Saturday 29 April 2017

MEDALI YA ABDULWAHID SYKES: MWENGE WA UHURU 1961 - 2011


Utangulizi
''Tarehe 27 Aprili, 1985 Julius Kambarage Nyerere, sasa akijulikana kama Baba wa Taifa, katika sherehe kubwa  katika viwanja vya Ikulu, alitoa jumla ya medali 3979 kwa Watanzania waliochangia katika maendeleo ya taifa. Kati ya wale ambao walipewa medali hizo alikuwa Sheikh abdallah Chaurembo. Wazalendo waliotajwa ndani ya kitabu hiki ambao walipigania uhuru wa Tanganyika, hakuna hata mmoja wao aliyekuwa katika orodha ile ya heshima. Baada ya siku chache kupita, Nyerere kama mtu aliyegutuka alimualika Dossa Aziz Ikulu. Dossa Aziz, wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika alikuwa mtu maarufu, mwenye nafasi, na kujiweza sana. Sasa Dossa baada ya miaka kupita hakuwa akifahamika tena na ule umaarufu na utajiri wake ulikuwa umetoweka. Alikuwa akiishi maisha ya kawaida kijijini Mlandizi, maili chache nje ya Dar es Salaam. Katika sherehe ya faragha Nyerere alimtunukia medali Dossa Aziz, rafiki yake wa zamani.'' 

(Kutoka, ''Maisha ya Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 - 1968)...'')

Jina la Abdulwahid Sykes (1924-1968) katika historia ya uhuru wa Tanganyika kwa sasa halihitaji kuelezwa sana. 

Historia yake imekuwa ni historia ya kusisimua unapomsoma kuhusu yale aliyofanya katika kuunda chama cha TANU 1954 akianza na kubadilisha mwelekeo wa TAA alipoingia katika uongozi wake 1950. 

Historia ya Abdul Sykes pia ina masikitiko pale baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 juhudi za makusudi zilipofanywa kulifuta jina lake katika historia ya TANU na uhuru wa Tanganyika na kwa hili si tu kuwa lilifutika jina lake peke yake bali na jina la mdogo wake Ally na la  baba yao Kleist Sykes aliyekuwa muasisi wa African Association mwaka wa 1929.


Kulia: Ilyas Abdulwahid Sykes, Daisy Abdulwahid Sykes, Mwandishi akiwa ameshikilia Medali ya Mwenge wa Uhuru
Misky Abdulwahid Sykes na Kleist Abdulwahid Sykes

Ilichukua miaka 50 kwa Abdulwahid na mdogo wake Ally kutunukiwa medali ya ‘’Mwenge wa Uhuru,’’ kama utambuzi wa mchango wao katika kupigania uhuru wa Tanganyika wakiwa bega kwa bega na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere waliyemfahamu mwaka wa 1952. 

Leo nimebahatika kuiona medali ya ''Mwenge wa Uhuru'' aliyotunukiwa Abdulwahid Sykes (post homous) na Rais Kikwete katika Viwanja vya Ikulu 9 Desemba, 2011 katika kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika.

Kuishika medali hii kwa mikono yangu kwangu kilikuwa kitu kilichokuwa na nafasi ya pekee katika moyo wangu. 

Medali ya mwenge wa Uhuru aliyotunukiwa Abdulwahid Sykes katika kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa
Tanganyika 2011
(Picha kwa hisani ya mjukuu wa Abdul Sykes Aisha Kleist Sykes)
Mwandishi akiwa Azam TV akifanya kipindi cha Saba Saba 2015

No comments: