Thursday 30 March 2017

TAAZIA: EYSHE ABBAS MAX 1951 - 2017

Eyshe Abbas Max

Sheikh Mtoro,

Dunia ni ndogo sana. Siku nne kabla ya Eyshe kufariki alinipigia simu na alikuwa na kawaida ya kunipigia simu sana na tukizungumza muda mrefu khasa alipokuwa kalazwa hospitali.

Basi tulizungumza na akaniomba kuzungumza na mke wangu na walizungumza kwa muda mrefu pia.

Eyshe tumejuana shule St. Joseph's Convent 1969 yeye akitokea St. Xavier na tulikuwa very close. Kwa kuzaliwa Eyshe alikuwa amenitangulia mwaka mmoja yeye kazaliwa 1951.

Maisha yalitutenganisha kila mtu akenda njia yake. Miaka ikapita. Siku moja kiasi cha kama miaka kumi na zaidi iliyopita Dr. Ramadhani Dau akanipigia simu kutoka Geneva nikiwa Tanga akanambia kuna mtu hapa anasema anakujua sana na angependa kuzungumza na wewe.

Alikuwa Eyshe na Dr. Dau alikuwa kampelekea zawadi kitabu cha Sykes akiwa hajui kuwa mimi na Eyshe tunafahamiana.

Hapo ndipo palipoanza mawasiliano yetu yaliyodumu hadi kifo chake na ni Eyshe ndiye aliyenifunza kutumia Skype kupiga simu.

Mwaka 2011 nilikuwa Berlin kiasi cha mwezi mmoja. Eyshe akanipigia simu kunialika nende nikamtembelee Geneva. Nilikwenda baada ya kupita Amsterdam kwa mmoja wa ndugu zake, Bi. Haki.

Kwa hakika Bi. Haki ni dada yetu sote na nilipomwambia kuwa nakwenda Geneva kwa Eyshe alifurahi sana akanambia kuwa kila akizungumza na Eyshe heshi kunitaja.

Wakati huo mimi nilikuwa natokea The Hague kwa kaka yangu  Prof. Mgone. Eyshe tulikuwa hatujaonana muda mrefu sana tariban miaka 35 ukitoa siku nilipokwenda kumpa pole alipofiwa na mama yake na yeye akaja Dar es Salaam kuzika.

Ninachotaka kukuambia ni kuwa Eyshe alikujakuwa mcha Mungu wa kupigiwa mfano.

Katika ukaribu wetu miaka hii kumi iliyopita Eyshe alinieleza mengi katika maisha yake na akataka tuandike kitabu.

Kuna nyakati katika hii miaka alikuwa akishangaa sana wakati nikimsomea vipande katika shajara (diary) yangu ambamo nimemtaja mathalan siku moja nilimwambia tarehe fulani uliniaga unakwenda Dodoma.

Nikamwambia kuwa hiyo ni ''entry,'' katika shajara yangu ya 1969,  basi alishangaa sana. 
Hakika utoto una raha zake.

Kuna hulka za binadamu hazibadiliki.

Alipokuja kunipokea Geneva, ''train station,'' nilimuona ni Eyshe yule yule tuliyejuana udogoni. Kuanzia kiatu chake hadi nguo zake amevaa, ''designer,'' nguo makhsusi kwa watu makhsusi zinazouzwa katika maduka makubwa.

Utanashati wake katika mavazi ulikuwa pale pale juu ya kuwa miaka ilikuwa imesogea. 
Eyshe akifanyakazi ILO na alikuwa, ''fluent in French.''

Muda wote niliokuwa Geneva nikimuona akizungumza Kifaransa na wajukuu zake na hata na wahudumu katika migahawa aliyokuwa akinipeleka.

Siku moja Geneva alinichukua, mgahawa mmoja akiwa na binti yake anaitwa Jamila pamoja na wajukuu zake Kauthar na Rawdha. Akanambia angependa mimi nimueleza mwanae, Bi. Jamila yeye alikuwaje tulipokuwa tunakua Dar es Salaam ya 1960.

Nilijua kuna kitu anataka mwanae ajifunze kutoka kwake. Basi mimi nilimweleza Jamila jinsi nilivyomjua mama yake na vipi tulivyokuwa shule.

Nilimwambia kuwa katika wasichana wazuri pale St. Joseph's Eyshe alikuwa mmojawao.

Nikamwambia pia alikuwa na kipaji cha kucheza dansi vizuri sana na cha michezo na timu yao ya Mkoa wa Dar es Salaam Basket Ball ilichukua kikombe 1968 (picha ya timu hii ninayo yuko Eyshe, Baby Ernest na Jennifer Gordon na hawa wote waliondoka Tanzania kwenda kutafuta maisha Ulaya). 

Nashindwa kuiweka picha hii hapa kwa kuwa wasichana wote wako katika, ‘’shorts,’’ yaani kaptula. Huko ndiko tulikotoka.

Nilimweleza Jamila mengi na nikamwambia kuwa Eyshe ndiye aliyenifanya mimi niache mpira kwa muda niende kucheza Basket Ball.

Sisi tulikuwa ‘’co- education,’’ na timu ya Basket Ball tukifanya mazoezi pamoja na wasichana.

Siku tunaagana alinichukua mgahawa mwingine na kabla ya hapo tulikwenda kwenye ''mall,'' akamnunulia mke wangu zawadi na akanipa salamu akasema, ''Mwambie Riziki mimi ni nduguye,'' (Riziki ni mke wangu).

Siku nilizokaa pale Geneva kwa kweli nilifurahi sana na siku nyingine tukivuka mpaka wa Switzerland kuingia France akinipeleka kwenye mgahawa alioupenda. Alitaka kulipa hoteli yangu nilipofikia nikamwambia hapana mimi natoka kwa Wajerumani nimefanya kazi na wamenilipa mapesa ya kutosha.

Hii hoteli alinichagulia yeye na akanambia iko karibu ya msikiti na akasisitiza kuwa niswali Fajr jamaa hapo msikitini na alinipeleka hadi msikitini niuone.

Eyshe alikuwa hasikizi muziki hata tukiwa kwenye gari yake na akanambia haangalii hata televisheni ila vipindi vya Qur'an.

Namshukuru Allah kwa kunikutanisha na Eyshe tukiwa watu wazima na namshukuru Allah kwa kumkuta ndugu yangu ameikamata dini kisawasawa. 

Lakini Eyshe, ‘’way back then 2011,’’ alinidokeza kuwa alikuwa mgonjwa.

Ukisoma hapo chini emal aliyonitumia 2014 wakati mimi nakwenda Hijja utaona anasema kuwa emal yangu ilimpita kwa kuwa alikuwa kalazwa hospitali.

Allah amghufirie madhambi yake na amlipe pepo Firdaus. Amin.

Soma emal moja aliyoniandikia wakati nakwenda hija 2014 Eyshe Max <eyshem@yahoo.com>:
To        Mohamed Said 10/22/14 at 12:40 AM
As salaam Aleykum,
I am sorry sikuona email yako in time before you left. Nilikuwa hospital, I hope all went well and that Allah akutakabaliye Hajj yako.
Hajj Mabroor wa Dhambi maghfur - Aamin.
You will let me know your experience, I know you have already done Hajj but this one is something else.

No comments: