Sunday 12 March 2017

KUTOKA JF: KACHERO WA WAINGEREZA ALIYEKUWA UBAVUNI KWA NYERERE









Maalim Faiza,
Nami nikijiuliza iweje Nchimbi kachoropoka ilhali kosa lake ndilo hilo la
wenzake?

Nikajisemea moyoni kuwa bila shaka ipo namna.
Katika TAA kulikuwa na mtu mmoja na katika wasomi wa wakati ule.

Huyu bwana alikuwa ameshika nafasi ya juu kabisa katika moja ya vyama
vya Waafrika ambavyo Waingereza walivisajili.

Katika harakati za Abdul Sykes kuibadili TANU kuanzia 1953 yeye alikuwa
ubavuni kwake.

Huyu bwana alikuwa kampita sana Abdul kwa umri kiasi siku nilipofanya
mahojianonae alinambia kuwa yeye kamuona Abdul na mdogo wake Ally
wakiwa watoto wadogo wameshikwa mikono na baba yao wakija msikiti
wa Kitumbini (ule wa zamani 1930s) kuswali sala ya Maghrib kila siku.

Akaendelea kunieleza kuwa wakati Abbas Sykes ni Balozi wa Tanzania
Sudan yeye alikwama uwanja wa ndege wa Khartoum na maofisa wa
uhamiaji wa Sudan walikataa kumruhusu kuingia mjini kwa kuwa hana
visa.

Anasema aliwaomba wampigie simu Balozi wa Tanzania ambae alikuwa
Abbas Sykes ili awajulishe yeye ni nani katika utumishi wa serikali ya
Tanzania.

Huyu mzee wangu akanambia Abbas Sykes aliposikia sauti yangu alikuja
mbio uwanja wa ndege tatizo likesha pale pale.

Lakini wakati huu tunafanya mazungumzo haya mimi nilikuwa sijajua kama
alikuwa, ''njagu, '' toka enzi za Waingereza.

Huyu mzee wangu akaja kuwa mmoja wa wanachama wa mwanzo wa TANU
na kiongozi wa juu na akisafiri na Nyerere kuitangaza TANU.

Mzee wangu huyu alifikia hadi kupokea fedha nyingi sana kutoka kwa George
Arnautoglo
 kuwaletea TANU.

Huyu George Arnautoglo alikuwa tajiri wa Kigiriki na alikuwa hawapendi
hawa Waingereza kwa kuwa walikuwa wanaikalia nchi yake Greece na wakati
ule Askofu Makarios alikuwa akipambana na ukoloni wa Waingereza nchini
kwake.

Lakini jinsi mambo nilivyokujayatathmini baadae si Abdul wala Nyerere
walikuwa wanajua kuwa wana nyoka ndani ya TANU.

Nimezungumza na Ally Sykes mengi sana na alinitajia wote waliokuwa
Special Branch lakini jina la huyu mzee wangu hakulitaja.

Ally Sykes akinambia kuwa Nyerere kamuudhi sana kuwabakisha katika
nafasi zao za kikachero watu wale wale ambao wakiwataabisha wao wakati
wa kudai uhuru.

Kachechero ambae Ally Sykes alikuwa hapungui mdomoni kwake alikuwa
Amiri Kweyamba mtu kutoka Bukoba.

Ally Sykes wakati ule wa kudai uhuru ndiye alikuwa mwandishi mkuu na
msambazaji wa makaratasi ya, ''uchochezi,'' na mara kwa mara makachero
wakimvamia nyumbani kwake Mtaa wa Kipata.

Inaelekea hata yeye pia kama kaka yeke na Nyerere hawakuwa wanajua
habari za huyu mzee wangu.

Siku nilipoelezwa habari za huyu mzee wangu nilipata mstuko mkubwa sana.
Kubwa ni kuwa wala mimi sikuzitafuta hizi habari.

Kachero mwenzie na huyu pia ni mzee wangu na huyu mzee alikuwa na
mapenzi makubwa sana kwangu kiasi akiniitikadi mie kama mwanae na
akinijulisha hivyo kwa kauli yake.

Siku moja akanambia, ''Mwanangu Mohamed leo nataka nikuambie jambo...''
Ndipo aliponipa habari za huyu mzee wangu.

Hapo ndipo nikarudi katika historia ya TANU na kuanza kuyajibu maswali
yale ambayo siku zote yakinitatiza.

Nilianza na Iddi Faiz Mafungo mweka hazina wa TANU na Al Jamiatul
Islamiyya fi Tanganyika na aliyekuwa mratibu wa safari ya kwanza ya
Nyerere UNO 1955.

Huyu alikamatwa Turiani akiwa njiani akitokea Tanga kwa Mwalimu
Kihere 
alipokwenda kuchukua mchango wa watu wa Tanga kwa safari
ya Nyerere UNO.

Huyu mzee wangu kwa kuwa alikuwa kiongozi wa juu wa TANU pale
New Street alikuwa anajua mipango yote ya safari ya Nyerere.

Sasa siku zote nikijiuliza vipi Special Branch walijua kuwa Idd Faiz
kenda Tanga kukusanya fedha za safari ya UNO na wakamvamia njiani?

Walijuaje?
Nikaja kwa Rashid Ali Meli.

Huyu Rashid Ali Meli alikuwa mmoja kati watu takriban hawazidi 20
waliohudhuria mkutano wa kwanza wa TANU Ukumbi wa Arnautoglo.

Rashid Ali Meli alikuwa mweka fedha Dar es Salaam Municipal Council.

Ilipodhihirika kuwa mfuko wa kumpeleka Nyerere New York UNO una
matatizo yeye akaenda kwenye sefu yake kazini akafungua akatoa
fedha kwa siri akamkabidhi Iddi Faiz atie katika safari ya Nyerere kwa
makubaliano kuwa TANU itarejesha hizo fedha haraka.

Siku ya pili baada ya Rashid Ali Meli kutoa fedha zile na kuzipeleka
TANU wakaguzi wakafika ofisini kwake kufanya ukaguzi.

Walijuaje?
Ikawa sasa jibu nimelipata.

Waingereza walikuwa na mtu wao katika uongozi wa juu wa TANU pale
New Street akiwapa taarifa zote kila zinapotokea.

Huyu mtu wao alikuwa huyu mzee wangu.

Yako mengi sana katika historia ya TANU ya hawa, ''nyoka wa vichwa 
saba,'' chembelecho Maalim Faiza.

No comments: