Wednesday 17 May 2017

KUTOKA FB: MJUWE YULE POLISI WANAYESEMA NI ‘JAMBAZI’ WA ATM NA HILMI HILAL

MJUWE YULE POLISI WANAYESEMA NI ‘JAMBAZI’ WA ATM
Salum Mohammed Bin Almasi alikuwa mtoto wa familia ya washika dini kutoka Kilwa Pande.
Salum Mohammed Bin Almasi aliyezaliwa mwaka 1989 ni mjukuu wa Sheikh Muhammad bin Abdulrahman Ash-Shadhily. Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi iliyopo Kilwa Kivinje kutoka darasa la kwanza mpaka la nne, kisha akahamia Masasi kwa mjomba wake, Dk. Tondwa, na kuendelea hadi kumalizia elimu ya msingi kwenye Shule ya Msingi ya Mkomaindo iliyopo Masasi, ambapo aliendelea na elimu ya sekondari katika Masasi Day kutoka Kidato cha Kwanza hadi cha Nne.
Baadaye akachaguliwa kuingia Kidato cha Tano kwenye shule ya Ndanda High School na akahamia Tambaza High School kwa kumalizia Kidato cha Sita kwa mchepuo wa Fizikia, Jiongrafia na Hisabati (PGM).
Kutoka hapo akadahiliwa katika Chuo cha Saint Joseph College of Engeering Campus cha Songea kusomea kozi ya “Computer Science”, lakini alishindwa kuendelea kwa kukosa mkopo na kuwa ametoka katika familia isiyokuwa na uwezo wa kifedha. Akakaa nyumbani hadi mwaka jana alipojiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kitivo cha Computing Centre (UCC) akisomea kozi ya “ICT in Networking” ngazi ya stashahada mpaka unamfika umauti alikua ni mwanachuo mwaka wa pili wa UCC, huku akiwa anakaa na kaka yake wa baba mmoja mama mmoja aitwae Alfi Mohammed Bin Almasi.
Kwenye picha ya hapo chini, kijana aliyejifunika kilemba ndiye huyo Salum Mohammad enzi za uhai wake, picha ya weupe kwa weusi ni Sheikh Muhammad Bin Abdulrahamani Al-Shadhily, babu wa marehemu naye enzi za uhai wake, na picha ya mwenye joho la buluu ni Sheikh Nuurdin Hussein Al-Shadhily ambaye pia ni miongoni mwa mababu wa marehemu Salumu Mohammed Bin Almasi.
Unapouzungumzia Uislamu, wazee hawa ni miongoni mwa waliofanya kazi kuimarisha dini na kudumisha amani na utulivu. Kwa hivyo, Salum Mohammed naye alikuwa imamu kwa historia ya kuzaliwa katika familia ya manguli wa elimu ya dini ya Kiislamu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku wazee wake hawa wakiwa wamejipatia elimu ya dini kutoka nchi mbalimbali wakitokea Kilwa Pande.
Kwa uwezo wa Allah, ukoo wa Salum Mohammed umeijenga Kilwa kuwa na uimara wa watu wenye kumjuwa Mungu na kuchukuwa kuwa Dini ndiyo utamaduni wao wa maisha. Ndio maana hata mavazi yao ni ya kidini popote wanapokuwepo, huku wakidumisha amani na upendo.
Kuvaa kanzu, kofia na msuli kwa watu wa Kilwa na au kutembea wakiwa na Yasin au msahafu ni sawa na Mmaasai kufunga lubega au kutembea na sime, ingawa kuna tofauti kubwa ya kumfananisha Mmaasai na mtu wa Kilwa Pande kwa vile hazijawahi kutokea aina yoyote ya machafuko Kilwa kama yatokeavyo huko kwenye jamii za wafugaji.
Tumeamuwa kuweka picha za masheikh wetu hawa wawili waliotangulia mbele ya haki ili kuweka kumbukumbu sawa juu ya marehemu wetu huyu, Salum Mohammed Bin Almasi, watu wamjuwe kuwa ni mtu aliyetoka katika familia ya aina gani. Tumeonesha pia kazi za kidini zilizofanywa na walimu wake hawa ndani na nje ya nchi hii bila kuhitalifiana na serikali au taasisi nyingine binafsi na za kidini hata mara moja.
Katika historia ya nchi hii, watu wa Twariqatul-Shadhily hawajawahi kuhitalifiana na serikali kwa kuwa wao daima hufundisha watu wengine dini ili wamjuwe na kumuabudu Muumba wao tu.
Marehemu Salum Mohammed Bin Almasi alishika dini na kushiriki ibada kama ilivyokuwa inafanywa kabla yake, huku babu yake mzaa mama aliyefariki miaka ya 1990, Sheikh Muhammad Bin Abdulrahman Al-Shadhily akiacha watoto wake na wajukuu zake WOTE wakiwa walimu wa dini popote wanapokuwepo katika ardhi hii ya Mwenyezi Mungu.
Kifo cha Salum Mohammed Bin Almasi kinaweza kuacha DOA kubwa ndani ya Shadhily, endapo uchunguzi hautofanyika na kupatikana majibu kwa kuwa ni jamii iliyojijengea heshima kubwa ya uadilifu na ukarimu popote wanapokuwepo.
Ni kweli kuwa njia zote za umauti hupangwa na Allah, ila tukio lenye mashaka hata likileta umauti kwa mwanadamu lapaswa kubainishwa na kuondolewa shaka. Ndio maana tunamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi watuambie kinaga lubaga, ili kama tuna kasoro tujirekebishe, baada ya kufanya uchunguzi huru na si kuruhusu maiti izikwe tu na familia yake tu.
Narudia. Sijawahi kusikia hata siku moja kuwa mtu wa familia ya Sheikh Muhammad Bin Abdulrahman ameiba hata penseli au mstari darasani. Kama hana, atakuomba umsaidie. Hawa ni watu ambao Allah amewajaalia utajiri wa imani na kusimamisha dini ya Kiislamu na si fedha.
Haya nimeyashudia mwenyewe tukiwa darasani na kila mwaka mwana familia yao anayekuja kuanza shule kutoka familia hiyo lazima awe mwalimu wa Dini au Imamu.
Polisi pitieni kumbukumbu za familia hii katika shule walizosoma kutoka Kilwa Sekondari, Ndanda, Chidiya, Songea Boys, Mtwara Technical hadi hapo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wakati tukingojea majibu ya maswali yetu kuhusu kifo cha mwenzetu huyu, tunawaombea kwa Allah awaongoze KATIKA njia iliyonyooka na kuifikia pepo ya Firdausi na awasamehe kwa yale yenye hitilafu ya kibinaadamu.
Muhimu ni kuwausia ndugu zetu Watanzania wote kuwa ifike muda tutambuwe Tanzania yetu ni kubwa na ina makabila mengi, tamaduni nyingi, na hata dini pia.
Sisi watu wa pwani ya Kilwa tumekuwa mfano wa kutokuwa na makabila, huku tukitambuwa utaifa wetu tu na dini yetu kuwa hata ndiyo mila yetu na ni nguzo yetu kitaifa. Tupeane pole Wanakilwa wote na Tariqatul Shadhily.
Naamini kama leo masheikh wetu hawa wagekuwa hai, ndiyo wangekua wasemaji wa hili. Allah awarehemu Sheikh Nuurdin Hussein Al-Shadhily na Sheikh Muhammad Bin Abdulrahman Alsl-Shadhily.
Pole sana Alfi Mohammed Bin Alma since. Najua umeumia sana kwa kuondolewa ndugu yako ulokuwa unalala naye kitanda kimoja, akiwa ametoka nyumbani Kilwa kuja kutafuta elimu hapa Dar es Salaam.
Allahu Akbar! Allahu Akbar! Allahu Akbar!
TANBIHI: Tanzia hii imeandikwa na Kassim Binge kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Zanzibar Daima.
http://www.mohammedsaid.com/2014/05/sakata-la-kilindi-na-mauaji-ya-kijiji.html

Image may contain: 3 people, people smiling, beard and closeup
Kwa habari zaidi ingia hapo:
http://www.mohammedsaid.com/2014/05/sakata-la-kilindi-na-mauaji-ya-kijiji.html

No comments: