
wanapita mitaani na kahawa zao ndani ya madeli ya shaba yanayong’aa kwa kupigwa
braso wakiuza kahawa na wao wenyewe wamevaa nadhifu, kikoi na kizubau na kofia
kichwani. Basi baraza ile kila muuza kahawa akipita ataitwa na kuagizwa apige
duru kwa wanabarza. Ikawa pale ile barza waungwana wale wanakunywa vikombe na
vikombe vya kahawa hadi wanapoagana Maghrib inapoingia.
Muuza Kahawa |
Mmoja wa wanabarza wa barza hii alikuwa babu yangu
Salum Abdallah ambae nyumba aliyokuwa anaishi ilikuwa inatazamana na nyumba ya
Kleist. Hawa walikuwa si majirani tu bali hata kazi wanafanya pamoja Tanganyika
Railways. Hii ilikuwa miaka ya mwanzo ya 1920. Kleist akiwa Karani wa Mahesabu
na babu yangu Mfua Vyuma kwenye karakana ya Railway iliyokuwa Arab Street sasa
Mtaa wa Nkrumah. Mle ndani kulikuwa na king’ora kikipigwa saa moja kamili
asubuhi barabara na saa saba mchana. King’ora hiki cha Railway kiliwasaidia
sana wakazi wa Kariakoo na Ilala kujua majira.
Mtu mwingine maarufu katika ile barza alikuwa Aziz
Ali, Mdigo kutoka Moa Tanga. Huyu Aziz Ali alikuwa mwamba katika miamba ya Dar
es Salaam. Alikuwa tajiri ‘’contractor,’’ wa kujenga, majumba, Mwafrika wa
kwanza kununua gari na kujenga nyumba ya vigae na vioo Mtoni. Nyumba hii hadi
leo ipo na sehemu hiyo katika Kilwa Road inaitwa Mtoni kwa Aziz Ali. Lakini
katika sifa hizi sifa yake kubwa sana Aziz Ali ilikuwa ujenzi wa misikiti na
kuihudumia misikiti. Hii ilikuwa miaka ya 1930 na hapakuwa na umeme Kariakoo.
Misikiti ilikuwa ikitumia karabai kuonea. Aziz Ali yeye alinunua karabai kwa
kila msikiti na ikifika Maghrib mwanae Hamza alikuwa akizitia mafuta na
kuziwasha kisha akizipeleka kila msikiti tayari kwa sala ya Maghrib. Inapomalizika
sala ya Isha alikuwa anapita tena katika ile misikiti kukusanya karabai zake na
kurudi nazo nyumbani kwao Mtaa wa Mbaruku na Kongo. Hii ndiyo ilikuwa kazi yake
kila siku. Aziz Ali alipokufa mwaka wa 1951 miaka miwili baada ya kifo cha
rafiki yake Kleist gazeti la Tanganyika Standard liliandika kifo chake kwa
maneno haya: ‘’Aziz Ali the Builder of Mosques is Dead,’’ yaani, ‘’Aziz Ali
Mjenzi wa Misikiti Amekufa.’’ Iko siku nilimtembela Rose Aziz mjukuu wa Aziz
Ali, mtoto wa Hamza Aziz. Rose akanionyesha picha katika ukumbi wake ya mtu
amevaa tarabushi akanambia, ‘’Mohamed unamuona mume wangu?’’ Nikiwa katika hali
ya kushangaa huku nikiikodolea macho ile picha Rose akaendelea, ‘’Huyu babu
yangu Aziz Ali.’’
Aziz Ali alikuwa na nyumba nyingi sana Dar es Salaam
na ndiyo zilikuwa moja ya utajiri wake. Katika nyumba hizi nyumba ambayo
imaecha historia ya pekee ni hii nyumba ya Mtaa wa Mbaruku na Congo kwa sababu
nyumba hii ilikuwa moja ya sehemu ambazo harakati za kupigania uhuru wa
Tanganyika zilianza. Nyumba nyingine
ilikuwa Mtaa wa Kipata kwa Ally Sykes, hapo zamani lilipokuwa duka la baba yake
na barza ya wazee. Nyumba nyingine ilikuwa Stanley Street kwa Abdul Sykes.
Nyumba hii ilikuwa pia ya Kleist na kulikuwa na duka la vifaa vya ujenzi katika
uhai wake. Hii ilikuwa mwanzoni mwa mwaka wa 1950. Mambo yalipamba moto sana
kuanzia mwaka huo pale vijana wazalendo walipoanza kufanya mipango ya kuunda
chama cha siasa halisi kupambana na ukoloni wa Muingereza. Hizi ndizo zikawa
nyumba ambazo Nyerere alikuwa akifika kuanzia mwaka wa 1952 kila anapokuja
mjini kutokea Pugu alipokuwa akifundisha. Mama Ali mke wa Aziz Ali bado yu hai,
Bi Mkubwa huyu ana mengi katika historia ya nyumba ile ya Mbaruku alipokuwa
akiishi na mumewe katika miaka ile ya 1940 na akaendelea kuishi hapo na wanawe
baada ya kifo cha mumewe. Hivi sasa Mama Ali anaishi Ilala na ni mtu mzima sana.
Ghorofa rangi nyeupe ndio alikua akiishii marehemu Mzee Azizi Ally alietoa mchango mkubwa sana katika harakati za uhuru wa nchi hii kwa kujitolea mali zake na nguvu zake kabla ya ujenzi wa ghorofa hili hapo nyuma ilikua nyumba ya chini nyumba zake zilipeana mgongo Mbaruku Kipande na Mbaruku na Kongo zote zilikua himaya zake mzee huyu alikua mfanya biashara na kampuni ya ujenzi nyumba yetu yeye ndie alikua mjenzi miaka hiyo na nyumba nyingi tu mjini mitaa ya Kariakoo yeye alikua anazijenga tena kwa kumlipa kidogo na baadae kummalizia malipo yake kwa makubaliano maalum na wala hajawahi kumshtaki mtu kumcheleweshea malipo yake. (Picha na Maelezo kwa hisani ya Suleiman Mavitu)
Mtaa wa Mbaruku na Kongo jirani na tawi la CCM Gerezani hii nyumba inayonekana hapo yenye fremu za kijani ndio nyumba ilikua ikitumika katika harakati za uhuru wa Tanganyika hapa ndipo alipokua anaishi marehemu Dossa Azizi na marehemu Hamza Azizi mola awalaze mahala pema peponi. (Picha na Maelezo kwa hisani ya Suleiman Mavitu)
Suleyman Said Mussa Maarufu kwa jina la Suleyman Mavitu |
No comments:
Post a Comment