Wednesday, 4 January 2017

WAZEE WA DK. RAWYA SAUD AL BUSAID WAZIRI WA ILIMU YA JUU WA OMAN KATIKA HISTORIA YA ZANZIBAR NA OMAN

Utangulizi

Makala iliyopita kuhusu Dr. Rawya Saud Al Busaid ilikuwa ikisomwa kwa kasi ambayo si ya kawaida. Fikra iliyonipitikia ni kuwa kazi ilikuwa nzuri wasomaji wameipenda lakini asubuhi siku ya pili ndipo iliponidhihirikia kuwa makala ile imekuwa, ‘’maarufu,’’  kwa sababu tofauti kabisa na makusudio yake. Baadhi ya wasomaji walianza kuniandikia kunifahamisha makosa yaliyokuwamo katika makala ile na hawakuishia hapo kunisahihisha tu bali waliniletea pia na habari za ziada kuhusu wadhifa wa Dr. Rawya katika Serikali ya Oman na kuhusu wazee wake. Dr. Rawya ni Waziri wa Ilimu ya Juu wa Oman na siyo kama kichwa cha habari kilivyoeleza. Sahihisho la kwanza na muhimu sana ni kuwa mama yake Dr. Rawya ni mtoto wa Bi. Jokha Nasser Lamki na siyo Mohamed Nasser Lamki. Mwandishi alikuwa kafanya kosa kwanza kwa kukosea nasaba ya Dr. Rawya na pili kwa kutoweka mizani sawa katika historia ya wazee wake.

Makala iliweka uzito mkubwa zaidi upande mmoja tu kwa babu yake mkuu Tip Tip na kutosema chochote kuhusu nasaba yake ya Ki Al Busaidi na mengineyo muhimu katika historia ya Zanzibar na Oman - Afrabia. 

Ujumbe niliokuwa napokea ulinifanya niingie katika maktaba yangu na kupitia nyaraka za zamani na vitabu vipya vilivyoandikwa miaka hii ya karibuni  kimojawapo kikiwa, ''Memoirs of an Oman Gentlemen from Zanzibar,'' ambacho nafurahi kusema kuwa alinizawadia mwandishi mwenyewe Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaidi baba yake Dr. Rawya na akaweka sahihi yake katika kitabu hicho:

Saud bin Ahmed Al Busaidi 

 
Kitabu hiki kina mengi ambayo kwa hakika yanamgusa Dr. Rawya moja kwa moja kama mzawalliwa wa Zanzibar achilia mbali kuwa mwandishi wa kitabu hiki ni baba yake mzazi na yeye kaandika utangulizi wa hiki kitabu.

Nimeguswa sana na taarifa katika moja ya ujumbe niliopokea ulionifahamisha kuwa Sheikh Saud bin Ahmed Al Busaidi ana ujamaa na Ahmed Said Abdallah Kharusi maarufu kwa jina la Bamanga. Historia ya Zanzibar ina mashujaa wengi na kizazi hiki cha leo hakiwezi kuwatambua hadi pale wao wenyewe wanapozungumza maisha yao kama alivyofanya mzee wetu Saud bin Ahmed Al Busadi au watu wengine wanapoeleza michango yao katika historia ya Zanzibar kama Muhammad Al - Marhuby alivyoandika kitabu cha maisha ya baba yake Sheikh Amor Ali Ameir Al Marhubi, ‘’Amor Ali Ameir His Life and Legacy My Father,’’ au Ahmed Rashad Ali alivyomueleza mwandishi maisha ya  Ahmed Said Abdallah Kharusi katika kuasisi chama cha Haki za Binadamu Zanzibar kama alivyoandika mwandishi hapo chini:

''Mwaka wa  1950 kilizuka chama Zanzibar kilichokuwa kikiendeshwa chini kwa chini kikiitwa, ''Haki za Kibinadamu,'' hiki ndicho kilichokuwa chama cha kwanza  visiwani kilichokuwa na msisimko wa siasa. Mtu aliyesababisha harakati hizi mpya alikuwa Ahmed Rashad Ali akishirikiana na rafiki yake Ahmed Said Kharus maarufu kwa jina la Bamanga. '' (Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 - 1968) uk. 199).

Kisa cha Bamanga na Ahmed Rashad Ali ni kisa cha kusisimua sana na lau kama isingekuwa kuchelea kutoka nje ya maudhui nimgekiweka chote hapa kuanzia mwanzo walipotawanya makaratasi ya siasa katika mitaa ya Unguja hadi kufikia kukamatwa na kupelekwa mahakamani. Kesi hii ilivutia hisia za Wazanzibari wengi sana kwa kuwa washitakiwa wote wawili walikuwa wanatoka katika koo mashuhuri za Zanzibar.

Juu ya haya yote mtafiti akiangalia chanzo cha siasa za vyama na ushindani hatokosa kuona kuwa alikuwa Ahmed Mohamed Nasser Lamki  mmoja wa wazee wa Dr. Rawya, ndiye aliyeonyesha njia na mwelekeo wa hali ya baadae ya Zanzibar kwa kuunda Zanzibar Nationalist Union (ZNU) baada ya kurudi Zanzibar akitokea Misri mwaka wa 1953. Lengo lilikuwa kuwaunganisha Wazanzibar chini ya chama cha kizalendo bila kujali asili au makabila yao ili kuwe na chama cha siasa kilichoshikana barabara kwa nia ya kudai uhuru na kujenga taifa moja. Ni jambo la kusikitisha sana kuwa mizizi hii iliyojengwa na mashujaa hawa wa uhuru wa watu wa Zanzibar bado haijaweza kujikita ardhini sawasawa sasa zaidi ya miongo sita.

Napenda kumaliza kwa kisa cha ''Al Samar,'' yaani ''msumari,'' jina alilopewa Sayyid Hammad bin Ahmed ''Al Samar,'' ambaye ni babu mkubwa wa Dr. Rawya kwa ushujaa katika moja ya vita alivyopigana kwa ajili ya nchi yake na moja ya vita hivyo ni dhidi ya Wareno. Ukimsoma shujaa huyu aliyepata kuwa Mkuu wa Majeshi ya Oman chini ya Sultan Sayyid Said inakukumbusha shujaa mwingine kutoka Zanzibar, Muhammad bin Khalfan bin Khamis Al Barwani maarufu kwa jina la Rumaliza aliyekuwa mshirika mkubwa wa Chief Mkwawa dhidi ya Wajerumani katika ardhi ya Tanganyika. Katika historia hizi kuna mengi ya kujifunza. Ikiwa tumefunzwa historia ya Vita Vya Waterloo na Trafalgar si kwa lolote ila kwa sababu ya ukoloni wa Muingereza leo tuko huru basi ni aula zaidi kwetu sisi kujifunza na kuijua historia iliyogusa nchi yetu kwa namna nyingi sana. Tutakuwa tunajidhulumu sisi wenyewe ikiwa tutajiaminisha kuwa historia hii si historia yetu na kwa si jingine ila kwa kusikiliza propaganda za wanasiasa.

Nahitimisha kwa kuomba radhi kwanza kwa Dr. Rawya mwenyewe na kwa  ndugu zangu wote ambao kwa namna moja au nyingine hawakufurahishwa na makosa au upungufu ya makala ile ya kwanza khasa kwa msisitizo wa kichwa cha habari kuwa Dr. Rawya ni kitukuu cha Tip Tip na nikaacha kueleza nasaba yake ya Busaid.

Kulia waliosimama ni  Ahmed Said Abdallah Kharusi (Bamanga)

No comments: