Wakati nafanya utafiti wa kitabu cha Abdul Sykes
nilikutana na matokeo manne ambayo wananchi walijikusanya na kufanya visomo au dua
kujikinga na dhulma za ukoloni wa Waingereza. Katika matukio haya manne ya
kumuomba Mungu ni tukio moja tu ndilo wafanyaji kisomo walichobainisha kuwa inayosomwa
ni ‘’Halal Badr’’ neno ambalo hivi sasa limekuwa maarufu midomoni mwa watu
wengi baada ya kuelezwa kuwa kutasomwa Halal Badr makhsusi kufuatia jaribio la
kumuua Mbunge wa Singida Mashariki, Mheshimiwa Tundu Lissu.
Nitarudi nyuma kiasi cha nusu karne na zaidi
kuangalia nafasi ya visomo katika kutafuta haki. Nitaaanza kwa kueleza
mazingira yaliyokuwapo wakati wa ukoloni hadi kusababisha wananchi kumgeukia
Mungu na kutaka msaada wake na hivyo kusoma Halal Badr.
Nakuwekea msomaji wangu yale niliyoandika katika
kitabu cha Abdul Sykes, kitabu ambacho ndani yake nimejaribu kueleza historia ya
uhuru wa na kuandika kuhusu Halal Badr
ili kwa yule ambae ni mgeni katika mambo haya apate picha kamili na Tanganyika
ili uweze kuona ilikuwa na kujua ni wakati gani wananchi waliamua kufanya dua
iwe Halal Badr au kisomo kingine kama kinga yao dhidi ya nguvu ambayo wao
waliona ni Mungu pekee ndiye angeliweza kuwapa nusra.
Labda tujiulize imekuwaje leo baada ya zaidi ya
nusu karne wananchi wanarejea katika mbinu ambazo wengi wanaona kuwa kuzirejea
tena katika Tanzaia huru ni kitu ambacho kidogo kinashangaza hasa kwa kuwa dini
kama inavyoelezwa kuwa haina nafasi katika uendeshaji wa serikali.
Naanza kwa kukuwekea hapo chini mara yangu ya
kwanza nilipokutana na huu makakati ambao kwa hakika ulikuwa mpya katika mbinu
za kudai haki kwa kukueleza vuguvugu la makuli katika bandari ya Dar es Salaam
pale walipoamua kupambana na dhulma za wakoloni kwa kusoma Halal Badr mwaka wa
1947:
‘’…kidogo kidogo Kleist alianza kumkabidhi Abdulwahid kazi
za African Association na mara akawa msaidizi wa baba yake katika siasa za Dar
es Salaam. Ilikuwa katika kutimiza haya ndipo Abdulwahid akajikuta anahusika na
ule mgogoro wa makuli ulioibuka bandarini Dar es Salaam ambao ulikuwa ukichemka
pole pole chini kwa chini kwa muda mrefu tangu kumalizika kwa vita. Hatimaye,
Abdulwahid alihusika na harakati za siri za wafanyakazi bandarini ambao, wakiwa
wamechoshwa na sheria za kazi za ukandamizaji na wakiwa wamechoka kunyonywa na
makampuni ya meli, walikuwa wanapanga kuitisha mgomo.
Chama cha African Association ndicho kiliwakilisha maslahi
ya wananchi wa Tanganyika na kimya kimya kiliunga mkono zile harakati za chini
kwa chini za wafanyakazi katika kutafuta haki zao. Abdulwahid, kijana mdogo
mwenye elimu na akiwa karibu zaidi na uongozi wa African Association kuliko
Mwafrika yoyote pale mjini, alichaguliwa kuongoza harakati za tabaka la
wafanyakazi zilizokuwa zinaibuka. Haya ndiyo mambo serikali ya kikoloni
ilihofia na ndiyo ilikuwa sababu ya kumfanyia khiyana asiingie Makerere.
Utawala wa kikoloni ulifahamu kuwa msukumo wa Kleist na mwanae aliyeelimika
ungeipa Tanganyika uongozi uliokuwa unakosekana Tanganyika na pengine hata
ndani ya Al Jamitul Islamiyya.
Ili kuifanya serikali iwasikilize mahali ambapo hapakuwa na
sheria za kazi, ilibidi iwekwe mikakati ambayo ingeifanya serikali iweke sheria
hizo katika vitabu vyake. Kamati ndogo ya siri iliundwa na Abdulwahid akatiwa
ndani ya kamati hiyo ili kuongoza mgomo uliokusudiwa. Kazi ya kamati hiyo
ilikuwa kupanga na kuratibu mikakati ya kuitisha mgomo ambao ungelisaidia
katika kuondoa ile dhulma iliyokuwepo. Makuli waliitisha mkutano pembeni kidogo
mwa mji, mahali palipokuwa pakijulikana kama ‘’Shamba kwa Mohamed Abeid,’’
katika bonde la Msimbazi. Sehemu hii ilichaguliwa makhususi mbali na macho ya
watu ili ipatikane faragha. Makuli walikula kiapo na kusoma, ‘’Ahilil Badr,’’
ili kujikinga na unafiki, usaliti pamoja na shari ya vizabizabina wangeokataa kugoma. Ubani ulifukizwa na Qur’an
ilisomwa. Wakijikinga na kiapo hicho cha mashahidi wa vita vya Badr na huku wakichochewa
na ushujaa wa mashahidi waliokufa katika katika
vita vya Badr wakipigana na washirikina wa Makka wakiwa pamoja na Mtume
Muhammad (Rehema na Amani za Mwenyezi Mungu Ziwe Juu Yake), makuli walichagua
tarehe 6 Septemba, 1947 kuwa ndiyo siku ya kuanza mgomo wao.
Mapema asubuhi moja kile kilichoanza kama mipango ya siri
dhidi ya makampuni ya Wazungu bandarini,
kililipuka na kuwa mapambano ya dhahiri. Watu katika mitaa jirani ya alipoishi
akikaa Abdulwahid walikuwa hawajatoka vitandani mwao alifanjiri moja
waliposikia vishindo na makelele vimetanda mtaani. Makuli, baadhi yao wakiwa
vidari wazi, walikuwa wameizingira nyumba ya Kleist, wakipiga makelele
wakimtaka Abdulwahid atoke nje. Makuli wale walipiga kwata njia nzima kutoka
bandarini huku wakitoa maneno ya kupinga ukoloni na wakiimba kupandisha morali zao. Tukio hili
halikuwa na kifani. Ilikuwa ni mara ya kwanza nchini Tanganyika kwa wananchi
kushuhudia katika mitaa ya Dar es Salaam uasi wa dhahiri kama huo dhidi ya
serikali ya kikoloni. Abdulwahid, wakati ule kijana mdogo kabisa, akichungulia
kupitia dirisha la chumba chake alichokuwa amelala, alishangazwa kuona umati
mkubwa wa watu nje ya nyumba yao. Aliweza kuwatambua baadhi ya wenzake katika
kamati ile ya siri iliyokuwa inapanga mipango ya mgomo. Alipotoka nje kuonana
nao makuli wenye hasira walimfahamisha kuwa mgomo ulikuwa umeanza na
wasingerudi kazini hadi madai yao yote yamekubaliwa…’’
Kisomo kingine
nilichokutana nacho wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika kilifanyika Lindi na
kisomo hiki kilifanywa na Sheikh Yusuf Badi lakini kwa kauli ya mpashaji habari
wangu kisomo hiki kilikuwa Tawasul na katika waliohudhuria kwa kutajiwa majina yao
walikuwa Suleiman Masudi Mnonji na Bi.
Sharifa bint Mzee:
Bi. Shariffa Bint Mzee |
‘’Nyerere aliporudi Lindi mwaka 1959, TANU ilikuwa ina nguvu
sana na ilikuwa imekumba kila mtu. Wale watumishi wa serikali wengi wao wakiwa
Wakristo, walio kuwa wakiibeza TANU
mwaka 1955 kwa sababu ilikuwa ikiongozwa na Waislam ëwasiokuwa na elimu,í
ukweli ulikuwa umewadhihirikia na sasa walikuwa wakionyesha heshima kwa chama.
Hawakuwa na khiyari na ilibidi waonyeshe heshima kwa sababu bwana mwenyewe,
yaani serikali ya kikoloni, ilikuwa na heshima kwa TANU. Serikali ilikuwa
imetambua kuwa dhamiri ya watu ya kukataa kutawaliwa haiwezi tena kupuuzwa.
