Sir Andy Chande |
Ilikuwa katikati ya miaka ya 1990 nikiwa afisa mdogo Makao
Makuu ya Tanzania Harbours Authority (THA) katika Idara ya Masoko iliyokuwa
ikiongozwa na Dr. Ramadhani Kitwana Dau. Idara hii ilikuwa idara ndogo kwa
maofisa ndani yake na ndiyo kwanza imeanzishwa.
Mimi nilipewa uhamisho kutoka
Idara ya Biashara kwenda Idara ya Masoko kwa kile nilichoelezwa kusaidia
kuanzisha idara mpya. Lakini ukweli ulikuwa mkurugenzi alikuwa anasafiri sana
nje ya nchi na pakawa hapana mtu idarani angalau wa kuishikilia idara kwa muda.
Lakini palikuwa na sababu nyingine. Ala kuli hali Dr. Dau alikuwa
tukifahamiana. Kipindi hiki Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi alikuwa Andy
Chande na Mkurugenzi wa Bandari wenyewe tukipenda kumuita DG yaani Director
General, alikuwa Athmani Janguo.
Ikasadifu kuwa Bodi ya Wakurugenzi inakutana chini ya
Mwenyekiti Andy Chande wakati Mkurugenzi wa Masoko Dr. Dau yuko nje ya nchi na
ametoa ‘’notice,’’ kuwa nafasi yake atakaimu Mohamed Said. Yote yaliyotakiwa
kutolewa taarifa kwa Bodi alikuwa kayatekeleza hivyo kazi yangu itakuwa
kufanya, ‘’short presentation.’’
Bandarini walipita wenyeviti wengi wa bodi lakini
ukurugenzi wa Andy Chande ulikuja na habari nyingine. Taarifa zilikuwa zikivuja
na kutufikia maofisa wadogo ilikuwa mabosi wetu walikuwa wakihenyeshwa na
Chande kiasi cha kulowesha vitambaa kwa kufuta jasho. Nikiri kwa kusema kuwa
habari hizi wakati mwingine zikitufurahisha maofisa wadogo kwa kusikia kuwa
wale waliokuwa wanatufanya sisi katika viti vyetu tuone kama moto umewashwa
chini yake Mungu katulipia na sisi kwa wao kupata saizi yao wa ‘’kuwanyanyasa.’’
Tukisikia habari kuwa Chande alikuwa hachukui posho ya
kikao. Tukipata habari kuwa mkurugenzi akichelewa kikao hamruhusu kuingia.
Yaani yeye mwenyekiti akiingia Board Room
na kukalia kiti chake cha enzi haingii tena mtu. Ilimuradi madereva wakikaa
katika magari yao kusubiri mabosi wao habari zilikuwa Chande hivi Chande vile.
Bila shaka hawa madereva walikuwa wanazinasa habari
hizi kwa kuwasikia mabosi wao wakizungumza wakati wakiwaendesha. Juu ya hayo yote kila mfanyakazi wa bandara alikuwa
anajua kitu kimoja kuhusu Chande nacho ni kuwa alikuwa tajiri kufru.
Haya mambo ya Freemasons wakati ule yalikuwa bado siri
kubwa ila mimi nikijua kuwa Chande alikuwa Freemason na nilijua kwa sababu mzee
wangu mmoja na yeye alikuwemo kwenye ‘’club,’’ hiyo kama mwenyewe alivyopenda
kuiita na hakuwa akimpenda sana Chande. Alikuwa akinambia,
‘’Natamani nimfanyie
ugomvi Chande lakini siwezi kwa kuwa tuko ‘’club,’’ moja na sheria zetu
zinatukataza kugombana wenyewe kwa wenyewe.’’
Huu ugomvi wao haukuwa wa leo ulianza miaka mingi
nyuma toka enzi za kupigania uhuru wao wakiwa TANU na siasa zao za Afrika kwa
Waafrika. Siasa ambazo Nyerere na TANU walizishinda. Ikawa sasa kila Chande
akichaguliwa katika nafasi na Nyerere nikifika ofisini kwa mpashaji wangu
habari itakuwa hiyo.
Ikawa sasa nimemfahamu Chande kutoka kwa mwanachama
mwenzake wa hiyo ‘’club,’’ yao. Siku moja nikamuuliza mzee wangu, ‘’Hii ‘’club,’’
yenu ni ‘’club,’’ gani?’’ Akanitazama usoni huku kakunja uso akaniuliza, ‘’Wewe
unaitakia nini?’’
Sikuuliza tena hilo swali lakini iko siku akanitajia.
Nikiwa nimeelemewa na habari za Chande nikawa sasa najitayarisha
kuingia katika kikao cha Bodi ya Mamlaka ya Bandari Chande akiwa Mwenyekiti
wake.
Bandari maofisa tukishonewa Kaunda Suti kama sare ya
kazi. Haikuwa lazima uvae kila ukija kazini lakini kwa yale niliyosikia kuhusu
Chande siku ile ya Bodi nilikuwa katika sare kwa kuzingatia kuwa kamba hukatikia
pabovu.
Kichekesho kikubwa katika hili ni kuwa mimi nilikuwa
ofisa mdogo mno na naamini hajapatapo ofisa wa ngazi yangu kukaimu nafasi kubwa
ya ukurugenzi. Ilikuwa hakuna mantiki na ni jambo lisilowezekana. Lakini kwa
kuwa nilikuwa idarani hapakuwa na jinsi ila nikaimu nafasi ya ukurugenzi na
hivi ndivyo nikajikuta nimeingia katika bodi
pamoja na wakurugenzi wa idara mbali mbali ambao kwangu ni mabosi wakubwa na hata
umri wamenipita kwa mbali sana.
Nimetulia kwenye kiti na wakurugenzi wenyewe na mara Chande
akaingia Board Rom kafatana na Mkurugenzi Mkuu Athmani Janguo.
Kikao kikaanza.
Ikawa Mwenyekiti Chande na Athmani Janguo wananong’ona
sauti ziko chini lakini aliyekuwa anazungumza ni Chande.
Wakurugenzi wametulia tuli.
Baada ya mazungumzo yao kule mbele Mkurugenzi Mkuu
akatuamuru sote tutoke tusibiri hapo nje. Naam. Si bure liko jambo niliiambia
nafsi yangu. Wakurugenzi wote wakawa wamesimama nje wamewaacha Mwenyekiti na
Mkurugenzi Mkuu wako ndani bila shaka wanaendelea mazungumzo muhimu.
Pale nje tukisubiri nawaangalia wazee wangu.
Walikuwako waliovuta sigara na kupuliza moshi juu hewani na walikuwapo pia
waliokuwa wanauma meno kwa ghadhabu.
Ilikuwa wazi wamefedheheshwa kwa kutolewa ndani ya
Board Room na kusimamishwa nje kwenye, ‘’corridor.’’ Kwangu mimi hii ilikuwa
mfano wa wanafunzi watukutu wakiotokewa darasani na mwalimu. Madirisha yalikuwa
wazi yakiingiza upepo wa Bahari ya Hindi lakini wazee wangu naona walikuwa
wanahisi joto maana wakijongea madirishani na kuchungulia nje kuiangalia Dar es
Salaam Port.
Haukupita muda mrefu tukaitwa ndani. Kilichokosewa
kikaelezwa kwa wakurugenzi na Mkurugenzi Mkuu akaahidi kuwa kitarekebishwa na
kurejeshwa kwenye kikao siku ya pili.
Ilipofika zamu ya Idara ya Masoko kufanya ‘’presentation,’’
Mkurugenzi Mkuu Athmani Janguo akamwambia Mwenyekiti wa Bodi Andy Chande kuwa
yeye ndiye atawasilisha.
Allah alikuwa kapokea dua zangu.
Vibweka vya Chande vilikuwa havijesha.
Kwa kawaida posho ya Wakurugenzi huwa inatolewa wakati
kikao kinaendelea. Mgawaji anapita kwa wakurugenzi mmoja mmoja anagawa bahasha.
Chande pale mbele alipokuwa amekaa akaona bahasha
zinatolewa akasema, ‘’Hapana kutoa fedha tunatoa fedha kwa watu wanaofanya
kazi. Acha kugawa.’’
Sikuweza kuamini masikio yangu.
Ikanidhihirikia kuwa kumbe yote niliyokuwa nayasikia
kuhusu Mwenyekiti Chande kumbe kweli.
Lakini baada ya kikao tuko ofisini tunaendelea na kazi
mgawaji akatuletea bahasha zetu. Siku ya pili Bodi inaendelea lakini Mkurugenzi
wa Masoko Dr. Dau akawa kesharudi safari.
Bismillah kuona sura yake tu baada ya salamu nikampa
taarifa ya kikao cha bodi jana na yote mengine ya biashara mpya kwangu yalikuwa hayana umuhimu.
Dr. Dau akanambia,’’Hivi asubuhi hii wakurugenzi wote
tumeitwa kwa DG kuna kikao kabla ya kikao cha bodi.’’
Baadae Dau alinambia kuwa Mkurugenzi Mkuu aliwaambia
kuwa hajapata kuhisi vibaya kama alivyohisi jana.
Tulipokuwa wadogo nilikuwa nikimsikia mama yangu
akisema kila anapomhadithia mtu aliyekuwa na mengi ya kueleza kuhusu yeye, ‘’Chini
kunakwenda watu.’’
Siku yangu moja na Andy Chande ilitosha kumwelewa na
kujua kwa nini juu ya yeye mali yake Kengele Tatu (sasa National Milling
Corporation) kutaifishwa bila ya fidia hakutetereka, hakukimbia nchi wala
hakugombana na Mwalimu Nyerere wala na serikali akabaki nchini na akaanza
biashara nyingine na akatajirika pengine kupita pale mwanzo. Huku akifanya
biashara zake alikuwa pia akitumikia bila kinyongo nafasi kadhaa alizokabidhiwa
na nchi.
Hakika chini kunakwenda watu.
No comments:
Post a Comment