UPATWE
LA KUKUPATA
Nshallah nawe upatwe,
yawapatayo wenziyo
Nyumbaniko ufuatwe,
penye mke na wanao
Kwa kipigo
ukung'utwe, umliliye mamayo
Kisha wambwe
makosayo, uzembe uzururaji
Nshallah wamkamate,
kwa kumteka mwanao
Machakani wamfite,
wamtende watakayo
Daima umtafute,
'simuone maishayo
Kisha huo udumeo,
tuone ukisimama
Nshallah waje wakute,
kushailima shambayo
Waje waikatekate,
waibwage mimeyayo
Na mwenyewe wakuvute,
ulimi na yako koo
Nawe yakupate hayo,
na mengineyo zaidi
Nshallah naisisite,
dua hii niombayo
La kupatwa likupate,
kuliko yawapatayo
Kwa majina uwaite,
utake faraja yao
Wasiitike na wao,
zaidi ya kukucheka
Nshallah uitafute,
nusura usiwe nayo
Si Chake Chake si
Wete, si Marumbi si Bweleo
Utengwe na watu wote,
uwe mpweke pekeyo
Ndipo yaje mautiyo,
Munguwo mukaonane
©MKG
18 Aprili 2017
Kulia: Mohammed Ghassany na Mohamed Said |
No comments:
Post a Comment