Nyerere alikuwa amelihutubia Baraza la Udhamini la Umoja wa Mataifa mara mbili,
mara ya pili ikiwa mwaka 1957. Ujumbe wa TANU ulikuwa wazi, watu wa Tanganyika
walikuwa tayari kujitawala. Kila siku zilivyopita ndivyo TANU ilivyopata nguvu.
Rashidi Salum Mpunga, dereva wa lori, aliweza kumshawishi na akafanikiwa
kumuingiza TANU mmoja wa masheikh wenye kuheshimiwa sana mjini Lindi na mshairi
maarufu, Sheikh Mohamed bin Yusuf Badi. Sheikh Badi alipoingia TANU kwa ajili
ya heshima yake na kukubalika na watu, idadi kubwa ya Waislam walimfuata na
kukata kadi za TANU. Nyerere alipokuja Lindi kujadili tatizo la kura tatu na
uongozi wa Jimbo la Kusini, Sheikh Yusufu Badi alimpokea Nyerere na madras
yake, wanafunzi wakimwimbia Nyerere kasda na kumpigia dufu. Kuanzia hapo sasa
kila mtu alijiunga na TANU. Si Mponda wala Kanisa lilikuwa na uwezo wa
kupambana na TANU kwa wakati ule. Polepole lakini na kwa kwa uhakika, TANU
ilingia ndani ya maeneo ya Kikristo huko Songea, Masasi, Tunduru na Newala,
nyumbani kwa Yustino Mponda.
Lakini matukio mawili ya kumbukumbu kubwa yalikuwa katika
safari ya pili ya Nyerere alipozuru tena Jimbo la Kusini. Kumbukumbu ya kwanza
ilikuwa tawaswil aliyosomewa Nyerere na Sheikh Yusuf Badi mwenyewe pamoja na
Waislam aliowachagua yeye sheikh mwenyewe maalum kwa hafla hiyo, pamoja na
waliochaguliwa na masheikh wengine.’’
Kisomo kingine na hiki ndicho maarufu ni kile
kilichofanywa nyumbani kwa Jumbe Tambaza Upanga ambacho Mwalimu Nyerere mwenyewe
amekieleza.
Kisomo cha nne kilifanyika Mnyanjani, Tanga
mwaka wa 1958 wakati TANU ilipokuwa inakabiliwa na tatizo la Kura Tatu:
‘’Siku kadhaa kabla ya kusafiri kwenda
Tabora kwenye ule mkutano mkuu wa mwaka wa TANU, Nyerere na Amos Kissenge,
Kaimu Katibu Mwenezi wa TANU, walisafiri kwenda Tanga kushauriana na uongozi wa
Kamati Kuu ya Taifa ya TANU Tanga kuhusu matatizo yaliyoletwa na Uchaguzi wa Kura
Tatu. Mkutano huu baina ya Nyerere, Kissenge na ule uongozi wa Tanga ulikuwa wa
siri sana. Tanga iliwakilishwa na Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Abdallah Rashid
Sembe, Ngíanzi Mohamed, Mustafa Shauri na Abdallah Makatta. Nyerere alizungumza
waziwazi na kwa ithibati ya moyo wake. Nyerere alikiambia kikao kile kuwa
amekuja Tanga kuomba wamuunge mkono kwa sababu ilikuwa ni matakwa yake TANU
lazima ishiriki katika ule uchaguzi wa kura tatu uliokuwa unakaribia hata
masharti yakiwaje. Nyerere aliuambia uongozi wa Tanga uliokuwa ukimsikiliza kwa
makini kuwa alikuwa amekuja kwao kwa sababu watu wa Tanga wanajulikana kwa
ufasaha wa lugha na kwa uwezo wao wa kuzungumza vizuri. Nyerere alisema
angehitaji hiki kipaji adimu cha watu wa Tanga kuunga mkono msimamo wake huko
Tabora. Nyerere alitoa hoja kwamba TANU lazima iingie katika uchaguzi kwa
sababu kuususia ni sawasawa na kukipa chama hasimu, UTP ushindi bila jasho
kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria. TANU ingedhoofika na hivyo ingekosa
sauti katika maamuzi yatakayotolewa na serikali katika siku zijazo.
Kufichuka kwa msimamo wa Nyerere wa
kutaka TANU iingie kaatika kura tatu kulishtua uongozi wa Tanga. Majadiliano
makali yalifuata uongozi wa Tanga ukionyesha upinzani wao kwa msimamo wa
Nyerere. Baada ya majadiliano ya muda mrefu Nyerere alifanikiwa kuwashawishi
wote wawili, Hamisi Heri na Mwalimu Kihere ambao ndiyo walikuwa wapinzani
wakubwa wa msimamo wa Nyerere na uchaguzi wa kura tatu. Nyerere
aliutahadharisha uongozi wa Tanga kuwa agenda ya kura tatu itakapokuja
anatabiri kupata upinzani mkali kutoka katika majimbo. Huko Tanga kwenyewe,
TANU ilikuwa ikikabiliwa na upinzani mkali kutoka UTP na serikali. Matawi
kadhaa yalikuwa yamepigwa marufuku. UTP
ilikuwa na nguvu Tanga kwa sababu wanachama wake wengi walikuwa wakimiliki
mashamba ya mkonge katika jimbo hilo. Kwa ajili hii chama kilikuwa kinaelemewa
na mashambulizi kutoka wa wapinzani. Wakati huo Tanga ilikuwa imetoa viongozi
wenye uwezo lakini wote walikuwa wamehamishiwa makao makuu mjini Dar es Salaam.
Wapangaji mikakati wazuri kama Peter Mhando alikuwa amehamishiwa Dar es Salaam
na kutoka hapo alipelekwa Tabora ambako si muda mrefu akafa. Elias Kissenge
vilevile alihamishiwa makao makuu kushika nafasi ya Katibu Mkuu wa TANU baada
ya Oscar Kambona aliyekuwa ameshika nafasi hiyo kwenda Uingereza kwa ajili ya
masomo. Uongozi wa TANU Tanga hata baada ya kujadili mbinu waliyopanga na huku
Nyerere akielekeza mikakati ambayo Mwalimu Kihere na Abdallah Rashid Sembe
wataitekeleza Tabora, bado uongozi ule ulikuwa na wasiwasi wa mafanikio ya
mpango huo. Kwa ajili ya wasiwasi huu, viongozi wa TANU wa Tanga walimuomba
Nyerere wawe pamoja ili ifanywe tawaswil waombe msaada wa Allah awape ushindi
dhidi yaa vitimbi vya Waingereza.
Maili tatu kutoka Tanga kipo kijiji cha
Mnyanjani ambako kulikuwako na tawi la TANU lililokuwa na nguvu sana likiongozwa
na Mmaka Omari kama mwenyekiti na Akida Boramimi bin Dai akiwa katibu. Mmaka
alikuwa kijana aliyekuwa akiendesha mgahawa pale kijijini na Akida bin Dai
alikuwa mwashi. Akida aliongoza tawi la vijana wa TANU ambalo baadae lilikuja
kujulikana kama Tanga Volunteer Corps (TVC). TVC ilikuwa sawasawa na Bantu
Group, ambayo wakati huo ilikuwa imekwishaanzishwa huko Dar es Salaam na
Tabora. Vikundi hivi mbali na kufanya shughuli za propaganda na kuhamasisha
wananchi halikadhalika viliifanyia TANU ujasusi. Nyerere na Kissenge
walichukuliwa hadi Mnyanjani na tawaswil ikasomwa. Waliohudhuria kisomo
hicho walikuwa Abdallah Rashid Sembe,
Sheikh Dhikr bin Said, Mzee Zonga, Hemed Anzwan, Salehe Kibwana aliyekuwa
mshairi maarufu, Akida Boramimi bin Dai na Mmaka Omari. Aliyechaguliwa kusoma
Quran Tukufu alikuwa mjomba wa Mwalimu Kihere, Sheikh Ali Kombora…’’
Kipo kisomo kilifanywa na wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo mwaka wa 1954/55 wakimnuia Town Clerk Mwingereza ambae alikuja
Kariakoo Market kukamata kadi za TANU ambazo Abdul Sykes alikuwa kaziweka
ofisini kwake na akiziuza pale sokoni. Ilikuwa Abdul apoteze kazi yake kama Market Master.
Wazee
wa pale sokoni walisoma Halal Badr.
In Shaa Allah iko siku nitakieleza hiki
kisa.
Shariff Abdallah Attas na Mzee Kisaka waliokuwa wakifanya kazi chini ya Abdul Sykes walikifahamu vizuri kia hiki.
No comments:
Post a Comment