Saturday 24 June 2017

BAADA YA KUONDOKA BABA WA TAIFA TANZANIA BADO INAUNGA MKONO PALESTINA? SIKU YA QUDS - STATE UNIVERSITY OF ZANZIBAR


Prof. Haroub Othman ameandika sana kuhusu msimamo wa Tanzania katika kuunga mkono harakati za  Palestina wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere. Waandishi wengi wa somo hili la harakati za Wapalestina kudai ardhi yao wamekuwa wakianza utafiti wa historia hii hapa Tanzania na juhudi za Mwalimu Nyerere katika miaka ya 1960 mara baada ya uhuru wa Tanganyika. Wakati nafanya utafiti wa kitabu cha maisha ya Abdul Sykes, (naamini kitabu hiki si kigeni masikioni mwa wasomaji wangu), nilikutana na Sheikh Ali Saleh katika utafiti, Imam wa Msikiti wa Kitumbini katika miaka ya 1930 na kwa wakati mmoja katika miaka ya 1940 alipata kuwa rais wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika.

Sheikh Ali Saleh ndiye aliyemleta Ali Mwinyi Tambwe Tanganyika akiwa mtoto mdogo kutokea Comoro. Ali Mwinyi Tambwe alikuja kuwa katibu wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika na mmoja wa viongozi wa TANU. Haya nitakayoeleza hapa kuhusu Sheikh Ali Saleh nilielezwa na Ali Mwinyi wakati wa utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes, (Sheikh Ali Saleh ni babu yake mwandishi maarufu kutoka Zanzibar, Hamza Zubeir Rijal, mtoto wa Mwalimu Zuberi Rijal muhitimu wa Oxford University katika miaka ya 1940). Kutokana na maelezo ya Ali Mwinyi Tambwe ndipo nilipokuja kujua kuwa alikuwa Sheikh Ali Saleh ndiye aliyeanza kuwapigania Wapelestina hapa Tanganyika akitumia membari ya Msikiti wa Kitumbini kabla ya Mwalimu Nyerere kusimama na kutoa msimamo wa Tanzania kuhusu Wapalestina kuanzia miaka ya 1960:

‘’...Sheikh Ali Saleh alikuwa ndiye imam wa Msikiti wa Ijumaa ukijulikana kwa jina maarufu, Msikiti wa Kitumbini. Jina hili lilitokana kwa kuwa msikiti wenyewe umejengwa sehemu iliyokuwa ikijulikana kama Kitumbini. Sheikh Ali Saleh alikuwa mtu shujaa asiyeogopa mtu. Wakati ule wa ukoloni bila woga wowote alikuwa akitoa khutba za hamasa katika sala ya Ijumaa akiunga mkono Waarabu wa Palestine dhidi ya uonevu wa Uingereza katika mgogoro wa Mashariki ya Kati. Mgogoro huu ingawa ulikuwa mbali sana na Tanganyika lakini ulikuwa mmoja wa migogoro iliyokuwa ikiitatanisha serikali kwa kuwa Waislam walikuwa wengi Tanganyika na waliona shida ya Waislam Palestine ni shida yao.’’ (Kutoka kitabu, ‘’Maisha na Nyakati za Abdulwahid Sykes (1924 – 1968)…’’).

Kwa historia hii ya Sheikh Ali Saleh inaonekana kuwa tatizo la Palestina lilipoanza kushughulikiwa Tanganyika, tatizo hili lilichukua sura ya kuwa ni tatizo lililowahusu zaidi Waislam kuliko watu wengine. Lakini huu ulikuwa wakati wa Waingereza wanaitawala Tanganyika. Uhuru ulipopatikana sera ya Tanzania ilikuwa ni kuwaunga mkono wote wanaodhulumiwa duniani pamoja na Wapelestina ingawa Nyerere alikuwa rais Mkatoliki. Katika kupinga dhulma Nyerere akawa ameacha historia kubwa sana. Baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka wa 1999, pametokea ndani ya Tanzania mabadiliko makubwa yaliyogusa sehemu nyingi katika misingi ambayo ndiyo ilikuwa utambulisho wa nchi. Mojawapo ya mabadiliko haya makubwa ni msimamo wa Tanzania kwa Israel na tatizo la Wapelestina. 

Leo Tanzania imefungua ubalozi Israel baada ya kukata uhusiano na nchi hiyo mwaka wa 1967 baada ya Vita Vya Siku Sita kati ya Israel, Misri, Iraq, Syria, Jordan and Lebanon. Katika vita hivi nchi hizi za Kiarabu zilishindwa vita vile vibaya sana. Kipigo hiki kilikuwa pigo kubwa sana kwa Wapalestina kwani kushindwa kwa nchi hizi za Kiarabu ilithibitisha nguvu kubwa za kijeshi za Wayahudi ambayo tafsiri yake ilikuwa ni nchi yao kuendelea kukaliwa na Mazayuni. Hali hii ilizidisha tatizo la ardhi ya Wapalestina kwani Wayahudi waliteka sehemu kubwa ya Misri na Syria achilia mbali tatizo la kuongezeka kwa wakimbizi. Vita vya Siku Sita mwaka wa 1967 vilifuatiwa na Vita Vya Yom Kippur mwaka wa 1973. Laiti kama si usaliti uliopitika katika uongozi wa Misri wakati vita vimeshamiri kwa Anwar Sadat kuzuia katika hali ya ushindi, majeshi ya Misri kusonga mbele katika uwanja wa mapambano, Israel ilikuwa isalimu amri. 

Katika kitabu chake, ‘’The Road to Ramadan,’’ Mohamed Heikal anaeleza barua aliyoandika Hafiz Al Asad kwenda kwa Sadat akimsihi kuendelea na mapambano. Barua hii haikumbadilisha Sadat. Kwa kitendo hiki cha kuacha mashambulizi dhidi ya Israel, majeshi ya Syria yakalazimika kupigana na Israel bila ya mshirika wake Misri na hii ikatoa ahueni kubwa kwa Wayahudi na matokeo yake ikawa Israel kunusurika. Inasemekana kwa usaliti huu ndipo vijana wa Ikhwan Egyptian Islamic Jihad ndani ya jeshi la Misri wakampitishia fatwa ya Sadat kuuawa na hakika hilo likafanyika mwaka wa 1981. Kitu muhimu kilichojitokeza katika Vita Vya Yom Kippur ilikuwa kule kujitokeza kwa mara ya kwanza udhaifu katika jeshi la Israel kuwa linaweza kushindika. Baada ya vita hizi mbili Wapalestina walifanya kile kilichokuja kujulikana kama Intifada kati ya mwaka 1987 – 1993 kisha mwaka wa 2000 – 2005. Intifada ilidhihirisha kwa Wayahudi kuwa mapambano dhidi yao kutoka kwa Wapestina bado yangalipo na hayatakoma.

Vita iliyokuja kumaliza kile kilichokuwa kimeaaminika na dunia kuwa Wayahudi hawawezi kushindwa katika vita, ni vita vya mwaka wa 2006 kati ya Hizbullah na Wayahudi. Vita vilipoanza fikra za wengi katika nchi za Kiarabu zilirejea katika Vita Vya Siku Sita vya mwaka wa 1967 na wengi waliamini kuwa Hizbullah watamalizwa kwa muda mfupi kwa kusagwasagwa na Israel. Hili halikutokea. Vita vilipiganwa kwa siku 34 katika mwezi wa Julai na Agosti hadi pale Umoja wa Mataifa ilipoingia kati na kuweka makubaliano ya kuweka silaha chini na kumaliza vita. Wayahudi kwa mara ya kwanza katika historia ya mapambano yao na Waarabu walionekana katika stesheni nyingi kubwa za televisheni duniani wakirudi Israel kutoka uwanja wa mapambano wameinamisha chini vichwa vyao. Israel ilikuwa kwa mara ya kwanza imeonja kipigo katika vita. Hapakuwa na shamrashamra ziliyozoeleka za ushindi dhidi ya majeshi ya Kiarabu. Hizbullah ilikuwa imevunja, ‘’myth,’’  ile fikra ya kuwa Wayahudi hawawezekani. Hassan Nasrallah kiongozi wa Hizbullah alikuwa akiuliza wakati wa vita, ‘’Wako wapi askari wa Kiyahudi mbona hatuwaoni katika uwanja wa vita? Tunachoshuhudia ni ndege za Kiyahudi wakipiga mabomu nyumba za raia.’’ Baada ya vita, ilipofika wakati wa kubadilishana mateka Wayahudi walipata fadhaa zaidi pale walipokuwa wao wanapokea majeneza ya askari wao waliouliwa vitani na Hizbullah na wao wakiwaachia huru askari hai wa Hizbullah.

Katika hali hii Tanzania imerudisha uhusiano na Wayahudi. Hili linaweza likaelezwa kwa kile ambacho ni katika kinachostaajabisha katika uhusiano kati ya mataifa ambayo Ukristo una nguvu kwa hiyo unaongoza serikali. Amerika ni taifa la Kikristo na rafiki mkubwa wa Israel lau kama Wayahudi ndiyo waliomuua Yesu, ambae wao kama Wakristo wote duniani wanamuitikadi ni ‘’Mtoto wa Mungu.’’ Kwa Wamarekani Israel ni rafiki na mshirika wake si adui abadan. Waamerika wana marafiki katika mataifa ya Kiislam kama vile walivyokuwa pia wana maadui wengi katika mataifa ya Kiislam. Ukristo umedhibiti vyema serikali ya Tanzania. Huu uhusiano baina ya Ukristo na Uyahudi unaweza kuwa moja ya sababu ya kuona Tanzania imerudisha uhusiano na Israel na balozi wake kujifaharisha na kibandiko cha Kiyahudi pale alipokwenda kujitambulisha kwa Wayahudi.





Ningependa kuhitimisha kwa kurejea katika historia ya Wayahudi na Tanzania hususan Tanzania Visiwani, yaani Zanzibar. Israel ilihusika sana lakini kwa usiri mkubwa katika kupinduliwa kwa serikali ya Sheikh Mohamed Shamte iliyokuwa ni muungano wa Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kwa jina linguine Hizbu na Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZNPP) ambayo Wayahudi waliingalia kwa jicho la kuwa ni, ‘’serikali ya Waarabu,’’ adui zao wakubwa chini ya Sultan wao Jamshid bin Abdullah. Hii ikawa moja ya sababu kubwa kwa wao kuisaidia Afro Shirazi Party  walichokiona chama cha Waafrika dhidi ya Hizbu chama cha ''Waarabu,'' katika Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964. (Katika maajabu ya historia ni kuwa Ali Mwinyi Tambwe aliyeletwa Tanganyika na Sheikh Ali Saleh akiwa mtoto mdogo alihusika sana katika kuipindia serikali ya Zanzibar akishirikiana na viongozi wa Tanganyika). Ukristo una nguvu kuja katika uongozi wa serikali Tanzania. Watendaji hawa Wakristo  katika serikali ya Tanzania kwa kuuhusisha Uislam na Uarabu si ajabu kuwa nafsi zao siku zote zilikuwa zinataka kuona Tanzania na Uyahudi wanakuwa pamoja katika uhusiano wa kimataifa. Zanzibar kama nchi yenye Waislam wengi na ikiwa ni sehemu ya muungano kwa hakika isingependa kuona Wayahudi wanarudi tena katika ardhi ya Tanzania lakini hawana la kufanya katika maamuzi makubwa na muhimu kama haya.

Huu ukiwa ndiyo ukweli ni nini khatma ya harakati za Wapelestina dhidi ya Israel katika kuungwa mkono na Tanzania?


Notes za mazungumzo

Mkuu wa Idara ya Lugha za Kigeni SUZA Dr, Ziddy

Wanafunzi wa SUZA wakifuatilia mada kuhusu Palestine


Mwandishi akiwasilisha mada kulia kwake ni Balozi Mdogo wa Iran Muhammad Dehghani na kushoto ni Ali Bagheri Mwambata wa Utamaduni Ubalozi wa Iran

Wakati wa Maswali na Majibu
Kushoto ni Prof. Haroub Othman, Ahmed Rashad Ali na Ahmed Islam wakiwa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere
wakisuburu kupanda ndege kwenda Makka kufanya Umrah mwaka wa 1997


No comments: