Thursday 18 May 2017

THOMAS SOUDT PLANTAN RAIS WA MWISHO WA TAA ALIYEKABIDHI CHAMA KWA VIJANA WADAI UHURU WA TANGANYIKA


Thomas Soudt Plantan

Utangulizi
Siku zote nimekuwa nikimkera mama yangu Bi. Maunda Plantan kupitia mwanae Khamisi Salum Khamis maarufu kwa jina la Mzee anipatie picha ya baba zake akina Plantan wote lakini jibu akinipa ni kuwa maktaba yake haijakaa vizuri. Leo kaniletea picha na katika hizo moja ni ya baba yake mzazi Mwalimu Thomas Soudt Plantan, rais wa mwisho wa TAA katika Waafrika wasomi waliosomeshwa na utawala wa Kijerumani. Thomas Plantan aliondolewa madarakani 1950 katika mapinduzi baridi yaliyoongozwa na mdogo wake Abdillah Schneider Plantan, mabadiliko yaliyowaingiza katika uongozi wa TAA vijana waliosomeshwa na utawala wa Kiingereza, Abdulwahid Sykes na Dr. Vedasto Kyaruzi. Ninanyanyambua kutoka kitabu cha Abdul Sykes (1924 – 1968) ili msomaji uwajue hawa wazee wetu walioweka misingi ya kuunda TANU na kupigania uhuru wa Tanganyika.
 ***
‘’…Wajerumani waliwaajiri Wazulu 400 kutoka Msumbiji kama mamluki na kujanao Tanganyika ili wapigane na Abushiri na Chifu Mkwawa. Pamoja na Kleist katika mji wa wa Dar es Salaam walikuwepo ndugu wa mbali watatu, Mwalimu Thomas Plantan, (hilo jina Mwalimu alipewa kwa sababu alikuwa Mwalimu wa shule), Schneider Abdillah Plantan na Ramadhani Mashado Plantan. 

Hawa Wazulu waliweza kutambulika kwa urahisi kutokana na majina yao ya Kikristo ingawa wao wenyewe walikuwa Waislam. Majina hayo yalikuwa na mchanganyiko wa majina ya Kijerumani, Kireno na Kiingereza; kama vile Kleist na Schneider ni majina ya Kijerumani; Mashado ambalo ni jina la Kireno na Thomas ni la Kiingereza. Wote hao, Kleist, Mwalimu Thomas, Schneider na Mashado baadaye walifanya kazi kubwa katika kupiga vita ukoloni na katika kuupeleka mbele Uislamu, kabla na baada ya uhuru. Bahati mbaya majina haya ya Kiislamu ya wazalendo hawa hayakujitokeza sana ba badala yake  walijulikana zaidi kwa majina yao ya Kizungu waliyoyarithi kutoka Wajerumani kupitia wazee wao wa Kizulu…

Ofisi ya Mwapachu pale Ilala ikawa kituo cha mijadala ya siasa nyakati za mchana.  Jioni vikao hivyo vya majadiliano vilihamia Tanga Young Comrades Club. Hiki kilikuwa kilabu maarufu cha kukutana, hasa kwa vijana maarufu na muhimu katika mji wa Dar es Salaam. Kilabu hiki kilikuwa New Street, Karibu na makao makuu ya TAA. Mijadala ya siasa nyumbani kwa Abdulwahid au katika ofisi ya Mwapachu Ilala au Tanga Club kidogo kidogo ikawa inaingia katika nadharia ya vile vijana wangeweza kuitoa TAA kutoka kwa wazee wale, ambao kwa hakika vijana waliwaona kama makapi ya utawala wa Kijerumaini.  Wakati ule mwaka 1949,  Mwalimu Thomas Plantan ndiye aliyekuwa rais wa TAA.  Katibu wake alikuwa Clement Mohammed Mtamila.

Si kwamba Tanganyika wakati ule ilikuwa na uhaba wa maswala ambayo yangeweza kuamsha mijadala ya siasa. Kulikuwa na mambo kadhaa ambayo kama yangetumiwa kwa ustadi na uongozi wa TAA, shida hizo zingeweza kuleta kwa watu hisia za manungíuniko na chuki dhidi ya serikali ya kikoloni. Unahitaji tu kuzipitia tahariri za Mashado Plantan katika gazeti la Zuhra ili kuweza kufahamu mambo yalivyokuwa nchini Tanganyika katika miaka ya 1950. Naye Mwalimu Thomas Plantan na damu yake ya Kizulu ya kupenda vita, baada ya kuwa yupo kwenye nchi yenye amani, aliielekeza banduki yake porini kuwinda wanyama. Hakuwa na muda kama rais wa TAA kushughulika na siasa. Uhodari wake katika kuwinda bado hadi leo unaweza kushuhudiwa nyumbani kwake Mtaa wa Masasi, Mission Quarters. Kuta za nyumbani kwake zimeshamiri mafuvu ya vichwa vya wanyama aliowaua huko porini. Kwa sabau alitumia wakati wake mwingi porini akiwinda,  hakuwa na muda wa kuitisha mikutano au kushughulikia mambo ya TAA. 

Makao Makuu ya TAA mjini Dar es Salaam yalikuwa kama vile yamegubikwa na usingizi mzito. Barua kutoka matawini hazikuwa zikijibiwa. Baya zaidi, hakukuwepo na mawasiliano yoyote na Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa, mjini New York ambalo ndilo lilikuwa likiitawala Tanganyika kama nchi ya udhamini. Hali ya wazee wa TAA ilikuwa na sura nyingi. Schneider alikuwa amekwisha onyesha chuki yake dhidi ya Waingereza na kwa ajili hiyo akawekwa kizuizini wakati wa Vita Vya Pili. Mashado Plantan alikuwa na gazeti lake Zuhra ambalo lilikuwa ndiyo sauti ya African Association. Lakini watu hawa walikuwa wazee na wamechoka. Hawakuwa na jipya katika siasa.

Walipochoshwa na uongozi huu wa wazee na walipoona hakuna lolote la maana liliokuwa siku moja wakati wa alasiri,  Abdulwahid na Mwapachu bila ya kumshauri mtu yeyote wakitokea Tanga Club, New Street, na kuivamia ofisi ya TAA na kufanya mapinduzi kwa kumtoa msobe msobe Clement Mtamila ofisini kwake. Abdulwahid alikuwa bingwa wa ngumi wa Tanganyika na Kenya katika kikosi chake wakati wa vita. Hakupata tabu sana kumtoa nje ya ofisi Mtamila.  Baada ya vurugu wazee walisalimu amri na wakaamua kuitisha uchaguzi makao makuu ya TAA. Mwezi Machi mwaka 1950, katika Ukumbi wa Arnatouglo, kijana wa Kihaya, Dr Vedasto Kyaruzi alichaguliwa kuwa rais na Abdulwahid Sykes katibu wake. Walipochukua uongozi, TAA ilikuwa na shilingi themanini na saba tu katika Barclays Bank. Huu ndiyo ulikuwa mwisho wa wazee,  kuongoza TAA nakuingia katika chama damu changa...''



No comments: