Asalaam Aleikum Warahmatullah Taala Wabarakatuh,
Siku kadhaa zilizopita niliandika taazia ndefu kuhusu msiba wa
Alhaj Kamanda Mohammed Chico.
Alhamdullilah, tulipokea simu, sms na emails nyingi mno za pongezi
kutoka kwa ndugu na jamaa wanaomfahamu hayati Chico.
Miongoni mwao wapo waliotoa ufafanuzi zaidi wa masuala ya
kihistoria ambayo yamezungumzwa kwenye makala ile, ambayo kwa namna moja ama
nyingine, ni lazima tuyafanyie marekebisho kidogo kuweka sawa mambo.
Kwanza ni kuhusiana na Twarika ya Dandarawi. Hii haswa asili yake
ni kule Misri kwenye kijiji kinachoitwa Dandara; ikasambaa kwenda sehemu
nyingine za Arabuni.
Sheikh Ahmed Haidar Mwinyimvua, Imam wa Masjid Mwinyikher akiwa
mwanafunzi pale al-Azhar Sheriff Cairo, amefika mara
nyingi kijijini Dandara kumtembelea muasisi wake.
Ukweli uliopo ni kwamba hapa kwetu ilianzishwa na Sheikh Ali Saleh
miaka kadhaa nyuma kabla uhuru ambapo wengi wetu tulikuwa
hatujazaliwa. Habari za Sheikh Saleh ni kubwa maana wanasema wasemao, alikuwa
ni mtu wa ‘makarama na walii’.
Mzee huyu, ambaye alipata kuwa mwajiriwa wa Shirika la Reli Afrika
Mashariki miaka ya nyuma hiyo, siku moja alimwendea Liwali wa wakati huo Sheikh
Ahmed Swaleh na kumwambia kwamba yeye sasa hataki tena kazi ila anataka
ashughulikie dandarawi tuu. Liwali akakataa akampeleka mbele ya DC Mzungu.
DC yule alikataa katukatu. Akiwa amewaacha pale ofisini kwake,
Mzungu[ alitoka nje kidogo alikoitwa. Mlangoni
akamwona mtu na majoho yake kamsimamia pale mlangoni na amefanana na yule
Sheikh Swaleh aliyemwacha ndani. Haraka akarudi ndani na alimkuta Sheikh yuko
pale pale alipomwacha. Hakuamini, akatoka tena mlangoni anamkuta mtu yule yule
na majoho yake. Akawa hana la kufanya ila kumruhusu Sheikh Swaleh aende zake
akafanye shughuli zake za twarika.
Sheikh Swaleh alitokea Unguja kwenye miaka ya 40 na mmoja wa
wajukuu zake ukooni kwao ni mwandishi mashuhuri wa makala wa gazeti la An-nnur, Sheikh
Ben Rijaal pamoja na golikipa wa zamani wa Timu ya Cosmopolitan, Abdulmout.
Mungu ndiye mkamilifu wa kila jambo!
Abdallah Tambaza.
No comments:
Post a Comment