Sunday, 5 March 2017

UKURASA KUTOKA SHAJARA (DIARY) YA MWANDISHI: ABDULRAHMAN BABU NA AHMED RAJAB


Kurasa kutoka shajara ya Mwandishi, May 1991, London

Leo alfajir nilikuwa napitia maktaba yangu nikakumbana na shajara (diary) yangu ya 1991. 

Hapo juu ni ukurasa wa tarehe 9 May. Huyo niliyemtaja kama, ‘’Ahmed,’’ ni Ahmed Rajab wakati ule alikuwa mhariri wa wa jarida, ''Africa Analysis,’’ na huyo, ‘’Babu,’’ ni Abdulrahman Babu, kwa ufupi wa maneno mkimbizi wa siasa kutoka Zanzibar.

''Mlamali,'' ni Mohamed Mlamali Adam wakati ule Mhariri wa Africa Events. Kumweleza Mlamali utahitaji kitabu kizima. 

Mlamali ana kalamu sijapatapo kushuhudia lakini kubwa ni ujuzi wake wa lugha ya Kiingereza.
Watu wengi hawamjui Mlamali.

Babu na Ahmed Rajab hawa ni watu mashuhuri hawahitaji kutambulishwa.
Tuko London.

Siku hiyo wakongwe hawa wa siasa za Afrika walinichukua kwenye mkutano wa "Africa Alert," Brixton kitongoji cha watu weusi nje ya London.

Wapinzani Cameron walikuwa wamegombana lakini wote wamekuja Uingereza kutafuta hifadhi kama wakimbizi wa siasa.

Babu na watu wengine maarufu waliokuwa wakiishi London na wao pia wengi wao kama wakimbizi walikuwa wanajaribu kuwapatanisha.

Hii ndiyo ilikuwa shughuli kubwa ya Afrika Alert.

Wakati nafika Brixton miezi michache iliyopita palitokea machafuko makubwa sana hapo.
Sikuweza kujizuia kuunganisha vurugu za Afrika na zile za pale Brixton.

Babu tulipokuwa peke yetu alinipiga maswali mengi sana kuhusu Tanzania na kwa hakika huwezi kuchoka kuzungumza na Babu kwani ni mtu wa maskhara sana na mwepezi wa kujishusha.

Kwa mara yangu ya kwanza nilipata fursa adhimu kumsikiliza Babu kwa karibu na pia nikamjua Babu na Mapinduzi ya Zanzibar kupitia kinywa cha Ahmed Rajab. 

Nilimsihi sana Babu kuandika historia ya mapinduzi na nikamwambia Ahmed Rajab aandike kitabu kuhusu maisha ya Babu.

Inasikitisha kuwa Babu hakuwahi kunyanyua kalamu kuandika historia ya mapinduzi na Ahmed Rajab sitosema kitu kwani huenda anaandika.

No comments: