Tuesday, 17 January 2017

MSIKITI WA BADAWY, SHARIFF HUSSEIN BADAWY NA SHARIFF MWINYIBABA MIAKA YA 1960


Shariff Hussein Badawy na  Sayyid Abdulla Baharoon Professor wa Ahgaff
 University, Al Mukallah, Yemen wakiongoza Zaffa Maulidi ya Lamu 2007

Kushoto Mwandishi, Shariff Hussein Badawy, Abdallah Miraj, Abdallah Tambaza
na Abdallah Kageta 

Kushoto Idd Simba, Shariff Hussein Badawy na Hamza Kassongo katika khitma
Dar es Salaam Saigon Club
Shariff Mwinyibaba Maulidi ya Lamu 2007



Sheikh Mohamed Ismail mwanafuzni wa Masjid Badawy Bingwa wa Kusoma Tajwid

Naweka hapo chini kisa cha Shariff Hussein na Shariff Mwinyibaba kama kilivyotokea miaka ya mwanzoni 1960 kama nilivyokiandika katika kitabu cha Abdul Sykes:

''...Sharif Hussein Badawiy na mdogo wake Mwinyibaba, walipewa notisi ya kuondoka nchini kama wahamiaji wasiotakiwa. Kilichofanya Shariff Badawiy afukuzwe nchini ni kauli aliyotoa Mwinyibaba katika maulid ya Mfungo Sita yaliyofanyika Mnazi Mmoja. ..''

''...Mwinyibaba akisukumwa zaidi na hamasa za ujana, alipanda kwenye membar ile ile ambayo muda mfupi uliopita sheikh mmoja maarufu alihutubu. Mwinyibaba aliwaeleza Waislam kuwa wao hawahitaji kumshukuru yeyote kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mwenyezi Mungu, vyovyote iwavyo sala ya Ijumaa ni fardh inayomuwajibikia kila Muislam na hana khiyari ila kuitekeleza, serikali iwe imetoa ruhusa au vinginevyo. ..''

''...siku ya pili yake serikali ikatoa amri Shariff Hussein afukuzwe nchini (Prohibited Immigrant)  au PI pamoja na mdogo wake Mwinyibaba ingawa yeye Shariff Hussein hakuwepo hata kwenye hafla ile ya maulid kwa kuwa alikuwa nje ya Dar es salaam. Shariff Hussein na Mwinyibaba ikabidi waondoke na kurudi kwao Kenya...'' 

Hivi ndivyo Shariff Hussein Badawy na Shariff Mwinyibaba walivyofukuzwa Tanganyika lakini katika miaka ya 1980 wakati wa utawala wa Rais Mwinyi zikafanyika juhudi za kuwafutia ile marufuku na wakaruhusiwa kuingia nchini.





Kushoto  Mohamed Hamiar, Shariff Hussein Badawy, Rais Mstaafu Sheikh Ali Hassan 
Mwinyi, Ali Mshare (pass) Salum Hamiar na Haj Sahib Maulidi ya Sheikh Ahmad Bakari 
Magomeni Mapipa 16 Januari 2017

Kufukuzwa nchini kwa wasomi hawa lilikuwa pigo kubwa sana kwa Waislam kwani Msikiti wa Badawy ambao ndipo walipokuwa palikuwa chimbuko la ilm ya dini na vijana wengi walikuwa wakisoma pale. Kubwa Masjid Badawy ilitoa wasomaji tajwid hodari kama Al Had Omar,  Ustadh Adam na Mohamed Ismail. Ukiondoa hilo hapo ndipo Sheikh Hassan bin Amir alikuwa akitoa darsa zake zilizokuwa zikjaza masheikh wengi na wanafunzi vijana. Ilikuwa ukiwaangalia wale masheikh waliomzuguka Sheikh Hassan bin Amir akidarsisha utashangaa na kujiuliza kumbe hata hawa masheikh na wao bado wanasoma? Darsa hii ilishamiri sana kiasi Augustus Nimtz katika kitabu chake, ''Islam and Politics in East Africa,'' kataja umashuhuri wa Sheikh Hassan bin Amir na darsa hii.

Photo of August H Nimtz Jr
Augustus Nimtz
(Huyu Nimtz alikaa sana Bagamoyo kwa Sheikh Mohamed Ramia akiteka ilm katika kile kisima kuhusu Tariqa Quadiriyya wakati wa utafiti wa tasnifu kwa Ph D yake; ''The Role of Sufi Order in Political Change,''  Indiana University, 1973).

Haukupita muda mrefu Waislam wakapata pigo jingine mwaka wa 1968 pale Sheikh Hassan bin Amir na yeye akakamatwa na kufukuzwa Tanzania Bara akarudishwa, ''kwao,'' Zanzibar.

Sheikh Badawy, Mundhari Khitami, Shariff Mwinyibaba and Author
Lamu Maulid 2007


No comments: