Chief Makwaia Mohamed Mwandu |
Nimeona tangazo la Busiya Chiefdom katika
mitandao ya kijamii na nikaangalia, ‘’clip,’’ yake. Hili ni tamasha linalofanyika
hapo Busiya kulipokuwa na uchifu wa Makwaia. Mwalimu Nyerere alifuta uchifu
katika baada ya uhuru wa Tanganyika lakini taratibu uchifu unarejea kwa kuona
umuhimu wa kuenzi asili za watu na utamaduni wao. Uchifu huu hauna mamlaka ya
utawala ila heshima na kumbukumbu.
Chief Michael Lukumbuzya |
Historia ya Mwalimu Nyerere na machifu
waliokuwapo Tanganyika toka enzi na enzi, kama baba yake Chief Edward Makwaia,
Chief David Kidaha Makwaia, Chief Abdallah Said Fundikira, Chief Haruna Msabila
Lugusha, Chief Thomas Marealle, Chief Makongoro, Chief Abdiel Shangali, Chief Kunambi, Chief
Majebele, Chief Adam Sapi Mkwawa, Chief Ngua na mkewe Mwami Theresa Ntare,
Chief Mang’enya, Chief Michael Lukumbuzya na wengineo ni historia yenye msisimko wa kipekee kabisa.
Nimebahatika katika maisha yangu kufahamiana na
baadhi ya hawa machifu katika siku zao za mwisho wa maisha yao na pia
kufahamiana na watoto wao kwa karibu na kutoka kwao nimejifunza mengi katika
yale yaliyokuwa katika fikra za wazee wao na yale waliyokuwanayo wao wenyewe
binafsi.
Kulia: Abraham Ally Sykes na Kibo Marealle nyumbani kwa Mwandishi Tanga1999 |
Kuwa hivi sasa uchifu wa Makwaia wa Busiya
Usukumani umerejea hakika ni kitendo cha kupigiwa mfano.
Kumbukumbu nyingi za machifu waliokuwapo aidha
zimekufa kabisa au hazipo na zile zilizokuwapo ziko taabani.
Labda nieleze kwa nini nimeguswa na uchifu Mkwaia
wa Busiya.
Nimeguswa na uchifu wa Busiya kwa kuwa kiongozi
wa uchifu huu ni rafiki yangu toka utotoni.
Nimejuana na Chief Edward Anthony Makwaia mwaka
wa 1967 sasa imepita miaka 50, yaani nusu karne.
Nilimfahamu Edward pale nilipoingia St. Joseph’s
Convent mwaka wa 1967 kujiunga na elimu ya sekondari na tulisoma darasa moja
hadi mwaka wa 1970. Yeye alikuwa anatolea Salvatorian College na mimi Kinondoni Primary School.
Katika miaka hii minne ya shule tuliingiliana
sana na Edward akawa rafiki yangu kipenzi na kupitia kwake nikajuana na jamaa
zake wengi kama akina Mwapachu na akina, Yunge na Gordon. Lakini katika maajabu
ya maisha ni kuwa hata kabla sisi hatujazaliwa wazee wetu kwa njia za ajabu
kabisa walikuwa na uhusiano wa hapa na pale.
Mmoja katika ukoo wa kina Yunge aliingiliana
sana na wazee wangu katika miaka ya 1950 na nina picha nilipiga na Kapufi Yunge
sote tukiwa watoto ingawa Kapufi alikuwa kanitangulia labda kwa miaka miwili
hivi. Picha hii ninayo katika maktaba na nikiitia mkononi nitaiweka hapa. Picha
hii ilikuwa ukutani kwa mama yangu mkubwa Bi. Mwanaisha bint Mohamed kwa
kipindi chote cha maisha yake na kila alipokuwa akiizungumza ile picha alikuwa
akimwita Kapufi, ‘’Chapa Ng’ombe,’’ kwa ajili ya ule Usukuma wake kwani
Wasukuma ni wafugaji wakubwa wa ng’ombe.
Picha hii ilipigwa mwaka wa 1956 katika studio
ya Gomes, iliyokuwa Acacia Avenue (Baada ya uhuru 1961 mtaa ukaitwa
Independence Avenue na sasa ni Samora Avenue. Huyu Gomes ndiye aliyepiga ile
picha maarufu ya waasisi wa TANU mwaka wa 1954).
Katika mwingiliano huu nikamkuta
Edward ambae siku zile tulizoea kumwita Teddy akiwa na udugu na jamaa zangu
wengi, mmoja wa ‘’cousin sister,’’ wake Lilian amabe tulizoea kumwita Lilly akiwa
ni binti ya Abbas Sykes. Mimi, Teddy, Lily (ambae tulikuwa sote St. Josephs),
Kleist Abdul Sykes, Ebby Abdul Sykes, Monalisa na Alma Ally Sykes ikawa sote
tumekuwa pamoja utotoni tukiwa na watoto
wa koo mashuhuri katika Dar es Salaam ya wakati ule kama akina Lyabandi, Abbas Max,
Sykes, Tsere, Singano, Bizuru, Msikinya, Lukindo, Mkwawa, Maharage, Masayanyika, Mang’enya, Muhuto, Fritsch, Kondo, Kafumba, Mzena, Bomani,
Kahama, Kharusi na nyingineo nyingi. Kundi hili ambalo ndilo rika langu sasa
sote sisi ni watu wazima na umri wetu wastani ni miaka 60.
Katika familia hizi kuna historia kubwa ambazo
kwa wakati ule wa utoto sikuzijua hadi nilipofika utu uzima. Historia ambazo
zinakwenda na historia ya Tanganyika kuanzia kupigania uhuru wa Tanganyika na
Zanzibar hadi kufikia mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka wa 1964. Historia ya mauaji
kwa Zanzibar hadi vifungo vya siasa na kudhulumiwa kwa mali kote Tanganyika na
Zanzibar.
Waasisi wa TANU Picha iliyopigwa na Gomes 7 Julai, 1954 |
Kulia: Ali Muhsin Barwani, Dr. Idarus Baalawy, Mohamed Shamte, Juma Aley na Ibun Saleh |
Ilinichukua miaka mingi kuja kuijua historia ya
ukoo wa Kharusi, Ibun na Shamte wa Zanzibar ingawa marafiki wawili wa baba yangu, Abdulaziz Twala na Jaha Ubwa walikuwa wameuawa baada ya mapinduzi. Ilinichukua miaka mingi pia kuja kuijua historia
ya Chief Kidaha Makwaia. Nilipigwa na bumbuazi siku nilipoambiwa kuwa Abdul Sykes alimtaka Chief Kidaha Makwaia awe Waziri Mkuu Tanganyika itakapokuwa huru kwa Chief Kidaha kuwa rais wa TAA kisha waunde TANU yeye Chief Kidaha akiwa rais wa TANU. Hii iikuwa katika miaka ya 1950 wakati ule Chief Kidaha mjumbe wa LEGCO.
Ilinichukua pia miaka mingi kuijua kwa undani historia
ya ukoo wa Sykes lau kama hawa walikuwa jamaa wa karibu sana na wazee wangu kuanzia mababu
zangu katika miaka ya 1920. Kwa hakika ilinichukua miaka mingi kuijua historia
ya babu yangu mwenyewe katika kupigania uhuru wa Tanganyika na kupigania haki
za wafanyakazi kupitia vyama vya wafanyakazi. Wakati ule sikuweza kutambua kuwa ule urafiki niliyokuwa nashuhudia baina ya Edward Makwaia na Kleist Sykes umetoka mbali kwa baba zao wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Sikuweza kwa wakati ule kujua kuwa ule ukaribu wa Wendo Mwapachu na Kleist ulitoka huko nyuma pia.
Kwa miaka ile ya utoto sisi watoto kutoka
familia hizi sote tulikuwa wamoja tukicheza pamoja wakati mwingine watoto wa
washindi na washindwa au ukipenda watoto wa waliodhulumu haki za watu na
wadhulumiwa tukiwa wamoja bila kujua yale yaliyopitikana siku za nyuma kati ya
wazee wetu na watawala waliokuwa madarakani.Ilinichukua miaka mingi kujua kuwa eneo lote la Upanga hadi kufikia Selender Bridge hadi Ikulu ilikuwa hodhi ya ukoo waTambaza hadi kufikia miaka ya 1800 na wakanyang'anywa na Wajerumani na hadi leo kuna makaburi ya mababu zao ndani ya Ikulu. Katka miaka ya 1980 waliamua kutoa ardhi iliyokuwa makaburi ya wazee wao Upanga ujengwe msikiti uliopewa jina, ''Masjid Maamur.'' Huu uliongeza misikiti inayowahusu Dar es Salaam kuwa mitatu wa kwanza ukiwa Masjid Mwinyikheri Akida ambao (una zaidi ya miaka 100 na ndiyo msikiti wa kale kupita yote Kariakoo) na Masjid Tambaza.
Kulia: Asya Kharusi na Sambayawo Nyirenda hawa wote ni madaktari wa binadamu. Baba yake Sambayawo, Alexander Gwebe Nyirenda ndiye aliyepandisha bendera ya Tanganyika Mlima Kilimanjaro usiku wa uhuru |
Kama ulivyo wastani wa umri wetu miaka 60 na miaka
ya utoto wetu ilikuwa katika 1960s na Waingereza waliipa jina miaka hii
wakaiita, ‘’The Roaring 60s,’’ na kwa hakika hii ilikuwa miaka ya aina yake.
Tulikulia katika mazingira na utamaduni wa aina yake. Waingereza walikuwa
wameondoka na wamewaachia utawala wazee wetu. Wazee wetu waliathirika na sisi watoto wao pia.
Waliokaa kulia: Yusuf Zialor, Wendo Mwapachu Kulia waliosimama ni Abdallah Tanbaza Abdul Mtemvu na Abdallah Mggambo |
Palikuwa na aina mpya ya maisha ambayo kwa kiasi
fulani yalitia afueni kwa wazee wetu kwa kukamata nafasi za kazi ambazo zamani
zilikuwa zikishikiliwa na Wazungu na Waasia.
Wazee wetu walikuwa wanapumua kutokana na kazi
ngumu ya kupigania uhuru katika miaka ya 1950.
Hata hivyo katika hali hii palikuwapo pia na
majeruhi ya harakati za ukombozi wa Tanganyika. Baadhi ya majeruhi hawa
walikuwa machifu ambao jana tu walikuwa watu wenye hadhi zao katika jamii
lakini ghafla baada ya uhuru kupatikana na Mwalimu Nyerere kufuta uchifu, machifu hawa wakajikuta katika hali ambayo hawakuitegemea kamwe.
Hii ni historia ya pekee inayohitaji ipatiwe
nafasi iandikwe.
Juu ya haya yote mmoja kati yetu watoto
tuliolelewa katika miaka ya 1960 wakati Tanganyika inapata uhuru wake kutoka
kwa Waingereza, leo ni Chief wa Busiya, utawala uliokuwa na nguvu katika wakati
wake.
Vipi Edward na watu wa Busiya wameweza kurejesha
uchifu wa mababu zao, vipi waliweza kumtawaza Chief Edward Anthony Makwaia na mengi mengine
nadhani iko siku yataelezwa.
Kwa sasa muhimu ni kuwa kila mwaka wakati wa
Saba Saba, Wasukuma wa Busiya huwa wanafanya tamasha kuhuisha utamaduni wao na uchifu
uliozaliwa upya wa Busiya.
Chief Edward Anthony Makwaia katika vazi la kichifu |
Chief Edward Anthony Makwaia akicheza ngoma ya Kisukuma 2016 |
Kulia: Edward Makwaia, Willliam Mfuko, Mwandishi na Khalid Abdallah |
Kulia: Mwandishi, Yusuf Zialor, Kleist Abdulwahid Sykes, Bubby, Abdallah Tambaza waliokaa kulia ni Abdul Mtemvu, Wendo Mtega Mwapachu na Kessy |
Kushoto Lilian Abbas Sykes akizungumza na Jaji Mark Bomani mwisho kulia ni Mohamed Chande Jaji Mkuu Mstaafu |
Mwandishi katika sherehe ya siku za kuzaliwa Iqbal Bapumia ''class mate,'' 1969 Picha kapiga Iqbal |
Kwa habari zaidi ingia:
- http://www.mohammedsaid.com/2014/06/chief-david-kidaha-makwaia.html
- http://www.mohammedsaid.com/2016/07/kutoka-fb-ali-mwakwere-kamuadhimisha.html
- http://www.mohammedsaid.com/2016/05/hamza-mwapachu-abdulwahid-sykes-na.html
- http://www.mohammedsaid.com/2016/12/zuberi-mtemvu-mpangaji-mikakati-watanu.html
- http://www.mohammedsaid.com/2016/06/babu-yangu-salum-abdallah.html
No comments:
Post a Comment